Monday, April 20, 2015

Waziri Membe: Hakuna Mtanzania katika mauaji ya Wageni Afrika Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Benard K. Membe (Mb.) akizungumza na Waandishi wa Habari nchini kuhusiana machafuko yanayoendelea nchini Afrika ya Kusini.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Balozi Irene Kasyanju (wa kwanza kulia) akiwa na  Mkurugenzi Idara ya Amerika na Ulaya Balozi Joseph Sokoine (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Uswisi, Mhe. Modest Mero wakimsikiliza Waziri Membe (hayupo pichani) alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari.   
Waandishi wa Habari wakimsikiliza na kunukuu taarifa kutoka kwa Waziri Membe ambaye hayupo pichani
Waziri Membe akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nao wakimsikiliza Waziri Membe (Hayupo pichani) 
Mwandishi wa Habari mkongwe  Bw. Jackton Manyerere akiuliza swali kwa Mhe. Membe
Mwandishi wa Habari kutoka Gazeti la Mawio Bi. Pendo Omary naye akiuliza swali kwa Waziri Membe.
Waziri Membe akijibu Maswali yaliyo ulizwa na Waandishi wa Habari 
Mazungumzo yakiendelea

Picha na Reginald Philip

==============================

TAARIFA KWA  VYOMBO VYA HABAR

Waziri Membe: Hakuna Mtanzania katika mauaji ya Wageni Afrika Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, amesema leo kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouawa katika mashambulizi dhidi ya wageni huko Durban na Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.

Mhe. Membe amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Watanzania watatu wameuwawa katika mashambulizii hayo siyo za kweli.


"Nimehakikishiwa na Waziri wa Usalama wa Afrika kusini, David Mahlobo, asubuhi hii kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouwawa, ambao ni raia wa Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland," ametaarifu Mhe. Waziri.

Amesema serikali ina taarifa kuwa kuna Watanzania watatu waliofariki dunia nchini Afrika Kusini, lakini hawakuuwawa katika mashambulizi ya wenyeji dhidi ya wageni.

"Watanzania hao ni Rashidi Jumanne, ambaye imetaarifiwa alipigwa risasi katika tukio la ujambazi, kilometa 90 nje ya mji wa Durban; mfungwa Athumani China Mapepe, aliyeripotiwa kuchomwa kisu gerezani wakati wa vurugu za wafungwa, na Ali Heshima Mohamed, ambaye alifariki hospitalini kutokana na ugonjwa wa TB," alieleza Mhe. Membe.

Mwili wa marehemu Mohamed ulirejeshwa nchini jana kwa mazishi. Mhe. Waziri alitaarifu kuwa kuna Watanzania 23 katika kambi iliyotayarishwa na serikali ya Afrika Kusini huko Durban kuhudumia wageni wanaokimbia mashambulizi hayo ya wenyeji, na kuwa utaratibu unafanywa kuwarejesha nyumbani raia 21 walioomba. "Wawili wamesema hawako tayari kurudi."

Mhe. Membe amesema taarifa ya Serikali ya Afrika Kusini inaonyesha kuwa hali ya utulivu imerejea Durban na Johannesburg katika saa 48 zilizopita kutokana na juhudi za Rais Jacob Zuma na kamati maalum ya mawaziri aliyoiteua kushughulikia mashambulizi hayo.

Mapema jana, Mhe. Membe alimwita Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Thamsanqa Dennis Mseleku,       na kuelezea kukerwa kwa Serikali na mauaji ya wageni na akataka hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha usalama wa Watanzania nchini Afrika Kusini.

Alisema Tanzania inaunga mkono taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambayo imelaani vikali mashambulizi ya Waafrika kutoka nje ya Afrika Kusini. Hata hivyo, Rais Mugabe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja mwa Afrika (AU), amesifia hatua zinazochukuliwa na serikali ya Afrika Kusini kukomesha mashambulizi hayo na kurejesha utulivu.

Mhe. Membe aliwataka Watanzania waishio Afrika Kusini na kwingineko nje ya nchi, kujitambulisha kwenye Balozi zetu ili iwe rahisi kufuatilia usalama wao na kuwasaidia yatokeapo majanga.

"Hatuna takwimu sahihi za idadi ya Watanzania waishio Afrika kusini kwa sababu wengi wao wamekwenda huko kwa njia za panya," alisema. Inakadiriwa kuna Watanzania 10,000 waishio Johannesburg na Durban. 

Akijibu swali, Mhe. Membe alisema Tanzania inapaswa kutumia utajiri mkubwa wa gesi asilia ilionao kuendeleza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyotengeneza ajira za kuvutia kwa vijana ili wasikimbilie nchi za nje na kuhatarisha maisha yao.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
20 Aprili, 2015.




Waziri wa Mambo ya nje akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) kwaajili ya kuzungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam
Waziri Membe akiingia katika ukumbi wa Mkutano kwaajili ya kuzungumza na waandishi we habari (hawapo pichani).
Waziri akizungumza na waandishi wa Habari  
Waziri Membe (Wa kwanza kulia) akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Radhia Msuya (Wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje Bi. Mindi Kasiga 
Mazungumzo yakiendelea
Waziri Membe akiongozana na Viongozi wa Wizara na baadhi ya Waandishi wa habari kuelekea nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.