TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kikao cha 15 cha Kamati ya
Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi
za Kusini mwa Afrika (The SADC Ministerial Committee of the Organ on Politics,
Defence and Security Cooperation), kitafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa
Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam tarehe 10-13 Julai, 2013.
Kikao hicho kinachohusisha
sekta ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kitatanguliwa na kikao cha Makatibu
Wakuu na Maofisa Waandamizi tarehe 10 na 11 Julai, 2013 na kitahudhuriwa na
Nchi zote wanachama wa SADC isipokuwa Madagascar, ambayo imesimamishwa
uanachama.
Mawaziri watakutana tarehe 13
Julai, 2013, chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa wa Tanzania, Mheshimiwa Bernard Kamilius Membe (Mb).
Pamoja na mambo mengine, Kikao
hicho kitajadili hali ya kisiasa Kusini mwa Afrika, uimarishaji wa Demokrasia,
Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Asasi
ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Mikataba ya ushirikiano katika Nyanja za Ulinzi
na Usalama pamoja na Ushirikiano baina ya SADC na Umoja wa Ulaya (EU).
Washiriki wa vikao vya Maofisa Waandamizi wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam
tarehe 9 Julai, 2013 wakati Mawaziri watawasili tarehe 12 Julai, 2013.
Kikao hicho cha Mawaziri kitafuatiwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi, utakaofanyika
Lilongwe, Malawi, tarehe 17-18, Agosti, 2013, ambao utahitimisha Uenyekiti wa
Tanzania wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, ulioanza tangu Agosti,
2012. Mwenyekiti anayefuata wa Asasi hiyo atakuwa Namibia wakati Uwenyekiti
wa SADC utachukuliwa na Malawi.
Nchi Wanachama wa SADC ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Sheli Sheli, Afrika
Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
IMETOLEWA NA:
WIZARA
YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM
8 JULAI, 2013