Wednesday, March 11, 2020

NAIBU WAZIRI DKT. NDUMBARO AKUTANA NA MABALOZI WA UINGEREZA, NORWAY NA KOREA


Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Balozi Sarah Cooke, Balozi wa Norway nchini Mhe. Balozi Elisabeth Jacobsen pamoja na Balozi wa Korea nchini Mhe. Balozi CHO tae-ick.

Dkt. Ndumbaro amekutana na mabalozi hao leo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili masuala ya kuongeza ushirikiano wa kidiplomasia pamoja na mikakati ya kujikinga na kupambana na homa ya virusi vya corona.

Pia, Mabalozi hao waliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Kushirikiana na Jumuiya ya  Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika –SADC kwa maamuzi yake ya busara kupitia mawaziri wa Afya ya kuamua vikao vyote vinavyoendelea kufanyika kwa njia ya mtandao yaani (Video Conference) ikiwa ni hatua mathubuti ya kukabiliana  na maambukizi ya Ugonjwa huo.

Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Balozi Sarah Cooke pamoja na Balozi wa Norway nchini Mhe. Balozi Elisabeth Jacobsen


Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Balozi Sarah Cooke akimuelezea jambo Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro. Katikati ni Balozi wa Norway nchini Mhe. Balozi Elisabeth Jacobsen.

Balozi wa Norway nchini Mhe. Balozi Elisabeth Jacobsen akimuuliza jambo Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro. Kushoto kwake ni Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Balozi Sarah Cooke.

Balozi wa Korea nchini Mhe. Balozi CHO tae-ick akiongea na Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro 


Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Balozi wa Korea nchini Mhe. Balozi CHO tae-ick wakifuatilia taarifa kuhusu mikakati ya kujikinga na kupambana na homa ya virusi vya corona

Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akimfafanulia jambo Balozi wa Korea nchini Mhe. Balozi CHO tae-ick  






Tuesday, March 10, 2020

DKT. NDUMBARO AFANYA MAZUNGUMZO NA MABALOZI WA PALESTINA NA USWISI NCHINI


Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Palestina nchini Mhe. Balozi Hamdi Mansour AbuAli Pamoja na Kaimu Balozi wa Uswisi nchini Bw. Leo Nascher, katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo ya Mhe. Dkt. Ndumbaro pamoja na Balozi wa Palestina, Mhe. Balozi Abuali walikubaliana kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi hasa katika sekta ya uwekezaji wa kiwanda cha dawa na vifaa tiba pamoja na kilimo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Dkt. Ndumbaro na Kaimu Balozi wa Uswisi nchini Bw. Leo Nascher mazungumzo yao yalihusu maandalizi ya mpango mpya wa maendeleo wa mwaka 2021-2024 baina ya Tanzania na Uswisi yanayoendelea.

Mpango wa maendeleo uliopo unatarajiwa kufikia ukomo mwaka huu 2020. Ambapo mpango mpya utajikita zaidi katika kuimarisha sekta ya afya, mazingira, utawala bora na kukuza ajira kwa vijana na wanawake nchini.

Masuala mengine yaliyojadiliwa yalihusu programu ya Ukuzaji Ujuzi wa Ajira nchini (Skills for Employment Tanzania) na shuguli zinazofanywa na NGOs za Uswisi zilizopo nchini.

Pia Kaimu Balozi huyo alieleza kuwa Uswisi itaendelea kusaidia mradi wa malaria na kuchangia fedha katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Kwa upande wake Mhe. Dkt. Ndumbaro alisifu uhusiano baina ya nchi hizi mbili kwa kueleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Uswisi katika kukuza zaidi mahusiano hayo.


Balozi wa Palestina Nchini Mhe. Balozi Hamdi Mansour AbuAli akimuelezea jambo Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea na Balozi wa Palestina Nchini Mhe. Balozi Hamdi Mansour AbuAli walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Kaimu Balozi wa Uswisi nchini Bw. Leo Nascher akiongea na Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akimfafanulia jambo Kaimu Balozi wa Uswisi nchini Bw. Leo Nascher wakati wa mazungumzo leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI WA SADC



Saturday, March 7, 2020

Wafanyabiashara Mumbai Wahimizwa Kutumia Air Tanzania

Ubalozi wa Tanzania nchini India wakishirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] waliandaa Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Mumbai ambapo wafanyabiashara wapatao 40 kutoka Tanzania, Maofisa kutoka Kituo Cha Uwekezaji [Tanzania Investment Centre] na “Air Tanzania” walikutanishwa na wafanyabiashara, wawekezaji na wasafirishaji wa bidhaa wa India wapatao 60.

Pamoja na mambo mengine kongamano hilo lililenga kuwakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji  na wasafirishaji wa bidhaa wa Tanzania na India ili kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania na India hususan, ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania kuja India. Wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa adhimu ya kubadilishana taarifa zinazohusu bidhaa zinazozalishwa kwa wingi Tanzania kwa minajili ya kupata  masoko zaidi ya bidhaa hizo na kuongeza idadi ya mizigo inayosafirishwa na ‘Air Tanzania’ kutoka Dar es Salaam kuja Mumbai.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alieleza, pamoja na mambo mengine, kuwa Kongamano hilo litasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kukutana na wenzao wa India na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua masoko zaidi ya bidhaa zao nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu bidhaa wanazozalisha nchini na faida zake.

 Kwa ujumla, India ina soko kubwa la bidhaa. Hivyo,matarajio ni kuona  kiwango cha bidhaa kutoka Tanzania zinazouzwa India kinaongezeka zaidi hususan, baada ya kurejeshwa tena kwa ndege za Shirika la Ndege, Tanzania, kati ya Dar es Salaam na Mumbai mwezi Julai 2019.  Balozi Luvanda alitoa rai kwa wafanyabiashara hao kutumia usafiri wa ‘Air Tanzania’ kwa kuwa ni wa uhakika, wa muda mfupi zaidi na pia bei yake ni nafuu. Aidha, Mhe. Luvanda aliwaomba wafanyabiashara hao kuongeza ushirikiano na Tanzania katika utalii, hasa ikizingatiwa kuwa India inatoa watalii zaidi ya milioni 20 kwa mwaka kutembelea nchi mbalimbali duniani.
Akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania, Bwana Patrick Ndekana alieleza historia ya Shirika hilo na hali ilivyo kwa sasa. Aidha, Bwana Ndekana aliwaeleza washiriki wa Kongamano kuwa Shirika hilo limejipanga kuhakikisha usafiri wa uhakika, bora na salama kwa kuwa linamiliki ndege mpya na za kisasa.

Vilevile, Bwana Ndekana alifafanua shabaha ya kuitisha Kongamano kuwa ilitokana na wadau mbalimbali kama vile wasafairishaji wa bidhaa kukosa taarifa za fursa za usafirishaji zilizopo kwenye shirika hilo. Hivyo, alieleza matarajio ni kuwa wadau hao wataweza kutumia zaidi usafiri wa Shirika hilo baada ya Kongamano hilo mahsusi.
Akiwasilisha mada kuhusu biashara na uwekezaji nchini Tanzania, Afisa kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania [TIC], Bwana Nestory Kissima alieleza kuwa Tanzania imefanya mabadiliko makubwa katika sera zake za kuvutia biashara na uwekezaji na amewaomba wafanyabiashara waliohudhuria kongamano hilo kuchangamkia fursa za biashara zilizopo Tanzania hususan, katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya asili ya biashara kama vile mkonge, pamba, korosho,madini,matunda mbalimbali kama vile parachichi, na nafaka mbalimbali pamoja na ununuzi wa mazao hayo ambayo yanahitajika sana nchini India.
Bwana Kissima alieleza kuwa, kwa kiasi kikubwa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini Tanzania yameboreshwa ikiwa ni pamoja na Serikali kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizokuwepo kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi. Jitihada hizo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye viwanda na miradi ya kimkakati ifikapo 2025.inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia uwekezaji 
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akihutubia wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Mumbai tarehe 05 Machi 2020.
Kaimu Mkurugenzi wa Air Tanzania akizungumza katika 
Kongamano hilo.

Bwana Nestory Kissima, kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania [TIC ] akiwasilisha mada katika Kongamano hilo.

Umati wa washiriki wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji wakifuatilia hotuba zilizokuwa zikiwasilishwa na wataalamu mbalimbali katika Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Mumbai tarehe 05 Machi 2020.

Friday, March 6, 2020

PROF. KABUDI AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA RAIS DKT MAGUFULI KWENDA KWA RAIS TRUMP

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akikabidhi ujumbe maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwenda kwa Rais wa Marekani Doland Trump. Anayeshuhudia ni  Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye pia anashughulikia masuala ya Afrika Mhe. Tibor Nagy mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Washington,Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Marekani Nchini Tanzania Dkt. Donald Wright (aliyevaa tai nyekundu) Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi mtendaji wa benki ya Dunia anayeiwakilisha Marekani Dkt. Jennifer "DJ" Nordquist katika makao makuu ya Benki ya Dunia Washington,Marekani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeiwakilisha Marekani Dkt. Jennifer "DJ" Nordquist  akimsikiliza kwa makini Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (hayupo pichani) mazungumzo yaliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya Dunia Washington,Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa na Mkurugenzi mtendaji wa benki ya Dunia anayeiwakilisha Marekani Dkt. Jennifer "DJ" Nordquist katika makao makuu ya Benki ya Dunia Washington,Marekani.Nyuma ya Prof. Kabudi ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi





Tanzania na Nepal Kuimarisha Ushirikiano

Waziri wa wa Mambo ya Nje wa Nepal, Mhe. Pradeep Gyawali alifungua rasmi ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu tarehe 02 Machi 2020.
Katika hotuba yake, Waziri Gyawali alieleza kuridhishwa kwake kutokana na uhusiano thabiti wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili ambapo zinashirikiana na kujenga hoja zinazofanana kwenye medani ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote, Kundi la 77 na nyinginezo.
Hata hivyo, Waziri Gyawali alielezea umati wa washiriki katika hafla hiyo kuwa kwa sasa, uhusiano huu unapaswa kujikita zaidi katika maeneo ambayo mbia mmojawapo anaweza kunufaika na ujuzi na uzoefu kutoka kwa mwenzake. Akataja maeneo ambayo Nepal imefanikiwa zaidi kama vile utalii wa kupanda milima ambapo Nepal inavyo vilele vya milima nane mirefu kuliko yote duniani ikiongozwa na Mlima Everest.
Awali akimkaribisha Mheshimiwa Waziri Gyawali, Balozi Baraka Luvanda anayeiwakilisha Tanzania nchini India na Nepal alielezea juu ya umuhimu wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima kuwa itasaidia kutoa huduma za Kikonseli kwa karibu zaidi na pia itasaidia kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili.
Balozi Luvanda alitaja maeneo ambayo yanaweza kutazamwa kama ya kuanzia kama vile (i) Kuwa na Makubaliano ya Mashauriano ya Kisiasa (Political Consultations) (ii) Kuwa na Makubaliano katika Sekta ya Usafiri wa Anga (Bilateral Air Services) ambapo “Air Tanzania” inaweza kuingia ubia na “Nepal Airline” (iii) Kuwa na Makubaliano kwenye sekta ambazo Nepal inafanya vizuri kama vile Utalii wa kupanda milima na Kilimo.
Bwana Rajesh Chaudhary, raia wa Nepal amekwishaanza rasmi kazi ya Uwakilishi wa Heshima baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kidiplomasia. 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nepal, Mhe. Pradeep Gyawali akizungumza katika hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu, Nepal tarehe 02 Machi 2020.

Balozi wa Tanzania nchini India na Nepal, Mhe. Baraka Luvanda akihutubia wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu, Nepal tarehe 02 Machi 2020.

Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal Bwana Rajesh  Chaudhary akihutubia katika hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu, Nepal tarehe 02 Machi 2020.

Balozi wa Tanzania nchini India na Nepal, Mhe. Baraka Luvanda (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nepal, Mhe. Pradeep Gyawali (wa pili kushoto), Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal, Bwana Rajesh  Chaudhary (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Wawakilishi wa Heshima mjini Kathmandu, Nepal, Bwana Pradeep Kumar Shrestha katika hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu, Nepal tarehe 02 Machi 2020.

Balozi wa Tanzania nchini India na Nepal, Mhe. Baraka Luvanda (wa pili kulia) akimkabidhi zawadi rasmi ya kitanzania-picha ya tingatinga Waziri wa Mambo ya Nje wa Nepal, Mhe. Pradeep Gyawali katika hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu, Nepal tarehe 02 Machi 2020.

Baadhi ya Wawakilishi wa Heshima wa nchi mbalimbali mjini Kathmandu, Nepal wakiwa kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Nepal iliyofanyika katika Hoteli ya Radisson Jijini Kathmandu, Nepal tarehe 02 Machi 2020.

Wednesday, March 4, 2020

DKT. NDUMBARO AKUTANA,KUFANYA MAZUNGUMZO NA MASENETA KUTOKA UFARANSA


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Maseneta sita (6) kutoka Ufaransa walioko kwenye ziara nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam ambapo ujumbe wa Maseneta hao unaongozwa na Mhe. Hervé Maurey, Mwenyekiti wao ambae pia ni Rais wa Kamati ya Bunge ya Mipango Miji na Maendeleo Endelevu pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Frederic Clavier.

Katika mazungumzo hayo ujumbe wa maseneta umeeleza kuridhishwa na jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi kupitia uwekezaji kwenye miundombinu na kutunza mazingira.

Kwa upande wake Naibu Waziri Dkt. Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuueleza ujumbe huo sekta ambazo Tanzania inaweza kushirikiana na Ufaransa ili kukuza zaidi ushirikiano baina ya nchi hizi mbili uliodumu kwa muda mrefu.

Ametaja sekta hizo kuwa ni pamoja na sekta ya kilimo na mifugo, madini, utafiti katika vyuo vikuu pamoja na utalii na utunzaji wa mazingira.

"Katika kipindi hiki Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeweka kipaumbele kuendeleza viwanda hususan viwanda vya kuongeza thamani, amesema Dkt. Ndumbaro.

Naibu Waziri aliongeza kuwa, "Tanzania ina mazingira bora ya uwekezaji na niwasihi tu mtufikishie taarifa hizi kwa wawekezaji wanaoweza kuja kuwekeza nchini katika viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na kiwanda cha kuunganisha magari," Amesema Dkt. Ndumbaro. 


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea na Ujumbe wa Maseneta sita (6) kutoka Ufaransa leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Mwenyekiti wa Ujumbe wa Maseneta kutoka Ufaransa, Bw. Herve Maurey (upande wa kulia mwa Naibu Waziri) akifafanua jambo wakati wa maongezi baina yao na Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Mwenyekiti wa Maseneta kutoka Ufaransa, Bw. Herve Maurey akimkabidhi zawadi Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro



Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Maseneta kutoka Ufaransa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Tanzania Kuuza Makontena 200 ya Maharage nchini Ubelgiji

Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji umepata soko kubwa la maharage machanga ya kijani yanayojulikana kama haricots vertz(green thin beans) nchini Ubelgiji. Soko hilo limepatikana baada ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kufanya mazungumzo  na uongozi wa juu wa kampuni ya CBG-Charlier-Brabo Group inayonunua maharage hayo kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuyauza katika supermarkets kubwa za Carrefour, Delhaize na Aldi za nchini Ubelgiji, Luxembourg na nchi nyingine za Ulaya.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika tarehe 3 Machi 2020, kampuni hiyo ipo tayari kununua containers kati ya 180-200 za maharage hayo kila mwaka kutoka Tanzania. 

Kupatikana kwa soko la maharage hayo nchini Ubelgiji ni habari njema kwa wakulima wa Tanzania na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo hususan wa aina hiyo ya maharage ambayo tayari Tanzania inayauza nchini Uholanzi.

Kampuni hiyo pia imeonesha utayari wa kununua aina nyingine ya maharage ijulikanayo kama red kidney beans na chickpea kwa kiwango cha containers 8 kila mwaka katika hatua za mwanzo.

Ubalozi wa Tanzania unatoa wito kwa Watanzania kuchangamkia upatikanaji wa soko hilo jipya nchini Ubelgiji kwa kuwasiliana na kampuni hiyo kupitia tovuti yao ya www.cbg.be au kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa maelekezo zaidi.

Maharage aina ya haricots vertz(green thin beans) yaliyopata soko nchini Ubelgiji.
Balaozi Jestas Abuok Nyamanga akiwa amebeba maharage yaliyopata soko la kununuliwa na kampuni ya  CBG-Charlier-Brabo Group ya nchini Ubelgiji. Kulia kwake ni Wim Vandenbus scheambayeni Meneja Mauzo na Ununuzi wa kampuni, na kushoto kwa Balozi Nyamanga ni Bi Martine Danneel, ambaye ni Afisa Mauzo wa kampuni. Kushoto zaidi kwa Balazo ni Dr. Geoffrey B. Kabakaki, Afisa Mkuu wa Ubalozi kwa masuala ya uchumi na biashara.
Balozi akiangalia bidhaa aina ya nanasi zilizokatwa na kuifadhiwa katika kopo na kampuni hiyo ambazo pia zinaweza kuagizwa kutoka Tanzania

Tuesday, March 3, 2020

DKT. NDUMBARO AKUTANA, KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CUBA NCHINI


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazugumzo na Balozi wa Cuba nchini Mhe. Prof. Lucas Domingo Hernandez Polledo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumo hayo viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika sekta ya afya nchin na Cuba imeiomba Tanzania kuinga mkono katika mpango wake wa kugombea kiti katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Pamoja na mambo mengine walizungumzia kuhusu jinsi ya kuboresha mahusiano yaliyopo katika kati ya Tanzania na Cuba, ambapo Cuba imekuwa mdau muhimu wa maendeleo ya sekta ya afya nchini.


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akimsikiliza Balozi wa Cuba nchini Mhe. Prof. Lucas Domingo Hernandez Polledo wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam




PROF. KABUDI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA UN, UNHCR


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić Pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Antonio Canhandula Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kabudi amewaeleza Bw. Milišić na Bw. Canhandula kuwa UN pamoja na UNHCR zimekuwa na mchango mkubwa kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza maendeleo pamoja na zile za kushughulikia masuala ya wakimbizi.

“Kwa ujumla UN imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za maendeleo endelevu ya kijamii, na kiuchumi hivyo Serikali itaendelea kuhakikisha inaendeleza uhusiano huu," Amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa nchini (UN) Bw. Milisic amesema kuwa uhusiano wa UN na Serikali ya Tanzania ni wa muda mrefu na hivyo ni jukumu la UN kuhakikisha inaimarisha uhusiano huo na kuuboresha.

 “Ni matumaini yangu kuwa uhusiano huu tutauboresha vizuri na kuimarisha kwa maslahi mapana na maendeleo endelevu ya taifa la Tanzania," Amesema Bw. Milišić

Nae Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Canhandula amesema wanatambua mchango mkubwa ambao Tanzania imekuwa ikiutoa kuhakikisha inaimarisha ulinzi wa maeneo ya wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kuishi kwa amani na utulivu pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu kama vile malazi na mavazi.

"Kwa kweli UNHCR tunafurahishwa na jinsi Serikali ya Tanzania ambavyo imekuwa ikipokea wakimbizi na kuwapatia baadhi ya mahitaji muhimu……tunaomba tuendeleze ushirikiano huu kwa maendeleo yetu," Amesema Bw. Canhandula.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimfafanulia jambo Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiisoma hati ya utambulisho mara baada ya kuipokea kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Antonio Canhandula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kabla ya kukabidhi hati ya utambulisho katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea hati ya utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Antonio Canhandula katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 



BALOZI MBELWA ATOA RAI KWA WAFANYABIASHARA WA TANZANIA

Mhe. Mbelwa Kairuki Balozi wa Tanzania nchini China, ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Tanzania ambao shughuli zao zinahushisha China, kuwa na subira ya kuzuru China wakati huu ambao tatizo la Corona Virus (COVID-19) bado linaendelea kushughulikiwa nchini humo.


Monday, March 2, 2020

MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI WA SADC KUFANYIKA TAREHE 16 - 17 MACHI


Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unatarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia tarehe 11 hadi 17 Machi, 2020 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa mkutano huo utafanyika kuanzia tarehe 12 hadi 17 Machi 2020 ambapo utatanguliwa na mkutano wa wataalamu pamoja na Makatibu Wakuu na kufuatiwa na mkutano wa mawaziri tarehe 16 - 17 Machi, 2020.

"Pamoja na mambo mengine, mkutano huu utahusisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mawaziri wa Fedha, Uchumi na Mipango pamoja na Mawaziri wa Viwanda na Biashara," Amesema Prof. Kabudi

Waziri Kabudi amesema kuwa mkutano huo utahudhuriwa na Mawaziri 16 kutoka Nchi wanachama wa SADC za Angola, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Comoro, Lesotho, Mauritius, Madagascar, Kongo DRC, Shelisheli, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania, Malawi, Botswana pamoja na Eswatini)

Aidha, Kwa mujibu wa Mhe. Waziri Kabudi, Mkutano huo utakuwa mkutano wa kwanzawa SADC wa Baraza la Mawaziri kuendeshwa kwa lugha ya Kiswahili baada ya lugha hiyo kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Jumuiya hiyo.

Prof. Kabudi aliongeza kuwa, mkutano huo utajadili masuala mbalimbali muhimu kwa mustakabali wa maendeleo na ustawi wa nchi wananchama wa SADC.

"Mktano huu utapokea taarifa na kutolea maelekezo taarifa za vikao mbalimbali vya kisekta vya kamati za mawaziri ambavyo vimefanyika nchini tangu Septemba 2019," Ameongeza Prof. Kabudi.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo ktk picha) kuhusu Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC utakaofanyika tarehe 11 – 17 Machi, 2020 Jijini Dar es Salaam. Kulia mwenye kilemba ni Bibi. Zamaradi Kawawa, akifuatiwa na Naibu Katibu MKuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi, kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Bibi. Agnes Kayola

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC utakaofanyika tarehe 11 – 17 Machi, 2020 Jijini Dar es Salaam