Monday, January 26, 2015

NEPAD yapiga hatua katika Utekelezaji wa Vipaumbele vyake, Dkt. Mayaki.

Picha ya pamoja ya Mawaziri wa Mambo ya Nje  wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika baada ya Mkutano wao kufunguliwa rasmi jijini Addis Ababa leo.  p


Na Ally Kondo, Addis Ababa

Kamati ya Uongozi ya NEPAD imekutana leo Jumatatu jijini Addis Ababa, Ethiopia kutathmini utekelezaji wa programu mbalimbali wa chombo hicho. Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shuguli za NEPAD kwa mwaka 2014, Mtendaji Mkuu wa NEPAD, Dkt. Ibrahim Mayaki  alieleza kuwa Chombo hicho kimepiga hatua kubwa katika maeneo ya kipaumbele iliyojiwekea.

Kwa upande wa miundombinu, Dkt. Mayaki alikumbusha Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliofanyika Darker, Senegal ambao ulijadili njia za kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya miuondombinu barani Afrika. Mkutano huo uliweka msingi wa kuainisha miradi 16 ya miundombinu yenye kukopesheka na yenye lengo la kupunguza tatizo la miundombinu barani Afrika. NEPAD kwa kuzingatia ushauri wa Wakuu wa Nchi, imeanzisha chombo maalum ambacho jukumu lake ni kutoa msaada wa kiufundi katika hatua za mwanzo za maandalizi ya miradi ya miundombinu.

Aidha, Dkt. Mayaki alieleza shuguli mbalimbali zinazofanyika kwa ushirikiano kati ya NEPAD na USAID katika utekelezaji wa mradi wa Umeme barani Afrika (POWER Africa Initiative). Mradi huo unalenga kuzalisha megawatts 30,000 za umeme kwa ajili ya familia na wafanyabiashara milioni 60 hususan, wanaoishi maeneo ya vijijini.

Dkt. Mayaki pia alitoa taarifa ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme-CAADP).  Alibainisha kuwa nchi 40 kati ya nchi wanachama 54 zimeweka saini Mkataba wa CAADP ambao unazitaka nchi hizo kutenga asilimia 10 ya bajeti ya Serikali kwa ajili ya kilimo. Aidha, nchi 25 zimeridhia mpango wa kuwekeza katika kilimo na usalama wa chakula.

Kwa upande wake, Mkurugenzi na Mratibu wa Utekelezaji wa Programu za NEPAD, Bibi Estherine Fotabong alizungumzia masuala ya Jinsia, Mabadiliko ya tabianchi na program za kusaidia kilimo ambazo zinalenga kuwawezesha wanawake na makundi mengine masikini ya wakulima kuwa na utaalamu, nyenzo na ujuzi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika shughuli zao za kilimo. Alisema kuwa itakapofika mwaka 2015, jumla ya wakulima milioni 25  watakuwa na teknolojia bora ya mazingira.

Bibi Fotabong alikumbusha kuwa NEPAD ni taasisi ya kwanza barani Afrika kuanzisha Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi ambao unatoa fedha kwa ajili ya masuala ya kiufundi, kujenga uwezo na utengenezaji wa sera kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa nchi za Afrika na Jumuiya za Kikanda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya NEPAD, Bibi Gnounka Diouf alisifu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya NEPAD kwa mwaka 2014 na kushauri kuwa mwaka 2015 utekelezaji wa program za NEPAD uwe wa kasi zaidi kwa kuwa mwaka huo ndio mwisho wa utekelezaji wa Malengo ya Milenia.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.