Wednesday, January 29, 2014

Waziri Mkuu wa Finland ahutubia Wadau wa Maendeleo

Waziri Mkuu wa Finland akitoa mada katika kikao maaulum kilichofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro. Kikao hicho kilijadili mbinu ambazo nchi za Afrika na Ulaya zikishirikiana kwa pamoja, zinaweza kuzitumia kukuza uchumi kwa faida ya wananchi wao. Katika mada yake Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuimarisha Jumuiya za Kikanda kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na utulivu wa kisiasa. Wazungumzaji wengine walisisitiza umuhimu wa Afrika na Ulaya kuwa na ushirikiano wenye uwiano sawa ambao utaleta maendeleo ya kiuchumi kwa pande zote mbili bila kudhulumiana. 





Wadau wakijadili fursa na changamoto za maendeleo katika nchi za Afrika na Ulaya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule wa pili kushoto akisikiliza kwa makini michango mbalimbali kuhusu kuboresha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi za Afrika na Ulaya.


Mjumbe akichangia mada.












Hafla ya Mapokezi Rasmi ya Waziri Mkuu wa Finland, Ikulu Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliyeketi kulia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Sadik Meck Sadik wakijadili jambo wakati wakiwa wanamsubiri Waziri Mkuu wa Findland, Mhe. Jyrki Katainen kuwasili Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Kikwete (kulia) akiongozana na Mgeni wake, Waziri Mkuu wa Findland kuelekea katika jukwaa maalum kwa ajili ya kupigiwa Nyimbo za Taifa na Mizinga 19 ya kumkaribisha rasmi Mhe. Waziri Mkuu nchini Tanzania. 

Rais Kikwete (kulia) na Mgeni wake, Waziri Mkuu wa Findland wakifurahia jambo huku wakielekea kwenye jukwaa maalum.

Rais Kikwete (kulia) pamoja na Mgeni wake, Waziri Mkuu wa Findland wakiwa wamesimama huku Nyimbo za Taifa za Mataifa yao zikiwa zinapigwa.


Mizinga 19 ikipigwa kwa ajili ya heshima ya Waziri Mkuu wa Findland.

Waziri Mkuu wa Findland anakagua gwaride.

Waziri Mkuu wa Findland akiwapungia viongozi na watu wengeine wakati alipokuwa anaingia Ikulu, Dar es Salaam.

Mazungumzo Rasmi


Rais Kikwete akitambulisha ujumbe wake kwa Waziri Mkuu wa Findland hayupo pichani kabla ya kuanza mazungumzo rasmi Ikulu, Dar es Salaam.

Ujumbe wa Rais Kikwete katika mazungumzo rasmi, kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb).

Wajumbe wengine.

Ujumbe wa Tanzania (kulia) pamoja na ule wa Finland katika mazungumzo rasmi Ikulu, Dar es Salaam.

Mhe. Membe kumwakilisha Mhe. Rais Kikwete Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa AU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bbernard K. Membe (Mb) akiwa katika moja ya vikao vya Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa. Mhe. Membe atamwakilisha Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kuanzia tarehe 30 hadi 31 Januari, 2014 mjini hapa.

==========================


WAZIRI MEMBE KUMWAKILISHA MHE. RAIS KIKWETE MKUTANO WA WAKUU WA NCHI WA AU ADDIS ABABA.

Na Mwandishi wetu, Addis Ababa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaotarajiwa kuanza kesho Alhamisi tarehe 30 Januari, 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa AU uliofanyika tarehe 27 na 28 Januari, 2014 ambao Mhe. Membe aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.

Kaulimbiu ya Mkutano wa mwaka huu ni “Kilimo na Usalama wa Chakula” unalenga kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha kilimo kinakuwa mkombozi wa watu Barani Afrika kwa kuwainua kiuchumi na kuondokana na wasiwasi wa njaa unaolikabili Bara hili mara kwa mara.

Mkutano wa Wakuu wa nchi pia utapokea Ripoti mbalimbali ikiwemo ile ya Kamati ya Kimataifa ya Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC) iliyokuwa chini ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali unatarajiwa kumalizika tarehe 31 Januari, 2013.

-Mwisho-




Waziri Mkuu wa Findland awasili Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb), mwenye tai nyekundu akiongozana na Waziri Mkuu wa Findland, Mhe. Jyrki Katainen ambaye amewasili nchini Tanzania usiku wa tarehe 29 Januari, 2014 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.


Waziri Mkuu wa Findland, Mhe. Jyrki Katainen wa kwanza kushoto akipeana mkono na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere alipowasili kwa ziara ya kikazi. Anayeangalia kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mohammed Mzale.


Mhe. Katainen akiendelea kusalimiana na viongozi waliojitokeza katika Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kumlaki. Katika picha hii, Mhe. Waziri Mkuu anasalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Dora Msechu.

Salamu zinaendelea, Bibi Victoria Mwakasege, Mkurugenzi Msaidizi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa naye akisalimiana na Waziri Mkuu wa Findland

Mhe. Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeketi kulia akibadilishana mawazo na mgeni wake Waziri Mkuu wa Findland alipowasili nchini usiku wa tarehe 29 Januari, 2014

Tuesday, January 28, 2014

TANZANIA YACHAGULIWA TENA MJUMBE BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA AU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU), mjini Addis Ababa akisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Baraza hilo. Wengine katika picha ni Mhe. Naimi Aziz, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Mhe. Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na Bw. Samwel Shelukindo, Afisa Mwandamizi kwenye Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa.
---------------------------------------------------------------------

Na Mwandishi wetu, Addis Ababa


Tanzania imechaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa Mjumbe wa Baraza la  Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC)  kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo tarehe 28 Januari, 2014 wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika, Tanzania na Ethiopia zimechaguliwa kuiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki katika Baraza hilo muhimu linaloshughulikia masuala ya amani na usalama Barani Afrika.

Tanzania ilichaguliwa kwa mara ya kwanza katika Baraza hilo mwaka 2012. Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliongoza ujumbe wa Tanzania katika uchaguzi huo.

Matokeo ya uchaguzi huo yanaonyesha kuwa Tanzania na Ethiopia zilipata kura 40 kati ya kura 50 zilizopigwa ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya kura zinazotakiwa huku Eritrea ikipata kura 13.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lina Wajumbe 15 wanaochaguliwa na Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika. Wajumbe hao wanaowakilisha Kanda tano ambazo ni Afrika ya Kati, Afrika Mashariki, Afrika Kaskazini, Afrika ya Kusini na Afrika Magharibi.

Malengo ya Baraza hili ni pamoja na kulinda amani na usalama Barani Afrika; kuzuia migogoro; kulinda amani na kujenga amani katika maeneo yenye migogoro; kusimamia demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu.

-Mwisho-



Tanzania na Algeria kudumisha ushirikiano

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ramtane Lamamra (hayupo pichani) walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini Addis Ababa. Mazungumzo hayo yalihusu ushirikiano kati ya Algeria na Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta ya gesi na umeme. Wengine katika picha ni Balozi Vincent Kibwana (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Togolani Mavura, Msaidizi wa Waziri na Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje.
Mhe. Lamamra naye akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yao.
Mhe. Membe akiagana na Mhe. Lamamra mara baada ya mazungumzo yao.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI






 Waziri Mkuu wa Finland kuzuru Tanzania

Waziri Mkuu wa Findland, Mhe. Jyrki Katainen atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania tarehe 29 na 30 Januari, 2014.Mhe.Katainen anategemewa kuwasili usiku wa tarehe 28 januari akitokea Addis Ababa, Ethiopia, na atafanyiwa mapokezi rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, kesho yake asubuhi.

Mhe. Katainen atafuatana na Waziri wake wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pekka Haavisto, na wafanyabiashara 25 wa Finland.

Baada ya mapokezi rasmi, Mhe. Waziri Mkuu wa Finland atafanya mazungumzo na Mwenyeji wake, Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam, na baadaye atashiriki majadiliano kuhusu ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi  kwenye hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro.

Wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Finland zitatiliana saini Mkataba wa Msaada wa Bajeti (General Budget Support) na Makubaliano ya Ushirikiano (Memorandum of Understanding) kwenye Nyanja za madini na misitu.

Mhe.Rais Kikwete atamwandalia mgeni wake chakula rasmi cha jioni, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 29 Januari, Mhe. Katainen anatarajiwa kuzuru Unguja  na kukutana na Rais  wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein. Kadhalika, atafanya mazungumzo na Wafanybiashara, wachumi na maafisa wa mashirika ya kimataifa jijini Dar es Salaam, pamoja na kutembelea bandari, kabla ya kuondoka nchini Januari 30 usiku.

 

IMETOLEWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

 

DAR ES SALAAM, JANUARI 27, 2014

Monday, January 27, 2014

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa AU wafunguliwa rasmi Addis Ababa

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma akitoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaofanyika Mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 27 na 28 Januari, 2014. Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi  na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mjini hapa tarehe 30 na 31 Januari, 2014.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa AU, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa inatolewa na Dkt. Dlamini-Zuma (hayupo pichani). Wengine katika picha ni Mhe. Naimi Aziz (kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Balozi Tuvako Manongi (kulia), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani akiwa na Wajumbe wengine wakifuatilia kwa makini hotuba ya Dkt. Dlamini-Zuma (hayupo pichani)
Makamishna wa AU na Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Dkt. Dlaini-Zuma  (hayupo pichani).
Mawaziri kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa baraza la mawaziri.
Kabla ya ufunguzi Dkt. Dlamini-Zuma aliwaongoza Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri kusimama kwa heshima na kumkumbuka aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Mzee Nelson Mandela aliyefariki dunia mwezi Desemba, 2013.
Picha ya Pamoja mara baada ya ufunguzi.
Mhe. Membe akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Mhe. Simbarashe Mumbengegwi (katikati) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Maite Nkoana-Mashabane
Maafisa Waandamizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia wakibadilishana mawazo nje ya Ukumbi mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri.
Bw. Bujiku Sakila, Afisa Mambo ya Nje akimweleza jambo Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri.



Na Rosemary Malale, Addis Ababa

Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) imetoa rai kwa nchi za Afrika kuongeza uzalishaji na uwekezaji katika kilimo kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa Pato la Taifa kwa nchi Barani Afrika.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma wakati akifungua Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza leo tarehe 27 Januari, 2014 Mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Dkt. Dlamini-Zuma alisema kuwa,  kwa Afrika kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 7 na zaidi ni vema kilimo kiwe kipaumbele kwa nchi wanachama, kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kwa nchi zao. Alisema kuwa kwa mwaka huu wa 2014 ni muhimu kuongeza uwekezaji katika kilimo, uzalishaji, kuboresha miundombinu na ujuzi ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika tafiti za kilimo.

Alisisitiza kuwa Kamisheni yake kwa mwaka huu imejipanga kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha kilimo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake ambao ndio kundi kubwa linaloshughulika na kilimo na chakula kwa kuwapatia  mafunzo, mitaji na kuwasaidia kuanzisha vikundi vya ushirika na masoko kwa bidhaa za kilimo. Pia, alieleza kuwa imefika wakati sasa kwa Afrika kuwa na kauli katika kupanga bei ya mazao na bidhaa zitokanazo na kilimo.

Aidha aliongeza kuwa, ili kufikia malengo hayo, Kamisheni ya Umoja wa Afrika itashirikiana na Taasisi nyingine za Kimataifa kama UNECA, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Nchi Wanachama, Vyama vya Kiraia na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi.
Dkt. Dlamini-Zuma alieleza kuwa Mkutano wa mwaka huu wenye kaulimbiu isemayo “Mwaka 2014 ni mwaka wa Kilimo na Usalama wa Chakula; Kuadhimisha miaka 10 ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP)” unalenga kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha kilimo kinakuwa ni mkombozi wa Watu Barani Afrika kiuchumi na kwa usalama wa chakula.

Katika hatua nyingine, Dkt. Dlamini-Zuma ametoa wito kwa Waafrika wote kutoa michango na mawazo yao kuhusu Muundo wa Agenda 2063 ambayo inalenga katika kujenga Afrika Tunayoitaka katika kipindi cha miaka 50 ijayo kuanzia mwaka 2014.

Aidha, aligusia migogoro inayoendelea kusumbua baadhi ya nchi za Afrika kama vile Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo alisema kuwa Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi na Jumuiya ya Kimataifa zitaendelea kushirikiana ili kuzisaidia nchi hizi kupata suluhisho la kudumu katika migogoro yao.

“Mwezi Mei mwaka uliopita wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Afrika tuliahidi  kwa watu wetu kuwa hatutavirithisha vizazi vijavyo vita na migogoro bali tuliapa kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha migogogro Barani humu inamalizwa kabisa hadi kufikia mwaka 2020” alisema Dkt. Dlamini Zuma. Vile vile, Dkt. Dlamini-Zuma alizipongeza nchi za Mali, Madagascar na Somalia kwa hatua waliyofikia katika kushughulikia migogoro yao.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri  ambao utamalizika tarehe 28 Januari, 2014 ni matayarisho ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ambao utafanyika mjini hapa tarehe 30 na 31 Januari, 2014. Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri unaongozwa na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

-mwisho-