Balozi wa Tanzania nchini India,
Mhe. Baraka Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi pamoja na Maafisa Ubalozi
wa nchi wanachama wa AALCO walioshiriki hafla ya maadhimisho ya miaka 63 ya kuanzishwa kwa shirika hilo, Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019.
=======================================================
Ushirikiano kati ya
Tanzania na Shirika la Mashauriano ya masuala ya Kisheria ya Nchi za Asia na
Afrika (AALCO) kuendelea kuimarika
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Balozi Baraka Luvanda
amemwakilisha Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria na Rais wa
sasa wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika
(Asia-Africa Legal Consultative Organization-AALCO) kwenye sherehe ya miaka 63
ya kuanzishwa kwake. Sherehe hiyo imefanyika Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba
2019 na kuhudhuriwa na nchi wanachama wageni waalikwa, wenyeji na mashirika ya
kimataifa yaliyopo New Delhi.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mhe. Mahiga, Balozi Luvanda
alielezea uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na AALCO na kueleza
kuwa utaendelea kudumishwa kwa manufaa ya pamoja.
AALCO ilianzishwa tarehe 15 Novemba 1956 kwa lengo la kuwa
chombo cha ushauri na ushirikiano katika masuala ya sheria za kimataifa kwa
nchi za Asia na Afrika. Toka kuanzishwa kwake AALCO imewezesha nchi wanachama
kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya sheria za
kimataifa na imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sheria za kimataifa.
Ushirikiano kati ya Tanzania na shirika hilo ulianza tangu mwaka
1965 ambapo Tanzania ilishiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa AALCO kama nchi
Mwangalizi na baadaye mnamo mwaka 1973 kama nchi mwanachama rasmi.
Mpaka sasa
Tanzania imeshaandaa Mikutano mikubwa 3 ya Mwaka ambapo Mkutano wa 25 wa AALCO
ulifanyika mwaka 1986 jijini Arusha, Mkutano wa 49 ulifanyika Jijini Dar es
Salaam mwaka 2010 na Mkutano wa 58 ulifanyika hivi karibuni, jijini Dar es
Salaam tarehe 21 hadi 25 Octoba 2019.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.