Friday, November 1, 2019

Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika, Nordic

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic (Norway, Denmark, Finland, Sweden na Iceland) unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Novemba 2019 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Akiongea na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe alisema kuwa mkutano huu utafunguliwa rasmi na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambapo hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.
Kwa mujibu wa Dkt. Mnyepe, mkutano huu utajumuisha jumla ya mawaziri 34 wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic pamoja na washiriki wengine ambao idadi yao inatarajiwa kufikia 250. Mawaziri watakaokuja kutoka nchi za Nordic ni wa nchi za Sweden, Norway, Denmark, Finland na Iceland. Kutoka nchi za Afrika watakuja Mawaziri wa Algeria, Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Comoros na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Nyingine ni pamoja na Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Lesotho, Mali, Malawi, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Niger, Rwanda, Senegal, Somalia, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda, Zambia, Zimbabwe na sisi wenyeji Tanzania. Aidha, mkutano huo utajumuisha Mawaziri, Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika katika nchi za Nordic, Mabalozi wa nchi za Nordic hapa nchini pamoja na watendaji wa Serikali. Kauli mbiu ya mkutano huu ni: "Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu"
"Mkutano huu unafanyika hapa Tanzania kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za Nordic ni wa kihistoria na wa kipekee. Ushirikiano huu ulianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika ambapo Wamisionari kutoka nchi hizo walikuja kufanya kazi hapa nchini kwenye sekta za afya na elimu. Katika sekta ya elimu, nchi hizo zilianzisha Kituo cha Kilimo cha Uyole na Kituo cha Elimu cha Kibaha kupitia Mradi wa Nordic-Tanganyika Project.

Ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Nordic ulichangiwa kwa kiwango kikubwa na falsafa zilizokuwa zinafanana kuhusu maendeleo ya watu, ukombozi wa Afrika, urafiki miongoni mwa viongozi wetu na nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika Bara la Afrika," alisema Dkt. Mnyepe
Katibu Mkuu aliongeza kuwa, "katika nchi za Afrika, Tanzania inapokea misaada mingi kutoka nchi za Nordic kuliko nchi nyingine yoyote. Kwa mfano kwa miaka mitano ya kuanzia mwaka 2013 hadi 2018, Tanzania imepokea takribani Shilingi za Kitanzania bilioni 900 kutoka nchi za Nordic. Nchi hizo zimekuwa zikisaidia sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo: elimu; afya; miundombinu; nishati; TEHAMA; utafiti; ukusanyaji wa kodi; bajeti; misitu; usawa wa jinsia; utunzaji wa mazingira; na ukuzaji wa sekta ya biashara,".

"Kufuatia ushirikiano huu wa kihistoria kati ya Tanzania na nchi za Nordic, nchi hizo ziliiomba Serikali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu kutokana na mahusiano na mazuri yaliyopo na hatua za kasi za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Kutokana na urafiki na historia hiyo hiyo Serikali ya Tanzania ilikubali kuwa mwenyeji wa mkutano wa mkutano huo na utafunguliwa na Mheshimiwa Rais. Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni, Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu," aliongeza Katibu Mkuu 
Aidha, mkutano huu, utajadili fursa za uwekezaji, biashara, amani na usalama na masuala mengine mtambuka, kama vile athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika mkutano huu, tutazungumzia pia mahusiano baina yetu na nchi moja moja hususan ubia wa kimaendeleo. Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano, wenzetu wa Afrika na Nordic watapenda pia kusikia uzoefu na mafanikio ya Tanzania kwenye sekta za afya, elimu, nishati, miundombinu, kilimo, utalii, ukusanyaji wa kodi, mafanikio ya vita dhidi ya rushwa, ujangili, madawa ya kulevya na maeneo mengine. 
Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen alisema kuwa mkutano huu utatoa pia fursa ya mazungumzo ya uwili (bilateral meetings) kati ya nchi za Nordic na nchi za Afrika.
"Ni imani yangu kuwa kupitia mkutano huu tutaweza kujadilili mambo mbalimbali ikiwemo hatua za kimaendeleo zilizofikiwa katika sekta mbalimbali hususan afya, huduma za kijamii, elimu na mazingira kibiashara na uwekezaji kwani Tanzania imekuwa na mahusiano mazuri na nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Nordic," alisema Balozi Elisabeth.  
Nae Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg alisema kuwa mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Sweden mwaka 2001 ambapo baada ya hapo mikutano kama hii ilikuwa inafanyika kwa kupokezana kutoka Bara la Afrika na nchi za Nordic. 
"Kwanza kabisa naipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, ni fursa kutumia mkutano huu kujadili masuala ya kibiashara, uwekezaji, amani na usalama kwa maslahi ya nchi za Afrika na Nordic," alisema Balozi Sjoberg. 

Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe alipokuwa akiongelea Mkutano wa 18 wa mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika na nchi za Nirdic jijini Dar es Salaam leo
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe na kulia ni  Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg.  
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano. Kushoto ni Mkuu wa Itifaki Kanali Wilbert Augustine Ibuge, akifuatiwa na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen. Kulia ni Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg. 
Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano, katikati ni Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen na kushoto ni Kushoto ni Mkuu wa Itifaki Kanali Wilbert Augustine Ibuge






No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.