Monday, June 10, 2024

BALOZI MUSSA AWAASA VIJANA KUWA MABALOZI WAZURI NJE YA NCHI


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa amewaasa vijana waliochaguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana maarufu kwa jina la “Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders” kuwa mabalozi wazuri katika mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 18 Juni, 2024 jijini Washington, Marekani.

Nasaha hizo zimetolewa katika hafla fupi ya kuwaaga vijana hao 26 ambayo ilihusisha makabidhiano ya bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni ishara ya kuitangaza na kuiwakilisha nchi katika heshima inayostahili iliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mtumba, Dodoma tarehe 10 Juni, 2024.

Balozi Mussa aliwapongeza vijana hao kwa kuonesha uwezo na jitihada binafsi kuchukua nafasi ya kuomba na kufanikiwa kupita katika mchujo wa vijana wengi walioihitaji fursa hiyo. Hivyo, ni wema wakazingatia mafunzo na kuhakikisha ujuzi na elimu watakayoipata inaleta manufaa kwao na kuwajengea uwezo vijana wengine waliopo nchini.

"Hii ni programu maalum ambayo itawajengea uwezo katika masuala ya uongozi hususani, uongozi katika masuala ya usimamizi wa umma, uongozi katika usimamizi wa biashara na uongozi katika masuala ya ushirikishwaji wa jamii yakiwa ni maeneo mtambuka katika ukuaji wa nchi za Afrika.” alisema Balozi Mussa.

Pia akawaeleza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za nchi husika pamoja na kujikita katika malengo yanayowapeleka nchini Marekani ili kufanikisha kutumia fursa hiyo kujenga uwezo katika maoneo yao husika ya kiutendaji sambamba na kuijengea nchi sifa nzuri.

Aidha, amewasisitiza kuzingatia tamaduni na mila za kitanzania wawapo nchini humo kwakuwa mafunzo hayo yanahusisha mataifa tofauti hivyo ni vema kuepuka changamoto mbalimbalii za kimaadili zinazoweza kuwaharibia sifa binafsi na taifa kwa ujumla. Vilevile, katika hilo akasisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi za ubalozi zilizopo jijini Washington.

Nao vijana wanaoenda kushiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendeleza kuimarisha ushirikiano mzuri na Serikali ya Marekani na hivyo kuwawezesha kushiriki kwa wingi katika mafunzo hayo ambayo pamoja na masuala mengine yatawajengea na kukuza uwezo katika teknolojia inayopatikana katika taifa hilo kubwa lililopiga hatua kimaendeleo sambamba na kukutana na wadau katika sekta husika.

Programu hii inatarajiwa kutimiza miaka 10 tangu ianzishwe mwaka 2014 ambapo imekuwa ikitoa mafunzo kwa washiriki kwa njia ya vitendo na kuingia darasani na hivyo, kuwawezesha kushiriki katika majukumu ya kijamii pamoja na kufanya ziara katika ofisi mbalimbali za umma na mashirika nchini Marekani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisisitiza jambo alipokuwa akiwaaga washiriki wa programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana(Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program)yatakayofanyika nchini Marekani.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akikabidhi Bendera ya Taifa kwa vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
Picha ya pamoja. 

KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KIKAO CHA SADC MASUALA YA SIASA NA DIPLOMASIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024.


Akifungua kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ngazi ya Makatibu Wakuu , Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia,  Bi. Etambuyu Gundersen aliwataka wajumbe kujadili na kutoa mapendekezo katika agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao ili hatimaye mapendekezo hayo yawasilishwe kwenye kikao cha Mawaziri kitakachofanyika mwezi Julai 2024 kwa ajili ya kuridhiwa.

 

Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Balozi Shelukindo amezishukuru na kuzipongeza Nchi Wanachama wa SADC kwa kufanikisha uundwaji na uzinduzi wa Sanamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliofanyika mwezi Februari 2024 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

 

Amesema  uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na idadi kubwa  ya wakuu wa nchi  wa Afrika  ulidhihirisha namna ambavyo  wanaenzi mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Mwalimu Nyerere kwenye Ukombozi wa  Nchi za Kusini mwa Afrika.

 

Kadhalika amesema  Tanzania inaendelea na mawasilianao ya ndani ili kukamilisha Mpango  wa Taifa  wa Utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 1325 kuhusu kuwawezesha Wanawake kushiriki  katika juhudi  za  kutatua, kuzuia na kudhibiti migogoro duniani huku akizipongeza nchi zilizokamilisha Mpango huo ikiwemo Zimbawe na Madagascar.

 

Vilevile, ametumia fursa hiyo kuzipongeza Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Madagascar kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika kwenye nchi hizo kwa amani na utulivu  tarehe 29 Mei 2024 mtawalia.

 

Amesema, kikanda uchaguzi katika nchi hizi mbili umeakisi viwango vya kimataifa vya demokrasia pamoja na kanuni na miongozo ya SADC kuhusu uchaguzi unaofuata misingi ya demokrasia.

 

Kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ajili ya kuandaa mkutano wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2024,  kimehudhuriwa na Nchi za Tanzania, Lesotho, Eswatini, Botswana, Angola, Namibia, Afrika Kusini, Shelisheli ,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Zimbabwe.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024
Katibu Mkuu, Balozi Shelukindo akichangia hoja wakati wa Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024. Kulia ni Afisa Mambo ya Nje anayeshughulikia Dawati la SADC, Bi. Shazma Msuya akinukuu taarifa ya kikao hicho. 

 
Kikao kikiendelea

Friday, June 7, 2024

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CANADA AKUTANA NA MABALOZI WA AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Melanie Joly akisalimiana na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Canada, Bw. Charles Faini wakati wa Mkutano kati yake na Mabalozi wa Afrika  uliofanyika hivi karibuni jijini Ottawa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Melanie Joly akizungumza na Mabalozi wa Afrika waliopo nchini humo uliofanyika hivi karibuni jijini Ottawa



 

Monday, June 3, 2024

MKUTANO WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI LINALOSHUGHULIKIA MASUALA YA EAC NA MIPANGO WAANZA ARUSHA


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Benjamini Mwesiga akichangia hoja kwenye Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha

Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umeanza leo tarehe 3 Juni 2024 jijini Arusha.

Mkutano huo wa siku tano kuanzia Juni 3-7, 2024 umeanza kwa Ngazi ya Wataalam na na baadaye utafuatiwa na Ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 6 Juni 2024 na kuhitimishwa na Mkutano Ngazi ya Mawaziri ukaofanyika tarehe 7 Juni 2024. 

Mkutano huo katika Ngazi ya Wataalam pamoja na mambo mengine utapokea na kujadili mapendekezo na taarifa mbalimbali za Jumuiya ikiwemo: Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya; Mapendekezo ya kuhuisha Mipango ya Jumuiya na Mipango ya Nchi Wanachama; Taarifa ya Wakurugenzi wa Masuala ya Kazi kuhusu Ukamilishaji wa Rasimu Iliyorekebishwa ya Sera ya Uhamiaji ya Wafanyakazi wa Jumuiya.

Masuala mengine yatakayo jadiliwa ni pamoja na taratibu za Uanzishwaji wa Jukwaa la Mashauriano kuhusu Uhamaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Kuidhinisha Sera na Mkakati wa Pili wa Mawasiliano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na Kuidhinisha Kalenda ya Shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha Julai – Desemba 2024.

Akifungua mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya forodha, biashara na fedha Bi. Annette Ssemuwemba amehimiza kuhusu umuhimu wa mkutano huo katika kusimamia utekelezaji na ufanisi wa sera na mipango ya Jumuiya ili kukidhi matarajio ya Wananchi. 

“Mtakumbuka kuwa takriban miaka miwili sasa hakupata fursa ya kufanya mkutano huu, kwa sababu hiyo kwa umoja wetu tutumie fura hii hadhimu kujadili na kutafuta majawabu yatakayotupa uelekeo mpya na sahihi wa kutekeleza na kusimamia kwa ufanisi sekta mbalimbali ikiwemo bishara na fedha kwa maendeleo ya Jumuiya yetu” Alieleza Bi. Annette Ssemuwemba

Vilevile mkutano huo unatarajiwa kufanya tathimini ya hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyoamuliwa kwenye mikutano iliyopita ikiwemo mpango wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na Uondoaji wa Vikwazo vya Biashara visivyokuwa vya kikodi,.

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Jumuiya, huku ujumbe wa Tanzania ukijumuisha Mkurugenzi wa Mawasiliano Balozi Mindi Kasiga, Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka, na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Benjamini Mwesiga ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe huo, wote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mkutano ukiendelea
Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akifuatilia Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha
Mkutano ukiendelea
Meza kuu wakiongoza Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha

KAMATI YA BUNGE YA NUU YASISITIZA UWAJIBIKAJI


Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imeisisitiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yake kwa wakati iliyo katika hatua mbalimbali.

 

Msisitizo huo umetolewa katika kikao cha ufuatiliaji kati ya kamati hiyo na Menejimenti ya Wizara kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma, tarehe 3 Juni 2024.

 

Akiwasilisha taarifa ya miradi ya ujenzi iliyo chini ya Wizara, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.), kwa niaba ya Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameeleza kuwa, Wizara imewekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara lililopo mji wa Serikali Mtumba, Dodoma na jengo la mihadhara la Kituo cha Uhusiano cha Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kilichopo Kurasini, jijini Dar es Salaam yanakamilika kwa wakati.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya NUU na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) alieleza juu ya umuhimu wa Wizara kushirikiana na Kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yake.

 

Aidha, wajumbe wa Kamati wamepongeza jitihada zilizofanywa na Wizara katika utekelezaji wa miradi na wamesisitiza weledi katika usimamizi wa matumizi ya kifedha na mikataba ya miradi ya ujenzi.

 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amewashukuru wajumbe wa Kamati ya NUU kwa kuendelea kuwa chachu katika usimamizi wa miradi inayotekelezwa na Wizara. Pia, amewaalika Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu unaotekelezwa katika eneo la Lakilaki, Arusha.

========================================

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) akifungua kikao cha kamati yake na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 3 Juni, 2024 Bungeni, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akiwasilisha taarifa ya Wizara ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tarehe 3 Juni, 2024 Bungeni, jijini Dodoma.

Mhe. Byabato akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo (Kulia) pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Eng. John Kiswaga (kati).

Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakifuatilia kikao.

Sehemu ya Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikifuatilia kikao.

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikifuatilia kikao.

Kikao kikiendelea.


Friday, May 31, 2024

MAWAZIRI WA BIASHARA ,VIWANDA, FEDHA NA UWEKEZAJI WA EAC WAAZMIA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA

Picha ya pamoja kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Mawaziri wanaosimamia sekta ya Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kuboresha ya mazingira ya biashara katika Jumuiya, huku wakitilia mkazo katika kuondoa vikwazo visivyo vya kodi, kurahisisha uvushaji wa mizigo mipakani, na kuimarisha utendaji wa miundombinu ya kusaidia biashara ikiwemo Vituo vya kutoa Huduma Pamoja Mpakani (OSBP). 

Vilevile wamekubaliana mapendekezo ya viwango mbalimbali vya ushuru wa forodha vitakavyo tumika katika mwaka wa fedha 2024/25 ambavyo vitachochea ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama.

Azma hiyo imefikiwa leo tarehe 31 Mei 2024 kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Akizungumzia kuhusu azma hiyo Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya kuwataka Watendaji na Viongozi walipo chini yao kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuondoa vikwazo vya kibiashara katika Jumuiya.

Waziri Nchemba aliongeza kutaja maeneo yaliyofanyiwa maboresho katika mkutano huo kuwa ni pamoja makubaliano kuhusu viwango vya tozo za barabara kwa Nchi Wanachama kutoka Dola za Marekani 16 hadi 10. 

Eneo jingine ni makubaliano ya utekelezaji wa mkakati wa Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) hasa kwa upande wa Tanzania na Kenya, ambapo Tanzania ilishaanza utelezaji wake. 

Jamhuri ya Kenya imeahidi kuanza kupitisha bidhaa za Tanzania katika mfumo wa himaya moja ya forodha mara moja na kufikia mwenzi Julai 2024, na kuleta wafanyakazi wake wa mamlaka ya forodha kwa ajili ya kuwezesha ukaguzi kabla mzigo haujaanza kuondoka ili mzigo usisimame mpakani. Hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano, usumbufu na upotevu wa mapato kwa Serikali na wasafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzani na Kenya.

“Tanzania tumekuwa tukikabiliwa na tatizo la msongamano wa maroli katika mipaka yetu ikiwemo Namanga, Sirari, Holili na Hororo, hii imechangiwa na kuto kuwepo kwa maafisa wa KRA upande wa Tanzania ambao wangesaidia kufanyia kazi nyaraka za kupitisha mzigo mpakani kabla gari husika halijafika mpakani tofauti na ilivyo sasa, utelezaji wa ahadi hii itasaidia kutatua tatizo hili lililo tusumbua kwa muda mrefu” Alisema Nchemba. 

Katika hatua nyingine Waziri Nchemba kwenye mkutano huo amewa ongoza Mawaziri wenzake kuzindua mfumo mpya wa Kielektroniki wa masuala ya forodha unaolenga kuongeza ufanisi katika biashara kwa kuweka mazingira ya uwazi, uwajibikaji na hatimaye kuongeza mapato kwa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya.

Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na mkutano ngazi ya Wataalam uliofanyika tarehe 27 hadi 29 Mei 2024 na ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 30 Mei 2024. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akifuatilia mkutano

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umejumuisha Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye pia aliongoza ujumbe wa Tanzania, Mhe. Shariff Ali Shariff, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji- Zanzibar, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud S. Kigahe.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akichangia jambo kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato wakishirikishana jambo kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Mawaziri Sekta ya Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji wa Afrika Mashariki wakishuhudia uzinduzi wa mfumo mpya wa Kielektroniki wa masuala ya forodha unaolenga kuongeza ufanisi na mapato kwa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud S. Kigahe wakifuatilia Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Benjamin Mwesiga wakifuatilia Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mhe. Shariff Ali Shariff (kushoto) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.