Tuesday, February 3, 2015

Rais wa Ujerumani awasili nchini kuanza ziara ya kitaifa


Rais wa Ujerumani, Mhe. Joachim Gauck pamoja na Mhe. Mama Schadt wakiteremka kwenye ndege mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza ziara ya kitaifa ya siku tano hapa nchini.
Mhe. Gauck akilakiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mohammed Gharib Bilal mara baada ya kuwasili nchini.
Mhe. Gauck na Mama Schadt wakipokea  maua kutoka kwa Watoto Elizabeth Jackson na Barqat Mvungi walioandaliwa kwa ajili ya mapokezi yake. 
Mhe. Gauck akiongozana na Mhe. Dkt. Bilal
Mhe. Gauck na Mama Schadt kwa pamoja na Mhe. Dkt. Bilal na Mkewe Mama Asha Bilal wakifurahia burudani ya ngoma wakati wa mapokezi yake.
Baadhi ya wakina mama wa Dar es Salaam waliofika kumpokea Rais Gauck wakipeperusha bendera ya Tanzania na Ujerumani kwa furaha 
Mhe. Rais Gauck akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Joseph Sokoine wakati wa mapokezi.
Mhe. Rais Gauck akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Philip Marmo wakati wa mapokezi yake.
Mhe. Gauck akifurahia jambo na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bibi Victoria Mwakasege aliyekuwepo uwanjani hapo kwa mapokezi. 
Rais Gauck akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Bw. Assah Mwambene


Picha na Reginald Philip.

Friday, January 30, 2015

Licha ya Changamoto nyingi, Bara la Afrika linapiga hatua, Zuma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Afrika Juu ya mabadiliko ya Tabia nchi,Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasilisha ripoti ya utendaji wa kamati hiyo katika mkutano wa Viongozi wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Addis Ababa Ethiopia.Mkutano huo ulimalizika jana
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Waziri Mkuu wa Sweden,Stefan Lofven jijini Addis Ababa Ethiopia jana.Tayari Rais Kikwete amerejea nchini baada ya kumaklizika mkutano wa wakuu wa nchi za umoja wa Afrika AU jijini Addis Ababa Ethiopia uliofanyika kwa siku mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akisoma makabrasha ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU unaofanyika kwa siku mbili jijini Addis Ababa kuanzia leo. Nyuma ya Mhe. Rais ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb). Waziri wa Jinsia na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Sophia Simba (Mb) na Balozi wa Tanznia nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz (mwenye ushungi).




Na Ally Kondo, Addis Ababa

Wakuu wa Nchi za Afrika wamekumbushwa kuwa, Mwaka 2015 umeingia lakini Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kama hazitapatiwa ufumbuzi ustawi wa bara hilo utaendelea kudumaa. Kauli hiyo ilikuwa inarudiwa mara kwa mara na viongozi waliopata fursa ya kuhutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa siku ya Ijumaa tarehe 30 Januari 2015.

Changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ugaidi, migogoro ya kutumia silaha, ukatili wa kutisha, biashara haramu ya binadamu, umasikini na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Walishauri katika mwaka wa 2015 lazima matatizo hayo yajadiliwe kwa kina kwa madhumuni ya kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu.

Alipokuwa anahutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Nkosazana Zuma alisema kuwa, licha ya changamoto hizo, Bara la Afrika linapiga hatua kimaendeleo na kwamba Agenda 2063 inayowasilishwa katika Mkutano huo inatoa wito kwa Serikali na sekta nyingine kushirikiana kwa pamoja ili kukuza uchumi kwa kuweka mkazo kwenye ubunifu katika sekta ya kilimo, usindikaji wa mazao na ujenzi wa miundombinu. 

Mhe. Zuma alisisitiza umuhimu wa kutumia fedha za ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya kipaumbele ambayo imezingatiwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka 10 ambao nao utawasilishwa katika mkutano huo.  Alieleza kuwa Sekretarieti imefanyia kazi pendekezo la kutafuta vyanzo mbdala vya fedha ambapo Mawaziri wa Fedha walijadili na ripoti yao itawasilishwa wakati wa mkutano huo. Umoja wa Afrika pia umeanzisha Mfuko Maalum utakaozinduliwa wakati wa mkutano huo kwa ajili ya kuhifadhi fedha hizo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-moon alieleza kuwa mwaka 2014, AU na UN zilishirikiana kutafuta amani katika nchi zenye migogoro. Alisema mafanikio makubwa yalipatikana na hivyo kusisitiza kuwa pande zilizosaini mikataba ya amani lazima zitekeleze vipengele vya mikataba hiyo. Alitoa mfano wa Mkataba wa Arusha na kusema kuwa pande zinazohusika zitekeleze makubaliano ya kugawana madaraka. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kukitokomeza kikundi cha waasi cha FDLR kinachoendesha uasi wake Mashariki mwa DRC.

Mhe. Ban Ki-moon pia aliwakemea viongozi wa Afrika wanaong’ang’ania madaraka. Aliwashauri viongozi hao waache tabia hiyo na kuruhusu demokrasia ichukue mkondo wake.

Rais wa Kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa pamoja na mambo mengine, alizungumzia mabadiliko ya mfumo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Alisema katika uongozi wake atafanya jitihada kuhakikisha kuwa mfumo wa Baraza hilo, chombo ambacho alikitaja kama kisichokuwa na demokrasia kuliko vyombo vyote duniani unafanyiwa mabadiliko.

Viongozi hao pia walihimiza juhudi za kutafuta tiba na chanjo ya ugonjwa wa Ebola na kusisitiza kuwa kampeni ifanywe ili nchi zilizoathirika na ugonjwa huo zisamehewe madeni.

Balozi Msechu awasilisha Hati za Utambulisho nchini Latvia na Lithuania


Balozi Dora Msechu akiwasilisha Hati zake za utambulisho kwa Rais wa Latvia, Mhe. Andris Berznins, Tarehe 27/01/015  
Baloz Dora Msechu akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais Andris Berznins
Balozi Dora Msechu akiwasilisha Hati zake za utambulisho kwa Rais wa Lithuania Mhe. Dalia Grybauskaite
Balozi Msechu akiwa katika picha ya pamoja na Rais Dalia Grybauskaite 

Rais Kikwete azindua majengo ya Ubalozi Paris, Ufaransa

Mhe. Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete kwneye picha ya pamoja na Waziri Bernard Membe na Balozi Begum Taj mara baada ya kuzindua majengo ya Serikali jijini Paris Ufaransa tarehe 28 Januari 2015.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imezindua majengo mawili jijini Paris, Ufaransa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mahsusi wa kumiliki majengo ya Serikali nje ya nchi.

Majengo hayo ya ofisi ya Ubalozi na makazi ya Balozi yaliyogharimu Serikali Euro milioni 22, yalizinduliwa rasmi na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Wanadiplomasia na Watanzania jijini Paris tarehe 28 Januari 2015.

Uzinduzi wa majengo hayo yenye ukubwa wa ghorofa nne kila moja na sehemu ya chini ya ardhi ya maegesho ya magari ni mafanikio ya Sera ya Mambo ya Nje ambapo kupitia mkakati wake wa miaka 15 wa kumiliki majengo nje ya nchi, umefanikisha mchakato wa manunuzi ulioanza mwaka 2012.

“Niwapongeze Wizara ya Mambo ya Nje kwa kufanikisha zoezi la ununuzi wa majengo haya kutoka Serikali ya New Zealand ambao ni marafiki zetu wa kweli wa maendeleo na niwashukuru kwa kutuvumilia wakati wote huu” alisema Rais Kikwete.

Akimkaribisha Rais kutoa hotuba yake, Mhe. Bernard Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje alisema umiliki wa majengo hayo ya Serikali jijini Paris ni uthibitisho wa ukomavu wa diplomasia ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Mheshimiwa Rais, ulituagiza kununua majengo jijini Washington D.C., tulifanya hivyo, jijini New York, tulifanya hivyo na sasa jijini Paris, tumetekeleza. Mkakati wetu ni kukamilisha maeneo ya kipaumbele ambapo sasa tuko mbioni kukamilisha mchakato wa kujenga kitega uchumi jijini Nairobi na Maputo” alisisitiza Waziri Membe.

Mkakati wa miaka 15 wa kumiliki majengo ya Serikali nje ya nchi unapata nguvu kutoka kwenye Sera ya Mambo ya Nje yenye muelekeo wa uchumi uliobuniwa mwaka 2002/03 japo utekelezaji wake ulianza rasmi mwaka 2007/08 baada ya Serikali kuanza kutenga fedha za miradi ya maendeleo kwa Wizara ya Mambo ya Nje.

Licha ya ununuzi wa majengo, mkakati huu pia unahusisha ujenzi na ukarabati wa majengo ya ofisi, nyumba za watumishi wa Serikali na kuendeleza viwanja vinavyomilikiwa na Serikali kwenye maeneo ya uwakilishi.

“Ununuzi wa majengo haya ni mafanikio makubwa. Sio tu imepunguzia Serikali mzigo wa kodi, lakini imetuwekea heshima kubwa hapa Ufaransa sisi kama nchi. Kama mjuavyo Ufaransa pia ni mojawapo ya Super Power (mataifa yenye nguvu), ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hivyo Tanzania kumiliki majengo ya kudumu jijini Paris ni ishara ya ukomavu wa diplomasia yetu” alihimiza Mhe. Taj Begum, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.


Hivi sasa Serikali kupitia Balozi zake nje ya nchi inamiliki majengo 97 ndani ya vituo 32 zikiwemo ofisi za ubalozi na nyumba za watumishi. Ifikapo mwaka 2017 wakati wa ukomo wa mkakati huu, namba hii itapanda zaidi hususan kwenye upande wa ofisi za Ubalozi.

Na Mindi Kasiga,
Paris, Ufaransa
29 Januari 2015


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa majengo hayo kwenye ukumbi wa sherehe wa nyumba ya Balozi. 

Watumishi wa Serikali ubalozini Paris kabla ya sherehe za uzinduzi

Thursday, January 29, 2015

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje amwakilisha Rais Kikwete kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa NEPAD


Meza Kuu wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa NEPAD uliofanyika leo jijini Addis Ababa. Wakuu wa Nchi pamoja na mambo mengine walisomewa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya NEPAD kwa kipindi cha mwaka 2014. Kubwa lilihusu uanzishwaji wa Mpango wa Kilimo unaozingatia mabadiliko ya tabianchi ambao unawalenga wakulima wadogo zaidi ya milioni 25 watakaokuwa wanalima kwa kutumia teknolojia isiyokuwa na athari katika tabianchi ifikapo mwaka 2025.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb) alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete katika Mkutano huo
    Anayefurahia jambo ni Bibi Zulekha Tambwe, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na nyuma yake ni Bw. Adam Issara, Katibu wa Naibu Waziri.           

Prof. Mbwette Rais mpya wa Baraza la Chuo Kikuu cha Pan African




Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Tolly Mbwette amechaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afrika (Pan African University) katika uchaguzi uliofanyika jijini Addis Ababa siku ya Jumatano tarehe 28 Januari 2015. Prof. Mbwette ambaye atahudumu nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, aliwashinda wagombea wengine wanne katika kinyang’anyiro hicho. 

Aidha, Bw. Ekwabi Mujungu amechagulikuwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Afrika inayoshughulika na  mapambano dhidi ya rushwa kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Uteuzi wao unatarajiwa kuthibitishwa na Walkuu Nchi na Serikali wa AU katika mkutano wao utakaofanyika Addis Ababa tarehe 30 na 31 Januari 2015. Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atashiriki mkutano huo.

Seikali kupitia Ubalozi wake wa Addis Ababa chini ya Balozi Naimi Azizi, ulipiga kampeni kuhakikisha kuwa wagombea hao wanashinda nafasi hizo



Wednesday, January 28, 2015

Waziri Membe akagua majengo ya mapya Ubalozi wa Tanzania nchini Paris

Majengo (mawili ya katikati) ya Ubalozi wa Tanzania Paris Ufaransa kama yanavyoonekana kwa nje siku ya uzinduzi rasmi tarehe 28 Januari 2015.

Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akipata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara Bw. John Haule wakati viongozi hao wakiwa kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya uzinduzi rasmi unaotarajiwa kufanyika baadae leo na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mhe. Membe akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw. John Haule kwenye ukaguzi wa nyumba ya makazi ya balozi ikiwa ni sehemu ya majengo mawili (ofisi za ubalozi na makazi ya balozi) yatakayozinduliwa baadaye leo na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Tanzania na China kuendeleza ushirikiano katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji


Mkurugenzi wa Eneo la  Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) nchini, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia akizungumza na Bw. Li Xuhang, Naibu Mkuu wa masuala ya Siasa katika Ubalozi wa China hapa nchini kuhusu mikakati ya Serikali ya Tanzanania katika kuhamasisha uwekezaji nchini katika Maeneo Maalum na kuimarisha ushirikiano na Serikali ya China katika masuala ya uwekezaji kwenye Maeneo Maalum. Mazungumzo  yao yalifanyika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Sehemu ya Wajumbe kutoka Ubalozi wa China hapa nchini waliofuatana na Bw. Li Xuhang.
Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na EPZA wakifuatilia mazungumzo kati ya Kanali Mstaafu Simbakalia na Bw. Li Xuhang. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. Nathaniel Kaaya, Bw. Lamau Mpolo (kushoto), Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa EPZA na  Bw. Iman Njalikai (kulia), Afisa Mambo ya Nje. 
Mazungumzo yakiendelea
Kanali Mstaafu Simbakalia akiwaeleza jambo Bw. Li na Afisa kutoka Ubalozi wa China mara baada ya mazungumzo yao.

Picha na Reuben Mchome







NEPAD yasaidia harakati za kutafuta tiba na chanjo ya ugonjwa wa Ebola, Prof. Ambali

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb) kulia akiongea na mmoja wa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Argentina walipokutana jijini Addis Ababa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.


Na Ally Kondo, Addis Ababa

Nchi za Afrika zimehimizwa kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa ajili ya kufanya tiba na chanjo za maribio dhidi ya ugonjwa wa Ebola. Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu na Mshauri wa Kituo cha Sayansi, Teknolojia na Ubunifu cha NEPAD, Prof. Aggrey Ambali  wakati alipokuwa anawasilisha mada kuhusu ugonjwa wa Ebola kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi wa NEPAD jijini Addis Ababa siku ya Jumanne tarehe 27 Januari 2015.

Prof. Ambali alieleza kuwa mashirika mengi yanayohusika na udhibiti wa madawa barani Afrika yanakabiliwa na ugumu wa kushughulikia masuala ya kimaadili na kanuni zinazosimamia tiba za majaribio kwenye nchi wanachama.

Alitoa mfano wa masuala ya kimaadili na kisera ambayo yanahitaji ufumbuzi ili kuwezesha kukusanya na kusafirisha damu na plasma kwenye nchi zinazohusika.

Kwa kuliona hilo, NEPAD kupitia Programu ya Afrika ya Kuoanisha Kanuni za Udhibiti wa Madawa inafanya kazi kwa kushirikiana na Jumuiya za Kikanda pamoja na Mashirika ya Kitaifa ya Udhibiti wa Madawa ili kupata nguvu inayohitajika ya kusimamia tiba za majaribio na kushughulikia masuala ya kimaadili

Kwa msaada wa NEPAD na Shirika la Afya Duniani, Jumuiya ya Afrika Mashariki inafanya tathmini ya pamoja ya chanjo ya Ebola ambayo itafanyika tarehe 02 – 04 Februari 2015. Nchi zinazolengwa kwa ajili ya majaribio hayo ni Tanzania, Uganda na Kenya lakini tathmini ya pamoja itafanywa na nchi zote za EAC.

Prof. Ambali alihitimisha mada yake kwa kusema kuwa tiba za majaribio kwa ajili ya chanjo mbili za Ebola yanafanyika huko Afrika Magharibi na majaribio mengine kadhaa yanatarajiwa kufanyika hivi klaribuni. 


Tuesday, January 27, 2015

EAC na ECOWAS zaonesha mfano, Zuma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb) kulia akimsikiliza Balozi wa Syria nje ya ukumbi wa mikutano jijini Addis Ababa. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz.


Na Ally Kondo, Addis Ababa

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bibi Nkosazana Zuma amezihimiza Jumuiya za Kikanda barani Afrika kuiga mfano wa EAC na ECOWAS ambazo zimefikia hatua za kuridhisha katika mtangamano wa kanda zao. Alisema mtangamano ni moja ya jambo muhimu katika kufikia malengo ya Bara la Afrika. Aliyasema hayo wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha Mawaziri wa AU jijini Addis Ababa siku ya Jumatatu tarehe 26 Januari 2015.
 
Bibi Zuma alibainisha kuwa Sekretarieti ya AU inakamilisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka 10 barani Afrika ambapo alitaja masuala mbalimbali yanayotakiwa kuzingatiwa ili kutekeleza mpango huo. Mpango huo unajumuisha miradi kama vile Soko moja la usafiri wa anga, mradi wa bwawa la umeme la Inga, Chuo Kikuu cha Pan African, reli ya mwendo kasi na mtandao wa barabara. Miradi mingine ni mtandao wa kielektroniki wa pan (Pan e-network), Eneo Huru la Biashara barani Afrika, Hati moja ya kusafiria ya Afrika na miradi ya kilimo.
 
Bibi Zuma aliahidi kupitiwa upya kwa uwezo unaohitajika katika utekelezaji wa mpango huo wa maendeleo. Hiyo inajumuisha kupitia upya uwezo wa taasisi za nchi wanachama, Jumuiya za Kikanda na AU pamoja na Asasi za Kiraia.  Maeneo yatakayoangaliwa katika zoezi hilo ni pamoja na taaluma na ujuzi unaohitajika hususan katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi, utafiti, usimamizi wa miradi na ubunifu ambavyo ni vitu muhimu katika kufikia dira ya bara la Afrika.
 
Aidha, alisema ukusanyaji wa mapato ya ndani ni kitu cha msingi, kwa kuwa kutalifanya Bara la Afrika kuwa na fedha za uhakika za kugharamia miradi inayokusudiwa.
 
Katika kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo, Bibi Zuma alisisitiza umuhimu wa kuangalia hatari zinazoweza kujitokeza. Alisema endapo bara la Afrika litashindwa kumaliza migogoro ya kutumia nguvu, kukabiliana na tishio la ugaidi na siasa kali, vitendo vya kutoaminiana, kasi ndogo ya mtangamano, vyote hivyo na vingine vingi vitadumaza mipango ya maendeleo.
 
Bibi Zuma aliendelea kueleza kuwa OAU/AU itakapofikisha karne moja, idadi ya vijana barani Afrika inakadiriwa kuwa kubwa kuliko rika yeyote nyingine. Hivyo, alisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa vijana ili kuwaandaa kuwa viongozi na katika nyanja nyingine za maisha kama vile ujasiliamali, sayansi na teknolojia.
 

Bara la Afrika lahimizwa kuvutia zaidi uwekezaji, Lopez


Bw. Lopez akiwasilisha hotuba jijini Addis Ababa
 

Na Ally Kondo,  Addis Ababa

Uchumi wa Bara la Afrika umeelezwa kuwa unakua kwa kasi zaidi ukilinganisha na mabara mengine duniani.  Hayo yamesemwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Uchumi ya Afrika, Bw. Carlos Lopez wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa AU jijini Addis Ababa, Ethiopia siku ya Jumatatu tarehe 26 Januari 2015.

Bw. Lopez alithibitisha kauli yake hiyo kwa kunakili ripoti mbalimbali  ikiwa  ni pamoja na ripoti ya Ernst & Young  inayosema kuwa Bara la Afrika ni la pili kwa kuvutia uwekezaji baada ya Asia ya Kusini-Mashariki.  Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa uwekezaji baina ya nchi za Afrika umeongezeka na kwa sasa unakua kwa asilimia 32.4 kwa mwaka.  Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, jumla ya akiba ya fedha katika Bara la Afrika itafikia Dola za Marekani trilioni 23 kutoka trioni 12 ifikapo mwaka 2030. Aidha, Financial Times limeripoti kuwa Soko la Hisa la London limeanza jitihada za makusudi kuongeza idadi ya makampuni ya Afrika katika soko hilo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya hisa ya makampuni hayo.

Aidha, Bw. Lopezi alieleza kuwa Afrika inazalisha asilimia 7 ya mafuta yote duniani na asilimia moja ya gesi asilia. Hata hivyo, Afrika ni msafirishaji mkubwa wa nishati nje ya Afrika, hivyo kwa namna yoyote ile Bara la Afrika litaonja athari za kuporomoka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia,  lakini ikumbukwe kuwa kwa kuwa nchi nyingi za Afrika zinaagiza mafuta kutoka nje, basi kuporomoka kwa bei za mafuta kutaleta nafuu kwa nchi hizo.

Aliendelea kueleza kuwa miradi ya usafirishaji wa gesi asilia inahama kutoka Australia na kwenda Afrika. Tanzania, Msumbiji na Nigeria zina matumani makubwa wa kuwa wazalishaji wakubwa katika sekta hiyo. Hiyo itasaidi kuboresha uchumi katika nchi hizo kwa kipindi fulani lakini zitakumbana na hali ngumu kutoka Marekani ambaye anatarajiwa kudhibiti soko la bidhaa hiyo.

Bw. Lopez alizisihi nchi za Afrika kuendeleza na kuimarisha uwekezaji kama ilivyofanya mwaka 2014. Alisema kuwa kati ya Dola trilioni 1.53 zilizowekezwa duniani   kote, asilimia 3.7 tu ndizo zilizowekezwa Afrika. Asilimia 20 iliwekezwa Latin Amerika na asilimia 30 iliwekezwa  Asia.

China kwa mfano, licha ya maneno yote yanayosemwa, iliwekeza chini ya asilimia 5 ya thamani ya uwekezaji iliyofanya duniani kote. Alisema kiwango cha uwekezaji kati ya India na China Barani Afrika kinalingana, ingawa China inazungumzwa zaidi.   Aidha, India na Malaysia kwa pamoja zina vitega uchumi vingi barani Afrika kuliko nchi yeyote ile inyoendelea.

Bw. Lopez alihitimisha kwa kusiisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutimiza ahadi yao ya kuwa na Makubaliano ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika ifikapo mwaka 2017. Alisema ili nchi za Afrika zikue kiuchumi, ziwe na fedha na ajira za kutosha hakuna budi soko lipanuliwe. Endapo nchi za Afrika litaunda Soko la Pamoja ifikapo mwaka 2017 litakuwa na ukubwa sawa na idadi ya watu wa China.