Wednesday, March 20, 2019

Balozi Mgaza aahidi kuandaa mafunzo zaidi kwa wataalam wa afya nchini

Daktari Bingwa wa Watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Evelyne Assenga akikabidhiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia, Hemedi Iddi Mgaza baada ya kumalizika kwa mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wanaolazwa ICU. Wengine katika picha ni wataalam wa afya kutoka Saudia Arabia. Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo leo, balozi huyo amesema wataendelea kuandaa mafunzo ya huduma za afya kwa wataalam mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo. Kauli hiyo imetolewa leo na balozi huyo wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kuhusu upumuaji kwa wataalam kutoka hospitali mbalimbali nchini ikiwamo Bugando, Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Benjamini Mkapa na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema kwamba Muhimbili itaendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam wa afya kutoka Saudia Arabia ili kuhakikisha wataalam wabadilisha uzoefu na wenzao kutoka Saudia Arabia. Mafunzo hayo yameandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Al balsam Cure and Care International Charity Organization.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Abdulhakiem Kattan wa Saudia Arabia akizungumza kabla ya shughuli ya utoaji vyeti kwa washiriki wa mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wa ICU.

Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo leo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Dkt. Martha Mkony akipokea cheti baada ya kumaliza mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wa ICU kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia, Hemedi Iddi Mgaza.
Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dkt. Amos Zakharia akifurahia baada ya kuwa miongoni mwa washiriki waliokabidhiwa cheti.
Baadhi ya wataalam walioshiriki mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wanaolazwa ICU.
Mtaalam wa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), Peter Bahati akikabidhiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia, Hemedi Iddi Mgaza.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Dkt. Jenifa Metodi akipongezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru baada ya kumaliza mafunzo hayo leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa afya kutoka Saudia Arabia na wenzao kutoka hospitali mbalimbali nchini.








Tanzania yashiriki mazoezi ya kijeshi ya pamoja nchini India

Kikosi cha wanajeshi kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania kinachoshiriki Mazoezi ya Kijeshi ya Pamoja nchini India yanayojulikana kama "Africa-India Field Training Exercise- AFINDEX-2019" kikiwa katika picha. Mazoezi hayo ambayo yanafanyika katika mji wa Pune nchini India yameanza tarehe 18 Machi 2019. Lengo kuu la mazoezi hayo pamoja na mambo mengine, yamelenga kujenga uwezo wa majeshi ya nchi zinazoshiriki kulinda amani katika vikosi vya Umoja wa Mataifa duniani ambapo India na Afrika inachangia wanajeshi wengi katika vikosi hivyo.  Mbali na Tanzania, nchi nyingine za Mataifa ya Afrika zinazoshiriki mazoezi hayo ya kijeshi ya pamoja na India ni Afrika ya Kusini, Benin, Botswana, Ghana, Kenya, Mauritius, Misri, Msumbiji, Namibia, Niger, Nigeria, Senegal, Sudani, Uganda, Zambia na Zimbabwe. 

Makamanda wa nchi zinazoshiriki mazoezi ya pamoja kati
 ya nchi za Afrika na India wakiwa katika gwaride la ufunguzi wa mazoezi hayo.
Picha ya pamoja


Tuesday, March 19, 2019

Tanzania yapeleka msaada wa chakula na madawa kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kutokana na kukumbwa na mafuriko


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Mhe. Ummy Mwalimu wakiwa na Balozi wa Malawi, Mhe. Glad Chembe Munthali (kushoto), Balozi wa Msumbiji, Mhe. Monica D.C. Mussa (wa pili kushoto) na Balozi Mdogo wa Zimambwe nchini, Mhe. Martin Tavenyika (wa tatu kushoto) wakati wa zoezi la kuwakabidhi  mabalozi hao  misaada ya dawa na chakula ambavyo Serikali ya Tanzania imetoa kwa nchi zao ambazo zimekumbwa na maafa yaliyosababishwa na mafuriko kufuatia tufani kali iliyolikumba eneo hilo la kusini mwa Afrika. Tukio hilo limefanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 19 Machi 2019

Mhe. Prof. Kabudi akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhe. Waziri Ummy kuhusu aina ya dawa zilizotolewa msaada kwenye nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kufuatia maafa yaliyosababishwa na mafuriko yaliyozikumba nchi hizo
Add caption
Sehemu ya magari yaliyobeba shehena ya msaada wa dawa na chakula kwa ajili ya waathirika wa mafuriko kwenye nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kama inavyoonekana kabla ya kuanza kupakiwa kwenye ndege
Askari wa Jeshi la Ulinzi wakishusha kwenye magari na kupakia kwenye ndege misaada ya madawa na chakula ambavyo Serikali ya Tanzania imetoa msaada kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe  ambazo zimekumbwa na maafa ya mafuriko kufuatia tufani kali iliyolikumba eneo hilo la kusini mwa Afrika
Askari hao wakiwajibika
Mhe. Prof. Kabudi akiwa ameongozana na Mhe. Waziri Ummy , Mabalozi na Viongozi mbalimbali mara baada ya kukamilisha zoezi la kuwakabidhi Mabalozi  misaada ya dawa na chakula vilivyotolewa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya nchi zao zilizopatwa na maafa yaliyosababishwa na mafuriko kufuatia tufani kali iliyozikumba baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe.
Picha ya pamoja


Mhe. Prof. Kabudi akiagana na Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica mara baada ya kukabidhi misaada kwa nchi zao

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mnyepe naye akiagana na Mhe. Balozi Monica

Brigedia Jenerali Francis Shirima  wa kikosi cha anga cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa jukumu la  kuipeleka misaada ya dawa na chakula katika nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe  ambazo zimekumbwa na maafa yaliyosababishwa na mafuriko kufuatia tufani kali iliyolikumba eneo la kusini mwa Afrika



Naibu Katibu Mkuu afungua mkutano kati ya Wabunge wa EALA na wadau kuhusu kilimo

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akifungua mkutano wa Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ambayo inakusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha bajeti katika sekta ya Kilimo kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mpaka kufikia asilimia 10. Mkutano huo umehudhuriwa na Wabunge wa Bunge hilo kutoka nchi wanachama. Ufunguzi wa mkutano  huo umefanyika katika Hotel ya Mt. Gasper iliyopo jijini Dodoma tarehe 19 Machi 2019.
Sehemu ya Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mhe. Adam Omari Kimbisa, Mhe. Dkt. Oburu Oginga na  Mhe. Nooru Adan Mohammed 
Juu na Chini ni sehemu ya wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano huo.




Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Joachim Otaru naye akifuatilia ufunguzi wa mkutano huo
Balozi Mwinyi akiendelea kuzungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo.
Wajumbe wengine wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo. Kushoto ni Mhe.Mhandisi Mohammed H. Mnyaa.

Mhe. Ramadhan Muombwa Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wadau kutoka sekta na taasisi mbalimbali waliohudhuria mkutano kuhusu namna ya kuboresha bajeti katika sekta ya kilimo kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.   









Monday, March 18, 2019

Mawaziri wakutana na Watanzania waishio Namibia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.), akiambatana na Waziri Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Issa Haji Ussi Gavu; Waziri wa Viwanda na  Biashara, Mhe. George Kakunda (Mb.) na  Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) leo tarehe17 Machi, 2019, wamepata fursa ya kukutana na jumuiya ya  Watanzania wanaoishi nchini Namibia na   kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo  upatikanaji wa vitambulisho vya taifa na hati za kusafiria,  maendeleo na hali ya siasa nchini, biashara kwa ujumla na mkakati wa serikali katika kunufaika uanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Miongoni mwa masuala mengine, mawaziri hao wamewataarifu Watanzania hao kuhusu juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na  serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo ambazo ni pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa uvujaji wa mapato; ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa; ukuaji katika sekta ya viwanda; ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika Korongo la Stiglers;kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo afya na elimu bure na mkakati wa Tanzania kujitanua kibiashara katika eneo la SADC.

Mhe. Prof. Kabudi amewataka Watanzania hao kuacha kuamini dhana kuwa, chema chajiuza na kibaya chajitembeza  na kuanza kuyasemea masuala mbalimbali mazuri ya Tanzania. Ametolea mfano uwepo wa uhitaji mkubwa wa vitu vyenye ubora vinavyozalishwa nchini kama vigae, nepi za watoto, korosho na mvinyo na kuwataka Watanzania hao kuitumia fursa hiyo kuwa mawakala wa bidhaa hizo nje ya nchi.Suala hilo limeungwa mkono na Watanzania hao ambao wameiomba Wizara ya Viwanda na Biashara kuwapa taarifa sahihi za kibiashara na kwa wakati.


 Kuhusu suala la kila Mtanzania kuwa na hati mpya ya kielektronikia ya kusafiria ifikapo mwaka 2020, Mhe. Prof. Kabudi amewataarifu Watanzania hao kuwa, serikali inaziboresha hati za sasa za kusafiria  kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Hivyo, ameitaka jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho vya kitaifa ambavyo ni moja ya vielelezo muhimu katika kuomba hati hizo mpya za kusafiria.

 Mhe.Prof. Kabudi amewahakikishia Watanzania hao kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kitengo cha Diaspora, kipo wazi muda wote ili kuwasaidia Watanzania wanaoishi nje ya nchi ili kuhakikisha wanapata vitambulisho hivyo vya taifa  kwa wakati.

Mawaziri hao wapo nchini Namibia kwa lengo la kuhudhuria mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC ambao umefanyika kuanzia tarehe 15 hadi 17 Machi, 2019.

Wajumbe walioshiriki katika mkutano huo wakifungua mkutano kwa kuimba wimbo wa taifa.

 Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ambao pia unawakilisha nchini Namibia, Richard Lupembe, akimkaribisha Mhe. Prof. Kabudi kwa ajili ya kufungua mkutano huo.

Sehemu ya Watanzania waishio nchini Namibia wakifuatilia mkutano huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, akifurahia jambo wakati wa mkutano huo.Pembeni yake ni baadhi ya Watanzania waishio Namibia.




Sunday, March 17, 2019

Waziri Kabudi awashukuru wajumbe wa wizara mbalimbali walioshiriki katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, akifungua kikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi(Mb.), na wajumbe wa wizara mbalimbali walioshiriki katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Council of Ministers).
Mhe. Kabudi ametumia kikao hicho kuwashukuru wajumbe wa wizara mbalimbaliza serikali zilizoshiriki katika mkutano huo kwa umakini ambao wameuonesha.

Mheshimiwa Kabudi akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.Kushoto kwake ni Waziri wa Viwanda na  Biashara, Mhe. George Kakunda (Mb.); na kulia kwake ni Waziri Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Issa Haji Ussi Gavu.

Makatibu wakuu na wajumbe walioshiriki katika kikao hicho.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bibi. Agnes Kayola akifuatilia mkutano huo.

Mkutano unaendelea

Mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC ujao kufanyika Tanzania



Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Council of Ministers), lililokuwa likiendelea na mkutano huko Windhoek, Namibia, limehitimisha mkutano huo  kwa Tanzania kuwakaribisha viongozi hao kushiriki katika mkutano unaofuata wa baraza hilo ambao utafanyika Dar es salaam, Tanzania, Agosti 2019.


Akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano waAfrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi(Mb.), ameelezea furaha yake kwa Tanzania ambayo ni miongoni mwa mataifa yaliyoshiriki katika ukombozi dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi katika nchi mbalimbali Kusini mwa Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuahidi kufanya maandalizi ya kutosha. 


Naye Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni  Naibu Waziri Mkuu wa Namibia na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah, amehitimisha mkutano huo kwa kuziomba nchi wanachama wa SADC zilizoshiriki katika mkutano huo  kuhakikisha masuala yaliyoafikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa kwa wakati.


Baadhi ya musuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa mipango na mikakati ya SADC; Taarifa ya Kamati ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Kamati ya Usimamizi wa Rasilimali watu; Hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Visiwa vya Komoro kujiunga na SADC na Mpango wa Kuanzisha chuo cha Uhawilishwaji cha SADC (SADC  University of Transformation).Masuala Uendelezaji wa viwanda katika kanda; Utekelezaji wa Mkakati wa Kanda wa Mawasiliano na Mabadiliko ya Kitaasisi katika Umoja wa Afrika(AU).

Waziri Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Issa Haji Ussi Gavu (mwenye tai ya bluu)Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, wakati wa mkutano huo.

Baadhi ya wajumbe wakiimba wimbo wa SADC wakati wa kuhitimisha mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC.

Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax, akiteta jambo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Saturday, March 16, 2019

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Canada nchini

Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pamela O’Donnell, Balozi wa Canada nchini. Mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika yalifanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salam tarehe 15 Machi, 2019.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa Tanzania na Canada ambao ulijengwa tangu enzi za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere.

Tanzania na Canada zimekuwa na ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya, biashara, uwekezaji, utawala wa Sheria pamoja na haki za binadamu.

Katika mazungumzo hayo, pamoja na mambo mengine, Mhe. Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa ushirikiano unaolenga kuleta tija katika kuinua maisha ya Watanzania.

Mhe. Dkt. Ndumbaro alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo kuhusu mafanikio ya Serikali katika kujenga uchumi na kuomba Serikali ya Canada iendelee kutoa ushirikiano kwa Tanzania kwa lengo la kuleta maendeleo zaidi kwa wananchi. Aidha, alimhakikishia  ushirikiano kutoka Wizarani ili kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya ushirikiano wa nchi hizi mbili.
Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini, Mhe. Pamela O’Donnel. 
Mazungungumzo kati ya Mhe. Dkt. Ndumbaro na Balozi O'Donnel yakiendelea huku  Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas A. Nyamanga akifuatilia mazungumzo hayo.

 Picha ya pamoja
==================================================


...MKUTANO KATI YA KAIMU MKURUGENZI WA IDARA YA ULAYA NA AMERIKA NA BALOZI WA ITALIA NCHINI

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas A. Nyamanga amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Roberto Mengoni, Balozi wa Italia hapa nchini.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 15 Machi 2019 yalilenga katika kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Italia hususan katika masuala ya kimataifa, utamaduni,  biashara na uwekezaji.

Aidha, walikubaliana kuimarisha ushirikiano zaidi na  kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

Bw. Nyamanga alimhakikishia Balozi huyo ushirikiano kutoka kwake na Wizara  kwa ujumla katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.


Pichani ni Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni

Bw. Nyamanga akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mengoni mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yao

Friday, March 15, 2019

Tanzania yashiriki katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika




Katibu Mtendaji wa  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Bi. Stergomena Tax, akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa  Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Council of Ministers),  unaofanyika Windhoek, Namibia, kuanzia tarehe 15 -17 Machi, 2019.  
Mkutano huu, unahudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mawaziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mawaziri wa Fedha pamoja nchi 16 wanachama wa SADC ambapo Tanzania inawakilishwa katika mkutano huu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.); Waziri Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Issa Haji Ussi Gavu; Waziri wa Viwanda na  Biashara, Mhe. George Kakunda (Mb.); na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.). 
Masuala yanayojadiliwa katika mkutano huu ni pamoja na  Taarifa ya Utekelezaji wa mipango na mikakati ya SADC; Taarifa ya Kamati ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Kamati ya Usimamizi wa Rasilimali watu; Hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Visiwa vya Komoro kujiunga na SADC na Mpango wa Kuanzisha chuo cha Uhawilishwaji cha SADC (SADC  University of Transformation).
Masuala mengine yanayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huu ni pamoja  na; Uendelezaji wa viwanda katika kanda; Utekelezaji wa Mkakati wa Kanda wa Mawasiliano; Mabadiliko ya Kitaasisi katika Umoja wa Afrika(AU); na Majadiliano ya Ubia Mpya Baina ya Nchi za Kundi la Afrika, Carribean na Pasifiki (ACP) na Umoja wa Ulaya (EU), baada ya mkataba wa Cotonou kumalizika mwaka 2020.
Mkutano huu umetanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu pamoja na maafisa waandamizi  uliofanyika kuanzia tarehe 11 - 14 Machi, 2019, Windhoek. Namibia. Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akifuatilia hotuba ya Katibu Mtendaji wa SADC.


Naibu Waziri Mkuu wa Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC, Mhe.Netumbo Nandi-Ndaitwah,  akitoa hotuba wakati wa mkutano huo.
Wajumbe  kutoka nchi za Tanzania, Zambia  na Afrika Kusini, wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC, Mhe. Nandi-Ndaitwah.


Mawaziri wa SADC wakiwa katika picha ya pamoja.