Thursday, November 21, 2019

MKUTANO WA 39 BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC WAANZA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeanza leo jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kukubaliana na agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Februari, 2020.

Mkutano huo wa siku saba umeanza leo kwa ngazi ya maofisa waandamizi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na utafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu kisha kuhitimishwa na Mawaziri wa Wizara za Kisekta zinazohusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki Novemba 27, 2019.

Ajenda za mkutano huo zinakadiriwa kuwa tisa ambazo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.

Agenda nyingine ni taarifa ya Baraza kwa Wakuu wa Nchi kuhusu utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayofiwa kwenye mikutano ya Wakuu hao wa Nchi na Kalenda ya Matukio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha kuishia mwezi Juni 2019.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini. 



Baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri ulioanza leo jijini Arusha kwa ngazi ya maofisa waandamizi
Baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri ulioanza leo jijini Arusha kwa ngazi ya maofisa waandamizi

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.