Sunday, April 5, 2015

Waziri Membe atoa wito kwa Watanzania kuwasaidia watu wasiojiweza kwenye jamii

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb)  akimtazama kwa furaha mmoja wa watoto yatima wanaolelewa kwenye kituo cha Nyumba ya Furaha na Amani kilichopo Kigogo Mburahati, Jijini Dar es Salaam. Waziri Membe alikitembelea kituo hicho wakati wa Siku Kuu ya Pasaka. 
Mhe. Membe pamoja na Mkewe Mama Dorcas Membe wakipata maelezo juu ya watoto waishio katika kituo hich kutoka kwa Sista Mary Bakhita


Mhe Membe akizungumaza wakati wa ziara yake kituoni hapo. Kulia ni Mama Dorcas Membe. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Paul Makonda akifuatiwa na Padri Timoth Maganga wa Kanisa Katoliki la Kigogo Mburahati
Watoto yatima wakiwa na walezi wao 
Sehemu ya Wazee  wanaolelewa na Kituo hicho wakimsikiliza Mhe. Waziri (hayupo pichani) alipowatembelea
Sehemu nyingine ya Wazee na Watoto
Waziri Membe akikata keki pamoja na Sista Bakitha kama ishara ya kusherehekea Siku Kuu ya Pasaka pamoja na  Watoto Yatima na Wazee wanaolelewa kwenye kituo cha Nyumba ya Furaha na Amani. Pembeni ni Mama Dorcas Membe nae akifurahia
Mhe. Wazriri akijumuika kwa chakula cha mchana pamoja  na watoto Kituoni hapo.
Watoto hao nao wakifurahia chakula cha mchana na Mgeni wa aliyewatembelea na kusheherekea nao Sikukuu ya Pasaka
Waziri Membe akitoa  msaada kwenye kituo hicho
Waziri Membe pamoja na Mkewe Mama Dorcas Membe katika picha ya Pamoja na Masista wanaolea watoto yatima katika kituo hicho
Waziri Membe akisaini kitambu cha wageni alipowasili katika kituo hicho.
Baadhi ya Watoto wanaolelewa katika kituoni hapo wakitoa burudani mbele Waziri Membe (Hayupo pichani).
Waziri Membe akizungumza na Waandishi wa Habari.
 Picha na Reginald Philip>


====================================================================
Waziri Membe atoa wito kwa Watanzania kuwasaidia watu wasiojiweza kwenye jamii

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuwasaidia watu wasiojiweza waliopo kwenye jamii wakiwemo watoto yatima, walemavu, wazee na wajane.

Waziri Membe ametoa wito huo hivi karibuni alipotembelea Kituo cha Kulelea Watoto Yatima na Wazee cha Nyumba ya Furaha na Amani kilichopo Mburahati Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Membe alisema kuwa katika jamii za watu kumekuwa na makundi ambayo yanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa watu wengine ambao kwa namna moja au nyingine wamejaaliwa kipato kidogo na afya. Alisema kuwa ni wajibu wa watu wa aina hiyo kuwasaidia wale wanaohitaji kama vile watoto yatima, walemavu, wazee na wajane.

Waziri Membe ambaye alikuwa amefuatana na Mke wake, Mama Dorcas Membe aliguswa sana na historia ya baadhi ya watoto yatima aliowatembelea kituoni wakiwemo wale waliotupwa jalalani na kuokotwa wakiwa kwenye hali mbaya.
 “Lipo kundi linalopata mateso na matatizo katika jamii zetu tunazoishi. Ni vizuri Watanzania tukajenga utamaduni wa  kutembelea sehemu kama hizi ili kujionea wenyewe hali halisi. Kwa kweli ni hali ya kusikitisha kuona baadhi ya watoto walitupwa na kuokotwa jalalani na wengine tayari wakiwa wamepata majeraha ya kung’atwa na mbwa. Hivyo ni wajibu wetu sote kuwasaidia kwa chochote kidogo tunachojaaliwa kupata”, alisema Waziri Membe.

Aidha, Mhe. Membe aliwapongeza na kuwasifu Masista wa Shirika la Mama Theresa  ambao ndio wasimamizi wa kituo hicho kwa kuwalea watoto, vijana na wazee wenye matatizo mbalimbali na kuwaomba waendelee kujipa moyo katika kazi hiyo kwani ni njia moja wapo ya kumtumikia Mungu.

Awali akimkaribisha Waziri Membe kituoni hapo, Sista Mkuu wa Kituo hicho, Sista Mary Bakhita, alisema kuwa wamefurahia sana ziara hiyo ya Mhe. Membe hususan katika Siku Kuu ya Pasaka kwani ni faraja kubwa kwao kwa Watoto na Wazee wanaolelewa kituoni hapo.

“Tumefarijika sana kula pasaka pamoja nawe Mhe. Waziri. Watoto na Wazee hawa wanajisikia vizuri pale wanapotembelewa na tunaomba uendelee na moyo huo huo”, alisema Sista Bakhita.

Wakati wa ziara hiyo Mhe. Membe na familia yake walitoa zawadi mbalimbali kwa kituo hicho ikiwemo vyakula, sabuni na fedha kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali kituoni hapo.



-Mwisho-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.