Tuesday, August 7, 2012

Rais Kikwete awasili Uganda; kujadili hali ya Usalama ya Mashariki ya Congo DR

RAIS Jakaya Kikwete yuko jijini Kampala, Uganda kuhudhuria mkutano maalumu wa wakuu wa nchi za maziwa makuu, ambao utajadili hali ya usalama katika Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Mkutano huo unatarajia kuwakutanisha Rais Joseph Kabila wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda, kuzungumzia ana kwa ana kuhusu hali halisi ya usalama katika eneo la Goma mashariki mwa DRC.

Kuitishwa kwa mkutano huo wa dharura kunatokana na shutuma za Rais Kabila na Umoja wa Mataifa kuweka bayana kuwa Rwanda imekuwa kikwazo kwa amani nchini DRC kwa kusaidia waasi wa kundi la M23.

Kundi hilo la M23 limekuwa likipambana na majeshi ya serikali ya DRC kwa muda mrefu na kwa sasa linashikilia baadhi ya maeneo katika Goma.

Hivi karibuni Rais Kabila kwa mara ya kwanza aliituhumu moja kwa moja Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa M23 wanaohatarisha amani mashariki mwa nchi yake.

Pia, aliitaka Rwanda kukoma kuingilia mambo ya ndani ya DRC na kusitisha mara moja uungaji mkono wake kwa waasi hao na kuuomba Umoja wa Afrika (AU) kuharakisha mpango wa kutuma majeshi ya kulinda amani katika eneo hilo.

Mbali na Rais Kabila, Umoja wa Mataifa ilityoa taarifa yake kuhusu hali ya usalama katika Goma na kuituhumu Rwanda kuhusika katika kusaidia waasi wa M23.

Hata hivyo, Rais Kagame amekanusha tuhuma hizo na kuiponda ripoti ya Umoja wa Mataifa kuwa haikufanyiwa utafiti wa kutosha kuhusu suala hilo.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Mwenyekiti wa Nchi za Maziwa Makuu, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ameitisha Mkutano huo ambao pamoja na mambo mengine ajenda kuu itakuwa ni kujadili changamoto ya usalama Mashariki ya Kongo ambako jeshi la serikali ya nchi hiyo linapambana na waasi wa M23 wanaoongozwa na Jenerali muasi Bosco Ntaganda.  
Mbali na kujadili usalama katika eneo la Goma, pia mkutano huo utatoa fursa kwa wakuu wa nchi wanachama kupata ripoti za masuala ya usalama.

Rais Kikwete, ambaye anachukuliwa kama kiongozi wa mfano na mwenye ushawishi mkubwa barani Afrika, aliwasili uwanja wa Ndege wa Entebe leo mchana akitokea Dodoma tayari kushiriki mkutano huo.

Mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, Rais Kikwete alipokewa na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dk. Ladislaus Komba na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.

Nahodha aliwasili mjini Kampala juzi jioni na kushiriki kikao cha awali kilichowahusisha mawaziri wa ulinzi na wale wa mambo ya nchi za nje, ambacho pia kilijadili hali ya usalama katika eneo la Goma.

 Pia, marais Kagama na Kabila ambao ndiyo wahusika wakubwa katika mkutano huo tayari wamewasili mjini hapa kushiriki mkutano huo, unatarajiwa kutoka na hali halisi ya usalama itakavyokuwa hapo baadaye kwenye eneo hilo.

Source:  FREDY MWANJALA, CHANNEL TEN

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.