. Kawasaki kutoka Japan nayo yaonesha nia ya kuanzisha kiwanda kitakachohudumia soko la Afrika na Nje
ya Afrika
Katika kutekeleza Diplomasia ya
Uchumi, Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki umeambatana na wawekezaji kutoka
nchini humo kwa ajili ya kuwekeza katika viwanda mkoani Simiyu ambavyo
vinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 2000.
Uwekezaji
huo utajumuisha kiwanda cha nguo pamoja na kiwanda cha kutengeneza vyombo vya majumbani
ambao una thamani ya dola za kimarekani milioni 50. Viwanda hivyo vitajengwa katika
eneo la Isanga Mjini Bariadi Mkoani Simiyu na vinatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka
2020.
Akizungumza
na vyombo vya habari katika eneo ambalo linatarajiwa kujengwa viwanda hivyo
mkoani Simiyu, mwekezaji huyo kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram ameahidi
kujenga viwanda viwili kimojawapo kikiwa ni cha nguo na kingine cha kutengeneza
vyombo vya nyumbani ikiwemo vikombe, sahani na glasi.
Bw.
Albayram amesema ameridhishwa na mazingira ya uwekezaji baada ya kutembelea
maeneo mbalimbali kwa lengo la kuangalia mazingira wezeshi kwa uwekezaji wa
viwanda, akiwa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof.
Elizabeth Kiondo mkoani Simiyu.
Aidha
ameitaka serikali kutatua baadhi ya changamoto ili kuuwezesha uwekezaji huo
kufanyika ikiwa ni pamoja na miundombinu yote muhimu hususani ya umeme ili
uwekezaji huo uanze mara moja baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu
zinazohitajika ikiwa ni pamoja na usajili wa kampuni na kutafuta hati miliki ya
ardhi.
“Tumeamua
kuwekeza Simiyu, kila kitu kikienda sawa kiwanda cha nguo kinaweza kujengwa na
kufanya kazi ndani ya miezi tisa mpaka mwaka mmoja, kiwanda cha vyombo vya
nyumbani miezi nane baada ya usajili wa kampuni nitarudi tena Simiyu
kukamilisha masuala ya hati miliki ya ardhi, sitaki kumuangusha Mhe. Balozi
maana amefanya mengi kwa ajili yetu,” alisema Albayram.
Nae
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo amesema mwekezaji
ameridhishwa na eneo hilo na kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kutoa
ardhi ya kujenga viwanda hivyo huku akibainisha kuwa ombi kubwa la mwekezaji ni
upatikanaji wa nishati ya kutosha kwa kuwa viwanda hivyo hutumia umeme mwingi.
Balozi
Kiondo ameongeza kuwa, hayo ni matokeo ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi
kwa vitendo, hivyo Ubalozi utaedelea kuhamasisha wawekezaji wengine zaidi kuja
kuweza nchini, hatimaye kufanikisha azma ya uchumi wa viwanda.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka alimhakikishia mwekezaji
huyo upatikanaji wa mahitaji yote muhimu na kuahidi kushirikiana na taasisi za
Serikali zinazohusika kuhakikisha anapata huduma zote kwa wakati na pasipo urasimu
wowote.
Kuhusu
suala la Umeme Mtaka amesema katika Bajeti ya mwaka 2019/20 Wizara ya Nishati
kupitia Shirika la umeme TANESCO imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo
cha kupozea umeme (substation) ambacho kitajengwa karibu na eneo la uwekezaji
huo.
Mtaka
ameongeza kuwa mtazamo wa mkoa wa Simiyu ni kuwa na viwanda vichache vitakavyoajiri
maelfu ya watanzania badala ya kuwa na viwanda vingi vinavyoajiri watu wachache
ili kuwezesha watanzania wengi kupata ajira.
Wakati
huohuo, Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa wakulima wa pamba kulima pamba kwa wingi
kwa kuwa kiwanda cha nguo kitakuwa mkombozi wa kuongeza thamani ya zao la pamba
na itauzwa kwa bei ya uhakika.
Naye
Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa pamba nchini, Bw. Boaz Ogola amesema kujengwa
kwa kiwanda cha nguo mkoani Simiyu kutasaidia wakulima wa pamba kupata soko la
uhakika kuondoa changamoto ya bei ya pamba kwa kuwa kitapanua wigo wa soko la
pamba, ambapo pamba inayotumika ni chini ya asilimia 20 - 25 ya pamba yote
inayozalishwa nchini.
Katika
tukio jingine kampuni ya Kawasaki Heavy Industries Ltd kutoka Japan imeonesha
nia ya kuanzisha kiwanda nchini ambapo kiwanda hicho kitahudumia soko la Afrika
na Nje ya Afrika.
Kawasaki
Heavy Industries Ltd ni kampuni nchini Japan ambapo imewekeza katika sekta
mbalimbali kama vile sekta ya usafiri (anga, reli na majini) nishati (cogeneration, energy plants, gas
tuibines, gas engines), vifaa vya viwandani (hydraulic components and systems,
robotics, industrial plants, environmental and recycling), pamoja na leisure
(motorcycle, off-road four wheel,JET SKI).
Naibu
Meneja wa Idara ya Mkakati wa Kimataifa, Kitengo cha Biashara cha Kampuni ya
Kawasaki Bw. Michio Kambe anatarajia kufanya ziara nchini Tanzania kuanzia
tarehe 21 hadi 26 Novemba 2019 ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Kituo
cha Uwekezaji Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji na Waziri wa Viwanda
na Biashara.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.