Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal akihutubia Mkutano wa NAM. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akisikiliza Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa NAM mjini Tehran, nchini Iran. Pembeni yake ni Mhe. Balozi Mohamed Maharage Juma, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Falme za Nchi za Kiarabu. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Dkt. Mohammed Gharib Bilal (katikati), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania uliohudhuria Mkutano wa NAM. Wengineo ni Mhe. Mahadhi Juma Maalim (MB) (wa tano kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wa sita kushoto), Msaidizi Mwandamizi wa Rais katika masuala ya kidiplomasia, Mhe. Balozi Mohamed Maharage Juma (wa nne kulia), Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Falme za Nchi za Kiarabu, Mhe. Balozi Celestine Mushy (wa tano kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa iliyopo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Dkt. Bilal ahutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa NAM
Na Ally Kondo, Tehran
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameelezea masikitiko yake kuwa hadi kufikia wakati huu, Umoja wa Mataifa umeshindwa kutimiza lengo lake la msingi la kuhakikisha kuwa dunia inakuwa na amani ya kudumu.
Dkt. Bilal alisema maneno hayo wakati anahutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) uliofanyika Tehran, Iran tarehe 30 Agosti 2012.
Makamu wa Rais alibainisha kuwa sababu ya Umoja wa Mataifa kushindwa kutimiza lengo hilo ni kutokana na ukosefu wa utashi wa kisiasa miongoni mwa nchi wanachama wa kufanya kazi kwa pamoja hususan, katika Baraza la Usalama.
Aliendelea kueleza kuwa sababu za kushinikiza kufanya mabadiliko katika Umoja wa Mataifa zinatokana na Umoja huo kushindwa kutimiza majukumu yake ya msingi. Alisisitiza kuwa endapo kutafanyika mabadiliko, Umoja wa Mataifa utakuwa ni chombo chenye demokrasia, uwazi na uwiano mzuri wa uwakilishi, hivyo utakuwa na uwezo wa kutekeleza na kutimiza majukumu yake ya msingi.
Ili kutimiza lengo hilo, Dkt. Bilal alihimiza mabadiliko katika Umoja wa Mataifa kwa hoja kuwa yataboresha uwezo wa Umoja huo katika kukabiliana na changmoto nyingi zinazojitokeza duniani, hususan migogoro ambayo inasababisha vifo vya watu wengi, uharibifu wa mali nyingi na kuchelewesha mipango ya maendeleo ya sehemu hizo kila siku.
Aliendelea kueleza kuwa Bara la Afrika limekuwa muhanga wa muda mrefu wa migogoro na vita na kubainisha kuwa Umoja wa Afrika na Jumuiya nyingine za kikanda zinafanya kila jitihada za kukabiliana na tatizo hilo.
Makamu wa Rais aliwaeleza Wakuu wa Nchi na Serikali wa NAM kuwa nchi yake, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya amani lakini inaonja athari za migogoro inayoikumba nchi jirani. Alitaja athari hizo kuwa ni pamoja na kuhifadhi maelfu ya wakimbizi kwa muda mrefu na kutapakaa kwa silaha ndogo ndogo na nyepesi. Alifafanua kuwa ingawa idadi ya kwa sasa wakimbizi wanaohifadhiwa Tanzania imepungua lakini tatizo la uharamia na wahamiaji haramu ambalo ni matokeo ya migogoro linaongezeka.
Kutokana na Tanzania kuathirika na migogoro ya nchi jirani, imekuwa mstari wa mbele kushiriki kikamilifu katika harakati za kutafuta amani duniani ikiwa ni pamoja na: juhudi za kidiplomasia, usuluhishi na pia kutoa wanajeshi wa kulinda amani katika nchi mbalimbali duniani pamoja na misaada mingine.
Dkt. Bilal aliwahakikishia viongozi wa NAM kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi nyingine kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi na yenye kuheshimu utu wa mtu bila kujali rangi wala dini yake.
Kwa kuzingatia hayo, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kutetea watu wanaokandamizwa kabla na baada ya uhuru. Alielezea namna Tanzania ilivyotumia nguvu na mali zake kwa kuongoza harakati za ukombozi duniani hususan, katika nchi za kusini mwa Afrika kuung’oa ukoloni na ubaguzi wa rangi.
Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa msemaji wa nchi zinazokandamizwa kudhalilishwa na kutawaliwa kimabavu. Kwa msingi huo, aliweka wazi msimamo wa Tanzania kuhusu Mamlaka ya Palestina kwamba ipewe haki yake ya kujiamulia mambo yake yenyewe.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.