Mazungumzo ya ushirikiano yakiendelea ======================================= |
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania
kufungua Ubalozi nchini Kuwait
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufungua Ubalozi
nchini Kuwait kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha wa
2014/2015.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) alipokutana na Mtukufu Sheikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa
Mambo ya Nje wa Kuwait nchini Kuwait siku ya Jumanne tarehe 14 Aprili, 2015.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wawili walisifu ushirikiano
uliopo baina ya nchi hizi mbili ambao ni wa kidugu na unalenga kuwanufaisha
wananchi wa nchi hizi.
“Kwa kufungua ofisi za Ubalozi, Kuwait ushirikiano huu wa kidugu
utaongezeka kwenye nyanja zote muhimu na utazaa matunda yatakayo wanufaisha
watu wetu, kwa nchi hizi mbili” alisisitiza Waziri Membe katika mazungumzo yake
na kiongozi huyo.
Kwa upande wa Kuwait, Serikali yao ilifungua ubalozi nchini
Tanzania Februari 2015 na Mhe. Jassem Ibrahim Al Najem kuwa Balozi wake wa
kwanza nchini Tanzania, mwenye makazi yake Jijini Dar es salaam.
Aidha, kwa sasa Tanzania inawakilishwa nchini Kuwait kupitia Ubalozi
wake uliopo Riyadh, Saudi Arabia.
Katika mkutano huo, Mtukufu Sabah Al-Khalid Al Sabah alisifu
jitihada za Tanzania kwenye kulinda na kuleta amani Barani Afrika hasusan
kwenye maeneo yenye migogoro. Alisema kuwa Serikali yake itaendelea
kushirikiana na Tanzania sio tu kwenye maeneo muhimu ya maendeleo lakini pia
hata kwenye ulinzi wa amani kwani ndio changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa
sasa.
Kuhusu misaada Barani
Afrika, viongozi hao walijadili suala la uratibu wa misaada mbalimbali ya
Serikali ya Kuwait Barani humo ambapo waliangalia uwezekano wa kuanzisha kituo
maalum nchini Tanzania kwa ajili ya kusimamia shughuli za uratibu wa misaada
hiyo.
Kwa sasa Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wake wa Maendeleo –
Kuwait Fund- imetoa Dola za Kimarekani Bilioni moja kwenye Umoja wa Afrika kwa
ajili ya usalama wa chakula Barani Afrika.
Awali Waziri Membe alikutana na Mhe. Abdulwahab A. Al-Bader,
Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait na kumshukuru kwa misaada mbalimbali
ya kimaendeleo wanayoendelea kuitoa nchini Tanzania na barani Afrika kwa
ujumla.
Aidha Waziri Membe alielezea kuwa maandalizi ya miradi mitano ya
umwagiliaji nchini Tanzania ambayo inayofadhiliwa na mfuko huo yamekamilika, na
kwamba sasa iko tayari kuanza. Aidha Waziri Membe na Mhe. Al-Bader walizungumzia
uwezekano wa mfuko huo kuikopesha Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ili iweze
kuendesha shughuli zake kikamilifu.
Waziri Membe yuko nchini Kuwait kwa ziara ya siku moja na
anatarajiwa kuondoka kesho kuelekea nchini Oman. Ujumbe wa Mhe. Membe nchini Kuwait unamjumuisha Bw. Peter Noni,
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Uwekezaji Tanzania, Balozi Simba Yahya, Mkuregenzi
wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya
Mambo ya Nje.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
15 Aprili 2015.