Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliason akizungumza wakati wa Mkutano kuhusu DRC na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika Addis Ababa. |
Mjumbe wa Sudan akisaini Mkataba wa Kujiunga na Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano ulio chini ya ICGLR |
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bibi Mary Robinson naye pia alikuwepo katika mkutano huo. |
Wajumbe wengine kutoka nchi wanachama wa ICGLR wakifuatilia mkutano. =============================== |
Na
Mwandishi Wetu, Addis Ababa
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ametoa rai kwa
Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kuweka nia mpya ili kutimiza lengo la kupatikana
kwa amani ya kudumu katika Nchi za Ukanda huo.
Mhe. Membe aliyasema
hayo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Ngazi ya Juu kuhusu Utaratibu wa Usimamizi wa
masuala ya Amani, Usalama na Ushirikiano
katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu uliofanyika mjini Addis Ababa,
Ethiopia pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika
(AU) unaoendelea mjini hapa.
Waziri Membe alisema
kuwa kumekuwa na hatua nzuri zilizofikiwa katika kutafuta amani ya kudumu DRC na
katika Kanda kwa ujumla. Hatua hizo ni pamoja na kusambaratishwa kwa kikundi
cha Waasi cha M23 huko Mashariki mwa DRC. Hata hivyo alisema bado kunahitajika
jitihada na nia madhubuti ili kuhakikisha migogoro isiyoisha inamalizwa kabisa.
“Tunayashukuru
Majeshi ya Ulinzi ya DRC kwa msaada wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa
Mataifa (MUNOSCO) na kile cha FIB ambapo tumeshuhudia kusambaratishwa kwa
Kikundi cha M23, tunapongeza pia jitihada za Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri
Museveni ambaye pia ni msuluhishi wa mgogoro huo kufuatia kusainiwa kwa Azimio
la Amani kati ya Serikali ya DRC na M23 hapo tarehe 12 Desemba, 2013”, alisema
Mhe. Membe.
Mhe. Membe aliongeza
kuwa umefika wakati sasa kwa watu na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kusema inatosha kwa migogoro isiyoisha ili
kuwawezesha kuwekeza nguvu na vipaji vyao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, kwa namna ya
pekee, Waziri Membe alimpongeza Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa katika Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Mhe. Bibi Mary Robinson na
Kamati yake ya Ufundi (TSC) kwa kazi nzuri waliyoifanya mwaka 2013. Kamati hiyo
ya Ufundi imefanikiwa kutoa Mpango Kazi kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa
Amani, Usalama na Ushirikiano wa Kanda.
“Nimeridhishwa na kazi inayofanywa na Kamati
hiyo ya Ufundi kwa kutoa Mpango Kazi
ambao unajitosheleza kwa ajili ya kuutekeleza Mpango wa Amani. Hivyo, tumekutana hapa
kuridhia mpango huo ili kila mmoja wetu aweke nia mpya ya kutekeleza yale yote
tuliyowahi kukubaliana chini ya Mpango wa Amani” alisisitiza Waziri Membe.
Aidha, wakati wa
Mkutano huo nchi za Kenya na Sudan zilisaini rasmi Mkataba wa kujiunga na
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Kanda ya Maziwa Makuu ( Peace, Security and Cooperation Framework).
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson.
-Mwisho-