Wednesday, April 3, 2024

WAZIRI WA DENMARK ATEMBELEA HOSPITALI YA CCBRT

 




Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa watendaji wa Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es salaam alipoitembelea kujionea jinsi hospitali hiyo inavyoendesha shughuli zake kwa Watanzania.

Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen akisikiliza maelezo jinsi mguu bandia unavyotengenezwa katika Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es salaam alipoitembelea kujionea jinsi hospitali hiyo inavyoendesha shughuli zake kwa Watanzania.

Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa watendaji wa Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es salaam alipoitembelea kujionea jinsi hospitali hiyo inavyoendesha shughuli zake kwa Watanzania.

ziara ikiendelea

maelezo yakiendelea kutolewa wakati wa ziara hiyo


Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen akiangalia  baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na wagonjwa katika Hospitali ya CCBRT jijini Dar es salaam alipoitembelea kujionea jinsi hospitali hiyo inavyoendesha shughuli zake kwa Watanzania.

  

Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen ametembelea Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es salaam na kujionea jinsi hospitali hiyo inavyoendesha shughuli zake kwa Watanzania.

Mhe. Jorgensen ametembelea sehemu zinazotoa Huduma ya matibabu kwa kına mama walioathiriwa na ugonjwa wa Fistula, sehemu ya uundwaji wa viungo bandia na mazoezi kwa watumiaji wa viungo hivyo bandia , urekebishaji wa uoni kwa watoto waliozaliwa na uoni hafifu au bila macho na wodi ya kijifungulia.

Mhe. Jorgensen ametembelea hospitali hiyo ya CCBRT ili kujionea jinsi fedha zinazotolewa na Serikali ya Denmark zinavyowezesha utoaji wa huduma bora kwa Watanzania

WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA BALOZI WA HESHIMA WA TANZANIA NCHINI DENMARK

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Denmark Bw. Simon Mears hayupo pichani walipokutana katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden Mhe. Grace Olotu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza na Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Denmark Bw. Simon Mears (wa kwanza Kushoto)  walipokutana katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, wa pili kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden Mhe. Grace Olotu na wa kwanza kulia Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme.

mazungumzo yakiendelea

 Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Denmark Bw. Simon Mears akizungumza kitu alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba hayupo pichani katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, anayesikiliza kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden Mhe. Grace Olotu.

 

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) amekutana na kuzungumza na Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Denmark Bw. Simon Mears katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Katıka mazungumzo na Bw. Mears Mhe. Waziri Makamba amempongeza kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya nchini Denmark kwa niaba ya Tanzania

Amemwambia kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kumpa ushirikiano utakaomuwezesha kutekeleza majukumu yake nchini Denmark.

Amesema Tanzania sasa inaangalia namna bora ya kufanya biashara na Denmark ili kuvutia Wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi nchini.

Amesema  Serikali inachukua hatua kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini ili kuvutia wawekezaji hivyo fursa hiyo itumiwe kikamilifu.

Naye Bw. Mears ameshukuru kukutana na mhe Waziri  na kuahidi kuendelea kufanyakazi aliyokabidhiwa kwa ufanisi .

Amesema Denmark ina nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya nishati ya kijani, nishati mbadala pamoja na usalama.

Tanzania na Denmark zimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara, uwekezaji, utalii, elimu na etc

Wednesday, March 27, 2024

WAZIRI MAKAMBA-AFRICA50 WAJADALI NAMNA YA KUSHIRIKIANA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisalimiana na na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse alipowasili katika ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (MP) amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse, katika ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma. 

Mazungumzo hayo yalijikita kujadili namna bora ya kushirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa miundombinu na miradi ya mazingira. Baadhi ya miradi iliyojadiliwa ni pamoja na mradi wa kusambaza umeme, ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani na usambazaji wa gesi jijini Dar es Salaam.

Bwana Ebobisse ameeleza kuwa Africa50 inaiona Tanzania kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji kutokana na mazingira mazuri yaliyowezeshwa kwa sera na sheria rafiki, hivyo imehamasika kuwekeza nchini katika miradi ya maendeleo ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuwaletea wananchi wake maendeleo. 

Waziri Makamba kwa upande wake ameeleza kuwa Serikali chini ya Uongozi imara wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatilia mkazo wa ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Ameongeza kuwa imani hiyo kwa sekta binafsi imeongeza mwitikio wa makampuni binafsi kutoka ndani na nje ya nchi kushirikiana na serikali katika kuendeleza na kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Africa50 ni taasisi ya kifedha yenye Makao Makuu yake Casablanca, Morocco ambayo imejikita katika nyanja mbili za uwekezaji ambazo ni; Maendeleo ya Miradi na Fedha za Mradi (Project Development and Project Finance) ikiwa na lengo la kuchagiza maendeleo ya miundombinu barani Afrika kwa kuzingatia umuhimu wa mchango wa mradi husika kitaifa na kikanda.

Tanzania ilijiunga na Afrika50 tarehe 14 Februari, 2023, kwa kusaini Mkataba wa Hisa za Usajili. 

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Mhe. Tim Watts MP. 

Mazungumzo hayo yameangazia masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Australia na Kimataifa hususan yanayolenga kutatua changamoto za amani na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya ya madola.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse yaliyofanyika katika ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba yaliyofanyika Mtumba jijini Dodoma
Mazungumzo yakiendeleo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo kwa njia ya simu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Mhe. Tim Watts MP.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo kwa njia ya simu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Mhe. Tim Watts MP.

Mazungumzo yakiendelea

Saturday, March 23, 2024

WAHIMIZA UMOJA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA KIUSALAMA MASHARIKI MWA DRC


Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) zimekumbushwa kuwa ni jukumu lao kufanya kazi kwa pamoja ili kumaliza changamoto za kiusalama zinazozikabili Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidiplomasia ya Congo (DRC).

 

Ukumbusho huo umetolewa na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichelema wakati anafungua Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC uliohitimishwa jijini Lusaka, Zambia Machi 23, 2024.

 

Katika Mkutano huo ambapo Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Philip Isdor Mpango pamoja na mambo mengine, ulilenga kutathimini hali ya usalama katika Kanda ya SADC. Ilielezwa kuwa hali ya usalama Mashariki mwa DRC bado hairidhishi, hivyo umetolewa wito kwa nchi wanachama na washirika wa maendeleo kuchangia rasilimali ili vikosi vya kulinda amani vilivyopo huko na vingine vitakavyopelekwa, viweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.

 

Ilibainishwa kuwa suala la kutafuta amani katika Kanda ni suala la kimkataba wa jumuiya hiyo na Itifaki ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, hivyo ni wajibu kwa mataifa hayo kuungana pamoja kukabiliana na changamoto za kiusalama.

 

Wachambuzi wa mambo wamesema kuwa mahudhurio mazuri ya viongozi katika ngazi ya Rais, Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu katika mkutano huo yanadhihirisha kuwa nchi za SADC zimedhamiria kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ya usalama nchini Msumbiji na DRC.

 

Marais walioshiriki Mkutano huo ni Mhe. Hakainde Hichelema wa Zambia, Mhe. Emmerson Mnangwa wa Zimbabwe: Mhe. Félix Tshisekedi was DRC; Mhe. Lazarus Chakwera wa Malawi; Mhe. Filipe Nyusi wa Msumbiji na Mhe. João Lourenço wa Angola. Nchi za Tanzania na Namibia ziliwakilishwa na Makamu wa Rais, Lesotho, Waziri Mkuu na Afrika Kusini na Botswana ziliwakilishwa na Mawaziri wa Ulinzi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Philip Isdor Mpango akisoma makabrasha ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Lusaka, Zambaia Machi 23, 2024. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Mhe. January Makamba (Mb)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Philip Isdor Mpango, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Mhe. January Makamba wakiimba nyimbo za Taifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Lusaka, Zambaia Machi 23, 2024.


TANZANIA –KENYA ZAKUBALIANA KUONDOA VIKWAZO VYA KIBIASHARA

Tanzania na Kenya zimekubaliana na kutia saini makubaliano ya kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru ili kuruhusu raia kutoka nchi hizo kufanya biashara baina yao kwa urahisi na kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Makubaliano hayo yamefikiwa na kutiwa saini na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano wakati wa Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024. 

Mkutano huo ulianza kwa ngazi ya watalaam kisha ngazi ya Makatibu Wakuu ambapo zaidi ya vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru zaidi ya 14 vilijadiliwa na kuwekewa mpango wa kuendelea kuviondoa vyote. Tanzania na Kenya ni wabia wakubwa wa biashara na hivyo kuondolewa kwa vikwazo hivyo vitasaidia kuongezeka mara dufu kiwango cha kifanyika kwa biashara baina ya mataifa hayo.

Viongozi wengine walioshiriki katika Mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masala ya EAC Balozi Stephen P. Mbundi, Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda wa Kenya Mhe. Peninah Malonza, Makatibu Wakuu wanaohusika na masuala ya uwekezaji, viwanda, biashara na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. Bernard Yohana Kibese na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mhe. Isaac Njenga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano wakionesha hati za makubalino ya kuondoa vikwako vya biashara visivyo vya kiforodha kwenye mkutano uliofanyika mjini Kisumu baina ya Tanzania na Kenya tarehe 22/03/2024. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano wakisaini makubalino ya kuondoa vikwako vya biashara visivyo vya kiforodha kwenye Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024. 
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Benjamin Mwesiga akichangia hoja kwenye Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024. 
Wajumbe wakifuatilia Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Mawaziri wa kuondoa vikwako vya biashara visivyo vya kiforodha uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024.

BILA YA AMANI, HAKUNA MTANGAMANO NA MAENDELEO

 

Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimetakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa nchi zao zinakuwa na amani, Umoja na utulivu na kutafuta ufumbuzi wa migogoro kwa kutumia njia zao wenyewe.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Mulambo Haimbe wakati anafungua Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

 

Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo baada ya Zambia na katika Mkutano huo, Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb).

 

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unapokea ripoti ya utekelezaji wa vikosi vya kulinda amani katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

 

Nchi Wanachama zimehimizwa kuimarisha zaidi mshikamano na kuchangia rasilimali walizonazo ili kuviangamiza vikundi vya waasi vinavyotishia amani kwenye Kanda ya SADC. Imeelezwa kuwa bila ya amani na Usalama katika Kanda hiyo, wananchi wasitarajie kufikiwa kwa mtangamano na maendeleo ya kweli.

 

Mkutano huo wa Mawaziri ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC utakaofanyika Machi 23, 2024 ambapo Tanzania itawakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) akisoma makabrasha yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024. Kulia kwake ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo

Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Mulambo Haimbe akisoma hotuba wakati ufunguzi wa Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

Wajumbe wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kulia) wakiimba nyimbo za taifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

Friday, March 22, 2024

NCHI ZA SADC ZAJIPANGA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA KIUSALAMA MASHARIKI MWA DRC NA JIMBO LA CABO DELGADO


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

Mkutano huo ni maandalizi ya Mikutano ya ngazi ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi na Serikali itakayofanyika tarehe 22 na 23 Machi 2024 mutawalia.

Wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Anamela Gundersen alisema mwitikio mkubwa wa wajumbe kushiriki mkutano huo ni ishara ya wazi kuwa nchi wanachama zimedhamiria kumaliza changamoto za kiuslama katika kanda ya SADC, hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashsriki, Mhe. January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) watashiriki Mkutano wa ngazi ya Mawaziri ambao umepangwa kufanyika mchana na utakamilisha agenda zitakazojadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiwa katika Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaofanyika Lusaka, Zambia 

Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Anamela Gundersen akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaofanyika Lusaka, Zambia 

Wajumbe wa Mkutano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaofanyika Lusaka, Zambia 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na wajumbe wengine wa mkutano wakiomba dua kwa dakika moja kufuatia vifo vya Rais wa Nambia, Hayati 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kulia) akiongea na Maj. Gen. Mbaraka Naziad Mkeremy kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania kabla ya kuanza mkutano 




Thursday, March 21, 2024

NAIBU WAZIRI WA USHIRIKIANO WA MAENDELEO WA SWEDEN AZURU NCHINI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipomlaki katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 21 – 22 Machi, 2023 na kupokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa jijini Dodoma.

Lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi uliopo kati ya Tanzania na Sweden. Pia kupitia ziara hiyo Serikali ya Sweden inatarajiwa kueleza dhamira ya kuongeza muda wa Mpango wa Maendeleo unaotarajiwa kafikia ukomo mwaka huu 2024.

Baada ya kuwasili Mhe. Janse amefanya mazungumzo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) ambapo katika mazungumzo yao wamejadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za viwanda, biashara, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu hususan uendelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (Bus Rapid Transit Project).

Viongozi wengine aliofanya nao mazungumzo jijini Dododma ni pamoja na, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.)

Vilevile, Mhe. Janse anatarajia kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk tarehe 22 Machi 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Tanzania na Sweden zilianzisha ushirikiano tangu mwaka 1960 ambapo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za nishati, tafiti, elimu, usimamizi wa mazingira, uchangiaji wa bajeti ya Serikali, biashara, viwanda, uwekezaji na miundombinu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias wakati wa mapokezi ya Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipomlaki katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma. Kando yao ni Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akijadili jambo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipowasili jijini Dodoma
Picha ya Pamoja
Mazungumzo baina ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) na  Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana yakiendelea jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana  Janse akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana  Janse yaliyofanyika jijini Dodoma
Picha ya pamoja

Tuesday, March 19, 2024


 


 

TAARIFA KWA UMMA

 

 

SEMINA MAALUM KUHUSU MPANGO WA BIASHARA WA NCHI YA UINGEREZA NA NCHI ZINAZOENDELEA KUFANYIKA TAREHE

 28 MACHI 2024, DAR ES SALAAM.

 

Dodoma, tarehe 19 Machi, 2024.

 

Semina maalum kuhusu Mpango wa Biashara wa nchi ya Uingereza na Nchi Zinazoendelea (UK Developing Countries Trading Scheme – DCTS) inatarajiwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Machi 2024, kuanzia saa 3:00 asubuhi.

 

Semina hiyo ya siku moja itafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na kufungwa na Mhe. Omar Said Shabaan, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar.

 

Semina hiyo ina lengo la kufahamisha wadau wa biashara  nchini juu ya fursa ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Uingereza kupitia Mpango wa Serikali ya Uingereza wa Kufanya Biashara na Nchi Zinazoendelea uliozinduliwa mwezi Mei mwaka 2023. Tanzania ni miongoni mwa nchi 65 ambazo Uingereza imezijumuisha katika mpango huo ili kuweza kuuza bidhaa zake bila kulipa ushuru na imeingia pia katika kundi la nchi ambazo asilimia 99 ya bidhaa zake zitanufaika na msamaha wa kodi.

 

Walengwa wa semina hiyo ni wadau wa biashara wenye nia ya kuuza bidhaa za aina mbalimbali katika soko la Uingereza. Wadau wanaweza pia kushiriki katika Semina hiyo kwa njia ya mtandao, kupitia link maalum ya mtandao wa “Teams” itakayotolewa kwa watakaojisajili kupitiahttps://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSdjoGDLwkXfu9PWlV7Oc3LOnn5tRyELsimZVUaMaFhCGFB1Mw/viewform

 

Aidha, wananchi wote wanaweza kuifuatilia Semina hiyo kupitia na chaneli ya YouTube ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ijulikanayo kama Ubalozi London (http://www.youtube.com/@ubaloziLondon).

 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali