Friday, September 15, 2023

TANZANIA ITAENDELEA KUHESHIMU MISINGI YA MTANGAMANO, DKT. BITEKO

Tanzania imeahidi kuwa itaendelea kuheshimu na kusimamia misingi ya mtangamano wa bara la Afrika kama ilivyofundishwa na kuachwa na waasisi wa Taifa hili, ili kufikia Afrika yenye ustawi na umoja.

Hayo yameelezwa leo Septemba 15, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati anafungua Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar.

Dkt. Biteko aliwambia wajumbe wa kikao hicho ambacho kinalenga kutoa mapendekezo ya kisera na miongozo ya kimkakati katika uendelezaji wa sekta ya miundombinu barani Afrika kuwa, Tanzania ipo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ambayo msingi wake ni kuimarisha mtangamano baina ya Tanzania na nchi inazopakana nazo, Afrika na dunia kwa ujumla.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa yenye urefu wa kilomita 1,800 inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani za Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lenye urefu wa kilomita 1,400 linalounganisha Tanzania na Uganda, Mradi wa Bwawa la Kuzalisha umeme wa Maji la Julius Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 kwa ajili ya matumizi ya Tanzania na nchi jirani na kufufua shirika la ndege ambalo kwa sasa lina ndege 12 zinazoiunganisha Tanzania na nchi zisizopungua 9 za Afrika.

Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana ili kufikia matarajio ya mamilioni ya Waafrika ya kuwa na miundombinu ya uhakika. Kufanikisha hilo, Dkt. Biteko alitoa wito kwa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, washirika wake na wabia wa maendeleo kuimarisha juhudi za utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ambayo ni muhimu katika kuimarisha biashara, kuongeza ajira na kukuza uchumi barani Afrika. 

Awali, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya miaka 10 ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Miundombinu Barani Afrika (PIDA), wajumbe waliainisha masuala mbalimbali ya kuzingatia ili awamu ya pili ya mpango huo, uweze kufanikiwa. Masuala hayo ni pamoja na kuwa na sera zinazoendana na mabadiliko ya dunia, kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu na kupeana taarifa muhimu ili kufanikisha uandaaji na utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ya miundombinu.

Kufanyika kwa mkutano huo nchini ni jitihada za Serikali ya awamu ya sita kupitia Ubalozi wake nchini Ethiopia, chini ya uongozi wa Balozi Innocent Shiyo za kukuza diplomasia ya uchumi na utalii wa mikutano. 

Wajumbe takribani 400 kutoka barani Afrika; washirika wa maendeleo, kama Benki ya Maendeleo ya Afrika, Exim Bank; Kamisheni ya Uchumi ya Afrika; watafiti na wanazuoni wa fani mbalimbali duniani wameshiriki mkutano huo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisoma hotuba ya ufunguzi wa Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko na wajumbe wengine katika meza kuu wakiimba Wimbo wa Taifa wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar

Wajumbe wakiimba Wimbo wa Taifa ambao ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo (wa tatu kushoto na Balozi wa Tanzania, Jamhuri ya Sudan, Mhe. Silima Kombo Haji (wa pili kushoto)

Kamishina wa Miundombinu na Nishati wa Umoja wa Afrika, Bibi Amani Abou-Zeid akihutubia Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar


Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Erick Ngilangwa na Bi. Maria Ndumbalo wakifuatilia kwa makini hotuba za ufunguzi


Wajumbe wakisikiliza hotuba za ufunguzi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiagana na baadhi ya wajumbe wanaoshiriki Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati baada ya kufungua kikao hicho




TANZANIA ,CUBA ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA ELIMU YA JUU NA KUFUNDISHA KISWAHILI NCHINI CUBA

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba kupitia elimu ya juu

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano waliyosaini kati ya Tanzania na Cuba kupitia elimu ya juu

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. William Anangisye na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Havana Prof. Miriam Garcia wakionesha Hati ya Makubaliano waliyosaini ya ushirikiano kati ya vyuo hivyo katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Havana nchini Cuba tarehe 14 Septemba 2023






Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Cuba zimesaini Hati za Makubaliano ya kushirikiana kupitia elimu ya juu, kubadilsihana wakufunzi na wanafunzi na kufundisha lugha ya kiswahili nchini Cuba na kutengeneza kamusi ya kiswahili na kihispaniola.

Makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba iliyofanyika jijini Havana na kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia.

Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam kilichowasilishwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. William Anangisye na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Havana Prof. Miriam Garcia

Katika makubaliano hayo Tanzania na Cuba zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kupitia wahadhiri, wanafunzi, masuala ya utafiti, sayansi, teknolojia, kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana na kutengeneza kamusi ya lugha ya Kiswahili na Kispaniola ili kusambaza matumizi ya kugha ya kiswahili nchini Cuba na nchi nyingine zinazozungumza lugha ya kispaniola.

Akizungumza katika hafla ya utuaji saini makubaliano hayo Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Polepole amesema Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano hayo ambayo yanatoa mwongozo maalum wa jinsi ya kutekeleza mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo.

"Haya ni mafanikio makubwa kwetu, Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano haya, sasa yatatoa mwongozo   maalum utakaowezesha taasisi husika za elimu ya juu kutekeleza kikamilifu mpango wa kusambaza na kueneza lugha ya Kiswahili  nchini Cuba," alisema Mhe. Balozi Polepole.

Makubaliano yaliyosainiwa ni kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Cuba ambapo Chuo Kikuu cha Havana kilikubaliana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kushirikiana katika masuala ya utafiti, sayansi na Teknolojia na kufanya kazi kwa pamoja ili kutunga Kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola.

 

Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknojia na Wizara ya Elimu ya Juu ya nchini Cuba ambayo yatawezesha ubadilishanaji wa wanafunzi, wahadhiri na watafiti katika eneo la sayansi na teknolojia ili kuwawezesha wahusika kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo hayo na hivyo kuleta tija na ufanisi kwa pande zote mbili.


 



DKT. MWINYI AZINDUA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI CUBA


 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.  Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba wakizindua Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Havana nchini Cuba katika hafla iliyofanyika jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.  Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa wakikata utepe wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba iliyofanyika jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.  Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano nchini Cuba kwa ajili ya kuzindua  Ubalozi huo katika hafla iliyofanyika jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023 kulia kwake ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Polepole na kushoto ni Mke wa Mhe. Dkt. Mwinyi Mama Mariam Mwinyi

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Havana nchini Cuba wakati wa hafla ya uzinduzi wa ubalozi huo iliyofanyika jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.  Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba iliyofanyika jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano nchini Cuba iliyofanyika jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023



 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.  Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Havana katika hafla iliyofanyika jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023.

 

Akizungumza katika uzinduzi wa Ubalozi huo Mhe. Rais Dkt. Mwinyi amesema kufunguliwa kwa Ubalozi huo mwaka 2019 kunaonesha nia ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Cuba na kujibu kitendo cha Cuba ilipofungua Ubalozi wake nchini mwaka 1962.

 

 

“kufunguliwa kwa Ubalozi huu mwaka 2019 kunaonesha nia ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Cuba na kujibu kitendo cha Cuba ilipofungua Ubalozi wake nchini mwaka 1962,” alisema Dkt. Mwinyi.

 

Amesema kufunguliwa kwa ubalozi huo mwaka 2019 kunarahisisha uratibu wa shughuli za nchi zetu katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo ya kijamii na kuwaletea maendeleo wananchi wa nchi hizo.

 

 

Dkt. Mwinyi ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje ya Cuba na Serikali ya Jamhuri ya Cuba kwa ushirikiano mkubwa ambao imekua ikiupatia Ubalozi wa Tanzania Havana tangu ulipoanzishwa mwaka 2019 hadi wakati huu kitu ambacho kimeuwezesha Ubalozi huo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

 

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namshukuru Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Cuba na Serikali ya Jamhuri ya Cuba kwa ushirikiano mkubwa ambao imekua ikiupatia Ubalozi huu tangu mwaka 2019 ulipofunguliwa, kitendo hicho kimeuwezesha Ubalozi wetu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” alisema Dkt. Mwinyi.

 

Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi huo Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa amesema Serikali ya Jamhuri ya Cuba inauthamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania na itaendelea kufanya hivyo kwani uhusiano uliopo ni wa kindugu na wa kihistoria na kufanya hivyo ni kuwaenzi waanzilishi wa mataifa hayo.

 

“Mhe. Rais na Wananchi wote wa Tanzania, Serikali ya Cuba inauthamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania na itaendelea kuuthmini, uhusiano wetu ni wa Kindugu na wa kihistoria na kufanya hivi ni kuwaenzi waanzilishi wa mataifa yetu,” alisema Mhe. Mesa

 

Mhe Mesa amesema Serikali ya Cuba inaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kufungua Ubalozi nchini Cuba na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuuwezesha Ubalozi huo kufanya kazi na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

 

Akizungumza awali Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Polepole amesema Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Cuba uhusiano ambao ni wa kindugu na hasa ikizingatiwa kuwa Cuba ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tanzania.

 

Amesema Tanzania imeendelea kushirikiana na Cuba katika sekta ya Afya na elimu ambapo wamekuwa wakibadilishana wataalamu kuanzia miaka ya 1960 hadi nyakati hizi kwa ajili ya kusaidia jamii za kitanzania katika eneo hilo.

 

 

Uzinduzi wa Ubalozi huo wa Tanzania Havana  uliofunguliwa mwaka 2019 ulihudhuriwa na Jumuiya ya Wanadiplomasia mbalimbali walioko jijini Havana.

 

 


Thursday, September 14, 2023

BALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI AZUNGUMZA NA ALIYEKUWA MWAKILISHI MKAZI WA UNDP MALAWI

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Malawi, Bw. Shigeki Komatsubara ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini humo mara baada ya mazungumzo baina yao yaliyofanyika katika Ubalozi wa Tanzania, Lilongwe hivi karibuni
===================================================================

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola amekutana kwa mazungumzo na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Malawi, Bw. Shigeki Komatsubara ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini humo.

 

 

Lengo la mazungumzo yao ambayo yalifanyika katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lilongwe hivi karibuni, lilikuwa ni kumuaga Bw. Komatsubara na kujadili ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.

 


Katika mazungumzo yao, Balozi Kayola alimshukuru Mwakilishi huyo Mkazi kwa kufika kumuaga rasmi na kumtakia kila la kheri anapokwenda kuwa Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania. Vile vile, alimpongeza Bw. Komatsubara kwa kumaliza muda wa uwakilishi nchini Malawi kwa mafanikio na kuahidi kuendelea kushirikiana nae anapotekeleza majukumu yake nchini Tanzania.

 


Kadhalika Mhe. Balozi alimweleza Mwakilishi Mkazi kuwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ni moja ya mashirika muhimu ya maendeleo yanayothaminiwa sana na Serikali ya Tanzania, hivyo anategemea kuendelea kufanya kazi na kushirikiana nae ili kusaidia Tanzania kufikia malengo ya maendeleo. Alimueleza kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaendelea kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta zote muhimu nchini na matokeo yake yanaonekana.

 


Bw. Komatsubara aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kuweka mipango ya Taifa inayoakisi mabadiliko ya dunia na kuipongeza Serikali kwa kuimarisha mikakati ya maendeleo kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania.

 


Pia alimshukuru Balozi Kayola kwa kutenga muda kuzungumza nae na aliahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi hata atakapokuwa nchini Tanzania. Aidha, ameuomba Ubalozi umpe ushirikiano mrithi wake hapa Malawi, Bi. Fenella Frost. 

 


Sunday, September 10, 2023

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI WATUMIA SIKU YA AFRIKA KUTANGAZA FURSA NA UTAMADUNI WA TANZANIA


Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola (mwenye nguo yenye nakshi za bendera ya Tanzania) akimshuhudia Waziri wa Viwanda na Biashara wa Malawi, Mhe. Simplex Chithyola akionja chakula cha kitanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Afrika yaliyofanyika jijini Lilongwe tarehe 09 Septemba 2023. Ubalozi wa Tanzania umeshiriki maadhimisho hayo kwa kutangaza fursa za uwekezaji, utalii kupitia Filamu ya The Royal Tour na kuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili.
 Mhe. Chithyola akifurahia chakula cha kitanzania alipotembelea banda la Tanzania wakati wa  Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Afrika yaliyofanyika jijini Lilongwe hivi karibuni. Wengine katika picha ni Mhe. Balozi Kayola na wageni wengine waliotembelea Banda la Tanzania.

   
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja

========================================

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  nchini Malawi umeshiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Afrika yaliyofanyika jijini Lilongwe tarehe 9 Septemba, 2023. 

 

Katika kutangaza Diplomasia ya Uchumi, Ubalozi wa Tanzania ulitumia fursa hiyo kutangaza fursa za Uwekezaji, kuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili na kutangaza vivutio vya Utalii kwa kuonesha Filamu ya The Royal Tour. 


Kadhalika Ubalozi ulishirikiana na Watanzania Diaspora wanaoishi Malawi kuonesha  Utamaduni wa Tanzania ikiwemo vyakula vya asili. 



Banda la Ubalozi wa Tanzania lilitembelewa na wageni wengi ambao walipendezwa na vyakula vya asili kutoka Tanzania. 

 

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa  Waziri wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Simplex Chithyola.

Saturday, September 9, 2023

WAZIRI MAKAMBA AKABIDHIWA RASMI OFISI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekabidhiwa ofisi rasmi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

 Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Waziri Makamba amemshukuru Dkt. Tax kwa ushirikiano aliompatia wakati wote tangu yalipofanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwishoni mwa mwezi Agosti 2023.

“Tangu Mheshimiwa Rais alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri umekuwa ukinipatia ushirikiano wakati wote, nakushukuru sana, pia nakutakia heri katika majukumu yako mapya” amesema Waziri Makamba

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Tax amesema alipohudumu katika Wizara alipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa menejimenti na watumishi wa Wizara na kumhakikishia Mhe. Waziri Makamba kuwa ana watumishi wachapakazi

“Wakati wa utumishi wangu hapa wizarani, nilipata ushirikiano mkubwa, hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana menejimenti na watumishi wote wa wizara kwa ushirikiano walionipa,” alisema Dkt. Tax

Amesema jukumu lililo mbele ya Wizara hii ni kutekeleza maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo kwa kutafuta fursa mbalimbali za kukuza uchumi na kuendeleza Diplomasia ya Uchumi

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax pia amemtakia utendaji kazi mwema Waziri Makamba na kuwashukuru Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) Katibu Mkuu Mkuu wa Wizara, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Naibu Katibu Mkuu, Menejimenti na watumishi wa Wizara. 

Makabidhiano hayo yalihudhuriwa pia na wajumbe wa menejimenti na baadhi ya watumishi wa wizara.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akikabidhiwa nyaraka mbalimbali na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akikabidhiwa nyaraka mbalimbali na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam










Friday, September 8, 2023

RAIS WA BURUNDI AREJEA NYUMBANI

 

Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye ameondoka nchini kurejea Burundi baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) uliofanyika nchini kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2023          
  

Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Alberet Chalamila katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye akiwaaga viongozi wa mbalimbali waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuaga tayari kwa safari ya kurejea Burundi baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) uliofanyika nchini kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2023

Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye akiwaaga viongozi wa mbalimbali waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuaga tayari kwa safari ya kurejea Burundi baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) uliofanyika nchini kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2023.
Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye akiwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akikagua gwaride maalum katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuaga tayari kwa safari ya kurejea nchini Burundi


Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye (kushoto) akiwa na Waziri wa Madini (kulia) akiwaaga wananchi waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuaga tayari kwa safari ya kurejea nchini Burundi baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) uliofanyika nchini kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2023
kikundi cha ngoma kikitumbuiza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuaga Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye kurejea Burundi baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) uliofanyika nchini kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2023

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akiwa katika chumba cha wageni maalum katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati wa kumsindikiza Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye aliyekuwa akiondoka nchinii kurejea nchini Burundi


Rais wa Jamhuri wa Burundi Mheshimiwa, Evariste Ndayishimiye ameondoka nchini kurejea Burundi baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) uliofanyika nchini kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2023.

 

Mhe.Evariste Ndayishimiye ameondoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa Dar es salaam na kuagwa na Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila.

 

Mkutano wa Wakuu wa nchi wa Jukwaa hilo ulihudhuriwa na Marais kutoka nchi za Kenya,Burundi, Senegal na mwenyeji Tanzania. Marais walioshiriki mkutano huo ni Mhe. William Ruto wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Evarist Ndayishimiye wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Macky Sall wa Jamhuri ya Senegal na mwenyeji wao Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi Rais wa Zanzibar.