Balozi Patrick Tsere (kushoto) akiwa na Balozi Mindi Masiga (kulia) wakimfuatilia Balozi Peter Kalaghe (hayupo pichani) akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo ya waandishi wa habari ya kuandika habari za kidiplomasia yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianio wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam |
Baadhi ya washiriki mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini wakimfuatilia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akifungua mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kufanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam |
Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari ya kuandika habari za kidiplomasia yaliyoandaliwa na Wizara na kufanyika katika Chuo cha Diplomasia cha Dar es Salaam |
Balozi Patrick Tsere akiongea na waandishi wa habari juu ya kuandika habari kwa kuzingatia uzalendo katika kulinda taswira ya Tanzania wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini yanayofanyika katika Chuo cha diplomasia jijini Dar es Salaam |
Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango , Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Justine Kisoka akizungumza katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na wizara na kufanyika katika chuo cha diplomasia jijini Dar es salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (aliyekaa katikati) katika picha ya pamoja na waandishi wa habari nchini baada ya kufungua mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amefungua mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini.
Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam, Balozi Mulamula amewataka watendaji wa Wizara kuhakikisha wanaimarisha mahusiano kati ya wizara na vyombo vya habari.
'Tuwe pamoja siku zote tuendelee kushirikiana, vyombo vya habari ni wadau muhimu, tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya nchi yetu,' alisema.
Amesema waandishi wa habari wanajukumu la kuilinda na kuitetea taswira ya Tanzania kupitia kazi zao na kuwataka waandishi wa habari nchini kuzingatia taswira ya nchi wakati wanatekeleza majukumu yao.
"Wanahabari, tuko hapa kuelimishana juu ya kuandika habari za kidiplomasia, niwaombe kwanza mhakikishe mnailinda taswira ya nchi, hii ni nchi yetu wote, ikiharibika taswira yake hata wewe uliyeandika pia utakutana na athari zake, hata uende wapi utajulikana kama Mtanzania. Mnapoandika mzingatie uzalendo na miiko ya taaluma ya uandishi wa habari," alisema Balozi Mulamula.
Pia aliongeza kusema mafunzo haya ambayo yatakuwa endelevu yanalenga pamoja na mambo mengine kutoa uelewa kuhusu masuala ya diplomasia ikiwemo Itifaki, Diplomasia ya Umma, Uzalendo na Mawasiliano ya kimkakati baina ya Tanzania na nchi zingine.
Kadhalika, aliwashukuru waandishi wa habari kote nchini kwa ushirikiano uliopo kati yao na wizara na kuwataka kuzingatia mafunzo yatakayotolewa kwao.
"Nawashukuru kwa ushirikiano na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa Wizara na Sera ya Mambo ya Nje inayosisitiza katika Diplomasia ya Uchumi. Nawaomba mzingatie mafunzo haya kwani yatakuwa na tija kubwa kwenu," alisisitiza Balozi Mulamula.
Awali akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali Waziri ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga alieleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini katika eneo la kuandika habari za kidiplomasia.
Amesema mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwani kufanya hivyo kutasaidia kuboresha uandishi na kuwa daraja kati ya Wizara na waandishi wa habari na hivyo kuwafikia wananchi wengi.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yamewashirikisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya hapa nchini.