Tuesday, August 21, 2012

Salamu za rambi rambi kwa Rais wa Ethiopia, Mheshimiwa Girma Wolde-Giorgis.

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS


Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

          Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya leo, Jumanne, Agosti 21, 2012, amepokea kwa mshtuko mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles Zenawi, kilichotokea jana usiku nje ya nchi ambako alikuwa anatibiwa.

Kufuatia taarifa hizo, Mheshimiwa Rais Kikwete, kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, Serikali yake na kwa niaba yake mwenyewe amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Ethiopia, Mheshimiwa Girma Wolde-Giorgis. 

Katika rambirambi zake kwa Mheshimiwa Wolde-Georgis, Rais Kikwete amesema: “Tanzania imepokea kwa mshtuko mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Mheshimiwa Meles Zenawi  kilichotokea jana usiku.”

Amesema Rais Kikwete: “Kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, Serikali yangu na mimi mwenyewe, natuma salamu zangu za dhati za rambirambi kwako, kwa wananchi wa Ethiopia na kupitia kwako kwa Mheshimiwa Azeb Mesfin, mjane wa marehemu na familia nzima ya Mheshimiwa Meles Zenawi. Tupo nanyi katika msiba huu mkubwa.”

“Kwa hakika, Ethiopia imempoteza kiongozi hodari, mwana mapinduzi na mpenda maendeleo. Kwa hakika,  Afrika imempoteza kiongozi wa kutumainiwa na msemaji hodari sana wa Bara letu. Daima tutamkumbuka Waziri Mkuu Zenawi kwa msimamo wake thabiti wa kutetea maslahi ya Afrika na ustawi wa watu wake. Mimi na Tanzania tumempoteza rafiki wa kweli” amesema Rais Kikwete na kusisitiza, “hakika tutaukosa mchango wake uliojaa busara, hoja zake za kusisimua na zenye mantiki sana.”

Rais Kikwete amemaliza kwa kuwaeleza wananchi wa Ethiopia: “Tunaungana nanyi katika wakati huu mgumu wa majonzi na tunamwomba Mwenyeji Mungu awape nguvu, moyo, subira na baraka zake ili muweze kuvuka kipindi hiki. Aidha, tunaungana nanyi na familia ya Marehemu Zenawi kumwomba Mola ampe mapumziko mema Marehemu Meles Zenawi.”

Waziri Mkuu Zenawi ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 57 amekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia tokea 1995 na kabla ya hapo alikuwa Rais wa nchi hiyo kati ya 1991 na 1995.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Agosti, 2012

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.