Na
Mwandishi wetu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kwa nyakati tofauti amekutana na
kufanya mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Denmark, Finaland na
Norway ambao wamekuja nchini kuhudhuria Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya
Nje wa nchi za Afrika na Nordic unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wamezungumzia na kukubaliana
kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri ya kirafiki na kihistoria yaliyopo
baina ya nchi hizo.
Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi amezieleza nchi
hizo kuhusu msimamo wa Serikali ya Tanzania katika kujiimarisha kiuchumi
kupitia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili iendelee kutoa elimu bure na bora kwa
watoto wa kitanzania, huduma bora za afya kwa watanzania, kuwezesha upatikanaji
wa maji safi na salama kwa wananchi wote na kufikisha huduma za Nishati kwa
watanzania wote hasa wa vijijini.
Amesema kwamba Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele
kwa Siasa za maendeleo ili kuhakikisha azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati na
wa viwanda inafikiwa.
“Tanzania haiangalii Siasa za nguvu, tunaangalia
Siasa za kuletea wananchi maendeleo, na kwa mpango huo tutaendelea kuimarisha
ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani na kumfanya kila mtanzania kulipa kodi ili
tuendelee kutoa elimu bure ya msingi na sekondari kwa watoto wa Kitanzania,
kuboresha huduma za afya hadi vijijini, upatikanaji wa maji safi na salama na
kuhakikisha huduma za nishati ya umeme zinawafikia watanzania wote hadi wa
vijijini,” alisema Prof. Kabudi.
Amewahahakishia mawaziri hapo kuwa Tanzania
itaendelea kuheshimu makubaliano ya Kimataifa hasa katika suala la wakimbizi na
kuwafanya watu wanaokuja kutafuta hifadhi za kisiasa nchini kwetu wana pata
hifadhi hizo.
Akizungumza alipokutana na Prof. Kabudi Waziri wa
Mambo ya Nje wa Denmark Mhe. Jeppe Koffod amemuhakikishia Prof. Kabudi Serikali
ya Denmark itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha
huduma za jamii kama vile utoaji wa elimu bure, huduma za afya na maji
salama.
Pia amesisitiza kwamba wataendelea kuunga mkono
mpango wa utoaji wa elimu ya ufundi nchini na kuwafanya vijana wa kike na wa
kiume Nchimbi kushiriki katika harakati za ujenzi wa taifa lao.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka
Haavisto ameahidi nchi yake kuendelea kuisaidia Tanzania katika maeneo ya
misitu, utawala bora, ukusanyaji mapato, haki za binadamu na Tehama.
Amesema Finland pia itaendelea kuisaidia Tanzania
kwenye Elimu kwakuwa Elimu imekuwa na mchango mkubwa na hivyo kutoa viongozi wa
baadae.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe.
Ine Eriksen Soreide ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kazi kubwa inayofanya
ya kupambana na rushwa na ufisadi na hivyo kuongeza imani ya Norway
kuwezesha zaidi nchini. Aidha, ameahidi kuwa nchi yake itaendeleza Ushirikiano
wake na Tanzania.
Prof. Kabudi pia amekutana na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Msumbiji Mhe. Jose Pacheco na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo
kuimaraisha mahusiano baina ya Msumbiji na Tanzania.
Mawaziri hao wako nchini kuhudhuria mkutano wa 18
wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 29 za Afrika na Nordic unaofanyika jijini
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.