Thursday, August 30, 2012

Kikao cha Mawaziri wa NAM


Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki kwenye Mkutano wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya Ukumbi wa Mkutano huo nchini Iran.  Pichani ni Balozi Celestine Mushy (katikati), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa iliyopo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Justin Seruhere (wa pili kulia), Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Bw. N.M Mboyi (wa kwanza kulia), Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Sera na Mipango.  Wengine ni Bw. Christopher Mvula (kushoto), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati na Bi. Eva Ng’itu, Afisa Dawati wa NAM hapa Wizarani. 


Balozi Mushy (wa pili kushoto-nyuma) akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Justin Seruhere (wa kwanza kulia-mbele), Bw. N.M. Mboyi (wa kwanza kulia-nyuma), Bw. Christopher Mvula (wa kwanza kushoto-nyuma) na Bw. Ally Kondo (kushoto-mbele), Afisa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.



Kikao cha Mawaziri wa NAM 

Na Ally Kondo, Tehran


Kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) kilianza nchini Iran siku ya Jumanne tarehe 28 Agosti, 2012 kwa kupitia na kuridhia nyaraka zilizoandaliwa na Wataalam katika kikao chao cha tarehe 26 na 27 Agosti, 2012.

Nyaraka hizo zimebainisha mapendekezo mbalimbali ambayo yatawasilishwa kwa  Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano wao utakaofanyika tarehe 30 na 31 Agosti, 2012, ili kotoa  mwongozo kwa nchi wanachama kwa ajili ya utekelezaji. Masuala yaliyojadiliwa katika nyaraka hizo ni kuhusu hali ya kisiasa, uchumi na kijamii duniani.

Baada ya Mawaziri kupitia na kuridhia nyaraka hiyo, walipewa fursa ya kuchangia kaulimbiu ya mkutano huo ambayo inahusu mfumo wa utawala wa amani duniani (Lasting Peace through Joint Global Governance).

Takribani, Mawaziri wote waliopata nafasi ya kuchangia walisisitiza umuhimu wa nchi za NAM kushirikiana katika kutekeleza mapendekezo yaliyokubaliwa pamoja na kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto ambazo zinazojitokeza duniani. Walizibainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na uvunjifu wa amani, maamuzi ya kibabe, migogoro ya kiuchumi, kuenea kwa silaha za maangamizi na mapigano ya kutumia silaha. Changamoto nyingine ni ugaidi, uharamia, mabadiliko ya tabianchi, biashara ya madawa ya kulevya na kitendawili cha kufanya mabadiliko katika Umoja wa Mataifa hususan, Baraza la Usalama.

Kuhusu hali ya kisiasa duniani, hususan katika Mamlaka ya Palestina, Mawaziri walisisitiza umuhimu wa nchi hiyo kupewa haki ya kuunda Taifa huru kwa kuzingatia mipaka ya kabla ya mwaka 1967. Aidha, waliitaka Israel kuyaachia maeneo yote ya Palestina inayoyakalia kwa mabavu pamoja na kuwaruhusu Wapalestina wanaoishi uhamishoni kurejea katika nchi yao.

Sanjari na hilo, Mawaziri walieleza kuwa mzozo unaoendelea nchini Syria utatuliwe na Wasyria wenyewe bila kuingiliwa kwa namna yoyote iwe kijeshi kutoka nje.    

Aidha, Mawaziri walitoa wito wa kuharakisha mchakato wa kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kuongeza  idadi ya  wanachama wa kudumu katika Baraza hilo kwa kuzingatia jiografia ya dunia. Hivyo, walionyesha athari zinazotokana na kuchelewa kulifanyia mabadiliko Baraza hilo, ni nchi zinazoendelea kushindwa kufikia malengo yake. Baadhi ya nchi zilishangazwa na vitendo vya nchi zinazojiita watetezi wa amani duniani, kumbe kwa mlango wa nyuma nchi hizo zinapiga ngoma ya kuchochea vita.

Kuhusu masuala ya kijamii, ilisisitizwa umuhimu wa kutambua na kuheshimu tamaduni za nchi mbalimbali. Kwa mfano nchi nyingi zilitahadharisha kuwa Jumuiya ya Kimataifa izingatie tofauti za tamaduni duniani inapoyafanyia kazi masuala ya haki za binadamu. Ilielezwa kuwa haki za binadamu zisitumike kama kisingizio cha kupandikiza tamaduni za kigeni katika nchi nyingine.

Aidha, ilisisitizwa kuwa ili kubadili hali ya mambo duniani hivi sasa, NAM sharti ibuni utaratibu wake wa kutatua mizozo, kubadilishana habari na taarifa za kitelejensia pamoja na kuunda chama cha wafanyabiashara na soko la hisa.   

Aidha, Mawaziri walipinga tabia iliyojijenga wakati huu ya nchi chache zenye nguvu kufanya maamuzi kwa niaba ya nchi nyingine. Kukabiliana na hali hiyo, ilisisitizwa umuhimu wa kuwa na uwiano mzuri wa uwakilishi katika taasisi za kimataifa zinazofanya maamuzi kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Taasisi za Fedha.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.