Monday, April 13, 2015

Taarifa kwa Vyombo vya Habari.

Taarifa kwa Vyombo vya Habari.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) ameanza ziara ya kikazi katika nchi za Qatar, Kuwait na Oman kuanzia tarehe 11 – 17 Aprili 2015.

Katika nchi ya Qatar, Mhe. Waziri atashiriki Mkutano wa 13 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuia Uhalifu na Haki za Wahalifu (Crimes Prevention and Criminal Justice). Aidha, Mhe. Waziri atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mhe. Dkt. Khalid Mohammed Al-Attiyah. Mazungumzo yao yatahusu masuala ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar; fursa za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini pamoja na fursa za ajira kwa Watanzania  nchini Qatar.

Atakapokuwa nchini Kuwait, Mhe. Membe ataonana na Mwenyeji wake, Mhe. Sabah al Khalid al Sabah, Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Waziri Mkuu wa Kuwait. Viongozi hao wawili wataongelea suala la Tanzania kufungua Ofisi ya Ubalozi nchini Kuwait. 

Aidha, Waziri Membe ataonana na viongozi wa Mfuko wa Kuwait kujadili suala la kufadhili miradi ya maendeleo nchini Tanzania.

Katika nchi ya Oman, Waziri Membe pia ataonana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. Yusuf bin Allawi bin Abdullah. 

Viongozi hao pamoja na mambo mengine, watajadili ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji.


Waziri Membe atarejea nchini tarehe 17 Aprili 2015.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 

Tarehe 13 April 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.