Tuesday, November 5, 2019

Rais Xi atembelea Banda la Tanzania Maonesho ya Pili ya Bidhaa za Nje.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Xi atembelea Banda la Tanzania Maonesho ya Pili ya Bidhaa za Nje.   
Dar Es Salaam, 05 Novemba 2019
Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje (China International Importation Expo) yamefunguliwa na Rais wa China, Mhe Xi Jinping tarehe 05 Novemba 2019.  Maonesho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Mataifa 64 akiwemo Rais wa Ufaransa Mhe Emmanuel Macron, Mawaziri Wakuu wa Jamaica; Serbia na Greece. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Innocent Bashungwa.

Baada ya kufungua maonesho hayo Rais wa China ametembelea Mabanda ya nchi tano likiwemo Banda la Tanzania.  Nchi nyingine ambazo Rais Xi ametembelea mabanda yao ni Ufaransa; Ugiriki; Serbia na Jamaica.

Katika ziara ya kutembelea Banda la Tanzania, Rais Xi Jinping alifuatana na Waziri Mkuu wa Jamaica; Greece na Serbia na kupokelewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Innocent Bashungwa na alitumia muda wa dakika 10 katika banda la Tanzania.  Rais Xi na wageni wake walipata maelezo kuhusu bidhaa mbalimbali za kilimo na madini zinazopatikana nchini Tanzania na vivutio vya utalii. Vile vile, Rais Xi alipokea salamu salaamu za  Mhe Rais Dk John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake Rais wa China ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje na ametuma salaamu za pongezi kwa Mhe Rais Magufuli kwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na China.  Aidha, Rais Xi alivutiwa zaidi na bidhaa ya korosho za Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo alitaka kufahamu zaidi juu ya upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko la China na bei ya Tanzanite. Alipewa majibu ya kutosha.

Maonesho ya Kimataifa yataendelea hadi tarehe 10 Novemba 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Banda la Tanzania
Banda la Tanzania lilivyopendeza

Bidhaa za Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje nchini China
Bidhaa za Tanzania zikiwa katika vifungashio bora kabisa zilivutia watu wengi katika maonesho hayo.

 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.