Thursday, June 18, 2015

Mawaziri wa EAC wawasilisha maamuzi ya Wakuu wa Nchi kwa Rais wa Burundi

  Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), akiwasilisha kwa Rais wa Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza maamuzi ya Mkutano wa  Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 31 Mei, 2015 Jijini Dar es Salaam. Mhe. Mwakyembe  aliongoza ujumbe wa Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ziara ya kikazi nchini Burundi tarehe 15 Juni, 2015.
Rais Nkurunziza akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula walipowasili kwa ajili ya kuzungumza nae.
Mhe. Rais Nkurunziza akizungumza na Ujumbe uliomtembelea.
=============================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliongoza ujumbe wa Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ziara ya kikazi iliyofanyika nchini Burundi tarehe 15 Juni, 2015.

Ziara hiyo imefanyika kufuatia maelekezo ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (The Emergency Meeting of the EAC Heads of State) ambao ulifanyika tarehe 31 Mei, 2015, Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa nchini Burundi hususan katika kipindi hiki ambacho wanaelekea kwenye uchaguzi Mkuu.

Dhumuni la ziara ya Mawaziri hao nchini Burundi lilikuwa ni kuwasilisha rasmi maamuzi yaliyotokana na kikao hicho ambacho kiliwaelekza Mawaziri kuwasilisha mara moja maamuzi yaliyotokana na kikao hicho kwa Serikali ya Burundi.

Kwenye Jopo hilo la Mawaziri hao alikuwepo Mhe. Shem Bageine, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda ambaye alifuatana pia na Mhe. Philemon Mateke Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya Mtagamano na Mhe. Elen Molekane, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini. Pia Katika Ujumbe huo alikuwepo Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Serikali ya Rwanda na Kenya ziliwakilishwa na Balozi zao nchini Burundi. Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo alimwakilisha Katibu Mkuu. Kwa upande wa Serikali ya Burundi alikuwepo Mhe. Leontine Nzeyimana, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mhe. Edourd Nduwimana Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi.

Akiwapokea Mawaziri hao, Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Burundi alisema kuwa amepokea maamuzi ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na tayari utekelezaji wake ulianza mara moja. Aliongeza kusema kuwa karibu asilimia themanini ya maamuzi hayo yameshatekelezwa ikiwemo kusogezwa mbele kwa tarehe za Uchaguzi Mkuu ambapo  kwa kuzingatia kalenda mpya, uchaguzi wa Wabunge na Madiwani utafanyika tarehe 29 Juni, 2015 na Uchaguzi wa Rais utafanyika tarehe 15 Julai, 2015.

Mhe. Rais Nkurunziza alifafanua kuwa, asilimia ishirini iliyosalia itatekelezwa baada ya Uchaguzi Mkuu kwa sababu inahitaji ushirikishwaji wa wananchi wote. Moja ya maamuzi hayo ni suala la kufanyia marekebisho Katiba ya Nchi; kuendeleza mazungumzo ya mustakabali wa Burundi na kufanyia marekebisho Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Aidha Mhe. Rais Nkurunziza alieleza kuwa, Serikali imeanza utaratibu wa kuvinyang’anya silaha vikundi vyote na hadi sasa tayari wamekusanya silaha laki moja. Pia Serikali imeanza kuchukua hatua za dhati za kuwarejesha Wakimbizi na kwamba mpaka sasa zaidi ya wakimbizi 40,000 wamesharejea Burundi na vilevile Vyama vyote vya siasa viko tayari kuendelea na uchaguzi kama ilivyopangwa na vinaendelea na kampeni.


Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
18 Juni, 2015







No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.