Saturday, July 21, 2012

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya awasili nchini

Mhe. Dkt. William Mgimwa (Mb.), Waziri wa Fedha, akisalimiana na Mhe. Jose Manuel Barroso, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya mara baada ya rais huyo na ujumbe wake kuwasili nchini jana kwa ziara ya kikazi ya siku tatu. Kushoto kwa Mhe. Mgimwa ni Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 

Mhe. Dkt. Mgimwa akiwa katika mazungumzo na Mhe. Barroso mara baada ya kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataiafa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana.
 
 
Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Kimataifa akifafanua jambo kwa Bw. Andris Piebalgs ambaye ni mmoja wa wajumbe waliofutana na Mhe. Barroso hapa nchini.
 

Balozi Dora Msechu (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa katika mazungumzo na mmoja wa wajumbe waliofuatana na Mhe. Barroso hapa nchini.
 
 
 
Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EU), Mhe. José Manuel Barroso akifuatana na Kamishina wa Maendeleo wa Umoja huo, Bw Andris Piebalgs, aliwasili nchini jana tarehe 20 Julai, 2012 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika masuala ya uchumi na siasa baina ya Tanzania na Umoja huo.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Barroso alipokelewa na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. William Mgimwa (Mb), Waziri wa Fedha, aliyekuwa amefuatana na Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Balozi Dora Msechu, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Aidha, akiwa nchini, Mhe. Barroso ataonana kwa mazungumzo na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 21 Julai, 2012 Ikulu, Dar es Salaam.

Pia, wakati wa ziara hiyo Mikataba sita ya misaada ya kifedha yenye thamani ya Euro milioni 126.5 kutoka Umoja huo itasainiwa pamoja na miradi mipya sita ya maendeleo kuzinduliwa ili kuwezesha upatikanaji wa maji safi, kuimarisha sekta ya usafiri wa barabara na miundombinu ya barabara za vijijini pamoja na kuimarisha masuala ya utawala bora na uwajibikaji.

Mhe. Barroso na ujumbe wake pia watatembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya hapa nchini ikiwemo Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es Salaam na miradi mingine ya maji iliyopo mkoani Mbeya.

Mhe. Barroso na ujumbe wake wataondoka nchini tarehe 22 Julai, 2012 kuelekea Brussels, Ubelgiji.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.