TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali ya
awamu ya tano haichukii wawekezaji, Dkt. Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli amesema Serikali ya awamu ya tano anayoiongoza inathamini
wawekezaji, tofauti na dhana ya baadhi ya watu kuwa wawekezaji katika awamu ya
tano wanaonekana kuwa ni maadui.
Mhe. Rais Magufuli alisema hayo wakati wa sherehe ya
kufungua mwaka 2019 ya wanadiplomasia (sherry party) iliyofanyika Ikulu jijini
Dar Es Salaam tarehe 08 Machi 2019, na kuhudhuriwa na Mabalozi na wawakilishi
wa mashirika ya kimataifa yaliyopo hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli alisema uamuzi aliochukua hivi
karibuni wa kuunda Wizara maalum ya uwekezaji ni ishara ya wazi kuwa Serikali
ya awamu ya tano inathamini wawekezaji, na kuwasihi wanadiplomasia kuitumia
wizara hiyo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo
ameifanyia mabadiliko.
Rais Magufuli alisema, Serikali yake imeshaanza
mpango kabambe wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutoa wito kwa wale wenye
dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini, waende mamlaka husika ili wahudumiwe. “Mwenye dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini,
aende Wizara ya Uwekezaji au Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, akikwamishwa huko aje kwangu ili nimkwamue huyo aliyekwamisha”, Rais
Magufuli alisema.
Wanadiplomasia walioshiriki hafla hiyo, walisisitizwa
kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za
kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, madini na viwanda vya nguo. “Serikali inahimiza uwekezaji
katika sekta zinazotumia malighafi zinazopatikana nchini na zitakazotoa ajira za
kutosha kwa vijana wa kitanzania kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi”. Rais Magufuli alisema.
Kuhusu utalii, Rais Magufuli alieleza kuwa,
Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, zikiwemo fukwe, uoto wa asili, malikale,
mbuga za Wanyama na kwamba Serikali imejipanga kutangaza vivutio hivyo, hususan,
vile vinavyopatikana kanda ya kusini. Mhe. Rais aliitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika
la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa uamuzi wake wa kuanzisha channel maalum ya
kutangaza vivutio vya utalii.
Kwa upande wa sekta ya madini, Serikali imejipanga
kudhibiti wizi, biashara ya magendo, kuanzisha masoko ya kuuza madini na
kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata madini, ili sekta hiyo iwe
na mchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi.
Aidha, Rais Magufuli alitumia hafla hiyo kuwaeleza wanadiplomasia,
mafanikio ya Serikali ya mwaka 2018, mafanikio hayo ni Pamoja na Serikali
kuendelea kulinda na kudumisha amani ya nchi; kukuza uchumi wa nchi ambapo katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2018, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tano barani
Afrika, uchumi wake umekua kwa kasi ikizidiwa na Ethiopia pekee.
Tanzania pia iliweza kudhibiti mfumuko wa bei na iliongoza
katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji wa Dola za
Marekani bilioni 1.18.
Mafanikio mengine ni Pamoja na ujenzi wa Miundombinu
ikiwemo: ujenzi unaondelea wa reli ya kiwango cha Kimataifa kutoka Dar Es
Salaam hadi Dodoma; ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa Mega Watts 2100 katika Mto Rufiji; ujenzi na upanuzi wa barabara
mbalimbali nchini; ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria; upanuzi wa bandari
za Dar Es Salaam, Mtwara na Tanga na kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali
nchini ikiwemo ujenzi wa Terminal 3 kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Serikali pia imepiga hatua katika kuboresha utoaji
wa huduma za kijamii katika sekta ya afya, elimu na maji. Kwa upande wa afya,
bajeti ya sekta hiyo imeongezeka kutoka bilioni 31 hadi kufikia bilioni 270
ambapo ujenzi wa vituo vya afya 305 umekamilika na ujenzi wa hospitali 67 za
Wilaya unaendelea, ukilenga kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Kuhusu elimu, Serikali imeendelea na mpango wake wa
kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza bajeti ya
kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Aidha, Miundombinu ya maji
imeimarishwa ambapo upatikanaji wa maji kwa maeneo ya mijini umefikia asilimia
80 na asilimia 65 kwa maneo ya vijijini.
Rais Magufuli alieleza kuwa mafanikio ambayo
Serikali ya awamu ya tano inaendelea kuyapata yanatokana na Ushirikiano na
mchango mkubwa kutoka kwa wanadiplomasia, na kuahidi kuwa Serikali yake
itaendelea kudumisha Ushirikiano huo.
Alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa,
watumishi wengi wa Serikali walishahamia Makao Makuu ya Serikali jijini Dodoma
na kuelezea matumaini yake kuwa, baadhi ya Balozi zitakuwa zimeshaanza mchakato
wa kuhamia Dodoma, ukizingatia kuwa Serikali imetoa viwanja bure kwa ofisi zote
za balozi.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
09 Machi 2019
|