Wednesday, October 26, 2022
Tuesday, October 25, 2022
DKT. MWINYI AWATAKA MABALOZI KUZINGATIA MASLAHI YA TAIFA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi kuzingatia maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanapotekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi.
Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022 kwa ajili ya kujitambulisha.
“Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi wahakikishe wanaangalia maslahi mapana ya Tanzania wanapotekeleza diplomasia ya uchumi, hususan uchumi wa buluu ambao ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” amesema Dkt. Mwinyi
Kwa Upande wake, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameahidi kuyafanyia kazi maagizo na miongozo mbalimbali inayotolewa na itakayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa weledi na wakati.
“Mhe. Rais napenda kukuhakikishia kuwa nitasimamia na kutekeleza yote uliyotuelekeza kwa wakati na kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” amesema Dkt. Tax
Katika ziara hiyo, Dkt. Tax alipata fursa pia ya kujitambulisha kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wameahidi kumpatia ushirikiano unaohitajika ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.
Naye Dkt. Tax amesema yupo tayari kwa ajili ya kazi ya kuitumikia nchi na kuhakikisha ushirikishwaji wa Zanzibar juu ya mambo ya muungano sambamba na fursa mbalimbali ikiwemo maazimio yanayopitishwa mbele ya jumuiya za kikanda na za kimataifa.
KATIBU MTENDAJI WA SADC AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokutana kwa mazungumzo na Katibu
Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Mpedi Magosi wakati wa ziara yake ya kikazi nchini
hivi karibuni.
Mhe. Dkt. Tax amesema lengo kuu la Jumuiya hiyo ni kuziwezesha kujikomboa
kiuchumi nchi za Kusini mwa Afrika. Lakini pia kuhakikisha nchi za ukanda huo
zinakuwa na amani na utulivu, hivyo Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi
zozote zinazofanywa na Sekretarieti hiyo ili kufikia malengo hayo.
Pia alivitaja vipaumbele vya Tanzania kwenye Jumuiya hiyo kuwa ni pamoja na
Amani na Usalama, Kilimo, Uchumi wa Buluu, maendeleo ya Miundombinu na
uchumi wa kidigitali.
Ameongeza kusema kazi kubwa ya Sekretarieti hiyo ni kusimamia kwa bidii
utekelezaji wa mipango, itifaki, na mikataba mbalimbali iliyokwishapitishwa au
kuridhiwa na nchi wanachama.
"Nakushukuru sana kwa kutenga muda wako na kuja kutembelea Tanzania.
Nakupongeza pia kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya ya kuongoza chombo muhimu
kinachosimia utekelezaji wa malengo ya Jumuiya yetu. Ushauri wangu kwako ni
kuendelea kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ambayo tayari yapo kwa
ajili ya utekelezaji" alisema Mhe. Dkt. Tax.
Kadhalika alimkumbusha Mhe. Magosi kuendeleza jitihada za kutangaza majukumu na
umuhimu wa Jumuiya hiyo katika Nchi Wanachama kwani bado Agenda na Madhumuni ya
Jumuiya hayajulikani ipasavyo miongoni mwa wananchi katika Nchi Wanachama.
Kwa upande wake, Mhe. Magosi alitumia
fursa hiyo kumpongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo mpya na
kumuahidi ushirikiano wake binafsi na kutoka katika Sekretarieti. Pia
alimpongeza kwa uongozi makini wa miaka nane kama Katibu Mtendaji wa
Sekretarieti ya SADC hususan katika uandaaji wa nyaraka ikiwemo
Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC wa mwaka 2020-2030.
Pia aliipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana
na Ugaidi na kwamba uwepo wa kituo hicho hapa nchini kunadhihirisha utayari wa
Tanzania katika kuhakikisha suala la usalama katika kanda linapewa kipaumbele.
Wakati wa ziara hiyo ya siku mbili hapa nchini kuanzia tarehe 24 hadi 25
Oktoba, 2022, Mhe. Magosi amekutana kwa mazungumzo na Mhe. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametembelea Kituo cha Kikanda cha
Kupambana na Ugaidi pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Ujumbe uliofuatana na Mhe. Masego wakifutilia kikao |
Ujumbe wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola (kushoto) wakifuatilia mazungumzo |
Mhe. Masego akimpatia zawadi Mhe. Dkt. Tax |
Picha ya pamoja |
Mhe. Masego akizunguza wakati alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi kilichopo Dar es Salaam |
Mhe. Masego alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi |
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Kayola (kushoto) wakati wa ziara ya Mhe. Masego kwenye Kituo cha Kupambana na Ugaidi |
Kikao kikiendelea |
Kikao kati ya Mhe. Masego na MSD kikiendelea |
Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo akimsikiliza Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Masego (hayupo pichani) |
Mhe. Masego akizungumza alipotembelea MSD |
Mazungumzo yakiendelea |
Mhe. Maseko akipokea zawadi ya barakoa zinazotengenezwa na MSD kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo. |
Picha ya pamoja |
TANZANIA YAIKUMBUSHA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUISADIA AFRIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI
Wito huo umetolewa na Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akihutubia maadhimisho ya miaka 77 ya
Umoja yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Oktoba 2022.
Amesema Mkataba huo unaitaka Jumuiya ya
Kimataifa kuzisaidia nchi za Afrika katika maeneo mbalimbali ikiwemo
kujenga uwezo, kubadilishana teknolojia na kuhakikisha nchi hizo
kiuchumi ili kuziwezesha kujitegemea katika kukabiliana na athari
zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
“Wiki mbili zijazo kuanzia leo, Mkutano wa 27 wa
Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utafanyika Sharm El Sheikh,
Misri. Ni kwa muktadha huo tunahitaji kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba
pamoja na mchango mdogo wa Afrika katika ongezeko la joto duniani, bado Afrika
ni Bara linaloathirika zaidi na mabadiliko hayo kutokana na uwezo mdogo wa
kukabiliana na changamoto hizo. Hivyo, tunaikumbusha Jumuiya ya Kimataifa
kutimiza ahadi kulingana na maelekezo katika Mkataba wa Paris,’’ amesema
Mhe. Dkt. Ndumbaro.
Aidha, Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania
itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza program
mbalimbali za maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu
kwa manufaa ya wananchi.
Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema, Tanzania inapoungana
na ulimwengu mzima kuadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa ni kielelezo
kinachowakumbusha wadau wote nchini kujiimarisha katika ushirikiano ili
kuiwezesha Tanzania kutekeleza pamoja na mambo mengine Mpango wake wa Maendeleo
wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Tatu wa Umoja wa
Mataifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu
inayosema “Maendeleo Yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi yote” imebeba
ujumbe mzito unaomkumbusha kila mmoja kuungana na kutafuta suluhu kwa
changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia pasipo kumwacha mtu yoyote nyuma.
Pia amesema Tanzania ipo kwenye hatua za mapitio
ya utekelezwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuwataka wadau
mbalimbali kushirikiana nayo ili kufanikisha mapitio hayo.
Vilevile, wakati wa maadhimisho hayo,
Mhe. Dkt. Ndumbaro ameuomba Umoja wa Mataifa kuitambua Lugha ya Kiswahili
kama Lugha rasmi ya Umoja huo.
“Tunapoadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa,
Tanzania inaikumbusha dunia kuwa wakati umefika sasa wa kuridhia Kiswahili kuwa
miongoni mwa Lugha rasmi za Umoja huo” alisema Dkt. Ndumbaro.
Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya
Kimataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea
kuhifadhi wakimbizi na kwamba Umoja wa Mataifa na Taasisi zake utaendelea
kushirikiana na Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema Umoja huo unachangia katika miradi
mbalimbali ya kuwainua kiuchumi wanawake na vijana walio katika mazingira
magumu ikiwemo kuchangia katika uunzishwaji wa madawati ya jinsia yaliyo chini
ya Jeshi la Polisi ambapo kwa mwaka huu madawati 400 yameanzishwa nchini kote.
Wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Ndumbaro
alipata fursa ya kuzindua Tovuti ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili.
Maadhimisho hayo ya aina yake yamehudhuriwa na
Viongozi na wadau mbalimbali wakiwemo Mhe. Tabia Mwita, Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa yaliyopo nchini.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Zlatan Milisic akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa |
Mhe. Dkt. Ndumbaro akifuatilia Wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa |
Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia alikuwa Mshereheshaji wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa , Bi. Ellen Maduhu akitoa mwongozo wa maadhimisho hayo kwa washiriki |
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Kibasila ya jijini Dar es Salaam wakitoa burudani na elimu kuhusu historia ya Umoja wa Mataifa kupitia sanaa ya uimbaji |
Mhe. Dkt. Ndumbaro akizindua rasmi Tovuti ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili |
Picha ya pamoja |
Monday, October 24, 2022
RAIS TSHISEKEDI AMALIZA ZIARA YA KITAIFA NCHINI
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Felix Tshisekedi amemaliza ziara ya Kitaifa ya siku mbili aliyoifanya nchini tarehe 23 na 24 Oktoba, 2022.
Rais. Tshisekedi ameagwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mapema kabla ya kuondoka, Mhe. Rais Tshisekedi ametembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Jijini Dar es Salaam na kujionea hatua mradi huo ulipofikia.
Rais Tshisekedi alipotembelea mradi wa ujenzi wa SGR, aliambatana na Waziri wa Maambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Juni 14, 2019 Rais Tshisekedi kwa mara ya kwanza alifanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - (TRC), Bw. Masanja Kadogosa wakati Rais Tshisekedi alipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa SGR Jijini Dar es Salaam. Mhe. Tshisekedi ameambatana na Waziri wa Maambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimuuliza jambo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - (TRC), Bw. Masanja Kadogosa wakati Rais Tshisekedi alipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa SGR Jijini Dar es Salaam |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi wakiwa katika jukwaa la salamu za heshima za kijeshi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kabla ya Rais Tshisekedi kuondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake |
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ziara yake nchini |
Rais wa Jamhuri ya KIdemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ziara yake nchini |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi waandamizi wa serikali wakimuaga Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Félix Tshisekedi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha ziara yake nchini |
Sunday, October 23, 2022
TANZANIA, DRC ZAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA NA UCHUMI
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inaedelea kuudhirihishia ulimwengu kuwa imedhamiria kushirikiana na wadau wote, zikiwemo nchi jirani ili kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote.
Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) nchini, Mhe. Felix Tshisekedi ambayo ni mwendelezo wa ziara kadhaa za viongozi wa kitaifa na mashirika ya kimataifa nchini ni kielelezo cha wazi cha kutambua nguvu ya ushirikiano katika kukuza uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla.
Rais Samia na mgeni wake, Rais Tshiseked katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar Es Salaam tarehe 23 Oktoba 2022, waliafikiana nchi zao ziongeze nguvu kuimarisha ushirikiano katika sekta za kiuchumi, miundombinu, biashara, usafirishaji, uwekezaji, ulinzi, usalama na mawasiliano.
Rais Samia aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kibishara ili kukuza biashara na kwamba mawaziri wa biashara wa pande zote mbili wameagizwa kulifanyia kazi suala hilo haraka iwezekanavyo.
"Ikumbukwe DRC ni mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika mikakati ya kuendeleleza miundombinu ya Jumuiya hiyo, kuna mpango wa kujenga ushoroba wa kati utakaounganisha Tanzania na DRC ili kukuza biashara na mtangamano baina ya nchi wanachama', alisema Rais Samia.
Kwa upande wake, Rais Tshisekedi alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama kwa sababu bila ya amani na usalama hakuna miradi itakayoweza kutekelezwa
“Sisi kwetu DRC usalama ni muhimu sana na ndiyo maana mimi kama Rais nimeweka mkazo wa kujenga na kuimarisha uhusiano wa kindugu na majirani zetu,” alisema Rais Tshisekedi.
Rais Samia na mgeni wake walishuhudia uwekaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula.
Uwekaji saini wa mkataba huo umekuja muda mfupi baada ya nchi hizo pia kusaini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama wakati wa Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya nchi hizo uliofanyika Jijini Dar Es Salaam mwezi Septemba 2022. Ikumbukwe pia Rais Samia alifanya ziara ya kitaifa nchini DRC mwezi Agosti 2022 mara baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika nchini humo ambapo Rais Tshesiked alikabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya hiyo.
Ziara hii ya Rais wa DRC na nyingine zilizofanywa na viongozi wa ngazi tofauti baina ya nchi hizi mbili pamoja na uamuzi wa Tanzania wa kufungua Ofisi ya Konseli Kuu katika mji wa Lubumbashi vinatajwa kuwa vitaimarisha uhusiano na kukuza biashara baina ya mataifa hayo mawili yenye utajiri mkubwa wa maliasili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam |
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi wakishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula Ikulu Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax akifuatilia Mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi na waandishi wa Habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam |