Saturday, June 20, 2015

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mara ya kwanza na Watumishi wote wa Wizara


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Libarata Mulamula akizungumza katika kikao chake cha kwanza na Watumishi wote wa Wizara tangu alipoteuliwa na Rais hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mkutano huo ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini  Dar es Salaam tarehe 20 Juni, 2015. Pamoja na mambo mengine Balozi Mulamula aliwahimiza Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje kufanya kazi kwa bidii, kuwa  na utii, nidhamu pamoja na unyenyekevu ili kufikia malengo katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Watumishi wa  Wizara wakimsikiliza Balozi Mulamula (hayupo pichani)
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje  wakimsikiliza Balozi Mulamula (Hayupo pichani).
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Mambo ya Nje wakimsikiliza Balozi Mulamula


Juu na Chini ni baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakiwa katika kikao na Balozi Mulamula

Baadhi ya Watumishi wakichangia hoja wakati wa mkutano kati yao na Katibu Mkuu, Balozi Mulamula ambaye hayupo pichani


Mkutano ukiendelea 
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Simba Yahya nae akizungumza machache mbele ya Watumishi wakati wa mkutano huo 
Balozi Mulamula kwa pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Simba Yahya wakishangilia  kwa furaha  wakati walipokutana na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Watumishi wa Wizara wakiwashangilia Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wakati wa mkutano pamoja nao.

Picha na Reginald Philip





Friday, June 19, 2015

Balozi Mulamula akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Msumbiji nchini

Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Vicente Veloso  alipofika Wizarani kwa ajili ya kuzungumza na  Balozi Mulamula kuhusu namna bora ya kuiamarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji  na pia kumpongeza kwa kuteuliwa na Rais kuwa Katibu Mkuu.
Mkutano ukiendelea huku wajumbe kutoka pande zote mbili wakisikiliza kwa makini. Wa pili kulia ni Bi. Zuhura Bundala, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bi. Talha Mohammed (kulia), Afisa Mambo ya Nje.

India yaipa Tanzania mkopo wa Dola Mil. 268 kwa ajili ya mradi wa maji katika miji ya Tabora, Igunga, Sikonge na Nzega

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) akiwa ameshikilia cheti kwa pamoja na Mwenyekiti wa Makampuni ya Kamal, Bw. Gagan Gupta. Bw. Gupta ni mfanyabiashara kutoka India ambaye amewekeza nchini Tanzania alikabidhiwa cheti cha kutambua mchango wake katika kukuza uchumi wa Tanzania. Cheti hicho alikabidhiwa siku ya Alhamisi jijini Delhi.



Na Ally Kondo, Delhi

Serikari za Tanzania na India zimewekeana saini Hati za Makubaliano kwa ajili ya kushirikiana katika kuendeleza sekta za maji, utalii, usafiri na usalama wa bahari pamoja na Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki.  Uwekaji saini wa hati hizo umefanyika jijini Delhi siku ya Ijumaa na kushuhudiwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi. Rais Kikwete yupo nchini India kwa ziara ya kitaifa ya siku nne aliyoianza tarehe 17 Juni 2015.

Kwa mujibu wa Makubaliano katika Sekta ya Maji, Serikali ya India itatoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 268.35 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya mradi wa maji katika miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na  vijiji vitakavyopitiwa na bomba kubwa la maji litakalojengwa kutoka Ziwa Victoria.

Mradi huo utakaojengwa kwa miaka miwili na nusu na kampuni kutoka India utaanza Mwaka ujao wa Fedha 2015/16 na unatokana na ahadi ya Rais Kikwete aliyoitoa kwa wananchi wa maeneo hayo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kujengwa kwa mradi huo, itakuwa faraja kubwa kwa watu wanaoishi maeneo hayo ambayo kwa Tanzania yanakabiliwa na ukame na kupata mvua chache kwa mwaka ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi. Watu takribani milioni 1.5 watafaidika na mradi huo utakapokamilika.

Mradi huo utakapokamilika utawaondolea wananchi adha ya kutembea mwendo mrefu kwa ajili ya kutafuta maji na badala yake watatumia muda mwingi kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali. Aidha, utawapa fursa watoto wa kike kujishughulisha na masomo pamoja na kutoa huduma za maji katika zahanati, vituo vya afya na mashuleni.


Kwa upande wa Makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya utalii, inatarajiwa kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka India kuja Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhandisi John Kijazi, India kila mwaka inatoa watalii milioni 128 kwenda nchi mbalimbali duniani, lakini kati ya hao ni watalii 27,000 tu, ndio wanakuja Tanzania.

Makubaliano yaliyosainiwa kwa ajili ya Chuo cha Takwimu, utakiondolea chuo hicho na uhaba wa wakufunzi na mzigo wa kugharamia wakufunzi kutoka India kwa kuwa, kuanzia sasa India itakuwa ikipeleka wakufunzi kwenye chuo hicho kwa  gharama zao.  




 


Banda la Wizara ya Mambo ya Nje lazidi kung'ara kwenye maonesho ya Utumishi wa Umma

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bw. Mkumbwa Ally akizungumzia ushiriki wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye maonyesho ya ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam
Afisa Mwandamizi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mashaka Chikoli akielezea utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje  na mafanikio ya Wizara  kwa  Mtayarishaji wa Vipindi vya Televisheni, Bw. Paschal Mayala.
Mkufunzi wa Chuo cha Diplomasia, Bw. Ali Masabo akielezea Kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo hicho ikiwemo kozi mpya ya Shahada ya Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia wakati akihojiwa na Bw. Mayala
Afisa kutoka Taasisi iliyo chini ya Wizara  ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC)  Bw. Rodney T. Mbuya naye akielezea ushiriki wa Taaisisi hiyo katika maonyesho ya Utumishi wa Umma
Mmoja wa Wananchi akisoma na kutazama picha za Mawaziri wa Mambo ya Nje tangu uhuru hadi sasa katika kitabu kilichomvutia kilichokuwa kinatolewa katika banda la maonyesho la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatiafa
Bw. Mayala akimhoji mwananchi aliyemkuta akisoma Kitabu cha Sera ya Mambo ya Nje na kuimwagia sifa Wizara ya Mambo ya Nje kwa juhudi zake katika kutekeleza Sera hiyo.  Wanaoshuhudia ni Bw. Khatibu Makenga, Afisa Mambo ya Nje na Rodney Mbuya  wa AICC. 
Wananchi wakiendela kupata maelezo juu ya majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na jinsi gani Wizara inatekeleza Diplomasia ya Uchumi 
Maafisa wakiwa akitika picha ya pamoja katika banda lao


Picha na Reginald Philip

Balozi Mulamula azungumza na Balozi wa Ufaransa nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Malika Berak, alipokuja kujitambulisha na kumpongeza Balozi Mulamula kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu. Pia walizungumzia masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kukuza mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizi mbili
Katibu Mkuu Balozi Mulamula akimwonyesha Balozi Berak Kitabu kinachozungumzia maendeleo ya Mji wa Kilwa.
Afisa Mambo ya Nje, Bi. Felisita Rugambwa akinukuu mazungumzo  yaliyokuwa yakiendelea kati ya Balozi  Mulamula na Balozi Berak (hawapo pichani)
Mazungumzo yakiendelea.
Picha na Reginald Philip


Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa IFAD nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberatta Mulamula akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi wa IFAD nchini Bw. Sana F.K. Jatta, alipokuja kumtembelea na kujadili juu ya ziara ya  Rais wa IFAD Mhe. Kanayo Nwanze mwezi Agosti 2015
Mmoja wa wajumbe aliyeambatana na Bw. Jatta akifafanua jambo kwa Balozi Mulamula.
Mazungumzo yakiendelea

Thursday, June 18, 2015

Tanzania na India zinaweza kufanya vizuri zaidi kibiashara. Rais Kikwete





Na Ally Kondo, Delhi

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa licha ya biashara kati ya Tanzania na India kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi endapo fursa zilizopo zitatumiwa ipasavyo.

Rais Kikwete alisema hayo alipokuwa anaongea na Watendaji Wakuu wa Makampuni Makubwa ya India jijini Delhi leo tarehe 18 Juni 2015.

Rais Kikwete yupo nchini India kwa ziara ya Kitaifa ya siku nne iliyoanzia Siku ya Jumanne tarehe 17 Juni, 2015. Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na India, kuaga na kuishukuru India kwa misaada inayotoa tokea uhuru hadi sasa pamoja na kuisihi nchi hiyo kumpa ushirikiano Rais atakayechaguliwa mara uongozi wake utakapokamilika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba 2015.  

 Katika kikao hicho, Rais Kikwete alibainisha masuala mbalimbali ambayo yanaifanya Tanzania kuwa chaguo la kwanza kwa Mfanyabiashara anayetaka kuwekeza. Alieleza Serikali imefanyia mabadiliko makubwa Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali ambazo sasa zinaruhusu na kuimarisha Uchumi wa Soko. Kutokana na mabadiliko hayo, hakuna mwekezaji anayetakiwa kuwa na khohu ya kutaifishwa vitega uchumi vyake endapo atawekeza nchini Tanzania. Aliendelea kueleza kuwa Tanzania ni mwanachama wa kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara, hivyo, mwekezaji yeyote ana uhuru wa kufikisha suala lolote katika kituo hicho ili kupata haki yake, endapo atahisi amedhulumiwa.

 Aliwambia Wakuu hao waje kuwekeza nchini kwa sababu Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu wa hali ya juu kwa muda mrefu na aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kudumisha amani na utulivu huo.

 Sanjari na amani na utulivu, Tanzania imejaliwa kuwa na fursa lukuki za uwekezaji katika sekta za kilimo; viwanda vya uzalishaji; kilimo cha biashara; madini; utalii; uchukuzi na usafirishaji; miundombinu kama vile reli, barabara na bandari; afya; elimu na ujenzi wa makazi. 

Kwa upande wa kilimo, Rais Kikwete alisisitiza umuhimu wa kufanya uwekezaji katika pembejeo hususan, matrekta ili nchi iachane na matumizi ya jembe la mkono. Uzalishaji wa mbolea na dawa za kuua wadudu wanaoshambulia mazao, uzalishaji wa mbegu za kisasa pamoja na kujenga viwanda vya kusindika mazao, matunda na nyama.

Aidha, alisema jiografia ya Tanzania inatoa fursa nyingi za uwekezaji hususan katika uchukuzi na usafirishaji. Hii inatokana na nchi nyingi zinazopakana na Tanzania kuwa hazina bandari, hivyo bidhaa zao wanazoagiza au kusafirisha nje ya nchi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam.

 Rais aliwambia wafanyabiashara hao kuwa, atakayekuja kuwekeza Tanzania ana uhakika wa soko kubwa la bidhaa zake ndani na nje ya  nchi. Alisema Tanzania ina fursa ya kuuza bidhaa zinazozalishwa nchini katika nchi za SADC na EAC bila kulipa ushuru. Nchi hizo kwa pamoja zinakadiriwa kuwa na soko la watu zaidi ya milioni 300. Aidha, nchi za EAC, SADC na COMESA zimekubaliana kuanzisha Eneo huru la Biashara ambalo litakuwa na soko la watu zaidi ya milioni 600.


Kwa upande wao, wafanyabiashra hao walivutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na walionesha dhamira ya kuwekeza, isipokuwa waliomba kuwepo na ushirikiano mzuri na serikali ili nia yao hiyo iweze kufanikiwa.



Press Release

Hon. Adel Al Jubeir, Minister of  Foreign Affairs of Saudi Arabia

PRESS RELEASE

Hon. Bernard K. Membe (MP), Minister of Foreign Affairs and International Cooperation of the United Republic of Tanzania has sent a congratulatory message to Hon. Adel Al Jubeir, Minister of Foreign Affairs of the Royal Kingdom of Saudi Arabia following his appointment as Minister of Foreign Affairs of the Royal Kingdom of Saudi Arabia.

  The message reads as follows;

“Hon. Adel Al Jubeir,
Minister of Foreign Affairs of the Royal Kingdom of Saudi Arabia,
RIYADH

Honourable Minister,

On behalf of the Government and People of the United Republic of Tanzania and indeed on my own behalf, I would like to take this opportunity to extend to you Honourable Minister our warmest congratulations for your appointment as Minister of Foreign Affairs of the Royal Kingdom of Saudi Arabia. Your appointment is a clear testimony of the trust His Royal Highness the King of Saudi Arabia has on your vast and rich knowledge on international affairs and ability to guide foreign policy of the Kingdom of Saudi Arabia.

I would like to assure you of my personal commitment as well as that of my Government to continue working closely with you and the Royal Government of the Kingdom of Saudi Arabia at both bilateral and multilateral levels.

While wishing you continued personal good health, happiness and prosperity and great achievements in your new roles, please accept the assurances of my highest consideration”.

Issued by: Ministry of Foreign Affairs and International Cooperation, Dar es Salaam.
18th June, 2015

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa UNFPA nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mwakilishi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) hapa nchini Dkt.Nathalia Kanem alipokuja kumtembelea Wizarani
Ujumbe alioambatana nao Dkt. Kanem ukifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Balozi Mulamula na Dkt. Kanem (hawapo pichani)
Dkt Kanem akichangia jambo huku Katibu Mkuu, Balozi Mulamula akimsikiliza kwa makini.
Katibu Mkuu Balozi Mulamula (kushoto) akimsikiliza Dkt. Kanem (hayupo pichani), huku Afisa Mambo ya Nje, Bi. Ramla Hamis (kulia) akinukuu mazungumzo hayo.
Balozi Mulamula na Dkt. Kanem wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa UNFPA

Picha na Reginald Philip

Balozi Mulamula akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Balozi Liberata Mulamula (kulia) akizungumza na Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Johnny Flento alipokuja kumtembelea na kufanya mazungumzo yaliyojikita katika kuboresha mahusiano baina ya Tanzania na Denmark.
Balozi Flento akizungumza huku Balozi Mulamula akimsikiliza. 
Mazungumzo yakiendelea huku Afisa Mambo ya Nje, Bi. Tunsume Mwangolombe akinukuu.

Picha na Reginald Philip

Wananchi wazidi kumiminika Banda la Mambo ya Nje Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma

Afisa kutoka Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bi. Asiya Hamdani akitoa maelezo  kuhusu majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa  kwa Wananchi waliokuja kutembelea Banda la Wizara lililopo katika Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni "Utumishi wa Umma katika Bara la Afrika ni Chachu ya Kuwawezesha Wanawake, Kuongeza Ubunifu na Kuboresha Utoaji Huduma Kwa Umma".
Afisa matukio msaidizi kutoka Taasisi ya APRM, Bi. Praxeda Gasper  akitoa maelezo kwa mwananchi aliyetembelea Banda la Wizara ya Mambo ya Nje.
Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Thobias Tarimo naye akielezea majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa mmoja wa wananchi waliojitokeza kwenye maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye Banda la Wizara hiyo. 
Mkufunzi wa Chuo cha Diplomasia kilichopo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Desderia Sabuni (wa kwanza Kushoto) naye akiwaelezea wananchi waliotembelea banda la Wizara ya Mambo ya Nje juu ya Kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo cha Diplomasia pamoja na majukumu ya Wizara kwa ujumla.
Wananchi wakiendelea kupata huduma kwenye Banda la Mambo ya Nje


Picha na Reginald Philip

Mawaziri wa EAC wawasilisha maamuzi ya Wakuu wa Nchi kwa Rais wa Burundi

  Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), akiwasilisha kwa Rais wa Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza maamuzi ya Mkutano wa  Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 31 Mei, 2015 Jijini Dar es Salaam. Mhe. Mwakyembe  aliongoza ujumbe wa Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ziara ya kikazi nchini Burundi tarehe 15 Juni, 2015.
Rais Nkurunziza akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula walipowasili kwa ajili ya kuzungumza nae.
Mhe. Rais Nkurunziza akizungumza na Ujumbe uliomtembelea.
=============================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliongoza ujumbe wa Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ziara ya kikazi iliyofanyika nchini Burundi tarehe 15 Juni, 2015.

Ziara hiyo imefanyika kufuatia maelekezo ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (The Emergency Meeting of the EAC Heads of State) ambao ulifanyika tarehe 31 Mei, 2015, Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa nchini Burundi hususan katika kipindi hiki ambacho wanaelekea kwenye uchaguzi Mkuu.

Dhumuni la ziara ya Mawaziri hao nchini Burundi lilikuwa ni kuwasilisha rasmi maamuzi yaliyotokana na kikao hicho ambacho kiliwaelekza Mawaziri kuwasilisha mara moja maamuzi yaliyotokana na kikao hicho kwa Serikali ya Burundi.

Kwenye Jopo hilo la Mawaziri hao alikuwepo Mhe. Shem Bageine, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda ambaye alifuatana pia na Mhe. Philemon Mateke Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya Mtagamano na Mhe. Elen Molekane, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini. Pia Katika Ujumbe huo alikuwepo Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Serikali ya Rwanda na Kenya ziliwakilishwa na Balozi zao nchini Burundi. Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo alimwakilisha Katibu Mkuu. Kwa upande wa Serikali ya Burundi alikuwepo Mhe. Leontine Nzeyimana, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mhe. Edourd Nduwimana Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi.

Akiwapokea Mawaziri hao, Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Burundi alisema kuwa amepokea maamuzi ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na tayari utekelezaji wake ulianza mara moja. Aliongeza kusema kuwa karibu asilimia themanini ya maamuzi hayo yameshatekelezwa ikiwemo kusogezwa mbele kwa tarehe za Uchaguzi Mkuu ambapo  kwa kuzingatia kalenda mpya, uchaguzi wa Wabunge na Madiwani utafanyika tarehe 29 Juni, 2015 na Uchaguzi wa Rais utafanyika tarehe 15 Julai, 2015.

Mhe. Rais Nkurunziza alifafanua kuwa, asilimia ishirini iliyosalia itatekelezwa baada ya Uchaguzi Mkuu kwa sababu inahitaji ushirikishwaji wa wananchi wote. Moja ya maamuzi hayo ni suala la kufanyia marekebisho Katiba ya Nchi; kuendeleza mazungumzo ya mustakabali wa Burundi na kufanyia marekebisho Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Aidha Mhe. Rais Nkurunziza alieleza kuwa, Serikali imeanza utaratibu wa kuvinyang’anya silaha vikundi vyote na hadi sasa tayari wamekusanya silaha laki moja. Pia Serikali imeanza kuchukua hatua za dhati za kuwarejesha Wakimbizi na kwamba mpaka sasa zaidi ya wakimbizi 40,000 wamesharejea Burundi na vilevile Vyama vyote vya siasa viko tayari kuendelea na uchaguzi kama ilivyopangwa na vinaendelea na kampeni.


Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
18 Juni, 2015







Wednesday, June 17, 2015

Balozi Mulamula akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Sudan nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Baloz Liberata Mulamula  akisalimiana na Balozi wa Sudan nchini Tanzania, Dkt. Yassir Mohammed Ali alipokuja kumtembelea Wizarani na kufanya nae mazungumzo pamoja na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Katibu Mkuu, Balozi Mulamula  akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Sudan, Dkt. Mohammed Ali. Kulia ni Afisa Mambo ya Nje, Bi. Talha Mohammed na kushoto ni Afisa kutoka Ubalozi wa Sudan nchini.
Picha na Reginald Philip

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na Balozi wa Norway nchini

Katibu Mkuu  wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Balozi Liberatta Mulamula (Kulia)  akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Hanne Maria Kaarstad. Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Norway.
Balozi Kaarstad akimweleza jambo Katibu Mkuu, Balozi Mulamula
Mazungumzo yakiendelea huku Bi. Tunsume Mwangolombe (kulia), Afisa Mambo ya Nje akisikiliza kwa makini.


Picha na Reginald Philip.