Tuesday, November 26, 2019

MKUTANO WA 39 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC KUANZA KESHO JIJINI ARUSHA

 Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliomalizika leo Jijini Arusha
 Makatibu Wakuu Jumuiya ya Afrika Mashariki wakijadili jambo wakati wa Mkutano wao. Kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Afrika Mashariki - Uganda, Bibi. Edith Mwanje, akifuatiwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki - Tanzania, Dkt. Faraji Mnyepe. Wengine ni Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara, Viwanda na Masula ya EAC - Sudani Kusini, Bw. Mou Mou Athian Kuol, akifuatiwa na Meja Generali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa - Uganda, Balozi Charles Karamba. Wengine pichani ni Katibu Mwandamizi, Wizara ya Afrika Mashariki na - Kenya, Dkt. Margaret Mwakima na katibu Mkuu, Office ya Rais Inayohusu masula ya Afrika Mashariki - Burundi, Balozi Jean Rigi. 



Makatibu Wakuu Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wao (Ngazi ya Makatibu Wakuu) uliomalizika leo jijini Arusha
Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akiwasilisha mada kwa Makatibu wakuu (hawapo pichani) wakati wa mkutano wa Makatibu wakuu wa EAC Jijini Arusha

   

Mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kwanza kesho tarehe 27 Novemba 2019  jijini Arusha.

Kuanza kwa mkutano huo kunafuatia kukamilika kwa Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ulioanza tarehe 25 na kumalizika tarehe 26 Novemba 2019.

Mkutano wa Makatibu Wakuu  pamoja na mambo mengine, umejadili masuala mbalimbali ya utekelezaji ya jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoa mapendekezo kwa mkutano wa ngazi ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta zinazohusiana na Jumuiya hiyo utakaoanza  tarehe 27 Novemba 2019.

Mkutano huu wa 39 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeandaliwa kwa lengo la kujadili na kukubabaliana na agenda zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Februari, 2020.


Monday, November 25, 2019

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA TDB

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mapema leo, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse ,Ikulu jijini Dodoma.

Bw. Tadesse akiwa ameambatana na ujumbe wake amewasili  uwanja wa ndege wa jijini Dodoma leo, Novemba 25, 2019 na kulakiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango, na Mkuu wa Itifaki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert  A. Ibuge. 

Akizungumza muda mfupi baada kumaliza mazungumzo na Mheshimiwa Rais Magufuli,  Bw. Tadesse amesema TDB itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania na kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili  ya kutekeleza miradi mbalimbali maendeleo nchini.

Mhe. Dkt. Mpango amesema TDB imekuwa moja ya Benki kinara ambayo imekuwa ikitoa mikopo ya masharti nafuu kwa Tanzania hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye miradi ya maendeleo.

Aidha, Bw. Tadesse akiwa nchini atatembelea maeneo mbalimbali sambamba na kujionea miradi ya maendeleo inayotelezwa na Serikali ikiwemo miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, mradi wa kuzalisha umeme wa Kilwa na miradi mingine ambayo mkopo kutoka (TDB) utaelekezwa.  

Bw. Tadesse amesifu jitihada zinazofanywa na Serikali katika kufanya mageuzi ya kiuchumi nchini na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya  Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika. 

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (katikati), Mkuu wa Itifaki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge (mweji vazi la Jeshi) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (Watatu kushoto) wakijongea usawa wa ndege kumlaki Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse alipowasili jijini Dodoma Novemba 25, 2019.
Mkuu wa Itifaki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akisalimiana na  Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse wakati anawasili jijini Dodoma. 
Viongozi na Watendaji wa Serikali wakiwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse mara baada ya kumlaki katika uwanja wa ndege jijini Dodoma. 
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse wakifurahia jambo mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dodoma


Picha ya pamoja


Sunday, November 24, 2019

BARUA HII IPUUZWE

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuutaarifu Umma wa Watanzania kuwa barua hii inayosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii inayodaiwa kutoka kwa Bw. Steyn kutelekezwa kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.Palamagamba John Kabudi (Mb) si ya kweli na anuani zilizotumiwa hazitumiwi na Wizara wala Wizara hivyo jamii IIPUUZE barua hiyo.
Taarifa zote rasmi zitatolewa kupitia mitandao rasmi ya Wizara na vyombo mbalimbali vya habari.

Friday, November 22, 2019

Tanzania yashiriki Mkutano kuhusu Madini ya Almasi nchini India

Tanzania inashiriki katika Mkutano wa  Mwaka kwa Nchi Wanachama wa KIMBERLEY PROCESSING SCHEME, unaofanyika Jijini New Delhi nchini India. Ujumbe wa Tanzania  katika mkutano huo  unaongozwa na  Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Stanslaus Nyongo. Mkutano huo unahusu nchi wazalishaji wa Madini ya  Almasi  na udhibiti wa biashara ya almasi  duniani. Ushiriki  wa Tanzania katika mkutano huo unalenga  katika  kupata uzoefu  kutoka nchi nyingine zinazofanya vizuri katika biashara ya Madini hayo ghali duniani.
Mkutano ukiendelea

Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Stanslaus Nyongo akiwa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka H. Luvanda alipotembelea Ubalozi huo tarehe 20 Novemba 2019 na kufanya mazungumzo na  Balozi  Luvanda.

Mhe. Nyongo na Balozi Luvanda wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini India.

WAZIRI KABUDI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CANADA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa na Balozi wa Canada nchini Mhe.Pamela O'Donnell walipokutana kwa mazungumzo Ofisi za Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akimsikiliza Balozi wa Canada nchini Mhe.Pamela O'Donnell alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Mhe.Pamela O'Donnell 



PROF. KABUDI AKUTANA NA BALOZI WA CANADA JIJINI DODOMA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell ofisini kwake jijini Dodoma


Prof. Kabudi na Mgeni wake wamezungumzia namna ya kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Canada kwa manufaa ya nchi zao ikiwa ni pamoja na sala la kukamatwa kwa ndege mpya ya Tanzania aina ya Bombardier Dash 8-Q400 iliyokuwa ikitengenezwa niching humo

Prof. Kabudi amempongeza Mhe. Balozi kwa Canada kuendelea kuwa rafiki mzuri wa Tanzania na kumtaka kuendeleza urafiki huo.

Amesema kazi kubwa na nzuri ya kupambana na rushwa na ubadhirifu wa fedha na mali za umma inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuwapatia maisha bora watanzania na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa Kati na wa viwanda.

Naye Balozi O’Donell amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania ya kuimarisha ukuaji wa Uchumi, utoaji wa huduma bora za afya, elimu ya msingi bure kwa watoto wa kitanzania na uboreshaji wa miundimbinu kwa maendeleo ya Tanzania









JKCI KUPOKEA MADAKTARI BINGWA KUTOKA CHINA


Thursday, November 21, 2019

MKUTANO WA 39 BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC WAANZA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeanza leo jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kukubaliana na agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Februari, 2020.

Mkutano huo wa siku saba umeanza leo kwa ngazi ya maofisa waandamizi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na utafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu kisha kuhitimishwa na Mawaziri wa Wizara za Kisekta zinazohusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki Novemba 27, 2019.

Ajenda za mkutano huo zinakadiriwa kuwa tisa ambazo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.

Agenda nyingine ni taarifa ya Baraza kwa Wakuu wa Nchi kuhusu utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayofiwa kwenye mikutano ya Wakuu hao wa Nchi na Kalenda ya Matukio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha kuishia mwezi Juni 2019.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini. 



Baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri ulioanza leo jijini Arusha kwa ngazi ya maofisa waandamizi
Baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri ulioanza leo jijini Arusha kwa ngazi ya maofisa waandamizi

Wednesday, November 20, 2019

INDONESIA KUWEKEZA TANZANIA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Indonesia kuwekeza Tanzania
Dodoma, 20 Novemba 2019

Mkutano wa Jukwaa la Viwanda kati ya Tanzania na Indonesia utafanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro jijini Dar Es Salaam tarehe 21 Novemba 2019. Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huo ambapo kampuni kubwa 21 za Indonesia zinazojihusisha katika masuala ya ujenzi wa miundombinu na usafirishaji; kilimo; usindikaji vyakula; utengenezaji wa nguo, vifaa tiba na madawa ya binadamu; na uchimbaji wa madini na taasisi zinazosimamia masuala ya uwekezaji Tanzania (TIC, TPSF, CTI, TCCIA) zitashiriki katika mkutano huo.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wadau mbalimbali wa Tanzania na Indonesia kubadilishana mawazo, uzoefu na ujuzi pamoja na kuweka mikakati ya kushirikiana katika sekta ya viwanda kwa faida ya pande zote mbili.  
Kutoka na nchi ya Indonesia kuwa ni kubwa kiuchumi Kusini-Mashariki mwa Asia na ipo nafasi ya 16 katika kundi la nchi 20 tajiri zaidi duniani (G20), na uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji nchini, ni dhahiri kuwa kongamano hilo litakuwa na matokeo mazuri katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.            

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 


Tuesday, November 19, 2019

UTURIKI KUWEKEZA UJENZI WA VIWANDA VYENYE THAMANI YA DOLA MILIONI 50 SIMIYU

. Kawasaki kutoka Japan nayo yaonesha nia ya kuanzisha kiwanda kitakachohudumia soko la Afrika na Nje ya Afrika

Katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi, Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki umeambatana na wawekezaji kutoka nchini humo kwa ajili ya kuwekeza katika viwanda mkoani Simiyu ambavyo vinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 2000.

Uwekezaji huo utajumuisha kiwanda cha nguo pamoja na kiwanda cha kutengeneza vyombo vya majumbani ambao una thamani ya dola za kimarekani milioni 50. Viwanda hivyo vitajengwa katika eneo la Isanga Mjini Bariadi Mkoani Simiyu na vinatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2020.

Akizungumza na vyombo vya habari katika eneo ambalo linatarajiwa kujengwa viwanda hivyo mkoani Simiyu, mwekezaji huyo kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram ameahidi kujenga viwanda viwili kimojawapo kikiwa ni cha nguo na kingine cha kutengeneza vyombo vya nyumbani ikiwemo vikombe, sahani na glasi.

Bw. Albayram amesema ameridhishwa na mazingira ya uwekezaji baada ya kutembelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kuangalia mazingira wezeshi kwa uwekezaji wa viwanda, akiwa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo mkoani Simiyu.

Aidha ameitaka serikali kutatua baadhi ya changamoto ili kuuwezesha uwekezaji huo kufanyika ikiwa ni pamoja na miundombinu yote muhimu hususani ya umeme ili uwekezaji huo uanze mara moja baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu zinazohitajika ikiwa ni pamoja na usajili wa kampuni na kutafuta hati miliki ya ardhi.

“Tumeamua kuwekeza Simiyu, kila kitu kikienda sawa kiwanda cha nguo kinaweza kujengwa na kufanya kazi ndani ya miezi tisa mpaka mwaka mmoja, kiwanda cha vyombo vya nyumbani miezi nane baada ya usajili wa kampuni nitarudi tena Simiyu kukamilisha masuala ya hati miliki ya ardhi, sitaki kumuangusha Mhe. Balozi maana amefanya mengi kwa ajili yetu,” alisema Albayram.

Nae Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo amesema mwekezaji ameridhishwa na eneo hilo na kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kutoa ardhi ya kujenga viwanda hivyo huku akibainisha kuwa ombi kubwa la mwekezaji ni upatikanaji wa nishati ya kutosha kwa kuwa viwanda hivyo hutumia umeme mwingi.

Balozi Kiondo ameongeza kuwa, hayo ni matokeo ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa vitendo, hivyo Ubalozi utaedelea kuhamasisha wawekezaji wengine zaidi kuja kuweza nchini, hatimaye kufanikisha azma ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka alimhakikishia mwekezaji huyo upatikanaji wa mahitaji yote muhimu na kuahidi kushirikiana na taasisi za Serikali zinazohusika kuhakikisha anapata huduma zote kwa wakati na pasipo urasimu wowote.

Kuhusu suala la Umeme Mtaka amesema katika Bajeti ya mwaka 2019/20 Wizara ya Nishati kupitia Shirika la umeme TANESCO imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme (substation) ambacho kitajengwa karibu na eneo la uwekezaji huo.

Mtaka ameongeza kuwa mtazamo wa mkoa wa Simiyu ni kuwa na viwanda vichache vitakavyoajiri maelfu ya watanzania badala ya kuwa na viwanda vingi vinavyoajiri watu wachache ili kuwezesha watanzania wengi kupata ajira.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa wakulima wa pamba kulima pamba kwa wingi kwa kuwa kiwanda cha nguo kitakuwa mkombozi wa kuongeza thamani ya zao la pamba na itauzwa kwa bei ya uhakika.

Naye Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa pamba nchini, Bw. Boaz Ogola amesema kujengwa kwa kiwanda cha nguo mkoani Simiyu kutasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika kuondoa changamoto ya bei ya pamba kwa kuwa kitapanua wigo wa soko la pamba, ambapo pamba inayotumika ni chini ya asilimia 20 - 25 ya pamba yote inayozalishwa nchini.

Katika tukio jingine kampuni ya Kawasaki Heavy Industries Ltd kutoka Japan imeonesha nia ya kuanzisha kiwanda nchini ambapo kiwanda hicho kitahudumia soko la Afrika na Nje ya Afrika.

Kawasaki Heavy Industries Ltd ni kampuni nchini Japan ambapo imewekeza katika sekta mbalimbali kama vile sekta ya usafiri (anga, reli na majini)  nishati (cogeneration, energy plants, gas tuibines, gas engines), vifaa vya viwandani (hydraulic components and systems, robotics, industrial plants, environmental and recycling), pamoja na leisure (motorcycle, off-road four wheel,JET SKI).

Naibu Meneja wa Idara ya Mkakati wa Kimataifa, Kitengo cha Biashara cha Kampuni ya Kawasaki Bw. Michio Kambe anatarajia kufanya ziara nchini Tanzania kuanzia tarehe 21 hadi 26 Novemba 2019 ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akioneshwa pamba inavyochambuliwa na mwekezaji kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram (mwenye shati jeusi) wakati walipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Ltd mkoani Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka (katika) akiwa na mwekezaji kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram (mwenye shati jeusi) pamoja na maafisa wa serikali pamoja na baadhi ya wafanyakazi wakitembea ndani ya kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Ltd mkoani Simiyu


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka (katika) akiwa na mwekezaji kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram (mwenye shati jeusi) na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo (mwenye gauni la kijivu) wakati walipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Ltd mkoani Simiyu. Wengine ni maafisa wa serikali pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho.



USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA SHIRIKA LA AALCO KUENDELEA KUIMARIKA

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akizungumza wakati hafla ya Maadhimisho ya Miaka 63 ya kuanzishwa kwa  Shirika la Mashauriano ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (AALCO) yaliyofanyika jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda [kushoto] akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Shirika la Mashauriano ya Masuala ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika [AALCO], Prof. Kennedy Gastron wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 63 ya kuanzishwa kwa shirika hilo, Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019
Mhe. Balozi Luvanda akiwa  katika meza moja na viongozi mbalimbali wakati wa maadhimisho ya miaka 63 tangu kuanzishwa kwa Shiriko la AALCO
Wageni waalikwa wakiwa kwenye maadhimisho
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi pamoja na Maafisa Ubalozi  wa nchi wanachama wa AALCO  walioshiriki hafla ya  maadhimisho ya miaka 63 ya kuanzishwa kwa shirika hilo, Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019.
=======================================================

Ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Mashauriano ya masuala ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (AALCO) kuendelea kuimarika

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Balozi Baraka Luvanda amemwakilisha Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria na Rais wa sasa wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (Asia-Africa Legal Consultative Organization-AALCO) kwenye sherehe ya miaka 63 ya kuanzishwa kwake. Sherehe hiyo imefanyika Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019 na kuhudhuriwa na nchi wanachama wageni waalikwa, wenyeji na mashirika ya kimataifa yaliyopo New Delhi.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mhe. Mahiga, Balozi Luvanda alielezea uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na AALCO na kueleza kuwa utaendelea kudumishwa kwa manufaa ya pamoja.

AALCO ilianzishwa tarehe 15 Novemba 1956 kwa lengo la kuwa chombo cha ushauri na ushirikiano katika masuala ya sheria za kimataifa kwa nchi za Asia na Afrika. Toka kuanzishwa kwake AALCO imewezesha nchi wanachama kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya sheria za kimataifa na imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sheria za kimataifa.

Ushirikiano kati ya Tanzania na shirika hilo ulianza tangu mwaka 1965 ambapo Tanzania ilishiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa AALCO kama nchi Mwangalizi na baadaye mnamo mwaka 1973 kama nchi mwanachama rasmi. 

Mpaka sasa Tanzania imeshaandaa Mikutano mikubwa 3 ya Mwaka ambapo Mkutano wa 25 wa AALCO ulifanyika mwaka 1986 jijini Arusha, Mkutano wa 49 ulifanyika Jijini Dar es Salaam mwaka 2010 na Mkutano wa 58 ulifanyika hivi karibuni, jijini Dar es Salaam tarehe 21 hadi 25 Octoba 2019.

Monday, November 18, 2019

TANZANIA YAKABIDHI SHEHENA YA KWANZA YA MBEGU ZA KOROSHO NCHINI ZAMBIA


Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia akihutubia adhira iliyojitokeza kwenye hafla fupi ya kukabidhi mbegu za korosho jimbo la Mongu, Zambia  tarehe 16 Novemba, 2019
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi 
shehena ya mbegu za korosho kwa Serikali ya Jamhuri ya 
Zambia katika hafla iliyofanyika mjini Mongu nchini humo. 

Korosho hizo zimekabidhiwa kufuatia ahadi ya Rais wa 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe 
Magufuli aliyoitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. 
Edgar Lungu kwenye uzinduzi wa Kituo cha Pamoja cha 
Huduma Mpakani (OSBP) Tunduma tarehe 5 Oktoba, 2019.

Katika tukio hilo Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Mhe. 
Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia, na

 kwa upande wa Zambia, Serikali aliwakilishwa na Waziri wa 

Jimbo la Mongu Mhe. Richard Kapita, Watendaji kutoka 

Serikalini na viongozi wa Kimila.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Kapita kwa naiba ya
 Serikali ya Jamhuri ya Zambia ametoa shukurani za pekee
 kwa Mhe. Rais Magufuli kwa  upendo aliouonesha
 kwa Zambia na kwa upekee kabisa kwa wananchi wa jimbo
 la Mongu.
 Aliongezea kusema wananchi wa Mongu 
wanamatumaini makubwa kuwa, mbegu hizo zitawapa 
chachu ya kuzalisha korosho kwa wingi na kunufaika 
kiuchumi kama ambavyo imekuwa kwa wananchi wa
 Tanzania
Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia (kushoto) na Waziri wa Jimbo la Mongu Mhe. Richard Kapita (kulia) wakijadili jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa hafla ya kukabidhi na kupokea korosho iliyofanyika Mongu, Zambia 
Waziri wa Jimbo la Mongu, Zambia  Mhe. Richard Kapita 

akihutubia hadhira iliyojitokeza kwenye hafla ya 

mapokezi ya mbegu za korosho
Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia, na Mhe. Mukela Manyindo Waziri Mkuu wa Jimbo la Mongu (katika ngazi ya kimila) wakikata utepe kuashiria mapokezi ya mbegu za korosho katika hafla iliyofanyika Mongu, Zambia 
Picha ya pamoja baada ya hafla ya kukabidhi mbegu za korosho
Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia (kushoto) na Afisa kutoka Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia wakifuatilia tukio lililokuwa likiendelea wakati wa hafla ya kukabidhi mbegu za korosho
Shemu ya wananchi wa Mongu, Zambia waliojitokeza kwenye hafla ya mapokezi ya mbegu za korosho