CHECK AGAINST DELIVERY
HOTUBA YA
MHESHIMWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KWENYE KILELE CHA SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI, MEI MOSI 2013, MBEYA
Ndugu Nortiburga Maskini, Kaimu Rais wa Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania;
Mheshimiwa Gaudensia Kabaka (Mb),Waziri wa Kazi na Ajira;
Mheshimiwa Celina Kombani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Utumishi,
Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu – TAMISEMI;
Mheshimiwa Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya;
Ndugu Alexio Musindo, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi
Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki;
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi;
Dkt. Aggrey Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama
cha Waajiri Tanzania (ATE);
Waheshimiwa Mabalozi;
Mheshimiwa Jaji Regina Rweyemamu, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi;
Wenyeviti na Makatibu wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali;
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa;
Waheshimiwa Wabunge;
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi;
Mabibi na Mabwana:
Shukrani
Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema, kwa kutuwezesha kukutana hapa mjini Mbeya kwenye maadhimisho
ya Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi kwa mwaka 2013. Nakushukuru sana Ndugu Nortiburga Maskini,
Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na viongozi wenzako
kwa kunialika nije kuungana na wafanyakazi wenzangu kuadhimisha siku hii adhimu
na ya kihistoria duniani. Shukrani nyingi nazitoa kwa Mheshimiwa Abbas
Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na wananchi wa Mbeya kwa kutupokea vizuri tangu
tulipowasili. Asanteni sana kwa ukarimu
wenu.
Vile vile nawapongeza viongozi wa Mkoa huu na wa
Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) kwa maandalizi
mazuri ya sherehe hizi. Kazi ya kuandaa
sherehe kubwa kama hii sio ndogo. Wenzetu
hawa wameifanya kwa mafanikio makubwa kama sote tuliopo hapa tunavyoshuhudia. Kwa niaba ya wafanyakazi wote nchini naomba
mpokee shukrani zetu nyingi kwa kazi nzuri mliyofanya.
Umuhimu wa Siku ya Wafanyakazi Duniani
Kwa
namna ya pekee nawapongeza sana wafanyakazi kote nchini kwa kuadhimisha siku
hii. Ni siku ambayo wafanyakazi duniani
kote wanakumbushana umuhimu wa mshikamano na umoja katika kudai na kutetea
maslahi na maendeleo yao. Kwa ujumla ni
siku ambayo wafanyakazi wanaungana pamoja kutafakari mustakabali wao. Wafanyakazi wa Tanzania wanayo kila sababu ya
kuisherehekea na kuienzi siku hii adhimu.
Ni siku yao ya kufanya tathmini ya jinsi wanavyotimiza wajibu wao wa
kutoa huduma na kuzalisha mali pamoja na kutambua changamoto zinazowakabili na
kuweka mikakati ya kuzikabili.
Pongezi
kwa Wafanyakazi Bora
Ndugu Kaimu wa Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Nawapongeza wafanyakazi wote waliopewa tuzo ya kuwa
wafanyakazi bora katika sehemu zao za kazi. Hongereni sana kwa mafanikio haya. Nina
uhakika kwamba wapo wafanyakazi wengine wengi ambao wanafanya kazi kwa bidii
katika maeneo yao ya kazi lakini hawakubahatika kupata tuzo. Naomba wasikate
tamaa, waendelee kuchapa kazi. Huenda na
wao watabahatika Mei Mosi ijayo. Napenda
kutumia nafasi hii kuwakumbusha wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii, umahiri
na weledi ili kuongeza tija kwenye maeneo yao.
Mnayo nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Nawaomba muitumie vizuri nafasi hiyo.
Kauli Mbiu ya Mwaka Huu
Ndugu Wafanyakazi;
Nawapongeza sana kwa Kauli Mbiu ya sherehe za mwaka
huu isemayo “Katiba Mpya Izingatie Usawa
na Haki kwa Tabaka la Wafanyakazi”.
Ni Kauli Mbiu yenye ujumbe maridhawa ambao umekuja wakati muafaka
kabisa. Nafurahi kwamba mmekumbuka jambo
zito na lenye umuhimu wa aina yake kwa mustakabali wa wafanyakazi nchini. Mimi na wenzangu wote Serikalini tunakubaliana
na maudhui ya Kauli Mbiu hiyo. Katiba ya nchi ambayo haitajali haki za tabaka
la wafanyakazi itakuwa na upungufu mkubwa sana.
Mimi binafsi naamini kwamba mambo muhimu ya wafanyakazi yatazingatiwa
katika Katiba mpya. Ni matumaini yangu
kuwa wafanyakazi waliitumia vizuri fursa ya kutoa maoni katika hatua ya awali
ya wananchi kutoa maoni yao na ile ya taasisi kutoa maoni yao. Pia katika hatua za Mabaraza ya Katiba na
Bunge Maalum, wafanyakazi watatoa maoni ya kuendeleza haki na maslahi yao ili
yajumuishwe katika Katiba.
Hata hivyo, ni vyema mkatambua kuwa Katiba
haiwezi kubeba kila kitu kuhusu masuala ya wafanyakazi. Baadhi ya masuala yanayohusu maslahi, usawa
na haki za wafanyakazi yamefafanuliwa na yataendelea kufafanuliwa kwenye sheria
husika kwa kuzingatia maazimio ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na matakwa ya
wafanyakazi na jamii. Hakikisheni kuwa
mnatoa mapendekezo yenu kuhusu sheria zilizopo ambazo zinahitaji kuboreshwa au
mambo yanayohitaji kutungiwa sheria.
Nawahakikishia ushirikiano na msaada wangu na wa wenzangu Serikalini.
Risala ya Wafanyakazi
Ndugu Kaimu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Nimesikiliza kwa makini risala iliyowasilishwa kwa
niaba yenu na Katibu Mkuu wa TUCTA, Ndugu Nicolas Mgaya. Ni risala ambayo
imeandaliwa vizuri sana. Imejitosheleza
kwa hoja, ina ushauri mzuri pamoja na
mapendekezo ya kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi. Napenda kuwahakikishia
kuwa tumepokea kwa mikono miwili ushauri na mapendekezo hayo. Tutayafanyia kazi na tutapeana taarifa ya
maendeleo yautekelezaje wake.
Nyongeza
ya Mishahara
Ndugu Wafanyakazi;
Nawashukuru sana kwa kutambua juhudi kubwa zinazofanywa
na Serikali za kuboresha maslahi na mishahara ya wafanyakazi. Kazi hii
tunaendelea nayo kila mwaka kulingana na ongezeko la tija katika uzalishaji na ukuaji
wa uchumi. Kwa mfano, katika kipindi chetu cha uongozi, tumeongeza kima cha
chini cha mshahara kwa watumishi wa umma karibu kila mwaka. Tulikuta kima cha chini kikiwa shilingi
65,000 tumekipandisha mpaka kufikia shilingi 170,000. Katika mwaka ujao wa fedha (unaoanza Julai), tunategemea kuongeza tena mshahara na kima cha
chini cha mshahara wa wafanyakazi katika sekta ya umma.
Mambo hayo yanawezekana kutokana na mafanikio
ambayo tumeendelea kuyapata katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Tumefanikiwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato
na kudhibiti ubadhilifu wa fedha za umma.
Kwa upande wa makusanyo ya kodi kwa mfano, mapato yameongezeka kutoka
wastani wa shilingi bilioni 541 kwa
mwezi mwaka 2011/12 hadi kufikia shilingi
bilioni 637 kwa mwezi mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18. Mapato yanapoimarika kama hivi, Serikali
inakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi wake, kutekeleza miradi ya
maendeleo na wakati huo huo kuboresha
zaidi maslahi ya wafanyakazi.
Pamoja na mafanikio hayo, lakini bado hatujafikia
mahali ambapo tunaweza kuongeza mishahara kama vile ambavyo tungependa sote
tupate. Hata kwa kiwango cha sasa
ambacho sote tunakubaliana hakitoshi bado mishahara inachukua sehemu kubwa ya
mapato ya Serikali. Kwa mfano, katika
mwaka ujao wa fedha, Serikali inatarajia kutumia shilingi trilioni 4.76 kati ya shilingi trilioni
10.5 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mishahara. Kwa maana hiyo, katika bajeti ya mwaka ujao
wa fedha mishahara peke yake itachukua asilimia
44.9 ya mapato ya ndani. Lakini mishahara sio matumizi pekee ya fedha za Serikali. Kuna majukumu mengine ya kuwahudumia wananchi
na kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa sababu hiyo hatuwezi kutumia mapato yote
ya Serikali au sehemu kubwa ya mapato hayo kwa mishahara peke yake. Lazima pawe na uwiano mzuri kati ya matumizi
ya mishahara na ya huduma muhimu ambazo Serikali inawajibika kutoa katika
jamii.
Narudia kuyasema haya kuwahakikishia wafanyakazi kuwa
Serikali kushindwa kuongeza mara moja mishahara kufikia viwango ambavyo sote
tungependa iwe hakutokani na roho mbaya, dharau au kutokujali. Bado uwezo hauruhusu kufanya hayo. Inshalla muda si mrefu uwezo huo tutaufikia.
Naamini hivyo kutokana na muelekeo wa ukuaji wa uchumi na hasa kama hakutatokea
kutetereka kwa sababu yo yote ile.
Kuhusu kima cha chini cha mshahara katika sekta
binafsi, Serikali imekamilisha utafiti kama ilivyoahidi. Kinachosubiriwa ni bodi za kisekta za
mishahara kujadili mapendekezo ya viwango vipya ili vianze kutumika mwaka ujao
wa fedha.
Kima
cha Chini cha Mshahara
Ndugu Wafanyakazi;
Katika risala yenu mmezungumzia suala la kupanga
kima cha chini cha mshahara kitaifa. Utaratibu huo tulikuwa tunautumia kabla ya
kutungwa kwa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 na
Sheria ya Taasisi za Kazi Namba 7 ya mwaka 2004. Utaratibu uliopo sasa wa kupanga kima cha
chini cha mshahara kisekta una faida zake kwa wafanyakazi kwa sababu sekta zinatofautiana
kwa uwezo. Hivyo sekta zinatakiwa kulipa
mishahara kwa mujibu wa uwezo wao wa kulipa.
Lakini, kama tunaona ipo haja ya kurejea utaratibu wa zamani wa kuwa na
kima cha chini ya mshahara kitaifa, Serikali ipo tayari kujadiliana na
wafanyakazi kuhusu jambo hili. Nina
uhakika muafaka juu ya suala hili utapatikana.
Punguzo
la Kodi ya Mapato
Ndugu Wafanyakazi;
Kama mtakumbuka, suala la kupunguziwa kiwango cha
kodi ya mapato inayotozwa kwa wafanyakazi nililizungumza mwaka jana, siku ya Mei
Mosi mjini Tanga. Nilisema kuwa mfumo huo
wa kodi unazingatia kipato cha mfanyakazi ambapo kiwango cha kodi hupanda kadri
kipato cha mfanyakazi kinavyopanda. Vile
vile, nilieleza kwamba mwaka 2007, Serikali iliamua kupunguza P.A.Y.E. (Pay As
You Earn) kutoka asilimia 18.5 hadi asilimia 15 na mwaka 2010/11
ilipunguzwa tena na kufikia asilimia 14.
Katika kikao chetu tulichokutana na viongozi wa
TUCTA tarehe 27 Februari, 2013 tulijadili suala hili na kukubaliana kwamba Serikali
iendelee kulichambua zaidi ili kutoa unafuu zaidi kwa wafanyakazi kila mwanya
unapopatikana. Nafurahi kuwaarifu kuwa kazi
ya uchambuzi imekamilika na maombi yenu yamesikilizwa. Waziri wa Fedha atafafanua
vizuri zaidi katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha wiki mbili
zijazo.
Sekta
ya Hifadhi ya Jamii
Ndugu Wafanyakazi;
Nawashukuru kwa pongezi zenu kuhusu maboresho ya sekta
ya hifadhi ya jamii hapa nchini. Tumechukua hatua kama tulivyoahidi. Katika kuboresha sekta hii, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imekamilisha tathmini ya afya ya kifedha
ya mifuko yote.
Tathmini hiyo imeonesha kuwa mifuko yetu ya hifadhi
ya jamii ipo kwenye hali nzuri kifedha na ni endelevu. Kwa Mfuko wa Pensheni
kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya malipo
ya michango ya wanachama waliokuwepo kabla ya mwezi Julai 1999 mfuko ulipoanzishwa
rasmi. Kwa kuanzia, mwaka ujao wa fedha,
Serikali italipa shilingi bilioni 50
ikiwa ni sehemu ya malipo hayo. Napenda
kuwatoa hofu wanachama wa Mfuko huo kuwa mafao yao yapo salama. Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Hakuna atakayestaaafu akakosa kulipwa mafao
yake.
Vile vile Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta
ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kushirikiana na Benki Kuu wameandaa na kutoa miongozo
ya uwekezaji yenye lengo la kuiwezesha mifuko ya hifadhi ya jamii kufanya
uwekezaji ulio salama na wenye tija unaomnufaisha mwanachama na taifa kwa
ujumla. Tangu kuanza kutumika kwa miongozo hiyo Mei 2012, uwekezaji wa mifuko hiyo
umeongezeka kutoka shilingi trilioni
3.38 mpaka shilingi trilioni 4.24.
Pia mali za mifuko zimeongezeka kutoka shilingi trilioni 3.74 hadi kufikia shilingi trilioni 4.73.
Aidha, Sheria
za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nazo zimefanyiwa marekebisho ambayo yanamwezesha
mtu yeyote anayeingia kwenye ajira kwa mara ya kwanza kuchagua Mfuko wowote wa hifadhi
anaoupenda na hivyo kuondoa ukiritimba uliokuwepo. Natoa wito kwa waajiri kuheshimu uhuru huu wa
mfanyakazi na kutomchagulia Mfuko wa kujiunga nao. Marekebisho hayo pia yameweka
adhabu kali kwa Mfuko unaochelewesha kulipa mafao ya mwanachama. Vile vile, napenda kuwafahamisha kwamba ile kero
ya mwanachama kukosa au kupunjwa mafao yake kama amechangia mfuko zaidi ya
mmoja imeondolewa. Hivi sasa inawezekana
mwanachama kuhamisha mafao yake kutoka mfuko mmoja kwenda mfuko mwingine.
Ndugu Wafanyakazi;
Kuhusu vyombo vya mashauriano vilivyopo kutatua madai
ya wafanyakazi, ni vyema kutambua kuwa vimeundwa kisheria. Na, utaratibu wa majadiliano uliopo baina ya
Serikali na wafanyakazi upo kisheria. Pale unapokuwepo upande ambao haukuridhika
na uamuzi ya vyombo hivyo, utaratibu unaruhusu kukata rufaa kwenye vyombo vya
juu mpaka Mahakama Kuu ya Tanzania
Kitengo cha Kazi. Huu ndio utawala wa sheria
ambao kila mwajiri, Serikali na vyama vya wafanyakazi vinao wajibu kuuzingatia.
Pamoja na kusema hayo, tumepokea ushauri wenu wa kuitaka Serikali ichukue hatua
kuimarisha zaidi utendaji na ufanisi wa vyombo vya mashauriano. Tutafanya hivyo.
Vile vile tutaendeleza utaratibu wetu mzuri wa
mashauriano tuliouanzisha yaani ule wa mimi kukutana na viongozi wa vyama vya
wafanyakazi kujadili kero za wafanyakazi.
Sote tunakubaliana kuwa utaratibu huu ni mzuri, hivyo tuwe tunakutana angalau
mara tatu kwa mwaka. Tayari mwaka huu tumeshakutana mara mbili yaani tarehe 27 Februari,
2013 na jana tarehe 30 Aprili, 2013 tulikubaliana tutafute fursa mapema baada
ya sherehe hizi tukutane. Tutafanya
hivyo.
Madai
Sugu ya Wafanyakazi
Ndugu Wafanyakazi;
Ninayo furaha kubwa kuwaeleza kuwa Serikali inaendelea
kulipa madai ya muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa
umma. Hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2013,
watumishi 11,820 kati ya watumishi 52,039 wamelipwa malimbikizo ya
mshahara ya jumla ya shilingi bilioni 12.6.
Watumishi 27,245 wenye malimbikizo
ya jumla ya shilingi bilioni 16
watalipwa muda wowote kuanzia sasa.
Madai yao yameshahakikiwa. Aidha,
madai ya watumishi 12,974 yenye thamani
ya shilingi bilioni 12.5 yapo kwenye
hatua ya uhakiki baada ya hapo yataingizwa kwenye mfumo wa malipo.
Tunaendelea
Kuimarisha Utendaji Serikalini
Ndugu Wafanyakazi;
Tunaendelea na mikakati ya kuimarisha utendaji kazi
na uwajibikaji Serikalini ili wananchi wahudumiwe vizuri na kama
inavyostahili. Hivi karibuni tumeridhia kuanzishwa
kwa mfumo mpya wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa maeneo ya
kipaumbele ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Lengo letu ni kuboresha na kuharakisha
utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Mfumo huo unatokana na mifano mizuri inayotumika katika nchi kadhaa
duniani ambako umewaletea ufanisi mkubwa.
Kilicho chema huigwa.
Kwa hapa nchini, tutaunda chombo maalum kitachokuwa
chini ya Ofisi ya Rais kuratibu mfumo huu mpya wa ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Tumeamua kuanza na maeneo sita ambayo ni utafutaji wa mapato, kilimo, maji, elimu, nishati na uchukuzi. Ni matumaini yetu kuwa mfumo huu utakapoanza
kutumika, utendaji kazi na kasi ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali utaimarika sana katika maeneo hayo.
Vile vile tunaendelea kuimarisha taasisi zetu zenye
majukumu ya kusimamia nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma ili ziweze
kutekeleza vizuri kazi zao na kwa ufanisi zaidi. Taasisi hizo ni pamoja na
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, TAKUKURU, Tume ya Maadili
ya Viongozi na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi
ya Umma (PPRA).
Ukuzaji
wa Ajira Nchini
Ndugu Wafanyakazi;
Kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani, nchi yetu
inaendelea kukabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira ambapo waathirika wakubwa
ni vijana na wanawake. Ukosefu wa ajira hapa nchini umefikia asilimia 12. Kwa kutambua ukubwa wa tatizo, Serikali imekuwa
inachukua hatua mbalimbali kuongeza fursa za ajira nchini. Hatua
hizo ni pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili vitega uchumi viongezeke
ili ajira zongezeke. Pia tunapanua fursa
za elimu katika ngazi zote na kuhimiza mafunzo ya ujasiriamali na ufundi. Aidha, Serikali inaendelea kukuza na
kuimarisha programu za kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe.
Inatia moyo
kuona kuwa juhudi hizo zinaanza kuzaa matunda.
Kwa mfano, kati ya Julai 2012
hadi Machi, 2013 jumla ya fursa za ajira 199,578
zimepatikana. Nafasi 142,832 zilitokana na miradi ya
maendeleo na nafasi 56,746 ni katika
fani mbalimbali kwenye utumishi wa umma. Aidha, kati ya Januari na Machi 2013, jumla
ya nafasi za kazi 2,562 zimetangazwa
na sekta binafsi iliyo rasmi kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Katika mwaka
wa fedha 2013/14 Serikali itaendelea kuongeza fursa za ajira katika sekta
mbalimbali hususan kwenye elimu, afya na miradi ya maendeleo itakayotekelezwa. Kati
ya mwaka 2013/14 – 2015/16, Serikali imeandaa programu ya kukuza ajira kwa
vijana itakayowezesha kupatikana kwa fursa za ajira 600,000.
Ndugu Wafanyakazi;
Kuhusu kuwezesha vijana kujiajiri, Serikali
inaendelea kuchangia mifuko maalum ya mikopo na misaada kwa vijana na wanawake
kupitia bajeti ya Serikali. Tumeamua
kuelekeza nguvu kwa vikundi vya vijana na wanawake waliojiunga pamoja kwa lengo
la kufanya shughuli za uzalishaji mali na huduma. Kuanzia Januari hadi Machi 2013, Serikali imetambua
vikundi vya vijana wajasiriamali 502
kutoka mikoa 17 ya Tanzania bara vinavyohitaji
mitaji. Vikundi hivyo vina jumla ya wanachama 5,385 (Wanawake 2,519 na
wanaume 2,866). Kazi hii inaendelea
katika mikoa mingine iliyosalia. Hatua itakayofuata itakuwa kuwawezesha kwa mitaji
na mafunzo ili waweze kujiajiri katika shughuli mbalimbali za biashara na
uzalishaji mali. Napenda kutumia fursa
hii kuwataka vijana ambao hawajaajiriwa kujiunga katika vikundi vya ushirika
ili iwe rahisi kuwajengea uwezo wao wa kufanya shughuli za uzalishaji.
Naomba uongozi wa mikoa na wilaya nchini utenge maeneo
maalumu yatakayowezesha vijana kufanya shughuli za uzalishaji na biashara. Hii
ni pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji ili vijana
walio tayari kujiajiri katika shughuli hizo wapewe.
Pia natoa wito kwa makandarasi na taasisi za umma
na binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa fursa kwa vikundi vya
vijana. Nawapongeza sana Shirika la
Nyumba la Taifa na VETA kwa kubuni mpango ambao utawasaidia vijana 5,000 kutengeneza na kuuza matofali
kwenye miradi ya ujenzi wa nyumba za NHC.
Shirika la Nyumba la Taifa limeonesha njia, wengine nao wajitokeze
kuwasaidia vijana wanaotaka kujiajiri.
Mabilioni ya JK
Ndugu Wananchi;
Tunakamilisha
taratibu za kuwekeza fedha zaidi katika Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi
(Maarufu kwa mabilioni ya Bwana Fulani).
Tutaweka utaratibu mzuri zaidi utakaofanya mfuko kuwa endelevu na
kunufaisha zaidi walengwa. Katika miaka
mitano ya uhai wa Mfuko huu tumejifunza kasoro mbili ambazo zitarekebishwa
katika utaratibu mpya. Kwanza kwamba
waliofaidika na mpango huo hawakuandaliwa ipasavyo. Na, pili, hapakuwepo na utaratibu mzuri wa
kufuatilia na kupima matokeo yake. Kasoro
hizo zitaepukwa safari hii.
Bahati nzuri programu inayotekelezwa na Wizara ya
Kazi na Ajira kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) na Benki ya CRDB
kwa vijana waliohitimu vyuo vya elimu ya juu nchini ili waweze kujiajiri katika
sekta ya kilimo na ufugaji inatoa mwongozo mzuri wa namna bora ya kuboresha
Mfuko huo. Katika programu hii, vijana
wanaopewa mikopo, kwanza hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali kisha ndipo hupatiwa mikopo. Utaratibu huo umeonyesha mafanikio makubwa. Vijana hao wameweza kujiajiri katika shughuli
za kilimo, ufugaji na usindikaji wa chakula na mafuta. Aidha, kutokana na shughuli zao hizo
wameweza kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa watu wengine.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia mafanikio hayo, nimeyakubali maombi kwa
Serikali kuidhamini programu hii.
Nimeitaka Wizara ilete Serikalini mapendekezo hayo tuidhinishe
rasmi. Kufuatia mafanikio hayo
nimeelekeza utaratibu wa program hii utumike kwa Mifuko ya Vijana, Wanawake na ule
wa Uwezeshaji wa Wananchi.
Mikopo ya Nyumba kwa Wafanyakazi
Ndugu
Wafanyakazi;
Mwaka wa jana niliunda Kamati Maalum au kwa lugha
maarufu Kikundi Kazi kikiongozwa na Gavana wa Benki Kuu na kushirikisha Mifuko
ya Pensheni na Shirika la Nyumba la Taifa kutoa mapendekezo juu ya namna ya
kuanzisha mpango wa mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi. Lengo langu ni kutaka tutengeneze mfumo wa kuwawezesha
wafanyakazi kupata mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kununua au kujenga
nyumba.
Nimearifiwa
kuwa Kikundi Kazi kimekamilisha kazi hiyo na wako tayari kunikabidhi
mapendekezo yao. Tutayafanyia kazi kwa
wakati muafaka na tutaarifiana mpango utakuwaje. Naamini mpango huu ukifanikiwa utakuwa ni
ukombozi mkubwa kwa wafanyakazi na utaongeza ari ya kujituma.
Maendeleo
ya Mkoa wa Mbeya
Ndugu Wafanyakazi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu nina mambo mawili ya
kuzungumzia. Jambo la kwanza, ninalopenda kulizungumzia ni masuala ya
maendeleo ya Mkoa. Nafurahi kwamba ndoto
ya Kiwanja cha Ndege cha Songwe imetimia.
Bado kazi chache ambazo tutazikamilisha miezi michache ijayo. Kinachofuata sasa ni matumizi ya kiwanja
hicho. Tumejenga kiwanja hicho ili
kisaidie kuchochea ukuaji wa uchumi hasa kilimo cha maua, matunda na mboga kwa
ajili ya kuuza nchi za nje. Nimeshatoa
maelekezo kwa viongozi wenu, kilichobakia ni ninyi kujipanga na kutumia fursa
hii. Suala la maji kwa jiji la Mbeya limekamilika,
tumekata mzizi wa fitina. Nimewaomba
mhakikishe usalama wa mradi huo na mtafute vyanzo vingine vya maji siku za
usoni. Ujenzi wa barabara ya Mbeya –
Lwanjiro – Chunya – Makongorosi unaendelea na tutahakikisha hausimami. Tunajiandaa kutekeleza ahadi za barabara ya Kikusya
– Itinda - Matema Beach, Itumba – Mbambo – Tukuyu; Mpemba – Isiongole - Ileje
na Mbalizi – Mkwajuni - Chunya. Soko la Mwanjelwa linalojengwa baada ya lile la
awali kuungua limekaribia kukiamilika.
Na, soko la Uhindini litajengwa kama la Mwanjelwa na kwa udhamini wa
Serikali Kuu. Nimepokea kilio chenu kuhusu ukubwa wa Mkoa,
tutalifanyia kazi.
Amani
na Usalama wa Nchi
Ndugu Wafanyakazi;
Pili, ni suala la upendo, amani na mshikamano
miongoni mwetu. Hili ni suala ambalo
nimekuwa nikilizungumzia mara kwa mara. Napenda kuchukua nafasi hii tena
kusisitiza kwamba sisi wote tunao wajibu wa kudumisha tunu hizi tulizorithi
kutoka kwa waasisi wa taifa letu.
Tusikubali kuichezea wala kuipoteza amani tuliyonayo. Ikipotea ni vigumu kuirudisha na inaweza isirudi
na Tanzania haitakuwa tena kisiwa cha amani.
Wanasiasa, viongozi wa dini, wafanyakazi, wakulima na wananchi kwa
ujumla wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa nchi yetu inabaki kuwa nchi ya amani
na utulivu. Tuwe wepesi kuyatambua na kuyaeupuka mambo yatakayosababisha
uvunjifu wa amani, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi wa nchi hii.
Kwa upande wetu, mimi na wenzangu Serikalini tumeanza
mazungumzo na viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali kujadili namna ya
kumaliza tofauti zilizoanza kujitokeza siku za hivi karibuni. Tumepiga hatua ya kutia moyo na bado
tunaendelea mbele. Jambo linaloleta
faraja ni kwamba wote wameona tulikokuwa tunaelekea siyo kuzuri na kwamba
tufanye kila tuwezalo tuepukane nako.
Sisi Serikalini tutaendelea kuzungumza na viongozi
wa dini wa pande zote na kuwaunganisha ili kuona maelewano yanarejea kama
ilivyokuwa zamani. Watanzania tuendelee
kuishi bila kubaguana au kuchukiana kwa dini zetu. Tutaendelea kuwa macho na kuwachukulia hatua
kali za kisheria wale wote watakaobainika kuchochea vitendo vya uvunjifu wa
amani bila kujali nafasi walionazo kwenye jamii, itikadi ya sisasa na dini
waliyonayo.
Hitimisho
Ndugu Wafanyakazi;
Mwisho, napenda kurudia tena kuwahakikishia kuwa
kila jambo mlilolitaja kwenye risala yenu tutalifanyia kazi. Ni wajibu wetu
kuwasikiliza, ni wajibu wetu kushughulikia masuala yenu, na ni wajibu wetu kushirikiana
nanyi ipasavyo. Tunatambua umuhimu wa
wafanyakazi kwa maendeleo ya taifa letu.
Mimi nawaahidi ushirikiano wangu binafsi na ule wa wenzangu wote
serikalini wakati wote. Tujenge nchi
yetu kwa pamoja.
Nawashukuru tena Viongozi wa TUCTA kwa kunialika
kwenye sherehe hizi muhimu. Nawashukuru
wafanyakazi pamoja na wananchi kwa kujitoleza kwa wingi. Hongereni kwa sherehe zilizofana sana. Sasa twendeni tukafanye kazi.
Asanteni kwa
Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.