Friday, November 8, 2019

IMARISHENI MIPANGO YA KUJIKOMBOA KIUCHUMI ILI KUACHAANA NA UTEGEMEZI- RAIS MAGUFULI AZIAMBIA NCHI ZA AFRIKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amezitaka  nchi za Afrika kuhakikisha zinaimarisha mipango ya kujikomboa kiuchumi ili ziweze kuwa huru kweli na kuachana na utegemezi.

"Viongozi wengi wa Afrika wametambua kuwa mustakabali wa nchi zetu uko mikononi mwetu na kwamba uhuru wa kisiasa hauwezi kuwa na maana sana endapo mataifa yetu yataendelea kuwa tegemezi kiuchumi,hatuwezi kuwa na uhuru wetu wenyewe endapo mataifa yetu yataendelea kuwa ombaomba," amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika kwa mara ya kwanza nchini.

Amesema kuwa kutafuta ukombozi wa kiuchumi ndio jukumu ambalo liko mbele yao viongozI wa Bara la Afrika na kuzitaka nchi za Afrika kuimarisha uhusiano na nchi za Nordic katika maeneo ya uwekezaji wa kibiashara na viwanda ili kuondokana na utegemezi kwa nchi nyingine.

Amezitaka nchi za Afrika kushirikiana kuwekeza katika viwanda ili  kuzalisha bidhaa kutoka katika malighafi ambazo nchi zinauwezo wa kuwa nazo.

"Ni lazima kujenga viwanda na kuchakata malighafi ambazo tutawauzia nchi nyingine na hivyo kuweza kujikomboa kutoka katika utegemezi wa mataifa mengine, hatuwezi kuwa huru kama tutaendelea kuwa na utegemezi kwa nchi zilizoendelea," alisisitiza mhe. Rais

Amesema Nchi za Afrika  zina kitu kikubwa cha kujifunza kutoka kwa nchi za  Nordic ambazo zina jumla ya watu milioni 27  huku Pato lao kwa mwaka likiwa ni Dola za Marekani trilioni 1.7  huku Tanzania yenye watu ni milioni 55, mara mbili zaidi ya nchi za Nordic  ikiwa na pato la taifa lenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 56.99.

"Tuna jambo kubwa la kujifunza kwa nchi za Nordic Tanzania tuko mara mbili zaidi kwao pata letu halifiki kwao, Tuko milioni 57 pata letu ni trillions 1.7 wenzetu  wako milioni 27 pata lao ni trillions 1.6," alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa ni lazima Afrika ijifunze kutoka katika nchi hizo ili kujua ni  wapi zimekosea, tuko hapa leo hii na hawa marafiki zetu tutumie nafasi hii kujifunza kutoka kwao.

Ameongeza kuwa Pato la nchi za Afrika lina thamani ya Dola za Marekani trilioni 2.334 huku pato la mtu mmoja likiwa ni wastani wa Dola za Marekani 62,963. Lakini kwenye nchi za Afrika ni wastani wa Dola za Marekani 1,945.
Amesema Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweeden; licha ya kuwa na eneo dogo (kilomita za mraba milioni 3.5) na idadi ya watu wapatao milioni 27 tu; zina uchumi mkubwa. Pato lao kwa mwaka jana (2018) lilikuwa na thamani ya Dola za Marekani trilioni 1.7.

Amezishukuru nchi za Nordic kwa kuliunga mkono bara la Afrika kuanzia wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika licha ya ukweli kwamba kwa wakati ule suala hilo lilikuwa gumu sana lakini nchi za Nordic zilikuwepo.

Mhe. Rais amezikaribisha nchi za Nordic, pamoja na mataifa mengine, yakiwemo ya Afrika, kuja kuwekeza nchini Tanzania ambapo kuna mazingira wezeshi ya uwekezaji ni muafaka na yanatabirika, kutokana na amani na utulivu wa kisiasa, lakini pia mwenendo wa ukuaji wa uchumi ni mzuri ambapo, kwa sasa, ni wastani wa asilimia 7.  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete mara baada ya kufungua mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania katika mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre(JNICC) jijini Dar es Salaam


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza wakati akifungua Mkutano  wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika - Nordic katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam

Waziri wa mambo ya nje wa Norway Ine Marie Eriksen Sereide akizungumza wakati akifungua Mkutano  wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika - Nordic katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe akifungua Mkutano  wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam

Thursday, November 7, 2019

PROF. KABUDI AKUTANA NA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NORWAY, FINLAND NA DENMARK

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Mhe. Jeppe Kofod wakati walipokutana ofisini jijini Dar es Salaam. Mawaziri hao wapo Dar es Salaam kuhudhuria mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 29 za Afrika na Nordic unaofanyika nchini. 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Mhe. Jeppe Kofod akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) wakati walipokutana jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkabidhi zawadi ya kamusi ya Kiswahili - Kiingereza Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Mhe. Jeppe Kofod wakati walipokutana jijini Dar es Salaam.  
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka Haavisto walipokutana jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka Haavisto akifafanua jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) wakati walipokutana jijini Dar es Salaam 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkabidhi zawadi ya kamusi ya Kiswahili - Kiingereza Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka Haavisto walipokutana jijini Dar es Salaam. Tukio hili lilishuhudiwa na Balozi wa Tanzania katika nchi za Nordic, Mhe. Dkt. Wilbroad Slaa na Naibu Katibu Mkuu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhan Mwinyi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Ine Eriksen Soreide walipokutana jijini Dar es Salaam.  
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkabidhi zawadi ya kamusi ya Kiswahili - Kiingereza Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Ine Eriksen Soreide walipokutana jijini Dar es Salaam.  
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Msumbiji Mhe. Jose Pacheco akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) walipokutana jijini Dar es Salaam.  

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Denmark, Finaland na Norway ambao wamekuja nchini kuhudhuria Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao wamezungumzia na kukubaliana  kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri ya kirafiki na kihistoria yaliyopo baina ya nchi hizo.

Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi amezieleza nchi hizo kuhusu msimamo wa Serikali ya Tanzania katika kujiimarisha kiuchumi kupitia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili iendelee kutoa elimu bure na bora kwa watoto wa kitanzania, huduma bora za afya kwa watanzania, kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wote na kufikisha huduma za Nishati kwa watanzania wote hasa wa vijijini.

Amesema kwamba Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele kwa Siasa za maendeleo ili kuhakikisha azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati na wa viwanda inafikiwa.

“Tanzania haiangalii Siasa za nguvu, tunaangalia Siasa za kuletea wananchi maendeleo, na kwa mpango huo tutaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani na kumfanya kila mtanzania kulipa kodi ili tuendelee kutoa elimu bure ya msingi na sekondari kwa watoto wa Kitanzania, kuboresha huduma za afya hadi vijijini, upatikanaji wa maji safi na salama na kuhakikisha huduma za nishati ya umeme zinawafikia watanzania wote hadi wa vijijini,” alisema Prof. Kabudi.


Amewahahakishia mawaziri hapo kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu makubaliano ya Kimataifa hasa katika suala la wakimbizi na kuwafanya watu wanaokuja kutafuta hifadhi za kisiasa nchini kwetu wana pata hifadhi hizo.

Akizungumza alipokutana na Prof. Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Mhe. Jeppe Koffod amemuhakikishia Prof. Kabudi Serikali ya Denmark itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha huduma za jamii kama vile utoaji wa elimu bure, huduma za afya na maji salama. 
Pia amesisitiza kwamba wataendelea kuunga mkono mpango wa utoaji wa elimu ya ufundi nchini na kuwafanya vijana wa kike na wa kiume Nchimbi kushiriki katika harakati za ujenzi wa taifa lao.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka Haavisto ameahidi nchi yake kuendelea kuisaidia Tanzania katika maeneo ya misitu, utawala bora, ukusanyaji mapato, haki za binadamu na Tehama.

Amesema Finland pia itaendelea kuisaidia Tanzania kwenye Elimu kwakuwa Elimu imekuwa na mchango mkubwa na hivyo kutoa viongozi wa baadae. 

Naye Waziri  wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Ine Eriksen Soreide ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kazi kubwa inayofanya ya kupambana na rushwa na ufisadi na hivyo kuongeza imani ya  Norway kuwezesha zaidi nchini. Aidha, ameahidi kuwa nchi yake itaendeleza Ushirikiano wake na Tanzania.

Prof. Kabudi pia amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji Mhe. Jose Pacheco na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo kuimaraisha mahusiano baina ya Msumbiji na Tanzania.

Mawaziri hao wako nchini kuhudhuria mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 29 za Afrika na Nordic unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Wednesday, November 6, 2019

Job Announcement at Organisation for the Prohibition of Chemical Weapons (OPCW)





PRESS RELEASE

Job Announcement at Organisation for the Prohibition of Chemical Weapons. 


Dodoma, 06 November, 2019 

The Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation has received vacancy notification from Organisation for the Prohibition of Chemical Weapons (OPCW) inviting qualified Tanzanians to apply for the post of Legal Adviser (Director) (D-2)


For more details on the vacant post kindly click HERE

Closing date for application is 16th October 2019. 


Issued by;
Government Communication Unit,
Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation,

Tuesday, November 5, 2019

MABALOZI WA NCHI ZA SADC, NEW DELHI WAENDELEA KUPAZA SAUTI KUPINGA VIKWAZO DHIDI YA ZIMBABWE

Balozi wa Tanzania nchini India na Mwenyekiti wa Kundi la Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Baraka Luvanda, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya SADC (SADC Day) yaliyofanyika Jijini New Delhi tarehe 02 Novemba 2019.
Wageni waalikwa wakimsikiliza Mhe. Balozi Luvanda (hayupo pichani) alipohutubia wakati wa hafla ya SADC Day
Mhe. Fortune Chasi, Waziri wa Nishati wa Zimbabwe na Mgeni Maalum akihutubia wakati wa hafla ya Siku ya SADC iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa Tanzania nchini, Jijini New Delhi tarehe 02 Novemba 2019

Mgeni rasmi wa hafla ya Siku ya SADC, Bwana Rajesh Swami, Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Sehemu ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika akihutubia wakati wa hafla ya Siku ya SADC iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa Tanzania nchini India, Jijini New Delhi tarehe 02 Novemba 2019.
Mhe. Balozi Luvanda akiwa na Mabalozi na Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya Siku ya SADC

Balozi Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Fortune Chasi, Waziri wa Nishati wa Zimbabwe ambaye alishiriki hafla ya Siku ya SADC kama Mgeni Maalum

Picha ya pamoja 
==================================================================

Mabalozi wa nchi za SADC, New Delhi waendelea kupaza sauti kupinga vikwazo dhidi ya Zimbabwe

Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliopo nchini India chini ya Uenyekiti wa Mhe. Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini humo walikutana katika hafla ya Siku ya SADC (SADC Day), iliyofanyika nyumbani kwa Balozi Luvanda jijini New Delhi, India tarehe 2 Novemba 2019.

Wakati wa hafla hiyo, Mhe. Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuelezea pamoja na mambo mengine, suala la kuondolewa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi za Ulaya dhidi ya Zimbabwe. Alieleza kuwa Tamko dhidi ya vikwazo hivyo liliwasilishwa rasmi kwenye Mamlaka za Serikali ya India siku ya tarehe 25 Oktoba 2019 siku ambayo iliamuliwa na Viongozi Wakuu wa Nchi za SADC kuwa siku maalum ya kupaza sauti dhidi ya vikwazo hivyo.

Kwa upande wake, Mgeni rasmi katika shughuli hiyo, Mkurugenzi katika Wizara ya Nje ya India, Sehemu ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bwana Rajesh Swami alieleza kuwa kwa miaka mingi uhusiano baina ya India na nchi za SADC umekuwa mzuri na kuwezesha biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na uhusiano wa mtu na mtu kuimarika kwa kiwango cha juu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Maalum, Mhe. Fortune Chasi, Waziri wa Nishati wa Zimbabwe, alimshukuru Balozi Luvanda, Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za SADC nchini India na Mabalozi wote wa nchi za SADC nchini humo kwa kuandaa hafla hiyo na jinsi walivyosimamia suala la kupaza sauti kupinga vikwazo dhidi ya nchi yake na kuwaomba waendelee na juhudi hizo hadi vikwazo hivyo vitakapoondolewa.

Rais Xi atembelea Banda la Tanzania Maonesho ya Pili ya Bidhaa za Nje.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Xi atembelea Banda la Tanzania Maonesho ya Pili ya Bidhaa za Nje.   
Dar Es Salaam, 05 Novemba 2019
Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje (China International Importation Expo) yamefunguliwa na Rais wa China, Mhe Xi Jinping tarehe 05 Novemba 2019.  Maonesho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Mataifa 64 akiwemo Rais wa Ufaransa Mhe Emmanuel Macron, Mawaziri Wakuu wa Jamaica; Serbia na Greece. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Innocent Bashungwa.

Baada ya kufungua maonesho hayo Rais wa China ametembelea Mabanda ya nchi tano likiwemo Banda la Tanzania.  Nchi nyingine ambazo Rais Xi ametembelea mabanda yao ni Ufaransa; Ugiriki; Serbia na Jamaica.

Katika ziara ya kutembelea Banda la Tanzania, Rais Xi Jinping alifuatana na Waziri Mkuu wa Jamaica; Greece na Serbia na kupokelewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Innocent Bashungwa na alitumia muda wa dakika 10 katika banda la Tanzania.  Rais Xi na wageni wake walipata maelezo kuhusu bidhaa mbalimbali za kilimo na madini zinazopatikana nchini Tanzania na vivutio vya utalii. Vile vile, Rais Xi alipokea salamu salaamu za  Mhe Rais Dk John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake Rais wa China ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje na ametuma salaamu za pongezi kwa Mhe Rais Magufuli kwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na China.  Aidha, Rais Xi alivutiwa zaidi na bidhaa ya korosho za Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo alitaka kufahamu zaidi juu ya upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko la China na bei ya Tanzanite. Alipewa majibu ya kutosha.

Maonesho ya Kimataifa yataendelea hadi tarehe 10 Novemba 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Banda la Tanzania
Banda la Tanzania lilivyopendeza

Bidhaa za Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje nchini China
Bidhaa za Tanzania zikiwa katika vifungashio bora kabisa zilivutia watu wengi katika maonesho hayo.

 



Monday, November 4, 2019

PROF. KABUDI AKUTANA NA MABOLOZI WA NCHI ZA AFRIKA NA NORDIC WALIOPO NCHINI, WAANDISHI WA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika kikao cha pamoja na mabalozi kutoka nchi za Afrika na Nordic wakizungumzia maandalizi ya mkutano wa 18 wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic utakaofanyika tarehe 7 - 8 Novemba 2019 jijini Dar es Salaam
Baadhi ya mabalozi kutoka nchi za Afrika na Nordic wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Hayupo pichani) wakati alipokutana nao kuzungumzia maandalizi ya mkutano wa 18 wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic utakaofanyika jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)  akizungumza na waandishi wa habari kuwaelezea maandalizi ya mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic unaotarajiwa kufanyika tarehe 7 - 8 Novemba 2019 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)  akiwaelezea waandishi wa habari maandalizi ya mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic unaotarajiwa kufanyika tarehe 7 - 8 Novemba 2019 jijini Dar es Salaam





Friday, November 1, 2019

Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika, Nordic

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic (Norway, Denmark, Finland, Sweden na Iceland) unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Novemba 2019 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Akiongea na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe alisema kuwa mkutano huu utafunguliwa rasmi na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambapo hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.
Kwa mujibu wa Dkt. Mnyepe, mkutano huu utajumuisha jumla ya mawaziri 34 wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic pamoja na washiriki wengine ambao idadi yao inatarajiwa kufikia 250. Mawaziri watakaokuja kutoka nchi za Nordic ni wa nchi za Sweden, Norway, Denmark, Finland na Iceland. Kutoka nchi za Afrika watakuja Mawaziri wa Algeria, Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Comoros na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Nyingine ni pamoja na Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Lesotho, Mali, Malawi, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Niger, Rwanda, Senegal, Somalia, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda, Zambia, Zimbabwe na sisi wenyeji Tanzania. Aidha, mkutano huo utajumuisha Mawaziri, Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika katika nchi za Nordic, Mabalozi wa nchi za Nordic hapa nchini pamoja na watendaji wa Serikali. Kauli mbiu ya mkutano huu ni: "Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu"
"Mkutano huu unafanyika hapa Tanzania kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za Nordic ni wa kihistoria na wa kipekee. Ushirikiano huu ulianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika ambapo Wamisionari kutoka nchi hizo walikuja kufanya kazi hapa nchini kwenye sekta za afya na elimu. Katika sekta ya elimu, nchi hizo zilianzisha Kituo cha Kilimo cha Uyole na Kituo cha Elimu cha Kibaha kupitia Mradi wa Nordic-Tanganyika Project.

Ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Nordic ulichangiwa kwa kiwango kikubwa na falsafa zilizokuwa zinafanana kuhusu maendeleo ya watu, ukombozi wa Afrika, urafiki miongoni mwa viongozi wetu na nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika Bara la Afrika," alisema Dkt. Mnyepe
Katibu Mkuu aliongeza kuwa, "katika nchi za Afrika, Tanzania inapokea misaada mingi kutoka nchi za Nordic kuliko nchi nyingine yoyote. Kwa mfano kwa miaka mitano ya kuanzia mwaka 2013 hadi 2018, Tanzania imepokea takribani Shilingi za Kitanzania bilioni 900 kutoka nchi za Nordic. Nchi hizo zimekuwa zikisaidia sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo: elimu; afya; miundombinu; nishati; TEHAMA; utafiti; ukusanyaji wa kodi; bajeti; misitu; usawa wa jinsia; utunzaji wa mazingira; na ukuzaji wa sekta ya biashara,".

"Kufuatia ushirikiano huu wa kihistoria kati ya Tanzania na nchi za Nordic, nchi hizo ziliiomba Serikali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu kutokana na mahusiano na mazuri yaliyopo na hatua za kasi za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Kutokana na urafiki na historia hiyo hiyo Serikali ya Tanzania ilikubali kuwa mwenyeji wa mkutano wa mkutano huo na utafunguliwa na Mheshimiwa Rais. Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni, Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu," aliongeza Katibu Mkuu 
Aidha, mkutano huu, utajadili fursa za uwekezaji, biashara, amani na usalama na masuala mengine mtambuka, kama vile athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika mkutano huu, tutazungumzia pia mahusiano baina yetu na nchi moja moja hususan ubia wa kimaendeleo. Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano, wenzetu wa Afrika na Nordic watapenda pia kusikia uzoefu na mafanikio ya Tanzania kwenye sekta za afya, elimu, nishati, miundombinu, kilimo, utalii, ukusanyaji wa kodi, mafanikio ya vita dhidi ya rushwa, ujangili, madawa ya kulevya na maeneo mengine. 
Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen alisema kuwa mkutano huu utatoa pia fursa ya mazungumzo ya uwili (bilateral meetings) kati ya nchi za Nordic na nchi za Afrika.
"Ni imani yangu kuwa kupitia mkutano huu tutaweza kujadilili mambo mbalimbali ikiwemo hatua za kimaendeleo zilizofikiwa katika sekta mbalimbali hususan afya, huduma za kijamii, elimu na mazingira kibiashara na uwekezaji kwani Tanzania imekuwa na mahusiano mazuri na nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Nordic," alisema Balozi Elisabeth.  
Nae Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg alisema kuwa mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Sweden mwaka 2001 ambapo baada ya hapo mikutano kama hii ilikuwa inafanyika kwa kupokezana kutoka Bara la Afrika na nchi za Nordic. 
"Kwanza kabisa naipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, ni fursa kutumia mkutano huu kujadili masuala ya kibiashara, uwekezaji, amani na usalama kwa maslahi ya nchi za Afrika na Nordic," alisema Balozi Sjoberg. 

Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe alipokuwa akiongelea Mkutano wa 18 wa mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika na nchi za Nirdic jijini Dar es Salaam leo
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe na kulia ni  Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg.  
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano. Kushoto ni Mkuu wa Itifaki Kanali Wilbert Augustine Ibuge, akifuatiwa na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen. Kulia ni Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg. 
Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano, katikati ni Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen na kushoto ni Kushoto ni Mkuu wa Itifaki Kanali Wilbert Augustine Ibuge






Wednesday, October 30, 2019

NAIBU WAZIRI AONGOZA UJUMBE WA WIZARA KWENYE KIKAO CHA KAMATI YA BUNGE

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akisoma taarifa kwenye kikao kati ya Wizara na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara  Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe

Naibu Waziri Mhe. Dkt. Ndumbaro leo ameongoza ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye kikao kati ya Wizara na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje , Ulinzi na Usalama kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Bunge jijini Dodoma. 
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Musa Azzan Zungu (MB), kwa pamoja wameipongeza Wizara kwa  kutekeleza vyema mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo katika vikao vilivyopita, sambamba na utekelezaji mzuri wa vipaumbele na malengo ya Wizara.
 
Kikao hicho kilitoa fursa kwa Wizara kuwasilisha kwa kamati taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, kikao hicho hutoa fursa kwa kamati kupokea na kujadili taarifa za Wizara pamoja na kutoa mapendekezo yake kuhusu masuala mbalimbali.


Kikao cha Wizara na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kikiendelea.
Sehemu ya Waheshimiwa Wabunge (Wajumbe wa Kamati) wakifuatilia taarifa ya Wizara iliyokuwa ikiwasilishwa wakati wa kikao. 
Sehemu nyingine ya Waheshimiwa Wabunge (Wajumbe wa Kamati) wakifuatilia taarifa ya Wizara iliyokuwa ikiwasilishwa wakati wa kikao. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Musa Azzan Zungu (MB), akichangia jambo wakati wa kikao.
Sehemu nyingine ya Waheshimiwa Wabunge (Wajumbe wa Kamati) wakifuatilia kikao.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AfDB) KUIPATIA TANZANIA ZAIDI YA SHILINGI TRILIONI MOJA KWA AJILI YA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA MSALATO WA JIJINI DODOMA PAMOJA NA BARABARA ZA MZUNGUKO JIJINI HUMO.

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imepongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli wa kuhamia Dodoma na kuahidi kuidhinisha kiasi cha dola za kimarekani milioni 455 sawa na zaidi ya shilingi za Kitanzania trilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato sambamba na ujenzi wa barabara za mzunguko Jijini  humo.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina ameyasema hayo katika Ofisi za Makao Makuu ya Benki hiyo yaliyopo Abijdan Nchini Ivory Coast wakati wa Mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na kuongeza kuwa benki hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli katika kipindi chake cha Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lakini pia kwa Tanzania.

Amesema Benki hiyo tayari imeshaidhinisha kiasi cha dola za marekani milioni 180 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko jijini  Dodoma na kwamba kiasi kingine cha dola za marekani milioni 275 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato kinatarajiwa kuidhinishwa na mapema mwezi Novemba 2019.

Dkt. Adesina ameongeza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika ina imani na mageuzi ya kiuchumi yanayotekelezwa chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu bila malipo,afya na maji pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na kuleta uwajibikaji katika taaisisi za uma na kwamba iko tayari kuunga jitihada hizo za serikali kwa kuwekeza katika sekta ya miundombinu..

Aidha Dkt. Adesina ameelezea nia yake ya kutaka kushudia bara la Afrika likipiga hatua kubwa za kimaendeleo sasa na kwa haraka na sio kusubiri baadae na kwamba katika kipindi chake cha uongozi katika Benki ya Maendeleo ya Afrika atapambana kuhakikisha azma hiyo inatekelezeka.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ushirikiano inayoutoa kwa Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na rais Dkt. John Pombe Magufuli ambayo kimsingi yalikuwa ni maono ya Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa nia ya kuiwezesha Tanzania kujitegemea kiuchumi na hatimae Bara zima la Afrika.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika iko tayari kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa yaani standard gauge railway ya kipande cha kutoka Isaka hadi Kigali nchini Rwanda na kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara baada ya kukamilika mchakato wa utoaji wa fedha hizo ambapo mazungumzo ya awali kuhusu ufadhili huo yameanza.

Pia Prof. Kabudi amemtaka Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt. Akinwumi Adesina kuimarisha ofisi za kanda za benki hiyo ili ziweze kutoa huduma zote za kibenki ili kusogeza huduma karibu na wanufaika wa benki hiyo sambamba na kuunga mkono miradi yote ya kimkakati inayounganisha nchi na nchi katika bara la Afrika ili kuboresha nakurahisisha huduma ya usafiri katika Bara la Afrika na hivyo kuwezesha biashara miongoni mwa nchi za Kiafrika na kujiletea maendeleo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi yuko Abijdan Nchini Ivory Coast kushiriki mkutano wa siku mbili wa dharura wa Mawaziri wa fedha uliondaliwa na Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB).


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Abidjan - Ivory Coast.
30 OCTOBER 2019



BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AfDB) KUIPATIA TANZANIA ZAIDI YA SHILINGI TRILIONI MOJA KWA AJILI YA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA MSALATO NA BARABARA MZUNGUKO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba  John Kabudi (Mb) akisalimiana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina Makao Makuu ya Benki hiyo yaliyopo Abidjan Nchini Ivory Coast.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba  John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina. Mazungumzo hayo yamefanyika Makao Makuu ya Benki hiyo yaliyopo Abidjan Nchini Ivory Coast.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba  John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina,mara baada mazungumzo yaliyofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo yaliyopo Abidjan Nchini Ivory Coast.Wengine katika picha ni viongozi wa AfDB na Afisa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania.