Friday, June 17, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE, CRDB PLC ZASAINI MAKUBALIANO KUTENGENEZA MFUMO WA DIASPORA DIGITAL HUB

Na Mwandishi wetu, Dar

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Benki ya CRDB Plc wamesaini Hati ya Makubaliano ya kutengeneza Mfumo wa Kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora, (Diaspora Digital Hub).

Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Akiongea katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Jijini Dar es Salaam, Balozi Sokoine amesema mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Serikali kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha Diaspora wa Tanzania waliopo sehemu mbalimbali ulimwenguni kupata huduma mbalimbali na kushiriki kidigitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo, biashara, uchumi na uwekezaji.

“Ushirikiano wa Wizara na Benki ya CRDB Plc ni wa muda mrefu na wenye mafanikio mengi katika kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya Tanzania. Wizara ina imani kuwa kupitia udhamini wa shilingi milioni 100 kutoka CRDB za kutengeneza mfumo wa Diaspora Digital Hub utaboresha huduma mbalimbali zenye kukidhi mahitaji ya Diaspora kote ulimwenguni,” amesema Balozi Sokoine

Balozi Sokoine ameongeza kuwa, mfumo huo pamoja na mambo mengine, utafungua uwezekano wa fursa zaidi za ushirikiano kati ya Wizara na Benki ya CRDB katika kazi ya uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya Balozi za Tanzania nje ya nchi.

Balozi Sokoine ameyataja baadhi ya mafanikio ya mfumo huo ambayo ni kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Tanzania kuhamasisha taasisi na watumishi wake kutumia ipasavyo mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma ili kuendana na mabadiliko ya dunia na kuongeza tija katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela amesema CRDB inaamini kuwa kuanza kwa Mfumo wa Kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) utakuwa na manufaa mengi kwa Serikali na Benki ya CRDB kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kusaidia kufahamu idadi ya Diaspora walioko ulimwenguni na kutunza taarifa za watanzania walioko nje.

“Diaspora Digital Hub itasaidia pia kupata taarifa za fursa za uwekezaji nchini na kuwatambua wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini, kuisaidia Serikali katika zoezi la sensa litakalo fanyika mwezi Agosti, 2022, kusaidia kupata taarifa sahihi za pamoja na kuisaidia Wizara kupanga bajeti yake” amesema Bw. Nsekela

Bw. Nsekela ameongeza kuwa mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Benki ya CRDB kuboresha zaidi huduma zake na kuwafikia wateja wengi wakiwemo Diaspora waliopo ulimwenguni.

“CRDB inaahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub unakamilika kwa wakati,” amesema Bw. Nsekela

Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza katika hafla hiyo amesema Mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub utakapokamilika utaiwezesha Serikali kuwa na kanzidata ya uhakika kuhusu Diaspora kote ulimwenguni.

“Mfumo huu pia utaiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa njia ya kidigitali ambapo uratibu wa masuala mbalimbali yanayotolewa katika mfumo huo utafanyika papo kwa papo.

Balozi Bwana aliongeza kuwa kupitia mfumo huo Serikali itaweza kufahamu kwa ufasaha idadi ya Diaspora, ujuzi, elimu walizonazo na mengine mengi. Kadhalika, Diaspora wenyewe wataweza kupata kupitia mfumo huo huduma mbalimbali kwa ajili ya mahitaji yao.

Ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Benki ya CRDB ni wa muda mrefu tangu 2010 wakati Kitengo cha Diaspora kilipoanzishwa. Ushirikiano huo umewezesha Benki ya CRDB PLC kuwa ya kwanza kuanzisha utoaji wa huduma kwa Diaspora ambapo hadi sasa zaidi ya Diaspora 30,000 wananufaika na huduma ya Tanzanite Account.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela akiongea wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza 'Diaspora Digital Hub' leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora  


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakisaini Hati ya makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakionesha Hati ya makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora baada ya kumaliza kusaini hati hiyo




Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora



Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Fedha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Swalehe Chondoma wakifuatilia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi kutoka Wizarani na wafanyakazi wa Benki ya CRDB baada ya kusainiwa kwa Hati ya makubaliano 



Thursday, June 16, 2022

SERIKALI YA DENMARK YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA TANZANIA

    

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) amefanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo wa Denmark, Mhe. Flemming Møller Mortensen (kushoto) pembezoni mwa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mazungumzo baina ya Mawaziri hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia pamoja na kuendeleza sekta za biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu na uchumi wa kijani.

Pia Waziri Mulamula ameishukuru Denmark kwa kuendelea kuwa mdau wa maendeleo kabla na baada ya Tanzania kupata uhuru wake mwaka 1961 na kwamba Serikali ya Tanzania inaendelea kusimamia kwa karibu mipango na miradi yote iliyoanzishwa kwa ushirikiano na Serikali ya Denmark.

Waziri wa Maendeleo wa Denmark, Mhe. Flemming Møller Mortensen (wa pili kushoto) akieleza kuhusiana na maeneo ya kimkakati ambayo Serikali ya Denmark itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuenzi ushirikiano wa kihistoria ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo mawili.

Waziri Mulamula akimkabidhi zawadi, Mhe. Mortensen

Ujumbe wa Tanzania ulioambatana na Mhe. Waziri Mulamula ukifuatilia mazungumzo.




 

TANZANIA NA SWEDEN ZAAHIDI KUONGEZA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Sweden, Bw. Magnus Nilsson pembezoni mwa  Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland

Mazungumzo ya viongozi hao yalihusu ushirikiano baina ya mataifa yao hususan kwenye sekta za biashara, mageuzi katika mifumo ya taasisi za umma, haki za wanawake na watoto.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana kufuatia misaada mbalimbali iliyotolewa na Serikali ya Sweden,  Waziri Mulamula amesema sekta ya nishati imepiga hatua kubwa nchini ambapo mashirika yote yanayosimamia sekta hiyo yameboresha utendaji wake pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Bw. Nilsson alieleza kuwa Sweden itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina yake na Tanzania pamoja na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano. 

Aidha, Bw. Nilsson ameahidi kuwa Serikali ya Sweden itaendelea kusaidia eneo la mageuzi ya kisekta ikiwa ni pamoja na kuziunganisha taasisi za Tanzania na Sweden zianzishe ushirikiano kwa lengo la kupeana uzoefu na kujenga uwezo.

Kadhalika, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mkazo katika masuala ya watoto, usawa wa jinsia na uhuru katika masuala ya siasa. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) amefanya mazungumzo wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden. Bw. Magnus Nilsson (kulia) pembezoni mwa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika nchini Finland tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Sweden, Bw. Magnus Nilsson (wa pili kulia) akizungumza na Mheshimiwa Waziri Mulamula (hayupo pichani). Pamoja naye ni ujumbe alioambana nao alipokuwa nchini Finland kushiriki Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mkutano ukiendelea, kushoto ni ujumbe wa Tanzania ulioambana na Mhe. Waziri Mulamula.

Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Finland mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo.

WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA FINLAND


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto pembezoni mwa  Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Serikali ya Tanzania na Finland zinashirikiana katika masuala ya ubunifu wa kutengeneza ajira, usimamizi wa fedha kwa taasisi za umma, kujenga uwezo kwenye masuala ya kodi pamoja na utawala bora.
Maeneo mengine ya kipaumbele katika ushirikiano huo ni pamoja na elimu,kuinua ubia kati serikali na sekta binafsi, kuhamasisha uwekezaji, umarishaji wa demokrasia na utawala wa sheria na kukuza biashara. 
Balozi wa Tanzania nchini Finland mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto akieleza utayari wa Serikali ya Finland katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Serikali yake na Tanzania.
Ujumbe ulioambatana na Mhe. Haavisto ukifuatilia mazungumzo.

Wednesday, June 15, 2022

WAZIRI MULAMULA ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO KWA NCHI ZA AFRIKA NA NORDIC

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amesisitiza umoja na mshikamano kwa nchi za Afrika na Nordic aliposhiriki Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.


Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto ambapo aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo kushiriki mjadala wa vijana wa Nordic – Afrika pamoja na ajenda nyingine za majadilianao baina ya mawaziri hao.

 

Akichangia mjadala wa vijana Mhe. Waziri Mulamula amewasihi vijana waliopata nafasi ya kushiriki katika masuala mbalimbali ya kimataifa kujitoa kwa dhati ili kuleta tija katika nchi zao pamoja na kusaidia vijana wengine kupata nafasi hizo.

 

Sambamba na hilo katika nafasi nyingine ya majadiliano ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic amesisitiza juu ya umoja na umuhimu wa kushirikiana katika  kukabiliana na changamoto za ulimwengu  kwa manufaa ya wote.

 

Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic pamoja na mambo mengine umejadili masuala ya amani na usalama, migogoro, mabadiliko ya Tabianchi, masuala ya kimataifa, vijana na wanawake.

Mkutano wa 19 wa Mamwaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic umependekeza Algeria kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 20 wa Mawaziri hao unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic baada ya kumalizika kwa mkutano wa 19 wa Mawaziri hao jijini Helsinki, Finland.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akifuatilia majadiliano katika mjadala wa vijana wa Nordic - Afrika amabo ulijikita katika namna ya kuwakwamua vijana kwa kuwapa ujuzi utakaowawezesha kujikwamua kiuchumi samabamba na kushirikikishwa katika masuala ya kijamii na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto ( kulia) akiongoza Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Finland uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mkutano ukiendelea.

Tuesday, June 14, 2022

WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA UONGOZI WA OFISI YA MPANGO WA USIMAMIZI WA MIGOGORO (CMI) YA NCHINI FINLAND

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongea na uongozi wa Ofisi ya Mpango wa Usimamizi wa Migogoro tarehe 13 Juni 2022 kwenye Makao  Makuu ya taasisi hiyo nchini Finland. Mazungumzo yao yalijikita kwenye masuala ya amani na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Pia Mhe. Waziri akaeleza amani na usalama wa ukanda huo ni kipaumbele kwakuwa huziwezesha nchi kupata utulivu wa kufanya shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa Taifa na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Kutoka kushoto ni Naibu Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Usimamaizi wa Migogoro, Bi. Hanna Klinge na Mkuu wa Mpango huo Kusini mwa Jwangwa la Sahara, Bi.Tiina Kukkamaa-Bah akitoa taarifa ya utekelezaji wa mipango mbalimbali  katika taasisi hiyo, hususani katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki.


Mazungumzo yakiendelea, Kulia kwa Mhe. Waziri ni Balozi wa Tanzania nchini Finland mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Tunsume Mwangombole wakifuatilia mazungumzo

Picha ya pamoja

 

WAZIRI MULAMULA ZIARANI NCHINI FINLAND



Helsinki, 14 Juni 2022


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amewasili nchini Finland kwa ziara ya siku 3 kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic (NORDIC-AFRICA) unaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland. 


Mkutano huo umeanza na hafla ya ufunguzi iliyofanyika tarehe 13 Juni 2022, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto.

 

Akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo Mhe. Haavisto alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kujiletea maendeleo baina ya nchi hizo marafiki.

 

Aidha, mkutano huu utahusisha nchi 5 za Nordic ambazo ni Finland mwenyeji wa mkutano wa sasa, Sweden, Norway, Iceland na Denmark na nchi za Afrika 25 marafiki wa Nordic. 

 

Mkutano huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje utahusisha Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika zinazowakilisha katika nchi za Nordic na Mabalozi wa nchi za Nordic wanaowakilisha katika Nchi shiriki za Afrika.

 

Wazo la kuanzisha mkutano huu lilianza mwaka 2000 ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Sweden mwaka 2001. Baada ya hapo mikutano kama hii inafanyika kwa kupokezana kutoka Bara la Afrika na upande wa Nordic.

 

Mwaka 2019 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huu ambapo nchi takribani 34 zilishiriki katika mkutano.

 

Wakati huo huo Mhe. Waziri Mulamula ametumia fursa ya ziara hiyo kutembelea Makao Makuu ya Ofisi ya Mpango wa usimamizi wa migogoro nchini Finland na kukutana na uongozi wa mpango huo. Lengo la likiwa kujadili masuala ya amani na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa kusini mwa Afrika.

 

Katika mazungumzo yake Waziri Mulamula ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala ya amani na usalama ili kuwezesha nchi za ukanda huo kufanya shughuli za kiuchumi na kuinua maendeleo ya taifa na wananchi kwa ujumla.


 -Mwisho-


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia hotuba wakati wa hafla ya ukaribisho kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland na mwenyeji wa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic (NORDIC - AFRICA), Mhe. Pekka Haavisto unaofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland. Kushoto ni Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini Finland, Dkt. Vesa Viitaniemi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto akifungua hafla ya kuwakaribisha wajumbe wa mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic unaofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki nchi humo.

Sehemu ya wajumbe wa mkutano huo wakifatilia hotuba ya Mhe. Haavisto.

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olotu (kati) pamoja na Afisa Ubalozi katika ubalozi huo wakisalimiana na wajumbe wengine wa mkutano wakati wa hafla hiyo.

Hafla ikiendelea, Mhe. Waziri Mulamula akisamilimiana na wajumbe wengine wa mkutano huo. Kulia ni Mhe. Balozi Liberata Mulamula.

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akifuatilia hafla ya ukaribisho ya mkutano huo.


Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akisalimiana na mshiriki wa mkutano huo.


 

 

 

Saturday, June 11, 2022

MAKATIBU WAKUU WANAOSIMAMIA SEKTA MBALIMBALI WA NCHI ZA EAC WAKUTANA JIJINI ARUSHA


Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu umefanyika leo tarehe 11 Juni 2022 katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.

Mkutano huo ambao umetanguliwa na mkutano wa Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Juni 2022 ulikuwa jukumu maalumu la kupokea na kupitia taarifa, agenda na mapendekezo yaliyotokana na Mkutano wa Maafisa Waandamizi kuhusu masuala mbalimbali ya Jumuiya na hatimaye, kuyawasilisha katika Mkutano wa Mawaziri utakaopangwa kufanyika baadaye mwaka huu. 

Miongoni mwa masuala yaliyojiri katika mkutano huo ni uzingatiwaji wa ripoti mbalimbali ikiwemo ripoti ya kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli za kiofisi/rasmi za Jumuiya. 

Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe

Viongozi wengine walioambatana naye ni pamoja na, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo, Katibu Mkuu Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji –Zanzibar Bi. Khadija Rajab Khamis, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Kh. Shaaban, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi. Wengine waliombatana naye ni Balozi Stephen P. Mbundi Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Bernard Haule Mkurugenzi Biashara, Uwek ezaji na Sekta za Uzalishaji na Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Maafisa kutoka Wizara mbalimbali. 

Mkutano huo uliofanyika kwa njia mseto (video na ana kwa ana) umehudhuriwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Saitoti Torume CBS ambaye ni Katibu Mkuu wa Hazina na Mipango kutoka Jamhuri ya Kenya 

Baraza la Mawaziri ni chombo cha kutunga sera za Jumuiya. Baraza hilo linajumuisha Mawaziri wanaosimamia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki au Ushirikiano wa Kikanda.

Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ni kufuatilia na kufanya mapitio ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa programu za Jumuiya na kuhakikisha utendaji kazi mzuri wa Jumuiya
Makatibu Wakuu wanaosimamia sekta mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki wakifurahia jambo kwenye Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini
Meza Kuu kutoka kulia ni; Bw. Severin Mbarubukeye Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Vijana Michezo na Utamaduni kutoka Burundi, Bi. Edith Mwanje Katibu Mkuu Wizara ya Afrika Mashariki kutoka Uganda, Bw. Saitoti Torume CBS, Katibu Mkuu wa Hazina na Mipango kutoka Kenya, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Bw. Adrea Aguer Ariik Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afrika Mashariki ya Jamhuri ya Sudan Kusini wakiwa kwenye Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini
Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Arusha.
Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Arusha.
Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Arusha

Friday, June 10, 2022

ITALIA KUANZISHA UPYA SAFARI ZA NDEGE ZANZIBAR

Na Mwandishi wetu, Dar

Katika kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi Serikali ya Italia imeahidi kuanzisha upya safari za ndege za moja kwa moja kutoka nchini humo hadi Zanzibar kuanzia tarehe 29 Juni 2022.

Ahadi hiyo imetolewa na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle wakati alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Natalia amesema kuwa kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia hadi Zanzibar zitasaidia kukuza biashara na utalii baada ya kusitishwa kwa safari hizo tangu mwaka 2019 kutokana na changamoto ya Uviko 19.

Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema kuanzishwa upya kwa safari hizo kutachangia kukuza pato la taifa kwani awali kabla ya janga la Uviko 19, Zanzibar ilikuwa inapata watalii 200,000 kwa mwezi kutoka nchini Italia.

“Safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia kuja Zanzibar zinategemea kuanza rasmi tarehe 29 Juni, 2022 na tunaamini kuwa kuanzishwa kwa safari hiyo kutachangia kukuza sekta ya utalii na uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema Balozi Mbarouk

Tanzania na Italia zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu, utalii, viwanda, maji, kilimo, nishati, pamoja na maendeleo ya sekta binafsi. 


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimueleza jambo na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle wakati alipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam