Wednesday, August 31, 2022

TANZANIA, QATAR KUSHIRIKIANA SEKTA YA AFYA

Katika jitihada za kutafuta fursa mbalimbali za ajira kwenye sekta ya afya, ujumbe wa Tanzania uliopo ziarani nchini Qatar umekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Hamad Medical Corporation (HMC) Jijini Doha, Qatar. 

Ujumbe huo wa serikali uliongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab. 

Viongozi hao wamejadiliana namna ya kuanza kutoa nafasi za ajira kwa watanzania. Watalaam wa sekta ya Afya nchini Tanzania walikuwa hawajaanza kuingia kwenye soko la ajira la Qatar na hivyo endapo Tanzania itafunguliwa nafasi hizo itaweza kupeleka watalaamu wake kufanya kazi nchini humo.

Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi, Idara ya Rasilimali Watu wa 'Hamad Medical Center', Bi. Sabeeha Amin Qasemi amesema kuwa hospitali hiyo imefurahishwa na hatua ambazo Tanzania inazichukua katika kuboresha sekta ya afya na kuahidi kuwa watatoa nafasi za ajira kwa wataalamu wa afya ambao hatimaye watapelekwa kwenye hospitali mbalimbali nchini Qatar. 

Naye, Prof. Katundu ameuhakikishia uongozi wa Shirika hilo kuwa Tanzania ina wataalamu wa afya wenye uwezo na uzoefu wa kutosha na endapo watapata fursa za ajira nchini humo watafanya kazi kwa bidii na weledi kwa kuzingatia sheria na taratibu za Qatar kwa kuwa watahiniwa hao hupatiwa mafunzo wakati na baada ya usaili wa ajira.  

Kwa upande wake, Balozi Fatma Rajab amesema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Qatar ili kuiwezesha Serikali hiyo kupata wafanyakazi bora zaidi katika sekta mbalimbali. 

Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi, Idara ya Rasilimali Watu wa 'Hamad Medical Corporation', Bi. Sabeeha Amin Qasemi akizungumza na ujumbe wa Serikali ya Tanzania uliongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab walipokutana kwa mazungumzo Jijini Doha, Qatar

Mmoja wa Mawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania akichangia jambo wakati wa mazungumzo ya vuiongozi hao yaliyofanyika Jijini Doha, Qatar

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu akielezea mkakati wa Serikali kwa uongozi wa 'Hamad Medical Corporation' Jijini Doha, Qatar. Wa kwanza kulia mwa Prof. Katundu ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu akielezea mkakati wa Serikali kwa uongozi wa 'Hamad Medical Corporation' Jijini Doha, Qatar


Mazungumzo baina ya Ujumbe wa Tanzania na Uongozi wa Hamad Medical Center yakiendelea Jijini Doha, Qatar



VACANCY ANNOUNCEMENT AT WORLD INTELLECTUAL PROPERTY ORGANIZATION


 

VACANCY ANNOUNCEMENT



 

Tuesday, August 30, 2022

MAWAKALA WA AJIRA BINAFSI WA TANZANIA, QATAR WAJADILI FURSA ZA AJIRA

Mawakala wa ajira katika sekta binafsi nchini Tanzania wamekutana na kujadili fursa za ajira na Mawakala wenzao wa ajira binafsi wa Qatar, Jijini Doha tarehe 30 Agosti, 2022.

Mawakala hao wameongozana na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Uratibu kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar, Bw. Hamad Ali Elfaifa amesema Qatar na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria ambao umedumu hadi sasa na wanapenda kuuendeleza kwa kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya ajira.

Bw. Elfaifa amewataka Mawakala wa ajira kutoka Tanzania kuzingatia sheria na taratibu za ajira pamoja na kushirikiana na Mawakala wenzao wa Qatar ili kuweza kupata wafanyakazi wenye ujuzi, maarifa na weledi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Vilevile, Bw. Elfaifa ameeleza kuwa katika kutekeleza Mkataba wa Ajira kati ya Tanzania na Qatar, sasa Tanzania imeingizwa kwenye mfumo wa ajira nchini Qatar ambapo mawakala wa Tanzania wataweza kupokea oda za kazi kutoka kwa Mawakala wa Qatar, hatua itakayowezesha watanzania wengi wenye sifa kunufaika na nafasi za kazi nchini Qatar

Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania, Prof. Katundu amesema Tanzania inajivunia kuwa na vijana wenye ujuzi na uzoefu katika fani mbalimbali hivyo wanaamini kuwa endapo vijana hao watapatiwa fursa za ajira nchini Qatar watasaidia kuboresha zaidi uchumi wa Qatar pamoja na Maisha yao.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA), Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Joseph Nganga amesema kuwa lengo kubwa la kuwakutanisha mawakala wa ajira binafsi wa Tanzania na wa Qatar ni kufahamishana taratibu za ajira kwa pande zote mbili ili kuweza kufanya kazi kwa ushirikiano na kupata waajiriwa wenye sifa stahiki.

“Mkutano wa leo umesaidia kufahamu taratibu zinazotakiwa ili kumpata mfanyakazi na stahiki zake hivyo mawakala wa nchi zote watumie fursa hiyo ipasavyo ambapo Mawakala wa Qatar wameonesha kuridhishwa na nidhamu ya vijana wanaoajiriwa kutoka Tanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana na mawakala kutoka Tanzania ili kuwapata wafanyakazi kwenye sekta mbalimbali,” alisema Bw. Nganga.

Mwaka 2014 Tanzania ilisaini mkataba wa makubaliano ya ajira na Qatar, ambapo kwa sasa Serikali ya Tanzania inaangalia namna ya kupata nafasi za ajira kwa Watanzania ili waende kufanya kazi nchini humo.

Ujumbe wa Chemba ya Biashara ya Qatar ukizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab Jijini Doha tarehe 30 Agosti, 2022

Ujumbe wa Chemba ya Biashara ya Qatar ukizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab Jijini Doha tarehe 30 Agosti, 2022

Mkuu wa Kitengo cha Uratibu kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar, Bw. Hamad Ali Elfaifa akizungumza na Mawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania na Qatar walipokutana Jijini Qatar kujadili fursa za ajira nchini humo

Kikao cha Mawawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania na Qatar kikiendelea Jijini Qatar

Kamishna wa Kazi, Wizara ya Kazi Zanzibar, Bw. Rashid Khamis Othman akizungumza na Mawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania na Qatar walipokutana Jijini Qatar kujadili fursa za ajira nchini Qatar

Mmoja kati ya Mawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania akieleza jambo kwa mawakala walioshiriki katika mkutano ulifanyika leo Jijini Doha, Qatar

Mmoja kati ya Mawakala wa ajira binafsi kutoka Qatar akieleza jambo kwa mawakala walioshiriki katika mkutano ulifanyika leo Jijini Doha, Qatar



TANZANIA NA SINGAPORE KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Serikali ya Tanzania na Singapore zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kihistoria uliopo baina yao ili kutekeleza kwa ufanisi malengo ya kiuchumi ya mataifa hayo.

Ahadi hiyo imetolewa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Singapore nchini mwenye makazi yake Singapore, Mhe. Douglas Foo yaliyofanyika tarehe 30 Agosti 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Balozi Mulamula alieleza kuwa ni muhimu kwa Tanzania na Singapore kuuenzi ushirikiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa yao kwa manufaa ya wananchi wake.

Pia alieleza Tanzania ina nia ya kushirikiana na Singapore katika maeneo mbalimbali ikiwemo: Kukuza shughuli za bandari, kilimo cha mbogamboga na matunda, usafirishaji wa mazao ya biashara kama vile kahawa na chai, biashara, utalii, ufadhili wa masomo na ushirikiano katika masuala ya utamaduni hususan kuanzisha makubaliano ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Singapore.

Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na: Kujenga uwezo katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, uwekezaji katika maeneo maalum ya viwanda, usafiri wa anga na ushirikiano katika masuala ya kikanda.

“Tanzania inawekeza katika kujenga uwezo wa rasilimali watu kwenye masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, pia kupitia uwepo wa mkongo wa mawasiliano wa taifa ina dhamira ya kutoa huduma ya mawasiliano nje ya mipaka yake” alisema Balozi Mulamula.

Kwa upande wa Mhe. Douglas Foo alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Singapore unatimiza miaka 40 tangu ulipoanzishwa hivyo, ni muhimu kuangalia maeneo yenye fursa za kiuchumi ili kuendelea kuimarisha ushirikiano kwa manufaa kwa pande zote mbili.

Tanzania na Singapore zinaunganishwa na uanachama wao katika Umoja wa nchi za jumuiya ya madola na hivyo ni fursa kwa mataifa hayo kuongeza maeneo ya ushirikiano kupitia makubaliano yatakayowezesha usimamizi wa karibu wa utekelezaji wa malengo katika maeneo husika ya maendeleo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini mwenye makazi yake nchini Singapore, Mhe. Douglas Foo alipomtembelea katika ofisi za Wizara tarehe 30 Agosti 2022 jijini Dodoma.

Mhe. Douglas Foo akifafanua juu ya uzoefu wa Singapore katika kusimamia makubaliano mbalimbali yanayoanzishwa na serikali yake kwa lengo la kukuza uchumi na kuinua maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Mazungumzo yakiendelea.
 Mhe. Balozi Mulamula akiagana na Mhe. Foo baada ya mazungumzo. 

MIRADI NANE YA KIPAUMBELE YAWASILISHWA TICAD8


Serikali ya Tanzania imewasilisha miradi nane ya kipaumbele yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.334 katika Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD8) uliohitimishwa tarehe 28 Agosti 2022 jijini Tunis nchini Tunisia. 

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) aliyaeleza hayo jana tarehe 29 Agosti, 2022 akiwa nchini Tunisia ambako alimwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo. 

Miradi hiyo nane ambayo itatekelezwa Tanzania Bara na Tanzania - Zanzibar imetajwa kuwa ni; ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete, ujenzi wa bwawa la kusambaza maji la Lugoda, Mufindi Mkoani Iringa, ukarabati wa barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kiwango cha lami, mradi wa umwagiliaji katika bonde la Ziwa Victoria, ujenzi wa njia ya umeme ya Songa-Fungu-Mkuranga, uanzishwaji wa maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi, kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam na ujenzi wa bandari nne za kisasa za uvuvi

Sambamba na miradi hiyo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa, licha ya Tanzania kunufaika na ujenzi wa daraja la Mfugale, mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II kupitia TICAD, vilevile amewasilisha maombi ya kukamilishiwa miradi mitatu ya ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili, Bandari ya Kigoma na mradi wa maji wa Zanzibar yenye thamani ya dola za Marekani milioni 343.8.

Mbali na kushiriki TICAD 8, Waziri Mkuu kwa nyakati tofauti alifanya mikutano ya pembezoni na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Dkt. Akihiko Tanaka, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Bw. Yasuteru Hirai na Mwenyekiti wa Bodi ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) Bw. Mutsuo Iwai 

Katika mazungumzo hayo Waziri Mkuu amewashukuru na kuwapongeza wadau hao kwa kuchangia katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa shule ya bweni ya wasichana wilayani Urambo iliyojengwa na JTI, ambapo pia ametoa rai kwa kampuni hiyo kuendelea kununua zao la tumbaku nchini sambamba na kuongeza kiwango cha ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima.

Waziri Mkuu vilevile amewapongeza watendaji wa Kampuni ya Mitsubishi kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umeme mkoani Kilimanjaro na akatoa rai waangalie uwekezekano wa kujenga kiwanda cha uzalishaji mbolea nchini.

Kwa upande wake Rais wa JICA Dkt. Tanaka, amemuahidi Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali katika kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali inayogusa maisha ya kila siku ya Watanzania, pia ameahidi kuwarudisha wafanyakazi waliokuwa wakijitolea katika sekta mbalimbali nchini ambao walilazimika kurudi Japan kwa sababu ya janga la UVIKO-19. 

Rais wa JICA Dkt. Tanaka alitumia fursa ya mazungumzo hayo kuelezea furaha yake na kufikisha shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia makala ya chapisho kuhusu TICAD 8. 

Miradi hiyo nane iliyowasilishwa TICAD8 ni yakipaumbele kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III).
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) akisalimiana na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Dkt. Akihiko Tanaka walipokutana kwa mazungumzo jijini Tunis nchini Tunisia.
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Dkt. Akihiko Tanaka yaliyofanyika jijini Tunis nchini Tunisia
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Mbarouk (Mb.) akichangia jambo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika baina ya Waziri Mkuu na Rais wa JICA.
Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya Waziri Mkuu na Rais wa JICA
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango - Zanzibar Bw. Aboud Mwinyi, akichangia jambo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika baina ya Waziri Mkuu na Rais wa JICA
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na ujumbe wake akiwa na katika picha ya pamoja na ujumbe wa JICA. 

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na ujumbe wake akiwa na katika picha ya pamoja na ujumbe wa JICA

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Bw. Yasuteru Hirai, yaliyofanyika jijini Tunis nchini Tunisia

8. 




Monday, August 29, 2022

UJUMBE WA SERIKALI YA TANZANIA WAENDELEA NA ZIARA NCHINI QATAR

 




Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab ukiwa katika mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi Qatar, Mhe. Mohammed Hassan Al-Obaidly Jijini Doha Tarehe 29 Agosti,2022

Kikao baina ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na ujumbe kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar kikiendelea Jijini Doha


Ujumbe wa Serikali ya Tanzania na ujumbe kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar ukiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao chao Jijini Doha

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu akimueleza jambo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Elimu ya Juu Qatar Mhe. Ibrahim bin Saleh Al Nuaimi wakati ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulipofanya ziara katika Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akimkabidhi zawadi Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usafirishaji ya MOWASALAT ya Qatar wakati ujumbe wa Tanzania ulipofanya ziara katika Ofisi hizo Jijini Doha 









TANZANIA NA QATAR ZAJADILI AJIRA WAKATI WA KOMBE LA DUNIA

Tanzania imeihakikishia Qatar kuwa ipo tayari kutoa vijana watakaoweza  kufanya kazi nchini humo, hususan katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya nguvukazi ni makubwa kutokana na nchi hiyo kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mpira wa Miguu wa  Kombe la Dunia yatakayochezwa mwezi Novemba 2022.

Hayo yameelezwa wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Ahmad Hassan Al-Hamadi yaliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha, Qatar tarehe 28 Agosti 2022. 

Mazungumzo hayo yamefanyika ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Mkataba wa Kazi uliosainiwa kati ya Tanzania na Qatar mwaka 2014.

“Tunawapongeza Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA litakaloanza mwezi Novemba mwaka huu. Aidha, napenda kukufahamisha kuwa Tanzania imewaandaa vijana wake  wenye ujuzi na hivyo tunaomba kupata nafasi za ajira na za viza (visa allocation) kwa ajili ya Watanzania kuweza kuja kufanya kazi huku hasa wakati huu wa kombe la dunia,” aliongeza Balozi Fatma 

Katika Kikao hicho, viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili hususan katika maeneo ya uwekezaji na biashara. Balozi Fatma alieleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa ya mazingira ya uwekezaji na biashara, hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Qatar kuja kuwekeza nchini katika maeneo mbalimbali kama vile utalii, kilimo, madini, maliasili, uvuvi na utamaduni.

“Napenda kukuhakikishia kuwa Tanzania inazo fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji na tunawakaribisha Serikali ya Qatar pamoja na wananchi wenu kuja kuwekeza nchini hususan katika sekta za utalii, madini, biashara na uwekezaji,” ameeleza Balozi Fatma.

Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, pia umehudhuriwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu,  Prof. Jamal Katundu, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza na Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, Bi Patricia Kiswaga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Ahmad Hassan Al-Hamadi akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha, Qatar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Ahmad Hassan Al-Hamadi akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha, Qatar. Wengine pichani ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu,  Prof. Jamal Katundu, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza na Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, Bi Patricia Kiswaga.



Sunday, August 28, 2022

JAPAN YATOA DOLA BILIONI 30 KUSAIDIA NCHI ZA AFRIKA


Serikali ya Japan imetangaza kutoa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 30 katika kipindi cha miaka mitatu (2022 – 2025) kwa Nchi za Bara la Afrika ili kuziwezesha kutekeleza programu na miradi ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi barani humo. 

Kiasi hicho cha fedha kimetangazwa kutolewa na Waziri Mkuu wa Japan Mhe. Fumio Kishida wakati wa mkutano wa 8 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Japan na Nchi za Afrika kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8 Summit) uliofanyika mjini Tunis nchini Tunisia terehe 27 - 28 Agosti 2022.

Kupitia Mkutano huo Mhe. Fumio amezihakijishia nchi za Afrika kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana nao kwa karibu kwa kuchangia maendeleo kupitia programu na miradi mbalimbali.

Mhe. Fumio pia amezihakikishia nchi hizo kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto zinazokwamisha juhudi za Afrika za kujikwamua kiuchumi. Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya Tabia Nchi na upungufu wa chakula.

Akizungumzia kuhusu kiasi cha fedha kilichotelewa, Mhe. Fumio amesema kupitia mpango wa TICAD sekta binafsi za pande zote mbili (Japan na Afrika) zimeendelea kustawi, hivyo Serikari yake itaendelea kuhamasisha Kampuni za Japan kuendelea kuwekeza Afrika katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo, Afya, nishati ya umeme na teknolojia. 

Kuhusu mgawanyo wa fedha hizo Mhe. Fumio amesema kuwa pamoja na TICAD kufanikiwa katika maeneo mengi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya na elimu, Japan katika kipindi cha miaka miatatu ijayo (2022/23-24/25) itaangazia pia maeneo muhimu yanayogusa maisha ya watu ya kila siku. 

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni mapinduzi ya kijani, Mabadiliko ya tabia nchi, kukuza uwekezaji, kuendeleza hali ya maisha ya Waafrika, ambapo kiasi cha Dola za Marekani bilioni 5 zitatolewa kufanikisha mpango huo. 

Maeneo mengine ni Afya na maendeleo ya rasilimali watu. Katika sekta ya afya Japan itachangia kiasi Dola za Marekani bilioni 1.08 kuiwezesha Afrika kukabiliana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria. Mhe. Fumio aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Serikali yake inatarajia kuwajengea uwezo zaidi ya watu 300,000 kutoka bara la Afrika katika sekta ya viwanda, afya, elimu, sheria na utawala.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameeleza umuhimu wa Bara la Afrika kuendelea kushikirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo katika ukuzaji wa uchumi. 

Mhe. Mjaliwa akiongelea madhara yaliyo sababishwa na athari za UVIKO 19 na Vita vya Urisi na Ukraine ikiwemo mfumuko wa bei wa bidhaa, ametoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kushirikiana na nchi za Afrika katika jitihada zake za kujigemea kiuchumi, ili kuhakikisha zinaendelea kutoa huduma bora na muhimu kwa wananchi wake na kuwawezesha wananchi katika shughuli zao zinazowagusa moja kwa moja kama vile kuendeleza kilimo na utalii.

Naye Rais wa Tunisia Mhe. Kais Saied ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa TICAD 8, akifungua mkutano huo amesema Japan ni mbia wa kweli wa maendeleo ya Afrika kwa kuwa wakati wote imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Afrika katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazolikabili bara hilo, na kuchangia katika kundeleza sekta mhimu kama vile elimu, kilimo, teknolojia, ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji, mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kutoa mikopo yenye riba ndogo na masharti nafuu. 

Mkutano wa 8 wa TICAD umehudhuriwa na zaidi ya washiriki 3000 kutoka nchi 55 za Bara la Afrika na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa, umebeba kauli mbiu isemayo “Kukuza Maendeleo Endelevu ya Afrika kwa ajili ya Waafrika” (“Promoting Africa-led, African-owned sustainable development”)
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaoendelea mjini Tunis, nchini Tunisia. Waliopo karibu naye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Mbarouk (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba (kushoto)
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Rais wa Tunisia Mhe. Kais Saied alipokuwa akiwasili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais de Congres mjini Tunis nchini Tunisia
Viongozi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika, Ujumbe wa Serikali ya Japan, watendaji na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa walioshiriki mkutano wa TICAD8 wakiwa katika picha ya pamoja. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Rais wa Tunisia Mhe. Kais Saied wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa TICAD8.

Saturday, August 27, 2022

MKUTANO WA NANE WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA TICAD WAANZA MJINI TUNIS, TUNISIA

Mkutano wa 8 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8 Summit) umeanza leo tarehe 27 Agosti 2022 mjini Tunis, Tunisia. Hii ni mara ya pili kwa mkutano huu kufanyika Barani Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya ule wa Kenya (TICAD 6) uliofanyika mwaka 2016. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anawakilishwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) katika Mkutano huu. 

Mkutano huo wa TICAD 8 utafanyika kwa siku mbili tarehe 27 na 28 Agosti 2022; na umetanguliwa na Kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika nchini Japan, kilichofanyika tarehe 25 Agosti 2022. Pamoja na masuala mengine, Mkutano huu unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063). 

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika. 

Agenda 2063 ilikubaliwa na viongozi wa Afrika wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika kwa lengo la kuliunganisha Bara la Afrika katika masuala ya kukuza uchumi; kuhamasisha utawala bora na utawala wa sheria; kuhakikisha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja; kuhakikisha amani na usalama unaimarika na kuiweka Afrika katika nafasi ya mchangiaji mkuu wa uchumi duniani

Mhe. Kassim Majaliwa katika mkutano huu anatarajiwa kuwa na mazungumzo ya pembezoni na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Fumio Kishida na watendaji wakuu wa kampuni na taasisi za Japan ikiwemo Shirika la Maendeleo la Japan (JICA); Kampuni ya Mitsubishi; Bodi ya Japan Tobacco Inc (JT Group); na Taasisi ya Japan inayojishughulisha na masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Afrika (Association of African Economy and Development - AFRECO). 

Tangu kuanza kufanyika kwa mikutano ya TICAD, Japan imekuwa ikiongeza kiasi cha fedha za mkopo wa masharti nafuu na msaada katika kuchangia maendeleo ya Afrika kutoka Dola za Marekani bilioni 0.6 kwa mwaka 1993 (TICAD 1) hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 20 kwa mwaka 2019 (TICAD 7). Kwa upande wa Tanzania misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka Japan imesaidia katika utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, afya, nishati ya umeme, kilimo na elimu.

Ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Japan unazingatia mwongozo wa Agenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu inayojikita kwenye kupunguza umasikini na kukuza maendeleo. Japan ni miongoni mwa washirika wakubwa wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania kupitia JICAkuanzia mwaka 1962. Tanzania ni nchi pekee inayoshirikiana na Japan katika maeneo matatu ya ushirikiano yaliyopewa kipaumbele na nchi hiyo ikiwemo, ushirikiano katika misaada na mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo; ujuzi na uzoefu kupitia program ya wajapani ya kujitolea chini ya Japan Overseas Cooperation Agreement; na fursa za mafunzo na masomo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaoendelea mjini Tunis, nchini Tunisia.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Tunisia Mhe. Najla Bouden alipowasili katika uwanja ndege wa kimtaifa wa Carthage mjini Tunis nchini Tunisia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa  kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) ulio anza kufanyika leo tarehe 27 Agosti 2022.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu wa Tunisia Mhe. Najla Bouden alipowasili mjini Tunis, Tunisia.

Friday, August 26, 2022

TANZANIA NA IRAN ZAAHIDI KUONGEZA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

Tanzania na Iran zimekubaliana kuibua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za biashara, kilimo, masoko, utalii, uwekezaji, afya, madini, nishati na utaalamu.

Hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mhe. Hossein Amirabdollahian yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Agosti 2022.

Waziri Mulamula ameeleza kuwa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini imekuja wakati muafaka ambapo, mataifa hayo mawili yenye uhusiano wa kihistoria yanatimiza miaka 40 tokea kuanzishwa kwa uhusianao wa kidiplomasia.

‘’Ziara hii inatupa muendelezo mzuri katika kuimarisha uhusiano wetu na kuangalia maeneo mapya ya kukubaliana kushirikiana” alisema Waziri Mulamula.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mhe. Hossein Amirabdollahian alieleza utayari wa nchi yake kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana utaalamu na uzoefu katika sekta mbalimbali za maendeleo ili uhusiano uliopo ulete faida za kiuchumi kwa manufaa ya mataifa hayo mawili. 

“Tumefungua ukurasa mpya wa uhusiano wa kidiplomasia kwa mataifa yetu, hivyo naamini kupitia ziara hii kutapatikana mafanikio yanayoonekana kwa maslahi ya mataifa yetu. 

Mhe. Hossein Amirabdollahian yupo nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 24 hadi 26 Agosti 2022  akiambatana na ujumbe wa Wafanyabiashara, Wamiliki wa Viwanda na Maafisa Waandamizi ambao pamoja na mambo mengine walishiriki kongamano la biashara lililofanyika Dar Es Salaam tarehe 25 Agosti 2022.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mhe. Hossein Amirabdollahian katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 26 Agosti 2022.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mhe. Hossein Amirabdollahian katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 26 Agosti 2022.

Picha ya pamoja, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mhe. Hossein Amirabdollahian  pamoja na ujumbe waliombatana nao katika mazungumzo yao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimuaga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mhe. Hossein Amirabdollahian mara baada ya kumaliza mazungumzo katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 26 Agosti 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha mmoja wa mjumbe aliyeambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mhe. Hossein Amirabdollahian baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma tarehe 26 Agosti 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mhe. Hossein Amirabdollahian katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 26 Agosti 2022.