Monday, August 6, 2012

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje 2012/2013




HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNARD KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013

 
UTANGULIZI
1.   Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

2.   Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza kwa umahiri mkubwa Bunge hili la Bajeti la mwaka 2012/2013.  Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Job Ndugai (Mb.), Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wanaokusaidia kuongoza Bunge hili kwa kazi nzuri wanayoifanya.

3.   Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu ya Nne. Chini ya uongozi wake Taifa letu limeendeleza utamaduni wetu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Nawaomba Watanzania wote tuendelee kudumisha hali hiyo ili kuimarisha umoja wetu ambao ni tunu isiyopatikana kwa bei yoyote.  

4.       Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine wote walionitangulia kuwapongeza kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wabunge wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa Rais mwezi Mei 2012. Nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge waliochaguliwa kipindi hiki kutokana na mabadiliko yaliyotokea kwenye nafasi mbalimbali humu Bungeni na ndani ya Serikali. Nampongeza pia Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge.

5.       Mheshimiwa Spika, kwa njia ya kipekee kabisa, niruhusu niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Wizara yangu kwa kuwa ndiyo inayosimamia masuala yote ya mambo ya nje, nawaahidi Waheshimiwa Wabunge ushirikiano wangu binafsi na ule wa Wizara nzima kwa kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

6.       Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru pia Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa William A. Mgimwa (Mb.), Waziri wa Fedha; pamoja na Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa hotuba zao za kina ambazo zimetoa ufafanuzi na miongozo kwa masuala mbalimbali muhimu ya Taifa letu kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa ujumla wake, naomba kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote waliotangulia kuwasilisha bajeti zao kwa kazi nzuri walizozifanya. Hotuba zao zote zimefafanua kwa kina masuala ya uchumi, siasa na jamii yanayohusu nchi yetu na hivyo kuigusa pia Wizara yangu kwa njia moja au nyingine.

7.       Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati na za uongozi mzima wa Wizara kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati kwa ushauri wao mzuri ambao wamekuwa wakiutoa mara kwa mara kwa Wizara yangu. Kamati hii imetoa mchango mkubwa sana katika kuiwezesha Wizara kukabiliana na changamoto zinazoikabili katika kutekeleza majukumu yake. Ninaamini ziara walizozifanya kwenye nchi mbalimbali kutembelea Balozi zetu zimewapa fursa ya kujionea wenyewe na kusikia kutoka kwa maafisa wetu changamoto mbalimbali zinazotukabili kama Wizara. Aidha, kwa ujumla, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao wanayoitoa Bungeni katika kuishauri Serikali.

8.       Mheshimiwa Spika, natoa shukrani na pongezi maalum kwa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Vilevile, nawapongeza na kuwashukuru Bwana John M. Haule, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Balozi Rajabu H. Gamaha, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Mabalozi na wafanyakazi wote kwa msaada mkubwa wanaonipa katika kuiongoza Wizara hii. Pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao, nawashukuru kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kutetea maslahi ya Taifa letu.

9.       Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee ziwaendee wananchi na viongozi wa Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Lindi na hasa wana-Mtama wote.  Napenda pia nimshukuru mke wangu Mrs. Membe na watoto wangu kwa upendo na uvumilivu waliouonesha kwangu.

10.   Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kueleza kwa kina kuhusu hotuba yangu, niruhusu niungane na Viongozi wote, Wazanzibari na Watanzania kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya meli ya MV Skagit iliyotokea Zanzibar. Kwa wale wote walioumia na wanaoendelea kujiuguza, namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu waweze kupona haraka.

11.   Mheshimiwa Spika, vilevile, natoa salamu za pole kwa wale Wabunge wote waliopatwa na misiba ya wapendwa wao. Kwa wote, namwomba Mwenyezi Mungu awape faraja na azilaze Roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina.

TATHMINI YA HALI YA DUNIA KWA KIPINDI CHA 2011/2012

 

HALI YA DUNIA

 

ULAYA NA MAREKANI


12.        Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, hali ya dunia kiuchumi, kisiasa na kijamii katika mwaka wa fedha 2011/2012 imekuwa ya mashaka makubwa na hivyo kuathiri utulivu katika nchi nyingi duniani. Hali hiyo imechochewa na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali duniani.

13.       Mheshimiwa Spika, eneo la Ulaya limeathirika sana kiuchumi kutokana na madeni pamoja na mdororo wa uchumi ulioikumba dunia katika kipindi cha mwaka 2008. Hali hii pia iliathiri kwa kiasi kikubwa sarafu ya Euro, uchumi wa nchi zilizo katika ukanda wa sarafu hiyo ujulikanao kamaEurozone” pamoja na nchi ambazo zinafanya biashara na nchi za Umoja wa Ulaya. Hali hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa Viongozi katika baadhi ya nchi hizo kama vile; Ufaransa, Ugiriki, Italia, Hispania na Ireland kushindwa katika Chaguzi Kuu au kushinikizwa kujiuzulu. Kwa upande wa Marekani nayo ilikumbwa na misukosuko ya uchumi iliyosababishwa pia na mdororo wa uchumi wa mwaka 2008. Hata hivyo, uchumi wake umeanza kutengemaa baada ya mdororo huo.

14.       Mheshimiwa Spika, kutokana na mdororo huo, nchi hizo zimelazimika kuchukua hatua kadhaa kunusuru uchumi wao ikiwa ni pamoja na kubana matumizi, kukopa zaidi ili kuwekeza katika sekta zenye kutoa ajira na kupunguza kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kulingana na ahadi zao za awali. Kuna kila kiashiria kuwa uchumi wa Ulaya na Marekani hautapata utulivu kwa muda mrefu na hivyo uwezo wao wa kutoa misaada kupungua kadiri siku zinavyokwenda. Wizara na Balozi zetu za nje zinaendelea kufuatilia kwa makini hali ya uchumi inavyoendelea duniani na kuishauri Serikali kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na hali hiyo ili kuimarisha uchumi wa Taifa letu na kuondokana na utegemezi.

ASIA

 

Mashariki ya Kati


15.       Mheshimiwa Spika, eneo la Mashariki ya Kati bado liko katika hali ya tahadhari. Nchini Syria hali imeendelea kuwa tete kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo ambako waasi wanapigana dhidi ya Serikali ya Rais Bashar al – Assad tangu Januari mwaka 2011 na tayari wameshaingia kwenye Mji Mkuu wa Nchi hiyo. Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) zikiongozwa na Msuluhishi wa Mgogoro huo, Dkt. Kofi Annan wameshindwa hadi sasa kufanikisha kusitishwa kwa mapigano. Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limegawanyika ambapo wajumbe wa kudumu wenye kura ya turufu wametofautiana juu ya uamuzi wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Serikali ya Syria. Tanzania inaunga mkono jitihada za Msuluhishi Kofi Annan na kuwaomba wadau wote kutoingilia na kushinikiza matakwa yao nchini Syria na badala yake kumuunga mkono Msuluhishi ili kumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani.

16.       Mheshimiwa Spika, aidha, kuendelea kukua kwa uhasama baina ya Iran na nchi za Magharibi kunaleta changamoto ya ustawi wa amani katika ukanda huo. Uhasama huo unaletwa na hofu kuwa nchi ya Iran inarutubisha madini ya urani yanayotumika kutengeneza silaha za nyuklia. Tayari, Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani ikishirikiana na nchi za Umoja wa Ulaya. Iran nayo imetishia kujibu mapigo kwa kufunga mlango wa Bahari ya Hormuz ambao hupitisha asilimia ishirini 20 ya mafuta yote ulimwenguni. Iwapo Iran itatekeleza uamuzi huo inaweza kuzusha vita ambayo italeta madhara makubwa kwa uchumi wa dunia. Hali hii ya mtafaruku baina ya Iran na nchi za Magharibi inaathiri pia mustakabali wa ukanda mzima wa Mashariki ya Kati kwa kuwa Iran ina ushawishi mkubwa kwenye siasa za nchi nyingine zenye machafuko kama vile Syria. Kuendelea kwa migogoro na machafuko katika ukanda wa Mashariki ya Kati kunaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia kwa sababu asilimia kubwa ya mafuta yanayotumika duniani hutoka katika ukanda huo. Pamoja na changamoto hizo, habari njema ni kwamba tayari Irani, Marekani, Nchi za Ulaya pamoja na wadau wengine wameshakubaliana kurejea kwenye meza ya mazungumzo na tayari mzunguko wa kwanza wa mazungumzo haya umeshafanyika. Imani yetu kama nchi ni kwamba wahusika wote kwenye mazungumzo hayo wataonesha utashi wa kweli wa kumaliza tatizo hilo kwa njia ya mazungumzo na si vinginevyo.

Mashariki ya Mbali


17.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mashariki ya Mbali hali ni tulivu ukiachilia majanga ya asili yaliyozikumba nchi za Japan, Ufilipino na Thailand na kusababisha athari za kijamii na kiuchumi kwa baadhi ya sekta, hususan viwanda na makazi ya watu. Hali ya kiusalama katika Peninsula ya Korea nayo imeonekana kutulia kidogo kufuatia mabadiliko ya uongozi nchini Korea Kaskazini baada ya kifo cha Rais Kim Jong-il aliyekuwa Rais wa Korea Kaskazini. Aidha, kwa upande wa Japan, hali ya kiuchumi imeanza kuimarika hasa baada ya kukumbwa na tukio la Tsunami la mwaka 2011 lililoathiri kwa kiasi kikubwa kinu cha nyuklia cha Fukushima.

AFRIKA


18.       Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwenye maeneo mengine duniani, Bara la Afrika nalo limeathiriwa na hali ya mitikisiko ya aina mbalimbali duniani, ikiwemo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Maendeleo ya Bara hili yameendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama, kisiasa, kiuchumi, kijamii, mabadiliko ya tabianchi, vitisho vya ugaidi, uharamia wa baharini, kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu kama vile chakula, matatizo ya nishati ya umeme na kukosekana kwa ajira. Pamoja na masuala hayo ya jumla, yapo baadhi ya masuala ambayo yanaweza yakaipambanua hali ya Barani Afrika kwa sasa, hasa katika kipindi hiki cha miezi sita iliyopita. Aidha, kuna masuala yanayozigusa baadhi ya nchi kama inavyoelezwa hapa chini:

Uchaguzi wa Uongozi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika


19.       Mheshimiwa Spika, suala kubwa lililotawala hali ya kidiplomasia Barani Afrika ndani ya mwaka wa fedha 2011/2012 ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Kama itakavyokumbukwa, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwezi Januari, 2012 wakati wa Mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika wa Wakuu wa Nchi na Serikali. Ushindani mkali ulizuka kati ya wagombea wawili waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Bw. Jean Ping wa Gabon, Mwenyekiti wa Kamisheni aliyemaliza muda wake na Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini. Mvutano huo ulisababisha Wakuu wa Nchi kushindwa kumchagua Mwenyekiti mpya wa Kamisheni hiyo baada ya wagombea wote wawili kushindwa kufikia theluthi mbili za kura zinazohitajika kisheria.

20.       Mheshimiwa Spika, kutokana na kukosekana mshindi, Wakuu wa Nchi na Serikali waliamua kuahirisha uchaguzi huo hadi kwenye mkutano wao wa 19 uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, mwezi Julai 2012. Katika uchaguzi huo, Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini, alifanikiwa kuibuka mshindi. Hivyo, Mama Zuma anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Kamisheni hiyo. Ushindi wa Bi. Nkosazana Zuma ni ushindi wetu pia kwa kuwa alikuwa ni mgombea wa SADC na Tanzania ilishiriki kikamilifu katika kampeni zake.

Misri


21.       Mheshimiwa Spika, hali ya kisiasa nchini Misri ilishuhudia matokeo ya machafuko yaliyopelekea kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Hosni Mubarak. Baada ya utawala wa Mpito ulioongozwa na Jeshi la nchi hiyo, hatimaye Chama chenye mlengo wa kushoto cha Udugu wa Kiislam (Muslim Brotherhood) kimefanikiwa kushinda uchaguzi huru uliofanyika Juni, 2012 kupitia mgombea wake Mheshmiwa Dkt. Mohammed Mursi. Wizara yangu itashirikiana na Serikali mpya na kuendeleza mahusiano mazuri baina ya nchi zetu mbili ikizingatiwa kuwa Misri ni mdau muhimu katika kufanikisha matumizi ya rasilimali za Bonde la Mto Nile kwa maslahi ya pande zote husika.

22.       Mheshimiwa Spika, ni vyema kutambua kuwa ingawa uchaguzi umefanyika bado hali ya kisiasa ni tete.  Hii ni kwa sababu licha ya kuwa Muslim Brotherhood wameshinda kwa kuwa na Wabunge wengi Bungeni na kushika Ikulu, bado Jeshi la Misri linaendelea kushika hatamu za uongozi.  Jeshi limevunja Bunge na ndilo linalofanya maamuzi makubwa.

23.       Mheshimiwa Spika, ni matumaini yetu kwamba hali hiyo tete ya kisiasa itatengemaa na hali kuwa nzuri. Tanzania itashirikiana na Serikali mpya ya Misri ili kuendeleza na kudumisha mahusiano yetu ya kirafiki na ya kihistoria.

Libya


24.       Mheshimiwa Spika, baada ya aliyekuwa Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Qaddafi kuuawa na Serikali yake kupinduliwa na wapinzani wa NTC, Libya ilikumbwa na matatizo ya usalama.  Mauaji ya Walibya weusi yaliendelea.  Hakukuwa na Serikali madhubuti, hakukuwa na Bunge na wala hakukuwa na taasisi za Kidemokrasia.

25.       Mheshimiwa Spika, Tanzania tulilaani mauaji ya Kiongozi huyo na tulisema kuwa tungalitambua Serikali ya NTC tu iwapo ingalikuwa na viongozi wa kuchaguliwa, Bunge, Mahakama na uundwaji wa Serikali ya mpito ambayo itajumuisha wadau kutoka vyama vyote vya siasa.

26.       Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa kwanza wa Kidemokrasia ulifanyika Libya mwezi Julai, 2012 kuchagua Wabunge 200.  Waombaji 3,000 walijitokeza kugombea nafasi hizo.  Pamoja na matatizo yote ya kiusalama, wananchi milioni moja na laki nane waliweza kuchagua Wabunge wao 200 na Bunge linategemewa kumchagua Rais na Waziri Mkuu katika kipindi cha siku 30 baada ya uchaguzi.  Zoezi hilo limekamilika. Aidha, Bunge limechagua kutoka miongoni mwao Wabunge 60 wa kuunda Baraza la kuandika Katiba mpya, na Baraza hilo limepewa siku 120 kuwakilisha mapendekezo ya Katiba kwenye Bunge lao. Mchakato huo umeanza.

27.       Mheshimiwa Spika, uongozi wa Serikali ya Libya umekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kikwete mjini Addis Ababa tarehe 15 Julai, 2012 na ukaeleza nia yake ya kutuma ujumbe Tanzania kuja kutoa taarifa ya hali ya usalama na kisiasa na kufufua rasmi mahusiano ya Kibalozi na Tanzania.  Tunausubiri ujumbe huo na sisi sasa tumeridhika na mchakato wa kujenga demokrasia unaoendelea nchini Libya.  Tanategemea kuletewa hati za Balozi mpya hivi karibuni na tutazipokea ili tuweze kurejesha huduma za Kibalozi kama ilivyokuwa mwanzo.

Somalia


28.       Mheshimiwa Spika, hali ya kisiasa na kiusalama nchini Somalia kwa sasa inatia matumaini ya kupatikana kwa amani kutokana na juhudi za Umoja wa Afrika pamoja na washirika wake katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa muda mrefu wa nchi hiyo. Serikali ya Mpito ya Somalia inatarajiwa kumaliza muda wake mwezi huu Agosti, 2012 na tayari rasimu ya Katiba kwa ajili ya Serikali mpya imeandaliwa na inatarajiwa kupitiwa na Baraza la Katiba linalojumuisha Wazee kutoka Koo zote tarehe 20 Agosti 2012. Kupatikana kwa Serikali mpya ambayo uhalali wake utatokana na wananchi wenyewe inatazamiwa kutoa fursa kwa Wasomali kujenga mustakabali mpya wa taifa lao.

29.       Mheshimiwa Spika, hali ya usalama katika mji wa Mogadishu sasa ni ya kuridhisha kutokana na jitihada za majeshi ya AMISOM na yale ya Kenya kudhibiti maeneo na miji muhimu iliyokuwa ngome ya Al-Shabaab. Pamoja na kuwa wamedhibitiwa, Al-Shabaab wameendelea kufanya matukio machache nchini Kenya ikiwa ni njia ya kulipiza kisasi. Hali hiyo imeleta hofu kwa watalii na wageni kutoka nje wanaotembelea ukanda wa Afrika Mashariki. Serikali zetu zinashirikiana kwa karibu katika kuimarisha usalama dhidi ya vitendo vya uharamia vya Al-Shabaab. Vivyo hivyo, hali ya usalama katika pwani ya Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden nayo inazidi kuimarika na matukio ya uharamia kupungua kutokana na operesheni inayoendelea kati ya nchi za pwani ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya. Katika mwaka 2011/12 peke yake, Jeshi la Wananchi liliweza kudhibiti matukio 27 ya uharamia. Tuungane kulipongeza jeshi letu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda mipaka ya nchi yetu. Tunachukua jitihada za makusudi kulisaidia jeshi letu kupata vifaa madhubuti kwa ajili ya ulinzi wa pwani yetu ambayo ina utajiri mkubwa wa gesi asilia dhidi ya maharamia hawa.

Ukanda wa Maziwa Makuu


30.       Mheshimiwa Spika, hali ya usalama mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ukanda wa Maziwa Makuu kwa ujumla nayo iko tete hata baada ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulimalizika na Rais Joseph Kabila kutangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake mkuu Bw. Etienne Tshisekedi.  Mapigano yameripotiwa kutokea hivi karibuni tarehe 6 Julai, 2012 Kaskazini Mashariki mwa DRC. Kikundi cha waasi kijulikanacho kama M23 kinachosemekana kinaongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda anayesakwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita kujibu tuhuma mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kinadaiwa kuhusika na mapigano hayo. Kikundi hicho kinasadikiwa kuyateka na kuyadhibiti baadhi ya maeneo ya Mashariki ya DRC yakiwemo Rutshuru, Bunagana na Kivu. Majeshi ya Umoja wa Mataifa yameingilia kati kwa kutoa ulinzi katika mji wa Goma, na tarehe 25 Julai, 2012 yalilazimika kutumia silaha kuwasambaratisha M23 kutoka kwenye maeneo wanayoyashikilia.
             
31.       Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, katika kikao chao tarehe 14 Julai, 2012 waliuomba Umoja wa Mataifa kuongeza wanajeshi wa kulinda amani kwa lengo la kudhibiti usalama wa mpaka kati ya DRC na Rwanda ili kurejesha hali ya kuaminiana baina ya nchi hizi mbili. Vilevile, walikubaliana kufufua mpango wa usuluhishi uliokuwa chini ya Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania na Mheshimiwa Olesegum Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria. Serikali ya Tanzania inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa na kiusalama nchini DRC kwa kuwa machafuko hayo yanatuathiri kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama. Ni kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete anahudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu utakaofanyika Kampala nchini Uganda kesho tarehe 7 Agosti, 2012.



MASUALA YA USHIRIKIANO WA KIKANDA

32.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara imetekeleza jukumu la uratibu wa masuala ya ushirikiano wa kikanda kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IOR-ARC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Kwa kuwa eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki limeelezewa vizuri na Waziri husika kwenye hotuba ya bajeti yake, niruhusu nidurusu masuala machache  yafuatayo:

Uenyekiti wa Tanzania katika Kamati ya Utatu ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC


33.       Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Agosti, 2011 Tanzania iliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.  Kutokana na uteuzi huo, Tanzania imeingia katika Kamati hiyo ya Utatu (Troika) ambayo kwa sasa inaongozwa na nchi ya Afrika Kusini. Ifikapo tarehe 17  Agosti,  2012 Tanzania itatwaa rasmi  Uenyekiti wa Asasi hiyo muhimu ya SADC ambayo itaipa jukumu la kusimamia, kufuatilia na kushiriki kwa kina katika masuala yote ya siasa, ulinzi na usalama ya Nchi za SADC, hususan katika nchi za Madagascar na Zimbabwe ambazo ziko kwenye agenda ya SADC Troika kwa sasa.


UTEKELEZAJI WA SERA YA DIPLOMASIA YA UCHUMI NA MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO 2011/2012 – 2015/2016


34.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kupata mgao kidogo sana wa bajeti isiyokidhi mahitaji katika mwaka wa fedha 2011/2012. Katika kipindi tajwa, Wizara yangu ilipata asilimia 44 tu ya Bajeti iliyoombwa.  Bajeti ndogo tunayopewa imekuwa changamoto kubwa katika kutekeleza  Diplomasia ya Uchumi kwa kiwango kinachostahiki. Hata hivyo, pamoja na mapungufu hayo, Wizara yangu kwa nafasi yake kama kiungo muhimu cha nchi yetu na nchi za nje imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na sekta binafsi kuhakikisha kwamba nchi yetu inafaidika kwa kadri iwezekanavyo na fursa mbalimbali zenye manufaa kwa nchi yetu katika sekta za uchumi na jamii. Juhudi zetu katika kutafuta fursa hizo zilizingatia vipaumbele katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 - 2015/16.  Niruhusu nitumie fursa hii kueleza kwa uchache mchango wa Wizara yangu kwenye sekta mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Sekta ya Nishati na Madini


35.   Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya nishati, Wizara yangu kupitia Ubalozi wetu nchini China imeshirikiana bega kwa bega na Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba  nchi yetu inapata mkopo wa Dola za Marekani bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam. Kama ilivyokwishaelezwa na Waziri wa Fedha hapa Bungeni, tayari mkataba wa kupata fedha hizo umekwisainiwa na Mheshimiwa Philip Marmo, Balozi wetu nchini China kwa niaba ya Serikali. Uzinduzi wa ujenzi wa Bomba hilo ulifanyika tarehe 21 Julai, 2012 Mkoani Mtwara. Ujenzi wa bomba hilo utaleta mapinduzi makubwa sana katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi. Bomba la zamani lilikuwa dogo na lisilokidhi mahitaji ya kusafirisha kiasi kikubwa cha gesi kwenda Dar es Salaam. Pindi ujenzi wa bomba hilo utakapokamilika fursa nyingi za uchumi zitafunguka na kuimarika hasa zile zote zinazotumia gesi.

36.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia ilikuwa mstari wa mbele katika kuishawishi Tume ya Uhifadhi Duniani (World Heritage Commission-WHC) na jumuiya ya kimataifa kukubali kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Selous ili kuruhusu uchimbaji wa madini ya urani kufanyika kusini mwa hifadhi hiyo.  Juhudi zetu zimezaa matunda ambapo mwezi Juni, 2012 WHC wameridhia hoja zetu, jambo ambalo huwa si rahisi kufanywa na Tume hiyo. Ushindi huu ni kielelezo cha nguvu ya ushawishi wetu na kuaminika kwetu duniani. Matarajio yetu ni kwamba Kampuni ya Uranium One kutoka Urusi itaanza kazi ya utafiti na hatimaye uchimbaji muda si mrefu mara baada ya kukamilisha taratibu zingine na Wizara husika za Maliasili na Utalii na Wizara ya Nishati na Madini.

37.       Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hofu za msingi juu ya usalama wa uchimbaji wa madini hayo, Wizara yangu imetoa pia msukumo katika upatikanaji wa wataalam na mafunzo na hivi karibuni Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini imekwenda Nchini Australia na Namibia kujifunza namna ya kuendesha miradi ya urani. Tanzania itatumia nafasi yake ya Ujumbe wa Bodi ya Shirika la Atomiki Duniani (IAEA) kupata kila aina ya utaalamu na uzoefu kuhakikisha kuwa uchimbaji wa madini hayo unafuata taratibu na viwango vya kiusalama vinavyotolewa na IAEA.

38.       Mheshimiwa Spika, jitihada za Wizara yangu kuufufua mradi wa umeme wa Stieglers Gorge nazo zinaanza kuzaa matumaini. Kufuatia jitihada za Wizara yangu, Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu walifanya Ziara nchini Brazil ambapo agenda ya mradi wa Stieglers Gorge ilipewa kipaumbele kikuu. Kutokana na ziara hizo, Kampuni ya Brazil ya ODEBRECHT na Shirika la RUBADA kwa upande wa Tanzania wameshasaini Makubaliano ya Awali (MoU) kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme ambao unakadiriwa utazalisha zaidi ya megawati 2,100 za umeme wa uhakika na wa bei nafuu. Wizara yangu itaendelea kufuatilia ili kuhakikisha Wataalam wanaotakiwa kuja tena nchini kwa ajili kufanya mapitio ya taarifa ya environmental impact assessment (EIA) na upembuzi yakinifu wanafanya hivyo ili mradi huo uweze kuanza mara moja.

 

Sekta ya Kilimo


39.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya kilimo, Wizara yangu imeshirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika kufanikisha upatikanaji wa teknolojia ya umwagiliaji kutoka nchini India chini ya makubaliano ya Mpango wa Maendeleo wa India-Afrika. Makubaliano mahsusi haya ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili yanayotokana na ziara ya Rais wa India hapa nchini mapema mwezi Februari 2012. Vilevile, Wizara yangu ilishiriki na kushuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Awali kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Jain Irrigation ya India mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kutekeleza kwa pamoja miradi ya umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Wizara yangu pia imeendelea kuishawishi Serikali ya India kutupatia mkopo kwa ajili ya awamu ya pili ya mradi wa Matrekta. Matumaini yetu ni kwamba juhudi hizo zitazaa matunda katika mwaka huu wa fedha.

40.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeshiriki katika kufanikisha ushiriki wa nchi yetu katika Mkutano wa nchi Tajiri na zenye Viwanda vikubwa duniani zinazojulikana kama G8 uliyofanyika nchini Marekani. Mkutano huo ulikuwa na mafanikio makubwa kwa sekta ya kilimo nchini baada ya mataifa hayo kutoa ahadi ya Dola za Marekani milioni 890. Aidha, makampuni binafsi ya nchi hizo yaliahidi kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 3 katika sekta ya kilimo. Katika mwaka huu wa fedha, Wizara yangu itaelekeza nguvu zake kuvutia wawekezaji kutoka nchi za Japan, Korea Kusini na China kuwekeza katika Ukanda wa Kusini wa SAGCOT na vilevile kuanzisha kanda nyinginezo za kilimo magharibi, kaskazini na mashariki mwa nchi yetu.   
  

Sekta ya Miundombinu


41.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Miundombinu, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi katika kutafuta misaada na mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara yangu kupitia Ubalozi wetu Japan, iliweza kuishawishi Serikali ya Japan kugharamia upanuzi  wa barabara ya Gerezani na Mwenge-Morocco. Hivi sasa tunaendelea na juhudi za kuwashawishi ndugu zetu wa Japan watusaidie kujenga barabara za juu (Flyovers) maeneo ya Tazara. Wameonesha utayari wao kutusaidia. Vilevile, Wizara yangu inaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kupata wawekezaji wa ujenzi wa barabara ya njia sita ya kutoka Ubungo hadi Chalinze chini ya mpango wa ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma (PPP). Matumaini yetu ni kwamba ujenzi wa barabara hizi utasaidia kupunguza tatizo sugu la msongamano wa magari jijini, Dar es Salaam na yale yanayokwenda mikoani  na nje ya nchi na hatimaye kupunguza madhara ya kiuchumi yatokanayo na msongamano mkubwa wa magari.

Sekta ya Maji


42.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya maji, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Wizara ya Fedha tumeweza kuishawishi Serikali ya India kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni 178.25 kwa ajili ya mradi  mkubwa wa maji katika miji ya Dar es salaam na Pwani. Hivi sasa mchakato wa kupata fedha hizo umefikia hatua za mwisho na bila shaka inatarajiwa mapema mwezi ujao Mkataba utasainiwa na utekelezaji wa mradi huo kuanza. Vilevile, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ujenzi, Nishati na Maji za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikisha upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 50 kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Uchumi ya Korea kwa ajili ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji Zanzibar.

Sekta ya Viwanda


43.       Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na juhudi za kuchangia katika sekta ya ukuaji wa viwanda. Kilicho dhahiri ni kuwa, kwa hali ya uchumi wetu kwa sasa, viwanda vinavyohitajika haraka ni vile vya msingi ambavyo vinatumia rasilimali za ndani, vinaongeza thamani na vinatoa ajira nyingi. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka huu wa fedha tutapata wawekezaji wa viwanda vya kutengeneza nyuzi za nguo kutoka Japan na China. Uwekezaji huu mkubwa sio tu utatengeneza ajira kwa wananchi wengi, bali pia utawahakikishia wakulima wetu wa pamba soko la uhakika kwani viwanda vyote hivi vikianza kufanya kazi, vitahitaji kiasi cha tani laki mbili za pamba. Hivi sasa nchi yetu inazalisha tani laki moja tu. Hivyo basi, ipo fursa kwa nchi yetu kuzalisha pamba kwa wingi zaidi kutokana na kuwepo kwa soko la uhakika nchini. Aidha, uko uwezekano mkubwa kwa Serikali ya Marekani kuendelea na Mpango wake wa AGOA ambapo bidhaa za nguo kutoka Afrika ikiwemo Tanzania, zitaendelea kupewa upendeleo maalum.

Sekta ya Ajira


44.       Mheshimiwa Spika, katika kuwatafutia ajira Watanzania nje, Wizara ikishirikiana na mamlaka husika za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekamilisha mchakato wa makubaliano ya kusaini mkataba wa ajira na nchi ya Qatar. Kwa sasa, Wizara yangu inatarajia kupokea ujumbe kutoka Qatar kuja hapa nchini kusaini mkataba huo ili Watanzania waweze kuchangamkia fursa hizo nyingi za ajira wakati Qatar ikijiandaa kuandaa Kombe la Dunia la mwaka 2022. Halikadhalika, jitihada za Wizara yangu katika kuvutia misaada na uwekezaji katika sekta za miundominu, zimechangia kuchochea uzalishaji wa ajira nyingi nchini. Tunatambua changamoto ya ajira bado ni kubwa lakini tunaendelea na jitihada hizi kwa kushirikiana na Sekta nyingine kadiri uwezo wetu wa kibajeti utakavyoruhusu.

 

Sekta ya Elimu


45.       Mheshimiwa Spika, mbali na kuendelea kutafuta fursa za mafunzo nje ya nchi, Wizara yangu kwa kushirikiana na Bunge lako Tukufu ilisimama kidete kupigania urejeshwaji wa fedha za ziada kiasi cha pauni za Uingereza milioni 29.5, zilizojumuisha kiasi tulicholanguliwa na kile kilichotolewa mlungula wakati wa ununuzi wa rada kutoka kampuni ya Kiingereza inayojihusisha na uuzaji wa silaha (BAE). Kama nilivyoahidi katika Bunge lako wakati wa kuwasilisha Kauli ya Serikali na baadae wakati nikiwasilisha Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2011/2012, fedha hizo zote zimerejeshwa Serikalini na sio kwenye Asasi za Kijamii. Kwa pamoja, jitihada zetu zimewezesha kuipatia sekta ya elimu shilingi bilioni 90 kama ambavyo Bunge hili limejulishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.

46.       Mheshimiwa Spika, sitakuwa nimetenda haki nisipomshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa msimamo wake thabiti na Mheshimiwa Spika kwa kuiunga mkono Serikali na kuteua Kamati ya Wabunge ambayo imefanya kazi ya kutukuka kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa Serikalini. Naomba nitambue mchango mahsusi wa Waheshimiwa Wabunge wote. Aidha, niwashukuru pia Mhe. Balozi Peter Kalaghe, timu yake na watumishi wa Wizara waliosimama kidete pamoja nasi kwenye suala hili lenye maslahi kwa taifa. Nimejifunza kuwa imo ndani yetu nguvu kubwa ya umoja pale tunapoweka kando maslahi yetu finyu ya vyama na itikadi na kusimamia maslahi mapana ya Taifa. Hii ndio Tanzania ninayoijua na kujivunia, Tanzania yenye umoja na Tanzania yenye kuthubutu. Tumeonesha uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yetu na historia itatupa tuzo njema na kulikumbuka Bunge hili kwa kazi hiyo nzuri.

MASUALA MTAMBUKA YALIYOTEKELEZWA NA WIZARA

 

Mradi wa Kiswahili kwenye Umoja wa Afrika


47.       Mheshimiwa Spika, lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika tangu mwaka 2004 katika shughuli za Umoja wa Afrika na Serikali yetu imekuwa ikigharamia wakalimani wa Kiswahili hadi mwaka 2008 ambapo Kamisheni ya Umoja wa Afrika ilichukua jukumu hilo. Serikali yetu inaendelea kushawishi nchi wanachama walau thelathini na sita ambayo ni theluthi mbili kuridhia Itifaki ya Marekebisho ya Mkataba wa Kuanzisha Umoja wa Afrika (Protocol on the Amendments to the Constitutive Act of the African Union). Kuanza kutumika kwa  Itifaki hiyo kutawezesha lugha ya Kiswahili kutumika katika shughuli za kila siku za Umoja wa Afrika.

48.       Mheshimiwa Spika, sambamba na juhudi hizo, mwezi Januari, 2012 Umoja wa Afrika umeanza kufundisha lugha ya Kiswahili katika Kituo cha kufundishia Lugha cha Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Tayari wamekwishajisajili wanafunzi 15 chini ya Wakufunzi wawili wa kujitolea kutoka Tanzania. Naomba nitambue mchango wao wa dhati na kuwapongeza kwa uzalendo wao. Mimi binafsi nilipata fursa ya kuwatembelea na kuwatia moyo mwezi Januari, 2012 wakati nikihudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa. Changamoto kubwa inayotukabili ni upatikanaji wa fedha za kuendesha Kituo hicho na walimu wa kutosha wa kufundisha. Mpango wa Serikali ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Utamaduni cha Kitanzania jijini Addis Ababa kwa lengo la kukuza utamaduni wetu na Lugha ya Kiswahili miongoni mwa jamii ya Wanadiplomasia na Watumishi wa Umoja wa Afrika. Tukifanikiwa katika hili tutakuwa tumetengeneza fursa za ajira kwa Wakufunzi wa Kiswahili pamoja na kupanua wigo wa fursa kwa Watanzania kufanya kazi katika Taasisi za Umoja wa Afrika.

Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)


49.       Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, umekamilika kwa Asilimia 95 na tunategemea kukabidhiwa mwezi Septemba 2012. Kituo hiki cha kisasa kinaweza kuhodhi Mikutano minne kwa mara moja, yenye idadi ya watu 1,600. Kituo hiki kitakuwa na huduma nyingine muhimu kama vile huduma za benki, afya, ukalimani na migahawa.  Kituo kimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri wa Watu wa China. Sanjari na Kituo hiki, pia Serikali hiyo imetoa msaada wa magari madogo na mabasi yapatayo 75 ambayo tayari yapo nchini kwa ajili ya kutoa huduma katika Kituo hicho. Kuanza kufanya kazi kwa Kituo hicho, kutachochea ajira nyingi zaidi za moja kwa moja na nyingine zinatarajiwa kutengenezwa katika sekta za huduma.

Kusimamia Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa


50.       Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia wajibu huu, Wizara imeshiriki kwenye majadiliano mbalimbali yaliyopelekea uwekaji saini Makubaliano ya Mikataba mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2011/2012 kama ifuatavyo:

1.           Mkataba wa mpaka wa Bahari kati ya Tanzania na Comoro, ambao uliosainiwa tarehe 05 Desemba, 2011 jijini Maputo – Msumbiji. Mkataba huu utahakikisha kuimarika kwa usalama wa mpaka wa Bahari baina ya nchi hizi mbili;

2.           Mkataba wa mpaka wa Bahari kati ya Tanzania na Msumbiji ambao ulisainiwa tarehe 05 Desemba, 2011 jijini Maputo – Msumbiji.  Kama ilivyo kwa Mkataba baina ya Tanzania na Visiwa vya Comoro, Mkataba huu utahakikisha usalama wa mpaka wa bahari baina ya nchi hizi mbili unaimarika;

3.           Muhtasari wa Makubaliano ya Mkutano wa Pili juu ya Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari (EEZ) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Visiwa vya Comoro  na Serikali ya Ushelisheli, uliosainiwa tarehe 07 Septemba, 2011 huko Port Louis, Mauritius. Utekelezaji wa makubaliano haya ni muhimu ili kuwezesha nchi zote husika kunufaika na ukanda wa kiuchumi wa Bahari ya Hindi;

4.         Makubaliano kati ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd (BCEG) kuhusu ujenzi wa Mount Kilimanjaro International Convention Centre ambayo yalisainiwa mwezi Agosti, 2011 mjini Arusha. Mkataba huu unatoa fursa ya kujengwa kwa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Jijini  Arusha ambao utaiingizia Serikali mapato na pia kuendelea kuitangaza Arusha na Tanzania kwa ujumla kupitia Diplomasia ya Mikutano; na mwisho

5.         Makubaliano ya Pamoja (MoU) kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na China Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC) mwezi Machi, 2012 kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Jinzao hapa nchini ili kuendeleza eneo hilo.

Mradi wa kuongeza Eneo la Bahari Nje ya Ukanda wa Kiuchumi (Exclusive Economic Zone - EEZ)


51.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa - New York, imekuwa ikiratibu na kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa kuongeza eneo la Tanzania la Bahari nje ya Ukanda wa Kiuchumi. Wizara ikishirikiana na Kamati ilioundwa kushughulikia suala hilo, imeendelea kufanya mawasiliano na Taasisi za Umoja wa Mataifa zenye jukumu la kupitia Maandiko ya Miradi kama hii ya nchi zote zilizofanikiwa kuongeza eneo la Bahari. Andiko la Mradi la Tanzania liliwasilishwa Umoja wa Mataifa mwezi Januari, 2012 na Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Aidha, mwezi Agosti, 2012 Timu ya wataalamu inatarajiwa kwenda kutetea Andiko hilo mbele ya “Commission on the Limits of the Continental Shelf” (CLCS), inayoendelea na mkutano wake ulioanza tarehe 30 Julai, 2012 na unaotarajiwa kumalizika tarehe 10 Agosti, 2012 huko New York. Wizara imeendelea kushiriki katika maandalizi ili kufanikisha utetezi unaotarajiwa.


 

Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano


52.       Mheshimiwa Spika, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs) ni nyenzo muhimu sana katika ufanikishaji wa utekelezaji wa  diplomasia ya uchumi. Ni katika Tume hizi mikataba ya msingi husainiwa ambayo huweka mazingira kwa sekta binafsi kuweza kupata unafuu na fursa katika nchi ambazo tuna Mikataba nazo. Kwa mfano, soko la tumbaku nchini China ni kubwa zaidi kuliko lile la Marekani lakini wakulima wa Tanzania wanashindwa kupenya katika soko hilo kutokana na kukosekana kwa mikataba ya aina hii baina ya nchi zetu mbili. Kutokana na ufinyu wa bajeti, tumeshindwa kutumia nyenzo hii vizuri kufungua na kufufua fursa za ushirikiano. Kwa kutambua umuhimu huo na kuzingatia ufinyu wa bajeti uliopo, tumedhamiria katika mwaka wa fedha 2012/2013 kufanya mikutano ya JPC walau na nchi tatu kwa kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 - 2015/2016.

53.       Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa, asili ya miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta nyingi nchini kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo inatokana na Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wizara ilifanikisha makubaliano kuhusu uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini. Makubaliano hayo yalifikiwa mwezi Julai, 2011  jijini Pretoria – Afrika Kusini. Lengo la Makubaliano haya ni kuzidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali hasa za uchumi.

54.       Mheshimiwa Spika, haya niliyoyataja ni maeneo machache tu ambayo Wizara yangu imeyafanya katika kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika sekta za uchumi. Yako mengine mengi ambayo tumewezesha kufanyika katika kila sekta nchini lakini kwa ufinyu wa muda siwezi kuyasema yote kwa muda nilionao.  Itoshe tu kuongelea haya machache kwa leo. Ninaliahidi Bunge lako Tukufu kwamba tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ya kwanza. Zipo fursa nyingi za ushirikiano huko nje ya nchi ambazo nchi yetu inaweza kunufaika nazo. Tumejidhatiti kunufaika na fursa zitokanazo na China-Afrika Forum (FOCAC), TICAD V, EU-Africa, EBA, AGOA, Turkey-Africa, SADC, NEPAD, Tume za Kudumu za Ushirikiano baina ya nchi yetu na mataifa mengine.  Tunachohitaji ni kuwezeshwa zaidi ili tufanye kazi hiyo kwa ufanisi zaidi.

NAFASI YA TANZANIA KATIKA JUMUIYA ZA KIMATAIFA NA KIKANDA


55.       Mheshimiwa Spika, bendera ya Tanzania imeendelea kupepea vyema katika medani za Kimataifa kutokana na uongozi mahiri wa Waasisi wa Taifa hili na uongozi uliopo kufuatia kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Watanzania katika Mashirika ya Kimataifa na Kikanda.  Wizara yangu imeendelea kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha Watanzania wengi wanajiunga na kufanya kazi kwenye Mashirika ya Kimataifa. Aidha, Tanzania imeendelea pia kugombania na kuchukuwa nafasi za uongozi kwenye mashirika mbalimbali ya Kimataifa.

56.       Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Perth, Australia mwezi Oktoba 2011. Tanzania ilichaguliwa kuingia kwenye Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Ministerial Action Group - CMAG) kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2013. CMAG ndiyo chombo chenye jukumu la kusimamia misingi, sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Madola. Kikundi Kazi hicho kinaundwa na jumla ya nchi tisa kati ya nchi 54 za Jumuiya hiyo. Kuchaguliwa kwa Tanzania kuingia kwenye Kikundi Kazi hicho kumezidi kudhihirisha imani ya Jumuiya ya Kimataifa kwa nchi yetu. Mbali na kuleta sifa kubwa kwa Taifa letu, nafasi hii inaipa nchi yetu nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya Jumuiya ya Madola na pia nafasi ya kuingiza na kusimamia maslahi yake kwenye Jumuiya hiyo.

57.       Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Dkt. Agness L. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuanzia mwezi Juni, 2012 hadi mwaka 2015. Nafasi hii ni muhimu kwani kati ya nchi 189 ambazo ni wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, nchi 37 tu ndio wanaingia kwenye Baraza Kuu la Shirika hilo. Dkt. Kijazi anakuwa ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kuteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirika hilo.

58.       Mheshimiwa Spika, Tanzania kupitia raia wake Prof. Chris Maina Peter, ilichaguliwa kwa kishindo kuwa Mjumbe kwa kipindi cha miaka mitano kwenye Kamisheni ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa katika uchaguzi wa wajumbe wa Kamisheni hiyo uliofanyika mwezi Novemba, 2011 Mjini New York, Marekani. Prof. Maina ni Mtanzania wa pili kuiwakilisha Tanzania kwenye Kamisheni hiyo, baada ya Mheshimiwa Balozi James L. Kateka ambaye alikuwa Mjumbe kwenye Kamisheni hiyo kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano (1997 - 2006). Balozi Kateka sasa ni Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Sheria za Bahari.

59.       Mheshimiwa Spika, Majaji wawili Watanzania – Jaji William Hussein Sekule na Jaji Joseph E. Chiondo Masanche nao walichaguliwa kuwa Majaji wa Mahakama inayorithi shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) katika uchaguzi uliofanyika New York, Marekani mwezi Desemba 2011.

60.       Mheshimiwa Spika, kupitia azimio namba 66/408 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwezi Novemba, 2011 lilimthibitisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Tanzania, Bw. Ludovic Utouh pamoja na Ofisi yake kuwa kwenye Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa kuanzia Julai, 2012 kwa kipindi cha miaka sita. Mafanikio haya yanatokana na umakini wa Wizara yangu kwa kufanya kampeni za uhakika hadi kufanikisha kuchaguliwa.

61.       Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Septemba, 2011 Tanzania imekuwa mjumbe katika Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kwa kipindi cha 2011/2012. Kuwemo kwenye Bodi hiyo, kunaipa nchi fursa ya kushiriki kwenye masuala nyeti na muhimu kama vile kwenye majadiliano kuhusu mipango ya nyuklia ya baadhi ya nchi. Bodi hiyo ina jukumu la kutathmini maombi ya nchi zinazoomba uanachama na kuthibitisha viwango vya usalama. Aidha, Bodi ndiyo inayomteua Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ambaye huthibitishwa na Mkutano Mkuu wa IAEA. Hii ni fursa nzuri kwa nchi yetu hasa ikizingatiwa kwamba Tanzania inayo malighafi ya urani.

62.       Mheshimiwa Spika, niruhusu nilitaarifu rasmi Bunge lako Tukufu kwamba Mtanzania mwenzetu, Dkt. Asha-Rose Migiro, amemaliza kipindi chake kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  Kwa hakika Dkt. Migiro amefanya kazi nzuri na kubwa iliyotukuka katika Umoja wa Mataifa. Ameiletea sifa nchi yetu na Bara la Afrika kwa ujumla kutokana na kumsaidia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban ki Moon. Kwa niaba ya Watanzania wote, ninamshukuru kwa kutuwakilisha vizuri na ninampongeza sana na kumkaribisha tena nyumbani ili aendelee kushirikiana na wananchi wenzake katika ujenzi wa Taifa letu. Aidha, napenda pia, kupitia Bunge lako Tukufu kumpongeza Dkt. Migiro kwa kuteuliwa tena kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Ugonjwa wa UKIMWI Barani Afrika.

63.       Mheshimiwa Spika, vile vile, nchi yetu ilijipatia sifa kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula akiwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Mkuu. Balozi Mulamula aliratibu, aliisimamia na kuongoza Jumuiya hiyo kwa mafanikio makubwa pamoja na changamoto nyingi zilizokuwepo katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Kutokana na kazi yake nzuri, ndio maana Mheshimiwa Rais amemteua sasa kuwa Msaidizi wake Mwandamizi wa Masuala ya Kidiplomasia.

MSIMAMO WA TANZANIA KATIKA MASUALA MBALIMBALI


64.       Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii duniani kote ambayo wakati mwingine yanahitaji nchi kuonesha msimamo wake kwa baadhi ya masuala hayo. Moja ya sifa kubwa ambayo Mwasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu Nyerere aliyotuachia ni kuweka misimamo kwenye misingi tunayoiamini kama Taifa.  Kutokana na hali hiyo, Tanzania kama nchi huru imeweza kuwa na misimamo yake kuhusiana na masuala hayo kama yanavyoelezewa hapa chini.

Suala la Mpaka Kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa


65.       Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la muda mrefu kati yetu na nchi jirani ya Malawi linalohusiana na mpaka kwenye Ziwa Nyasa.  Tatizo lenyewe ni kwamba Malawi wanadai kuwa Ziwa lote Kaskazini ya Msumbiji kuelekea Ruvuma na Mbeya ni mali yao kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland uliowekwa saini tarehe  1 Julai 1890.

66.       Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa upande wetu tunasema kuwa mpaka wa kweli kati yetu na Malawi unapita katikati ya Ziwa hivyo kufanya eneo lote la kaskazini mashariki ya Ziwa kati ya Latitude digree 9° na digree 11° kuwa mali ya Tanzania kwa mujibu wa Mkataba huo huo wa Heligoland (Ango-German Agreement) wa mwaka 1890 ambao ulikubali kuwa kwa vile kuna maeneo ya mpaka ambayo hayana mantiki, pande zinazohusika zikutane na kurekebisha kwa kuunda “Border Commissions”.  Aidha, tunazo ramani ambazo Waingereza wenyewe (ambao wakati huo walikuwa wakitawala Nyasaland na Tanganyika) walikubaliana kurekebisha na hivyo kusogeza mpaka katikati kama ulivyo mpaka kati ya Malawi na Msumbiji.

67.       Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo hili, mwaka 2005 Marehemu Rais Bingu wa Mutharika, alimwandikia Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa Mkapa akimtaka waunde Kamati ya kuliangalia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.  Awamu ya Nne ikaendeleza kwa kuunda Kamati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kuliangalia tatizo na kulitolea mapendekezo.  Kama zilivyokutana mwaka 2010, mwaka 2012 zilikutana tena ili kuendeleza mazungumzo ya mwaka 2010 na pia kujadili matukio ya kuonekana kwa ndege ndogo ndogo za utafiti wa mafuta na gesi kwenye Ziwa Nyasa zikitafiti hadi pwani ya Ziwa hilo upande wa Tanzania.

68.       Mheshimiwa Spika, baada ya majadiliano makubwa kati yetu na Malawi, Serikali yetu iliwataka wenzetu wa Serikali ya Malawi pamoja na kampuni za utafiti au uchimbaji kusitisha mara moja shughuli zote za utafiti hadi majadiliano yatakapokamilika.  Ni matumaini yetu kuwa wenzetu wa Malawi wametuelewa.  Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa mgogoro huu mbele ya safari kutatuliwa na Msuluhishi badala ya sisi wenyewe.

69.       Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ya mgogoro bado iko mezani kwa majadiliano. Kufuatia maelekezo ya Marais  wa pande mbili, Mawaziri wa Mambo ya Nje na wataalamu wetu wa masuala ya mipaka, ulinzi na usalama tulikutana Dar es Salaam tarehe 27 Julai, 2012 kujadili kwa kina  mgogoro na kuupatia suluhu ya kudumu.  Majadiliano yanaendelea vizuri na tumekubaliana kuwa wakati tukiendelea na mazungumzo, nchi zote zijiepushe na shughuli zozote kwenye Ziwa Nyasa ambazo zinaweza kutafsiriwa kuathiri maslahi ya nchi mojawapo. Kwa makubaliano haya, naomba niwatoe hofu wananchi wa mikoa ya Mbeya na Ruvuma kuhusu hali ya usalama mpakani mwa nchi yetu na Malawi. Chini ya uongozi wa Serikali ya CCM, wananchi wa Tanzania daima watakuwa salama dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama. Tumefanya hivyo tokea uhuru na hatutachelea kufanya vinginevyo wakati wote tukiwa madarakani. Hili limeelezewa katika Ibara ya Nane, aya ya 191 na 192 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 - 2015.

Mgogoro wa Morocco na Sahara Magharibi


70.       Mheshimiwa Spika, Tanzania ina uhusiano mkubwa na wa kihistoria na Jamhuri ya Sahara Magharibi.  Itakumbukwa kuwa nchi ya Sahara Magharibi inapakana na Morocco, Mauritania na Algeria ilikuwa ni koloni la Hispania.  Wakoloni hao waliondoka Sahara Magharibi mwaka 1975 na wakati wananchi wanajiandaa kujitawala, ghafla nchi yao ikavamiwa na nchi jirani za Mauritania na Morocco. Mauritania iliondoka na Morocco ikaendelea kuikalia Sahara Magharibi tangu wakati huo yaani 1975 hadi sasa. Wananchi wa Sahara Magharibi walianza kazi upya ya kudai uhuru wao kutoka kwa jirani yao na Mwanachama wa OAU, Morocco. Mwaka 1976 Umoja wa Afrika uliamua kuitambua Sahara Magharibi kama mwanachama wa OAU.  Morocco ikajitoa kwenye Umoja huo.  Kwa kuwa Tanzania ilikuwa ndiyo Makao Makuu ya vyama vya Ukombozi Barani Afrika, kuanzia mwaka 1963, ukombozi wa Sahara Magharibi ulikuwa ni moja ya agenda yetu kuanzia wakati huo hadi sasa.

71.       Mheshimiwa Spika, msimamo wa Tanzania kuhusu Sahara ya Magharibi, haujabadilika na upo pale pale.  Tunataka wananchi wa Sahara Magharibi waachwe waamue kupitia kura ya maoni (referundum) iwapo wanataka kujitawala (independence) wenyewe au wanataka kuwa chini ya Himaya ya utawala wa Morocco.  Huo pia ndio msimamo wa AU na Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1992.  Serikali ya Morocco imekataa kura ya maoni (referendum) na badala yake wanataka Sahara Magharibi iwe sehemu ya Himaya ya Morocco.  Wamekataa kwa sababu wanajua kuwa wakikubali kura ya maoni kufanyika, wananchi wa Sahara Magharibi watataka kujitawala.

72.       Mheshimiwa Spika, Tanzania inauomba Umoja wa Mataifa kuendelea na jitihada zake za usuluhishi na tunaitaka Serikali ya Morocco kubadilika.  Tupo tayari kuwa na mahusiano na Morocco bila ya kuathiri msimamo wetu na Sahara Magharibi.  Tunafanya hivyo kwa Israel na Palestina.

Ziara za Viongozi


73.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuratibu ziara za Viongozi wa Kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nje ya nchi. Ziara hizo zimekuwa na mafanikio na faida kubwa kwa nchi yetu, hasa katika kulinda na kuendeleza maslahi ya kitaifa ya kiuchumi na kijamii, kukuza mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbali mbali, Mashirika ya Kimataifa na Kikanda, Kampuni za Kimataifa na hata watu binafsi.

74.       Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba ziara hizo zinaendelea kuwa na tija pamoja na kupunguza gharama katika mazingira ya kiuchumi tuliyonayo, kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais, Wizara yangu imeanza kuchukua hatua mbalimbali kupunguza utegemezi wa ziara hizo pekee katika kupata mafanikio mbalimbali, hususan ya kiuchumi. Miongoni mwa mikakati hiyo ni:

1.           Kupunguza ukubwa wa ujumbe katika misafara ya Viongozi Wakuu;

2.           Kuwatumia Wawakilishi, hususan Mawaziri katika safari mbalimbali hatua ambayo inapunguza gharama kwani anaposafiri Waziri huongozana na wajumbe wachache sana;

3.           Kuelekeza nguvu katika kuziimarisha Balozi zetu ikiwa ni pamoja na kufungua Balozi Ndogo katika maeneo yenye maslahi ya kiuchumi kwa Taifa; na

4.           Kutoa kipaumbele katika kufungua Ofisi za Wawakilishi wa Heshima katika maeneo muhimu ambayo Tanzania haina Uwakilishi.

75.       Mheshimiwa Spika, katika kudumisha mahusiano na nchi nyingine, nchi yetu imeendelea kutembelewa na wageni mbalimbali katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri na Viongozi wengine wa Kimataifa. Katika diplomasia, kutembelewa na wageni ni daraja muhimu la kukuza mahusiano na pia ni kielelezo cha sera za nchi yako kukubalika na Mataifa mengine yakiwemo Mashirika ya Kimataifa.

76.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha uliopita wa 2011/2012 tulitembelewa na Marais kutoka Ivory Coast, Somalia, Uganda, Liberia na Malawi. Vilevile, tulitembelewa na Makamu wa Rais kutoka Burundi, Kenya, Zambia, Iran na Afrika ya Kusini. Wageni wengine mashuhuri waliotembelea nchini ni pamoja na Prince Charles wa Uingereza na mkewe Duchess of Cornwall Camilla Parker, Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia na  Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Donald Kaberuka na wengineo. 

77.       Mheshimiwa Spika, Tanzania imepokea idadi kubwa ya mawaziri kutoka nchi mbalimbali duniani kama vile China, Uingereza, Japan, Sweden, Finland, Afrika ya Kusini, Korea ya Kusini, Korea ya Kaskazini, Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu. Wizara inaendelea kutekeleza mwongozo unaowataka viongozi wanaofanya ziara nchini Tanzania pia kutembelea Zanzibar.

78.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka fedha wa 2011/2012, Viongozi wafuatao walitembelea Zanzibar: Mwana wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles na Mkewe Camilla; Mfalme wa Ashanti wa Ghana; Waziri wa Uingereza wa Maendeleo ya Afrika; Waziri wa Finland wa Maendeleo ya Afrika; Waziri wa Afya wa Finland; Waziri wa Afya wa Marekani; na Waziri wa Afya wa Norway.


CHANGAMOTO MBALIMBALI ZINAZOIKABILI WIZARA NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA


79.       Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali, Wizara yangu imekumbwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Changamoto hizo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na kuendelea kupungua kwa bajeti ya Wizara kila mwaka.  Aidha, kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi  ya Dola ya Marekani ambayo hutumiwa na Balozi zetu nje nako kunasababisha bajeti kuendelea kutokukidhi mahitaji. Ufinyu wa bajeti umesababisha Wizara na Balozi zetu kushindwa kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya uchumi. Kuendelea kupewa bajeti ndogo kumesababisha, pamoja na matatizo mengine, madeni makubwa, wafanyakazi kutolipwa stahili zao na uchakavu wa magari na majengo. Aidha, ufinyu wa bajeti umechangia kwa kiasi kikubwa kwa Wizara kushindwa kuwarejesha nyumbani watumishi waliomaliza muda wao Balozini na kuwapeleka wengine kutoka Makao Makuu. Kama nilivyosema hapo awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalam (NUU) imetembelea Balozi zetu mbalimbali na kujionea hali halisi. Ninaamini Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati hiyo watakuwa wasemaji wazuri wa matatizo yanayozikabili Balozi zetu kutokana na ufinyu wa bajeti.

80.       Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha changamoto hizo zinapungua, Wizara yangu imepanga kuwa na majengo ya vitega uchumi katika baadhi ya Balozi zetu ili kusaidia kuongeza mapato na kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipia pango katika maeneo hayo. Katika hatua nyingine, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhusu uwezekano wa kutumia utaratibu wa mikopo ya nyumba (Mortgage Financing) katika Balozi zetu badala ya utaratibu wa sasa ambao una gharama kubwa kwa Serikali. Vile vile, Wizara yangu katika mwaka huu wa fedha imepanga kuwasiliana na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ili kuwaomba waruhusu Balozi zetu zitumie utaratibu wa “hire and purchase” kununua vifaa mbalimbali kama vile magari ya uwakilishi na hivyo, kupunguza gharama.

81.       Mheshimiwa Spika, ninayo kila sababu ya kuwapongeza wafanyakazi wa Wizara yangu walioko Wizarani na Ubalozini kwa uvumilivu na kujitolea kwa moyo wao wote katika mazingira haya magumu. Wafanyakazi wameendelea kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu na uadilifu mkubwa sana. Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tumekuwa tukiihusisha kwa karibu kuhusu changamoto hizi na wameshuhudia hali hii kila walipopata fursa ya kutembelea Balozi zetu. Tunawashukuru kwa kuielewa hali yetu halisi na kushirikiana nasi katika kushauri namna bora ya kuondokana na changamoto hizo. Nasi tunauchukulia ushauri wao na ule wa Kambi ya Upinzani kwa umakini mkubwa sana.

UTAWALA NA MAENDELEO YA WATUMISHI WIZARANI NA KWENYE BALOZI ZETU


82.       Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteua Mabalozi – kuiwakilisha nchi yetu huko Kenya, Misri, Msumbiji, Uganda, Oman, Zambia, Italia, Ubelgiji na China. Vile vile, aliwateua Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa na Naibu wake pamoja na Wakurugenzi tisa katika Wizara yangu ambao wana hadhi ya Balozi.

83.       Mheshimiwa Spika, hadi sasa Wizara yangu ina jumla ya watumishi 430 ambapo kati yao 249 wapo Makao Makuu ya Wizara, 18 wapo ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar na 163 wapo kwenye Balozi zetu.  Kwa kipindi cha Julai, 2011 hadi Juni, 2012 jumla ya watumishi 50 walihudhuria mafunzo ndani na nje ya nchi. Kati ya hao, 17 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi 33 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi.

84.       Mheshimiwa Spika, kwa kipindi hicho hicho, jumla ya watumishi 58 walipandishwa cheo baada ya kutekeleza majukumu yao vizuri pamoja na kutimiza masharti ya Miundo ya Utumishi inayosimamia kada zao.  Vile vile, watumishi 51 walithibitishwa kazini baada ya kumaliza muda wa mwaka mmoja wa majaribio baada ya kuajiriwa, na watumishi wanne walibadilishwa vyeo baada ya kujiendeleza na kupata sifa za kada husika.

85.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeweka mkakati wa kuongeza idadi ya watumishi kutoka Zanzibar katika kada ya Maafisa Mambo ya Nje kwa kuwapatia fursa Wanafunzi 18 kutoka Tanzania Visiwani kuingia kwenye Chuo chetu cha Diplomasia. Dhamira ya Wizara ni kuona kwamba, pindi watakapomaliza na kufaulu masomo hayo waweze kuajiriwa kwenye Wizara yangu kulingana na nafasi za ajira mpya tutakazokuwa nazo.

 

TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA

         

Chuo Cha Diplomasia


86.       Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kukisaidia Chuo ili kiweze kutekeleza majukumu yake kama yalivyo kwenye nia na madhumuni ya uanzishwaji wake. Lengo ni kukiwezesha Chuo kuendelea kutoa mafunzo na kufanya utafiti katika masuala ya diplomasia, uhusiano wa kimataifa, stratejia, usuluhishi wa migogoro, ujenzi wa amani, kutoa ushauri na kuendesha mafunzo ya muda mfupi. Lengo tarajiwa ni kukifanya Chuo kuwa taasisi bingwa ya elimu ya juu na ushauri katika nyanja hizo pamoja na kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika masuala ya utekelezaji wa shughuli zake.

87.       Mheshimiwa Spika, tatizo la umiliki wa ardhi limemalizika baada ya Chuo kupatiwa Hati ya Umiliki wa eneo lake. Kwa kuwa Chuo kinaendelea kupanuka ni wazi kuwa eneo la sasa kwa Chuo haliwezi kukidhi mahitaji hayo. Hivyo,  Serikali kupitia Wizara yangu imeendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Hadi sasa eneo la ekari 1,000 limeshapatikana. Vile vile, tathmini ya kulipa fidia ya ardhi imekwishafanyika ambapo Serikali inapaswa kulipa shilingi bilioni 2.5 kwa wananchi wa eneo la Buma lililopo Wilayani Bagamoyo na Wizara inaendelea kufuatilia upatikanaji wa fedha hizo kutoka kwa mamlaka husika.

Kituo Cha Kimataifa Cha Mikutano Cha Arusha (AICC)


88.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Kituo kimeweza kukaribisha wastani wa mikutano 64 kwa mwaka.  Kati ya mikutano hii asilimia 30 ya mikutano ni ya kimataifa na asilimia 70 ni ya kitaifa. Idadi hiyo ya mikutano imeweza kuleta Arusha wageni wanaokadiriwa kufikia 44,578 kila mwaka.  Kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2011 Kituo kiliweza kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa 15 na ya kitaifa 47 iliyoingiza nchini wageni wanaokadiriwa kufikia 35,000.

89.       Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo kimeendelea kupata hati safi ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa kwa wakati kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2011. Kituo kilipata faida ghafi ya shilingi milioni mia tano thelathini na moja, elfu mia sita na tano mia tatu na ishirini (531,605,320/=) na kinaendelea kufanya shughuli zake kwa ufanisi na bila kuwa tegemezi kwa Serikali Kuu.  Katika kipindi cha mwaka 2012/2013, Kituo kimepanga kuingiza mapato ya shilingi bilioni tisa, milioni mia sita arobaini na tano, elfu mia tatu hamsini na tisa na mia saba  (9,645,359,700/=) kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato na baada ya kutoa gharama za uendeshaji, Kituo kinategemea kupata ziada ghafi ya shilingi milioni miatano ishirini na tano, elfu mia moja hamsini na tisa, mia sita sitini na nne  (525,159,664./=).

90.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kufuatilia kuhusiana na kujengwa kwa Kituo kipya cha mikutano mjini Arusha kitakachoitwa Mt. Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC).   Mradi huu ni moja ya miradi itakayofadhiliwa na Serikali ya Watu wa China kupitia benki yao ya Exim. Napenda kuipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo, Menejimenti na wafanyakazi wote wa AICC na pia kuwatakia mafanikio mema katika kazi zilizo mbele yao.

Mpango wa Kujitathmini kwa Utawala Bora

 Barani Afrika (APRM)


91.       Mheshimiwa Spika, kazi ya tathmini ya utawala bora hapa nchini imeendelea kufanyika kwa  ufanisi mkubwa. Kwa kuwa Taarifa ya tathmini iliyokuwa imetayarishwa mwaka 2009 haikufanyiwa uhakiki kama ilivyotarajiwa. taarifa hiyo ilihuishwa ili kurekebisha takwimu mbalimbali zilizokuwa zimepitwa na wakati lakini pia kuakisi mabadiliko ya kisiasa yaliyokuwa yametokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. APRM Tanzania kwa kushauriana na Sekretarieti ya Afrika Kusini na Wizara, iliandaa pia Taarifa mahsusi ya Zanzibar. Hatua hii ilitokana na maoni ya mara kwa mara ya wadau wa Zanzibar hasa Makatibu Wakuu na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa ingawa suala la APRM ni la Muungano, ingekuwa ni busara ikaandaliwa taarifa mahsusi ya Zanzibar kwa nia ya kurahisisha utekelezaji wa changamoto zitakazobainishwa. Taarifa hiyo nayo ilikamilishwa na kuwa sehemu ya Taarifa ya nchi iliyokuja kufanyiwa tathmini na uhakiki na Timu ya Wataalamu wa kutoka nchi za Afrika tarehe 2 hadi 23 Machi 2012.

92.       Mheshimiwa Spika, wataalam wa Country Review Mission wapatao 20 waliwasili nchini mwezi Machi 2012. Wakiwa nchini walikutana na Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Serikali ya Muungano,  Makamu wa Kwanza wa Rais (SMZ), Makamu wa Pili wa Rais (SMZ), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wawakilishi wa Serikali, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, Wabunge, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Jumuiya ya Wafanya Biashara, Washirika wa Maendeleo pamoja na Asasi zisizo za Kiserikali ili kupata maoni yao. Aidha, Wataalam hao, waligawanyika katika makundi mawili tofauti walitembelea mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini Pemba, Mtwara, Mbeya, Dodoma, Arusha, Kagera, Ruvuma na Kigoma.

93.       Mheshimiwa Spika, katika mikutano mbalimbali iliyofanyika masuala yafuatayo yalijitokeza ambapo pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu, maeneo mengine yaliyoonekana kuwa ni tunu na yanayopaswa kuenziwa ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, utaratibu wa kurithishana madaraka kwa amani kila baada ya uchaguzi mkuu, Muafaka wa kisiasa Zanzibar na kazi nzuri inayofanywa kwa uhuru na uwazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

94.       Mheshimiwa Spika, Tanzania inatarajia kufanyiwa tahmini kwenye Kikao cha nchi wenza zinazoshiriki katika mchakato Januari, 2013 badala ya Julai, 2012 kutokana na Timu hiyo ya APRM kutokuweza kukamilisha taarifa yao katika muda ambao ungetoa nafasi kwa Serikali yetu kutoa majibu na kuyawasilisha kwenye Kikao cha APRM cha Tathmini cha Wakuu wa Nchi kilichofanyika Julai, 2012 mjini Addis Ababa. Ninaipongeza Bodi ya Uendeshaji ya APRM kwa kazi nzuri walioifanyia nchi yetu.       

MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012


95.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Wizara yangu ilipangiwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni mia moja ishirini na tano, mia moja na mbili milioni na mia nane sabini na tano elfu (125,102,875,000/=). Kati ya fedha hizo shilingi bilioni themanini, mia sita na mbili milioni na mia nane sabini na tano elfu (80,602,875,000/=) ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni arobaini na nne na milioni mia tano (44,500,000,000/=) ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Aidha, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara (Recurrent Budget), shilingi bilioni sabini na sita, mia tatu themanini na saba milioni na mia moja themanini na saba elfu (76,387,187,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (OC) na  bilioni nne, mia mbili kumi na tano milioni na mia sita themanini na nane elfu (4,215,688,000/=) ni kwa ajili ya mishahara.

96.       Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Balozi zake ilitegemea kukusanya kiasi cha shilingi bilioni kumi na nne, mia nane sabini na mbili milioni na mia nne tisini na mbili elfu (14,872,492,000/=). Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2012 kiasi cha shilingi bilioni kumi na tatu, mia nane hamsini na tatu milioni, mia nne arobaini na tisa elfu na mia tano hamsini na tisa (13,853,449,559/=) ikiwa ni makusanyo ya maduhuli balozini na Makao Makuu. Kiasi hiki cha fedha ni sawa na asilimia 93 ya makusanyo ya fedha zote za maduhuli zilizokadiriwa kukusanywa balozini na Makao Makuu kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

97.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2012 Wizara ilikuwa imepokea kutoka HAZINA jumla ya shilingi bilioni mia moja na ishirini na tatu, milioni mia nane themanini na nne elfu mia saba sabini na nane na mia saba themanini na saba (123,884,778,787/=) ikiwa ni pungufu ya asilimia 0.97 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, Mishahara, pamoja na bajeti ya Maendeleo. Kiasi cha shilingi bilioni tisini na saba, milioni mia mbili arobaini na moja elfu mia mbili thelathini na tisa, mia saba themanini na saba (97,241,239,787/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida pamoja na Mishahara ikionyesha   ongezeko la asilimia 20.64 ya bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

98.       Mheshimiwa Spika, ongezeko hili limechangiwa na kuibuka kwa majukumu mbalimbali ya kitaifa ambayo awali hayakupangiwa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti kama vile; Ujio wa Timu ya Ukaguzi kuhusu Mpango wa Kujitathmini Wenyewe kuhusu Utawala Bora (APRM) kutoka Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Mchakato wa maandalizi pamoja na uzinduzi wa Majadiliano ya Ubia Nadhifu (Smart Partnership Dialogue), Ujumbe na ushiriki wa Tanzania katika Kikosi Kazi cha Kamati ya Mawaziri ya Jumuiya ya Madola (CommonWealth Ministerial Action Group – CMAG), Mchakato wa ujumbe wa Tanzania katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika pamoja na Ujumbe wa Tanzania katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.

99.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bajeti ya Maendeleo, Wizara hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2012 imepokea kutoka Hazina shilingi bilioni ishirini na sita, mia sita arobaini na tatu milioni na mia tano thelathini na tisa elfu (26,643,539,000/=). Kiasi hiki ni sawa na asilimia 59.87 ya bajeti yote ya Maendeleo iliyotengwa kwa Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012.  Ikumbukwe kuwa Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ilipunguzwa kwa kiasi cha shilingi 16,898,098,757/= kutokana na hali ya mapato ilivyodhihirika.


MALENGO YA WIZARA KATIKA MWAKA WA FEDHA WA 2012/2013


100.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kama yalivyoainishwa katika hotuba hii.  Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza malengo yake iliyojiwekea kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015.  Msisitizo utakuwa ushiriki wa Wizara katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016. Naomba kusisitiza na kukumbusha Wizara nyingne kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni Wizara mtambuka na hivyo inahusika na ufanikishaji wa miradi mingi inayotekelezwa na Wizara, Idara na Taasisi nyingine mbalimbali za Serikali. Kama nilivyoeleza hapo awali, Wizara yangu ina nafasi kubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

101.    Mheshimiwa Spika, kama sehemu ya kuendeleza na kuhimiza njia mbadala za kukabiliana na changamoto zinazotokana na bajeti inayoendelea kupungua kila mwaka, pamoja na mambo mengine, Wizara inatarajia kufaya mambo yafuatayo:

             i.            Kufungua Balozi Ndogo katika miji ya Uturuki, Loss Angeles (LA), California, Lubumbashi na Guangzhou; ambazo sanjari na kuendeshwa kwa gharama nafuu zinaweza kukusanya maduhuli mengi kupitia utoaji wa viza na tozo, hivyo kuongeza idadi ya watalii na kukuza biashara nje ya zile nchi tulizozoea (traditional allies) zilizoko Ulaya ambazo uchumi wake unayumba kwa sasa;

           ii.            Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPC) -Wizara inatarajia kuitisha mikutano ya Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano angalau kwenye nchi tatu kwa lengo la kuzifufua tume hizo na kupanua fursa za ushirikiano, hususan masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini;

          iii.            Watanzania Waishio Ughaibuni (Diaspora) - Nafurahi kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa kufuatia Mheshimiwa Rais kuteua Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora mapema Mei, 2012 Wizara yangu sasa ipo katika mchakato wa kuandaa Sera na Mpango wa Kitaifa kuhusu masuala ya Diaspora ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwahusisha Watanzania hao katika kuchangia maendeleo ya nchi yao. Hatua hii muhimu itasaidia kuainisha wigo wa kisera, ushiriki wa wadau na majukumu ya Wizara, Idara na Taasisi nyingine katika kufanikisha ushirikishwaji wa Watanzania waishio ughaibuni kuchangia katika maendeleo ya taifa. Ni azma ya Wizara yangu kuona kuwa mchakato huu unakamilika mapema ili kutoa mwongozo kwa wadau na kurahisisha uelewa wa pamoja kuhusu mikakati bora ya kuwatambua na kuwashirikisha diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi yao;

          iv.            Majukumu ya Kimataifa - Wizara imejipanga kutumia kikamilifu nafasi za Tanzania kimataifa katika kipindi hiki zikiwemo uenyekiti wa asasi ya SADC organ Troika na ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika kukuza taswira ya nchi yetu nje na kukuza ushirikiano          wa Tanzania na nchi zilizoendelea ambazo ndizo zinafanya vizuri kiuchumi kwa sasa;

            v.            Utatuzi wa Migogoro na Uimarishaji wa Amani - Tanzania imeendelea kuwa nchi ya kutumainiwa katika ulinzi na ujenzi amani Barani Afrika. Kumejitokeza haja kubwa ya uzoefu wetu kutakiwa na nchi nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani katika nchi zinazotoka katika migogoro. Serikali imeamua kujikita katika kutumia uzoefu wetu na sifa hii katika kupanua maslahi ya nchi yetu kwa kuitikia fursa hizo. Tunajipanga kutumia Wanadiplomasia wetu wastaafu na waliopo katika kutafuta suluhu ya migogoro. Lengo ni baadae kuanzisha taasisi ya usuluhishi wa migogoro katika Chuo chetu cha Diplomasia. Uwepo wa Taasisi hiyo nchini Tanzania itavuna mikutano mingi na hivyo kuingizia nchi fedha za kigeni, kupanua sekta ya utalii na kutoa fursa ya kujenga urafiki na kupanua maslahi yetu kwa nchi nyingi zaidi. Tutatumia fursa zetu za kuwa Mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika na Uenyekiti wa Asasi ya SADC kufanikisha azma hiyo; na

          vi.            Ulinzi wa Amani - sambamba na mkakati huo, eneo la ulinzi wa amani (peacekeeping operations) ni eneo jipya tunalotaka kulipa kipaumbele. Azma hiyo inakwenda sambamba na uanzishwaji wa Chuo cha Ulinzi wa Amani (Peacekeeping School) nchini kwa ushirikiano wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Canada. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa tayari Hati ya Awali ya Makubaliano (MoU) imesainiwa mwaka huu. Kuanza kwa Chuo hicho kutatoa fursa kwa vijana wetu kujenga uwezo wa kushiriki katika operesheni za Ulinzi wa Amani, vijana wetu wa jeshi kupata uzoefu na mbinu mpya za kivita nje ya nchi, kuwezesha Watanzania wa fani mbalimbali kupata ujuzi na utaalamu na kuweza kushiriki kwenye operesheni za AU na UN (Civilian Peacekeeping Mission) ambako kwa sasa ushiriki wetu ni mdogo kutokana na kukosa stadi za aina hii.

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2012/2013


102.     Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu kazi zilizotajwa hapo juu, Wizara yangu imepangiwa kiasi cha shilingi bilioni tisini na nane, mia tatu thelathini na tisa milioni na mia saba na saba elfu (98,339,707,000/=) kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni themanini na moja, milioni mia sita themanini na sita, mia tano na tatu elfu (81,686,503,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, shilingi bilioni kumi na sita, mia sita hamsini na tatu milioni na mia mbili na nne elfu (16,653,204,000/) ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo. Aidha, jumla ya shilingi bilioni sabini na sita, mia tano arobaini milioni na mia tano ishirini na moja elfu (76,540,521,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na  bilioni tano, mia moja arobaini na tano milioni na mia tisa themanini na mbili elfu (5,145,982,000/=) ni kwa ajili ya Mishahara.

103.     Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara; shilingi bilioni moja, mia tano arobaini na tisa milioni na mia tisa ishirini na tano elfu (1,549,925,000/=) ni kwa ajili ya mchakato wa APRM, shilingi bilioni moja, mia tano na nne milioni, mia tano sabini na nne elfu na mia nne sabini na nane (1,504,574,478/=) ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na shilingi bilioni mbili, mia tano ishirini na sita milioni, mia tisa sabini na tatu elfu na mia nne sitini na mbili (2,526,973,462/=) ni kwa ajili ya fedha za Mshahara na Matumizi ya Kawaida ya Chuo cha Diplomasia.

104.     Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara yangu, kupitia Balozi zake, inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni kumi na sita, milioni mia nane themanini na mbili elfu mia mbili thelathini na moja, mia tatu na thelathini (16,882,231,330/=) kama maduhuli ya Serikali. Kwa maana ya utekelezaji wa Bajeti, kiasi hiki cha maduhuli tayari kimehesabiwa kama sehemu ya Matumizi ya Kawaida ya Bajeti ya Wizara yangu.

105.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.