Friday, November 8, 2019

IMARISHENI MIPANGO YA KUJIKOMBOA KIUCHUMI ILI KUACHAANA NA UTEGEMEZI- RAIS MAGUFULI AZIAMBIA NCHI ZA AFRIKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amezitaka  nchi za Afrika kuhakikisha zinaimarisha mipango ya kujikomboa kiuchumi ili ziweze kuwa huru kweli na kuachana na utegemezi.

"Viongozi wengi wa Afrika wametambua kuwa mustakabali wa nchi zetu uko mikononi mwetu na kwamba uhuru wa kisiasa hauwezi kuwa na maana sana endapo mataifa yetu yataendelea kuwa tegemezi kiuchumi,hatuwezi kuwa na uhuru wetu wenyewe endapo mataifa yetu yataendelea kuwa ombaomba," amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika kwa mara ya kwanza nchini.

Amesema kuwa kutafuta ukombozi wa kiuchumi ndio jukumu ambalo liko mbele yao viongozI wa Bara la Afrika na kuzitaka nchi za Afrika kuimarisha uhusiano na nchi za Nordic katika maeneo ya uwekezaji wa kibiashara na viwanda ili kuondokana na utegemezi kwa nchi nyingine.

Amezitaka nchi za Afrika kushirikiana kuwekeza katika viwanda ili  kuzalisha bidhaa kutoka katika malighafi ambazo nchi zinauwezo wa kuwa nazo.

"Ni lazima kujenga viwanda na kuchakata malighafi ambazo tutawauzia nchi nyingine na hivyo kuweza kujikomboa kutoka katika utegemezi wa mataifa mengine, hatuwezi kuwa huru kama tutaendelea kuwa na utegemezi kwa nchi zilizoendelea," alisisitiza mhe. Rais

Amesema Nchi za Afrika  zina kitu kikubwa cha kujifunza kutoka kwa nchi za  Nordic ambazo zina jumla ya watu milioni 27  huku Pato lao kwa mwaka likiwa ni Dola za Marekani trilioni 1.7  huku Tanzania yenye watu ni milioni 55, mara mbili zaidi ya nchi za Nordic  ikiwa na pato la taifa lenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 56.99.

"Tuna jambo kubwa la kujifunza kwa nchi za Nordic Tanzania tuko mara mbili zaidi kwao pata letu halifiki kwao, Tuko milioni 57 pata letu ni trillions 1.7 wenzetu  wako milioni 27 pata lao ni trillions 1.6," alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa ni lazima Afrika ijifunze kutoka katika nchi hizo ili kujua ni  wapi zimekosea, tuko hapa leo hii na hawa marafiki zetu tutumie nafasi hii kujifunza kutoka kwao.

Ameongeza kuwa Pato la nchi za Afrika lina thamani ya Dola za Marekani trilioni 2.334 huku pato la mtu mmoja likiwa ni wastani wa Dola za Marekani 62,963. Lakini kwenye nchi za Afrika ni wastani wa Dola za Marekani 1,945.
Amesema Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweeden; licha ya kuwa na eneo dogo (kilomita za mraba milioni 3.5) na idadi ya watu wapatao milioni 27 tu; zina uchumi mkubwa. Pato lao kwa mwaka jana (2018) lilikuwa na thamani ya Dola za Marekani trilioni 1.7.

Amezishukuru nchi za Nordic kwa kuliunga mkono bara la Afrika kuanzia wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika licha ya ukweli kwamba kwa wakati ule suala hilo lilikuwa gumu sana lakini nchi za Nordic zilikuwepo.

Mhe. Rais amezikaribisha nchi za Nordic, pamoja na mataifa mengine, yakiwemo ya Afrika, kuja kuwekeza nchini Tanzania ambapo kuna mazingira wezeshi ya uwekezaji ni muafaka na yanatabirika, kutokana na amani na utulivu wa kisiasa, lakini pia mwenendo wa ukuaji wa uchumi ni mzuri ambapo, kwa sasa, ni wastani wa asilimia 7.  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete mara baada ya kufungua mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania katika mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre(JNICC) jijini Dar es Salaam


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza wakati akifungua Mkutano  wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika - Nordic katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam

Waziri wa mambo ya nje wa Norway Ine Marie Eriksen Sereide akizungumza wakati akifungua Mkutano  wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika - Nordic katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe akifungua Mkutano  wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.