Picha ya pamoja
==================================================================
Mabalozi
wa nchi za SADC, New Delhi waendelea kupaza sauti kupinga vikwazo dhidi ya
Zimbabwe
Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliopo nchini India chini ya Uenyekiti
wa Mhe. Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini humo walikutana katika hafla
ya Siku ya SADC (SADC Day), iliyofanyika nyumbani kwa Balozi Luvanda jijini New
Delhi, India tarehe 2 Novemba 2019.
Wakati wa hafla hiyo, Mhe.
Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuelezea pamoja na mambo mengine, suala la
kuondolewa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi za Ulaya dhidi ya
Zimbabwe. Alieleza kuwa Tamko dhidi ya vikwazo hivyo liliwasilishwa rasmi
kwenye Mamlaka za Serikali ya India siku ya tarehe 25 Oktoba 2019 siku ambayo
iliamuliwa na Viongozi Wakuu wa Nchi za SADC kuwa siku maalum ya kupaza sauti
dhidi ya vikwazo hivyo.
Kwa upande wake, Mgeni rasmi
katika shughuli hiyo, Mkurugenzi katika Wizara ya Nje ya India, Sehemu ya
Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bwana Rajesh Swami alieleza kuwa kwa
miaka mingi uhusiano baina ya India na nchi za SADC umekuwa mzuri na kuwezesha
biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na uhusiano wa mtu na mtu kuimarika
kwa kiwango cha juu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni
Maalum, Mhe. Fortune Chasi, Waziri wa Nishati wa Zimbabwe, alimshukuru Balozi
Luvanda, Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za SADC nchini India na Mabalozi wote wa
nchi za SADC nchini humo kwa kuandaa hafla hiyo na jinsi walivyosimamia suala
la kupaza sauti kupinga vikwazo dhidi ya nchi yake na kuwaomba waendelee na
juhudi hizo hadi vikwazo hivyo vitakapoondolewa.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.