Tuesday, January 27, 2015

Bara la Afrika lahimizwa kuvutia zaidi uwekezaji, Lopez


Bw. Lopez akiwasilisha hotuba jijini Addis Ababa
 

Na Ally Kondo,  Addis Ababa

Uchumi wa Bara la Afrika umeelezwa kuwa unakua kwa kasi zaidi ukilinganisha na mabara mengine duniani.  Hayo yamesemwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Uchumi ya Afrika, Bw. Carlos Lopez wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa AU jijini Addis Ababa, Ethiopia siku ya Jumatatu tarehe 26 Januari 2015.

Bw. Lopez alithibitisha kauli yake hiyo kwa kunakili ripoti mbalimbali  ikiwa  ni pamoja na ripoti ya Ernst & Young  inayosema kuwa Bara la Afrika ni la pili kwa kuvutia uwekezaji baada ya Asia ya Kusini-Mashariki.  Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa uwekezaji baina ya nchi za Afrika umeongezeka na kwa sasa unakua kwa asilimia 32.4 kwa mwaka.  Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, jumla ya akiba ya fedha katika Bara la Afrika itafikia Dola za Marekani trilioni 23 kutoka trioni 12 ifikapo mwaka 2030. Aidha, Financial Times limeripoti kuwa Soko la Hisa la London limeanza jitihada za makusudi kuongeza idadi ya makampuni ya Afrika katika soko hilo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya hisa ya makampuni hayo.

Aidha, Bw. Lopezi alieleza kuwa Afrika inazalisha asilimia 7 ya mafuta yote duniani na asilimia moja ya gesi asilia. Hata hivyo, Afrika ni msafirishaji mkubwa wa nishati nje ya Afrika, hivyo kwa namna yoyote ile Bara la Afrika litaonja athari za kuporomoka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia,  lakini ikumbukwe kuwa kwa kuwa nchi nyingi za Afrika zinaagiza mafuta kutoka nje, basi kuporomoka kwa bei za mafuta kutaleta nafuu kwa nchi hizo.

Aliendelea kueleza kuwa miradi ya usafirishaji wa gesi asilia inahama kutoka Australia na kwenda Afrika. Tanzania, Msumbiji na Nigeria zina matumani makubwa wa kuwa wazalishaji wakubwa katika sekta hiyo. Hiyo itasaidi kuboresha uchumi katika nchi hizo kwa kipindi fulani lakini zitakumbana na hali ngumu kutoka Marekani ambaye anatarajiwa kudhibiti soko la bidhaa hiyo.

Bw. Lopez alizisihi nchi za Afrika kuendeleza na kuimarisha uwekezaji kama ilivyofanya mwaka 2014. Alisema kuwa kati ya Dola trilioni 1.53 zilizowekezwa duniani   kote, asilimia 3.7 tu ndizo zilizowekezwa Afrika. Asilimia 20 iliwekezwa Latin Amerika na asilimia 30 iliwekezwa  Asia.

China kwa mfano, licha ya maneno yote yanayosemwa, iliwekeza chini ya asilimia 5 ya thamani ya uwekezaji iliyofanya duniani kote. Alisema kiwango cha uwekezaji kati ya India na China Barani Afrika kinalingana, ingawa China inazungumzwa zaidi.   Aidha, India na Malaysia kwa pamoja zina vitega uchumi vingi barani Afrika kuliko nchi yeyote ile inyoendelea.

Bw. Lopez alihitimisha kwa kusiisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutimiza ahadi yao ya kuwa na Makubaliano ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika ifikapo mwaka 2017. Alisema ili nchi za Afrika zikue kiuchumi, ziwe na fedha na ajira za kutosha hakuna budi soko lipanuliwe. Endapo nchi za Afrika litaunda Soko la Pamoja ifikapo mwaka 2017 litakuwa na ukubwa sawa na idadi ya watu wa China.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.