Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekipongeza Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kwa kutoa mafunzo yenye lengo la kuwanoa vijana katika masuala ya uongozi hususan kwenye stadi za Uongozi na Majadiliano.
Mhe. Balozi Kombo ametoa pongezi hizo leo Agosti 22, 2025 alipokitembelea Kituo hicho ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa lengo la kujitambulisha, kufahamu majukumu yake pamoja na kuangalia maendeleo ya mradi wa jengo la vyumba vya mihadhara. Akizungumza na wanafunzi kutoka Taasisi za Umma na Sekta binafsi wanaoshiriki mafunzo ya muda mfupi kuhusu stadi za Uongozi na Majadiliano chuoni hapo, Mhe. Waziri Kombo amewataka kuzingatia mafunzo hayo ambayo yatawajenga katika masuala ya uongozi, uzalendo na majadiliano, fani ambazo ni muhimu katika ulimwengu wa sasa wa kutumia diplomasia na uhusiano na mataifa mbalimbali kunufaika kiuchumi. Amesema washiriki hao wana bahati kubwa kupatiwa mafunzo katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ambacho pia baadhi ya wakufunzi wake ni Mabalozi na Wanadiplomasia wabobevu kwenye masuala ya uhusiano wa kimataifa na Diplomasia kwa ujumla. “Kwenu ninyi washiriki wa mafunzo haya mna bahati kubwa ya kufundishwa na wanadiplomasia nguli akiwemo Balozi Modest Mero ambaye ni miongoni mwa wanadiplomasia waliowahi kuhudumu kwa nafasi ya kuiwakilisha nchi yetu katika Umoja wa Mataifa nchini Marekani. Hivyo, Balozi Mero kwa wasifu wake ni fursa kubwa kwenu washiriki kupokea elimu ya masuala ya stadi za uongozi na majadiliano”, amesema Mhe. Kombo. Wakati wa ziara hii Mhe.Kombo amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo hicho, Mhe. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dkt. Felix Wandwe ndc, baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Kituo hicho na Viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki. |