Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinaimarisha
mipango ya kujikomboa kiuchumi ili ziweze kuwa huru kweli na kuachana na
utegemezi.
"Viongozi wengi wa
Afrika wametambua kuwa mustakabali wa nchi zetu uko mikononi mwetu na kwamba
uhuru wa kisiasa hauwezi kuwa na maana sana endapo mataifa yetu yataendelea
kuwa tegemezi kiuchumi,hatuwezi kuwa na uhuru wetu wenyewe endapo mataifa yetu
yataendelea kuwa ombaomba," amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amesema hayo
jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje
wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Amesema kuwa kutafuta
ukombozi wa kiuchumi ndio jukumu ambalo liko mbele yao viongozI wa Bara la
Afrika na kuzitaka nchi za Afrika kuimarisha uhusiano na nchi za Nordic katika
maeneo ya uwekezaji wa kibiashara na viwanda ili kuondokana na utegemezi kwa
nchi nyingine.
Amezitaka nchi za Afrika kushirikiana
kuwekeza katika viwanda ili kuzalisha bidhaa
kutoka katika malighafi ambazo nchi zinauwezo wa kuwa nazo.
"Ni lazima kujenga
viwanda na kuchakata malighafi ambazo tutawauzia nchi nyingine na hivyo kuweza
kujikomboa kutoka katika utegemezi wa mataifa mengine, hatuwezi kuwa huru kama
tutaendelea kuwa na utegemezi kwa nchi zilizoendelea," alisisitiza mhe.
Rais
Amesema Nchi za
Afrika zina kitu kikubwa cha kujifunza
kutoka kwa nchi za Nordic ambazo zina
jumla ya watu milioni 27 huku Pato lao
kwa mwaka likiwa ni Dola za Marekani trilioni 1.7 huku Tanzania yenye watu ni milioni 55, mara
mbili zaidi ya nchi za Nordic ikiwa na pato
la taifa lenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 56.99.
"Tuna jambo kubwa la
kujifunza kwa nchi za Nordic Tanzania tuko mara mbili zaidi kwao pata letu
halifiki kwao, Tuko milioni 57 pata letu ni trillions 1.7 wenzetu wako milioni 27 pata lao ni trillions 1.6,"
alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa ni lazima Afrika ijifunze kutoka katika
nchi hizo ili kujua ni wapi zimekosea,
tuko hapa leo hii na hawa marafiki zetu tutumie nafasi hii kujifunza kutoka
kwao.
Ameongeza kuwa Pato la nchi za Afrika lina thamani ya
Dola za Marekani trilioni 2.334 huku pato la mtu mmoja likiwa ni wastani wa
Dola za Marekani 62,963. Lakini kwenye nchi za Afrika ni wastani wa Dola za
Marekani 1,945.
Amesema Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweeden;
licha ya kuwa na eneo dogo (kilomita za mraba milioni 3.5) na idadi ya watu
wapatao milioni 27 tu; zina uchumi mkubwa. Pato lao kwa mwaka jana (2018)
lilikuwa na thamani ya Dola za Marekani trilioni 1.7.
Amezishukuru nchi za
Nordic kwa kuliunga mkono bara la Afrika kuanzia wakati wa harakati za ukombozi
wa Afrika licha ya ukweli kwamba kwa wakati ule suala hilo lilikuwa gumu sana
lakini nchi za Nordic zilikuwepo.
Mhe. Rais amezikaribisha
nchi za Nordic, pamoja na mataifa mengine, yakiwemo ya Afrika, kuja kuwekeza
nchini Tanzania ambapo kuna mazingira wezeshi ya uwekezaji ni muafaka na
yanatabirika, kutokana na amani na utulivu wa kisiasa, lakini pia mwenendo wa
ukuaji wa uchumi ni mzuri ambapo, kwa sasa, ni wastani wa asilimia 7.