Saturday, May 25, 2013

OAU/AU IMEFANIKIWA: MEMBE





OAU/AU IMEFANIKIWA: MEMBE

Na Ally Kondo

Umoja wa Afrika (OAU/AU) umepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 25 Mei, 1963.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Umoja huo iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam tarehe 25 Mei, 2013.

Mhe. Membe alieleza kuwa, AU imefanikiwa kutimiza lengo la kuzikomboa nchi zote za Bara la Afrika isipokuwa Saharawi kutoka katika tawala za kikoloni. Alisema katika kufanikisha hilo, Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa kwani, Makao Makuu ya Ukombozi ya AU yalikuwa hapa nchini.

Kuhusu Demokrasia na Utawala Bora katika nchi za Afrika, Mhe. Waziri alisema kuwa AU imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa wanachama wake wanaheshimu utawala wa sheria kwa kuweka sheria kali za kukomesha tabia ya kuingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi. Sheria hizo ni pamoja na; nchi inayotawaliwa kijeshi kusimamishwa uanachama wa AU, kuwekewa vikwazo vya kiuchumi pamoja na Kiongozi wa Mapinduzi kutoruhusiwa kuwania nafasi ya Urais katika uchaguzi wa kidemokrasia.

Kutokana na msimamo huo, AU imefanikiwa kupunguza matukio ya mapinduzi katika nchi za Afrika tangu ilipoanzishwa. “Afrika imeshuhudia matukio ya mapinduzi matano katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ukilinganisha na matukio 34 yaliyotokea kabla ya kipindi hicho”. Mhe. Membe alisikika akisema.

Katika kukabiliana na migogoro inayozuka mara kwa mara katika nchi za Afrika, alisema kuwa, AU imebadilisha kipengele ambacho kilikuwa kinakataza nchi za Afrika kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Hivyo, kutokana na mabadiliko hayo nchi za Afrika sasa zinaweza kuingia katika nchi nyingine kulinda amani.

Kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi, Mhe. Waziri alisema kuwa hatua kubwa imefikiwa, hususan kupitia Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda, kama vile SADC, EAC na ECOWAS. Hata hivyo alibainisha kuwa, ukosefu wa miundombinu imara kama barabra na reli, kuunganisha Bara zima la Afrika ni kikwazo katika kufikia malengo ya kiuchumi kwa nchi nyingi za Afrika.

Sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Afrika (OAU/AU) zilipambwa na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasha mwenge wa AU, maandamano na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya utamaduni. Aidha, sherehe hizo zilihudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimatafa hapa nchini, wanafunzi na wananchi.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.