Wednesday, April 15, 2015

Tanzania kufungua Ubalozi nchini Kuwait

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Mhe. Skeikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah,  Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait. Waziri Membe alifanya ziara ya siku moja nchini humo tarehe 14 Aprili, 2015 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Waziri Membe akimtambulisha kwa Mhe. Skeikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah,  Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Simba Yahya.
Waziri Membe akimtambulisha kwa Mhe. Skeikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah,  Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), Bw. Peter Noni. 
Mazungumzo ya ushirikiano yakiendelea
=======================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania kufungua Ubalozi nchini Kuwait

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufungua Ubalozi nchini Kuwait  kabla  ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha wa 2014/2015.

Kauli hiyo imetolewa   na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) alipokutana na  Mtukufu Sheikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah,  Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait nchini Kuwait siku ya Jumanne tarehe 14 Aprili, 2015.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wawili walisifu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili ambao ni wa kidugu na unalenga kuwanufaisha wananchi wa nchi hizi.

“Kwa kufungua ofisi za Ubalozi, Kuwait ushirikiano huu wa kidugu utaongezeka kwenye nyanja zote muhimu na utazaa matunda yatakayo wanufaisha watu wetu, kwa nchi hizi mbili” alisisitiza Waziri Membe katika mazungumzo yake na kiongozi huyo.

Kwa upande wa Kuwait, Serikali yao ilifungua ubalozi nchini Tanzania Februari 2015 na Mhe. Jassem Ibrahim Al Najem kuwa Balozi wake wa kwanza nchini Tanzania, mwenye makazi yake Jijini Dar es salaam.

Aidha, kwa sasa Tanzania inawakilishwa nchini Kuwait kupitia Ubalozi wake uliopo Riyadh, Saudi Arabia.

Katika mkutano huo, Mtukufu Sabah Al-Khalid Al Sabah alisifu jitihada za Tanzania kwenye kulinda na kuleta amani Barani Afrika hasusan kwenye maeneo yenye migogoro. Alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania sio tu kwenye maeneo muhimu ya maendeleo lakini pia hata kwenye ulinzi wa amani kwani ndio changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa.

Kuhusu misaada  Barani Afrika, viongozi hao walijadili suala la uratibu wa misaada mbalimbali ya Serikali ya Kuwait Barani humo ambapo waliangalia uwezekano wa kuanzisha kituo maalum nchini Tanzania kwa ajili ya kusimamia shughuli za uratibu wa misaada hiyo.

Kwa sasa Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wake wa Maendeleo – Kuwait Fund- imetoa Dola za Kimarekani Bilioni moja kwenye Umoja wa Afrika kwa ajili ya usalama wa chakula Barani Afrika.

Awali Waziri Membe alikutana na Mhe. Abdulwahab A. Al-Bader, Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait na kumshukuru kwa misaada mbalimbali ya kimaendeleo wanayoendelea kuitoa nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Aidha Waziri Membe alielezea kuwa maandalizi ya miradi mitano ya umwagiliaji nchini Tanzania ambayo inayofadhiliwa na mfuko huo yamekamilika, na kwamba sasa iko tayari kuanza. Aidha Waziri Membe na Mhe. Al-Bader walizungumzia uwezekano wa mfuko huo kuikopesha Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ili iweze kuendesha shughuli zake kikamilifu.

Waziri Membe yuko nchini Kuwait kwa ziara ya siku moja na anatarajiwa kuondoka kesho kuelekea nchini Oman. Ujumbe wa Mhe. Membe  nchini Kuwait unamjumuisha Bw. Peter Noni, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Uwekezaji Tanzania, Balozi Simba Yahya, Mkuregenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam

15 Aprili 2015.






H.E Mkapa delivers Lecture to Foreign Affairs Staff on Economic Partnership Agreement


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania awasilisha mada kwa Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje


Waziri Membe awasili Nchini Kuwait

Mhe. Bernard Membe akiwasili hotelini nchini Kuwait kwa ziara ya siku moja ambapo atakutana na kufanya mzaungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait na Mkurugenzi Mkuu wa Kuwait Fund.
Mhe. Membe na ujumbe wake wakimsikiliza Mhe. Najib na kuangalia picha za viongozi mbalimbali wa Kuwait. 
Waziri Membe kwenye picha ya pamoja na baadhi na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao kwenye nchi ya Kuwait na Tanzania. (Wa kwanza kushoto) ni Mhe. Prof. Abdillah Omari, Balozi wa Tanzania nchini Kuwait mwenye makazi yake Saudia Arabia na (kulia) ni Mhe. Nassem Ibrahim Al Najib, Balozi wa Kuwait nchini Tanzania.

Kamati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar yatembelea Wizara ya Mambo ya Nje

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Rajab Gamah akifungua kikao  kati ya Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar inayosimamia Ofisi za Viongozi za Kitaifa  kushoto ni Mwenyekiti wa Jimbo la Kwamtipura Mhe. Hamza Hassan Juma kulia ni Mwenyekiti wa Jimbo la Wawi, Mhe. Saleh Nassor Juma.  
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi wa Kitaifa wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Balozi Gamaha (hayupo pichani)
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara za Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Rosemary Jairo (kushoto) akiwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Bictoria Mwakasege (katikati)  na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Bw. Elibariki Maleko  wakati wa kikao kati ya  Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Kikao kikiendelea.

Picha na Reginald Philip 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb),akimkaribisha Wizarani Waziri wa Mambo ya Nje wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe El-Anrif Said Hassane kwa mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro.
Balozi wa Comoro hapa Nchini Mhe.Dr.Ahamada El Badaoui Mohamed(kushoto)akisalimiana na Naibu Waziri Dkt.Mahadhi huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro Mhe.El-Anrif Said Hassane(katikati) akishuhudia.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe.Dkt.Mahadhi Juma Maalim (Mb),akifurahia jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro wakati wakiendelea na mazungumzo yao.
Katibu wa Naibu Waziri, Bw.Adam Misara (kulia) pamoja na Afisa Mambo ya Nje, Bw.Mudrick Soragha wakinukuu mazungumzo kati ya mhe. Mahadhi na Mhe. Hassane (hawapo pichani).
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe.Dkt.Mahadhi Juma Maalim (Mb),akifafanua jambo katika kikao hicho.

Picha na Reuben Mchome

Tuesday, April 14, 2015

Mkutano wa Waziri Membe na viongozi wa Kuwait Fund nchini Kuwait katika picha

Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa akisalimiana na Mhe.  Abdulwahab A. Al-Bader, Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait mara baada kuwasili ofisini kwake kwa mkutano leo tarehe 14 Aprili 2015.

Waziri Membe akiwatambulisha wajumbe alioongozana nao kwenye kikao hicho kilichofanyika Kuwait City leo Jumanne tarehe 14 Aprili 2015.


Kikao kikiendelea

Mhe.  Abdulwahab A. Al-Bader, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait akipokea maelezo kuhusu Benki ya Maendeleo ya Tanzania kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw. Peter Noni ambaye aliongozana na Mhe. Membe kwenye mkutano huo.




Mhe. Bernard Membe akiwa kwenye picha na Abdulwahab A. Al-Bader, Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (kati) pamoja na Balozi Yahya Simba, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Wizara ya Mambo ya Nje.


Picha ya pamoja
Ujumbe wa Waziri Membe ukiondoka baada ya kumaliza mkutano na viongozi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait - Kuwait Fund.

Monday, April 13, 2015

Mapokezi ya Waziri Membe nchini Kuwait katika Picha

Mhe. Bernard Membe akiwasili hotelini nchini Kuwait kwa ziara ya siku moja ambapo atakutana na kufanya mzaungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait na Mkurugenzi Mkuu wa Kuwait Fund.  

Aliyeongozana na Waziri Membe ni Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Nassem Ibrahim Al Najib ambaye alimpokea uwanja wa ndege.

Waziri Membe kwenye picha ya pamoja na baadhi na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao kwenye nchi ya Kuwait na Tanzania. (Wa kwanza kushoto) ni Mhe. Prof. Abdillah Omari, Balozi wa Tanzania nchini Kuwait mwenye makazi yake Saudia Arabia na (kulia) ni Mhe. Nassem Ibrahim Al Najib, Balozi wa Kuwait nchini Tanzania.

Mhe. Membe ujumbe wake wakimsikiliza Mhe. Najib na kuangalia picha za viongozi mbalimbali wa Kuwait.

Msafara wa Mhe. Membe ukitokea airport kuelekea hotelini ambapo atakaa kwa siku leo tarehe 13 usiku hadi 14 usiku, Aprili 2015 (usiku) moja kabla ya kuelekea Oman kuendelea na ziara yake.

Waziri Membe yupo Nchini Quatar Kikazi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Bernard Membe (Mb.) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Quatar Mh. Dkt. Khalid Mohamed Al Attiyah, walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuendeleza mahusiano kati ya Tanzania na Quatar pia kutangaza Fursa za uwekezaji nchini Tanzania. Waziri Membe yupo nchini Quatar kwa madhumuni ya kushiriki mkutano kuhusu Kuzuia Uhalifu na Haki za Waalifu. 
Mazungumzo yakiendelea
Waziri Membe akiwa Katika picha ya pamoja na Bw. Noel Kaganda Mshauri wa maswala ya kisheria wa Rais wa kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mhe. Sam Kahamba Kutesa.

Taarifa kwa Vyombo vya Habari.

Taarifa kwa Vyombo vya Habari.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) ameanza ziara ya kikazi katika nchi za Qatar, Kuwait na Oman kuanzia tarehe 11 – 17 Aprili 2015.

Katika nchi ya Qatar, Mhe. Waziri atashiriki Mkutano wa 13 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuia Uhalifu na Haki za Wahalifu (Crimes Prevention and Criminal Justice). Aidha, Mhe. Waziri atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mhe. Dkt. Khalid Mohammed Al-Attiyah. Mazungumzo yao yatahusu masuala ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar; fursa za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini pamoja na fursa za ajira kwa Watanzania  nchini Qatar.

Atakapokuwa nchini Kuwait, Mhe. Membe ataonana na Mwenyeji wake, Mhe. Sabah al Khalid al Sabah, Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Waziri Mkuu wa Kuwait. Viongozi hao wawili wataongelea suala la Tanzania kufungua Ofisi ya Ubalozi nchini Kuwait. 

Aidha, Waziri Membe ataonana na viongozi wa Mfuko wa Kuwait kujadili suala la kufadhili miradi ya maendeleo nchini Tanzania.

Katika nchi ya Oman, Waziri Membe pia ataonana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. Yusuf bin Allawi bin Abdullah. 

Viongozi hao pamoja na mambo mengine, watajadili ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji.


Waziri Membe atarejea nchini tarehe 17 Aprili 2015.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 

Tarehe 13 April 2015

Saturday, April 11, 2015

Balozi Kairuki akutana na Balozi wa India kuzungumzia Mahusiano kati ya Tanzania na India

 Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki (kulia) akiwa na Balozi wa India hapa Nchini Mhe. Debnath Shaw wakiwa katika mazungumzo yaliyohusu kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na India.
Balozi wa India hapa Nchini Bw.Debnath Shaw,akisisitiza jambo kwa Balozi Mbelwa Kairuki katika mkutano huo,huku afisa mwandamizi Wizara ya Mambo ya Nje Bw.Luangisa EFL(kulia) akisikiliza kwa makini na kushoto ni katibu Muktasi wa balozi wa India hapa nchini Bi.Deepay naye akifuatilia mazungumzo hayo.
Balozi Mbelwa Kairuki akizungumza na afisa mwandamizi wa wizara ya Nje Bw.Luangisa huku Balozi wa India na Katibu wake wakifuatilia kwa makini.
………………………………
Picha na Reuben Mchome

Friday, April 10, 2015

Rais amteua Mhe. Mgaza kuwa Balozi wa Saudi Arabia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mhe. Hemed Iddi Mgaza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue imesema uteuzi huo ulianza Machi 27.

Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Mgaza alikuwa Ofisa Mambo ya Nje Mkuu, Daraja la Pili na Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mhe. Mgaza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Abdillah Omar ambaye mkataba wake wa utumishi umekwisha.