TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Watanzania wahimizwa kuchangamkia ajira za
UN
Tanzania licha ya kuwa miongoni mwa nchi
zinazoongoza duniani kwa kuchangia vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa
Mataifa, lakini ajira za raia wake kwenye Sekretarieti ya Umoja huo ni ndogo
mno. Kauli hiyo ilitolewa leo na
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Bi.
Huda Hanina ambaye yupo nchini kwa ajili ya kutoa semina kwa Watanzania
itakayowawezesha kuwa na ujuzi na mbinu za kuomba ajira katika Umoja wa
Mataifa.
Semina hiyo
inahusisha washiriki kutoka Vyuo Vikuu, vyombo vya ulinzi na usalama, Wizara na
mashirika ya umma inafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius
Nyerere jijini Dar Es Salaam tarehe 26 hadi 28 Novemba 2018.
“Tanzania kwa
sasa inashika nafasi ya 12 katika nchi zinazochangia vikosi vya kulinda amani
duniani na utendaji wa vikosi hivyo unajulikana na kila mtu, hivyo,
Sekretarieti inapenda kuona raia wa kawaida wanaajiriwa ndani ya Umoja wa Mataifa
ili watoe mchango kama unaotolewa na vyombo vya usalama”, Alisema
Alieleza kuwa
Umoja wa Mataifa una wanachama 193 kati ya hao, nchi ambazo raia wake wameajiriwa
na Umoja huo ni 168 pekee ikiwemo Tanzania yenye watumishi 91 ambao ni chini ya
nusu asilimia ya watumishi wote wa Umoja huo.
Bi. Hanina
aliwasihi washiriki wa semina hiyo na Watanzania kwa ujumla kuingia katika
Tovuti ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, https://careers.un.org
ili kufuatilia ajira zinazotangazwa na kuangalia inayofaa kulingana na ujuzi
mtu alio nao na kutuma maombi.
Alisisitiza umhimu
wa kuandaa wasifu kulingana na sifa zilizoainishwa na nafasi husika. Alisema
tatizo kubwa linalowakabili watu wengi wakiwemo Watanzania ni kuandaa wasifu
unaokidhi viwango kulingana na kazi iliyotangazwa. “Watu wengi wanaandaa historia badala ya
wasifu, kitu ambacho sio sahihi. Kinachotakiwa ni kuandaa wasifu ambao unaainisha
ujuzi na sifa zinazotakiwa katika kazi iliyotangazwa”. Alisema.
Washiriki wa
semina hiyo wamehimizwa ujuzi waliopata wawafundishe Watanzania wengine ili
katika kipindi kifupi kijacho Watanzania wengi waweze kuomba ajira na hatimaye
kuajiriwa kwenye Umoja wa Mataifa.
Semina hiyo imekuja
kufuatia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia
Ofisi yake ya Uwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa jijini New York
kufanya maombi maalum kwenye Umoja huo ya kuwapatia Watanzania mafunzo na mbinu
za kupata ajira katika chombo hicho kikubwa duniani.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar
Es Salaam, Tanzania
Tarehe
27 Novemba 2018
|
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu akitoa neno la ukaribisho katika semina ya kuwajengea uwezo Watanzania wakuwa na mbinu na ujuzi wa kuomba na kupata ajira kwenye Umoja wa Mataifa. |
|
Mwakilishi kutoka Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Bi. Huda Hanina akitoa somo kwa washiriki wa semina kuhusu ujuzi na mbinu za kuomba na kupata ajira katika Umoja wa Mataifa. |
|
Sehemu ya washiriki wa semina kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wizara, wahitimu wa vyuo vikuu, Wizara na mashirikia ya umma wakisikiliza kwa makini somo lililokuwa linatolewa. |
|
Semina inaendelea |
|
Bi. Hanina akiendelea kutoa somo kwa Watanzania ili waweze kuwa na mbinu na ujuzi za kufanya maombi na kupata ajira kwenye Umoja wa Mataifa. |