Tuesday, January 27, 2015

EAC na ECOWAS zaonesha mfano, Zuma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb) kulia akimsikiliza Balozi wa Syria nje ya ukumbi wa mikutano jijini Addis Ababa. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz.


Na Ally Kondo, Addis Ababa

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bibi Nkosazana Zuma amezihimiza Jumuiya za Kikanda barani Afrika kuiga mfano wa EAC na ECOWAS ambazo zimefikia hatua za kuridhisha katika mtangamano wa kanda zao. Alisema mtangamano ni moja ya jambo muhimu katika kufikia malengo ya Bara la Afrika. Aliyasema hayo wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha Mawaziri wa AU jijini Addis Ababa siku ya Jumatatu tarehe 26 Januari 2015.
 
Bibi Zuma alibainisha kuwa Sekretarieti ya AU inakamilisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka 10 barani Afrika ambapo alitaja masuala mbalimbali yanayotakiwa kuzingatiwa ili kutekeleza mpango huo. Mpango huo unajumuisha miradi kama vile Soko moja la usafiri wa anga, mradi wa bwawa la umeme la Inga, Chuo Kikuu cha Pan African, reli ya mwendo kasi na mtandao wa barabara. Miradi mingine ni mtandao wa kielektroniki wa pan (Pan e-network), Eneo Huru la Biashara barani Afrika, Hati moja ya kusafiria ya Afrika na miradi ya kilimo.
 
Bibi Zuma aliahidi kupitiwa upya kwa uwezo unaohitajika katika utekelezaji wa mpango huo wa maendeleo. Hiyo inajumuisha kupitia upya uwezo wa taasisi za nchi wanachama, Jumuiya za Kikanda na AU pamoja na Asasi za Kiraia.  Maeneo yatakayoangaliwa katika zoezi hilo ni pamoja na taaluma na ujuzi unaohitajika hususan katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi, utafiti, usimamizi wa miradi na ubunifu ambavyo ni vitu muhimu katika kufikia dira ya bara la Afrika.
 
Aidha, alisema ukusanyaji wa mapato ya ndani ni kitu cha msingi, kwa kuwa kutalifanya Bara la Afrika kuwa na fedha za uhakika za kugharamia miradi inayokusudiwa.
 
Katika kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo, Bibi Zuma alisisitiza umuhimu wa kuangalia hatari zinazoweza kujitokeza. Alisema endapo bara la Afrika litashindwa kumaliza migogoro ya kutumia nguvu, kukabiliana na tishio la ugaidi na siasa kali, vitendo vya kutoaminiana, kasi ndogo ya mtangamano, vyote hivyo na vingine vingi vitadumaza mipango ya maendeleo.
 
Bibi Zuma aliendelea kueleza kuwa OAU/AU itakapofikisha karne moja, idadi ya vijana barani Afrika inakadiriwa kuwa kubwa kuliko rika yeyote nyingine. Hivyo, alisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa vijana ili kuwaandaa kuwa viongozi na katika nyanja nyingine za maisha kama vile ujasiliamali, sayansi na teknolojia.
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.