|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena
Tax akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Ubalozi na Uwakilishi wa
Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa mataifa Vienna, Austria. Pamoja naye
ni Naibu Waziri wa Austria aneyeshughulikia masuala ya Ulaya na Uhusiano
wa Kimataifa Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal ambaye alihudhuria hafla
hiyo ya ufunguzi iliyofanyika tarehe 12 Juni, 2023. |
|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena
Tax akiwa na Naibu Waziri wa Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya
na Uhusiano wa Kimataifa Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal wakipongezana baada ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna,
Austria. |
|
Kaimu
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Vienna
nchini Austria Bi. Elizabeth Rwitunga akizungumza katika hafla ya
kuzindua Ubalozi wa Tanzania Vienna terehe 12 Juni, 2013 |
|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena
Tax akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania
jijini Vienna Austria. |
|
Mhe. Dkt. Tax akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna Austria. |
|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena
Tax akiwa na Naibu Waziri wa Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya
na Uhusiano wa Kimataifa Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal wakinyanyua
mikono baada ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna,
Austria. |
|
Naibu Waziri wa
Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa Mhe.
Peter Launsky-Tieffenthal akizungumza wakati wa hafla ufunguzi wa
Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna, nchini Austria. |
|
Baadhi ya wanadiplomasia waliopo jijini Vienna walioshiriki hafla ya ufunguzi rasmi wa
Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna wakifuatilia ufunguzi huo. |
|
Waziri
wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa
na Naibu Waziri wa Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na
Uhusiano wa Kimataifa Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal katika picha ya
pamoja na Diaspora wa Tanzania nchini Austria walioshiriki hafla ya ufunguzi rasmi wa
Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna |
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Ubalozi na Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa jijini Vienna nchini Austria.
Akizungumza katika uzinduzi huo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax
(Mb.) amesema kufunguliwa kwa Ubalozi huo ni mafanikio yanayoimarisha uhusiano
wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Austria na Taasisi za Umoja wa Mataifa zilizopo
jijini Vienna na kinaonesha jinsi Tanzania inavyoipa kipaumbele Austria.
“Kufunguliwa kwa Ubalozi huu
ni mafanikio makubwa ambayo yanaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya
Tanzania na Austria na Taasisi za Umoja wa Mataifa zilizopo hapa jijini Vienna
na kinaonesha kwa vitendo kuwa Tanzania inaipa kipaumbele Uhusiano wake na Austria,”
alisema Dkt. Tax.
Ameishukuru Serikali ya
Austria na Wizara inayoshughulikia masuala ya Ulaya na uhusiano wa Kimataifa
kwa ushirikiano mkubwa ambao imekua ikiupatia Ubalozi wa Tanzania Vienna tangu
ulipoanzishwa hadi kufikia siku ya uzinduzi.
Akiongelea uhusiano uliopo Dkt.
Tax amesema Tanzania na Austria zimeendelea kufaidika na uhusiano mzuri kati
yao kupitia maeneo mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu na hivyo kuchangia
maendeleo ya kiuchumi kwa faida ya wananchi wake.
Amesema Serikali ya Tanzania
inathamini uhusiano na ushirikiano na wadau wote ambao wanapambania agenda moja
za kulinda na kukuza amani na usalama pamoja na kupambana na uhalifu wa
kupangwa, rushwa, ugaidi na amewaomba kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta
maendeleo endelevu kwa manufaa ya watu wote.
“Serikali ya Tanzania
inathamini uhusiano na ushirikiano na wadau wote ambao tunapigania agenda moja,
ajenda hizi ni kama kulinda na kukuza
amani na usalama, kupambana na uhalifu wa kupangwa, rushwa, ugaidi na mengine
mengi , nawaomba tuendelee kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo
endelevu kwa manufaa ya watu wote,” alisisitiza Dkt. Tax.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa Ubalozi huo jijini Vienna Naibu Waziri anayeshughulikia Masuala ya
Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa wa Austria Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal
amesema Austria inapongeza uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kufungua Ubalozi
wake Austria na kuungana na nchi nyingine 16 za Afrika zenye Ubalozi nchini
humo na kuahidi kuusaidia Ubalozi huo kwa kila hali ili kufikia malengo ya kuanzishwa
kwake.
“Austria inapongeza uamuzi wa Serikali ya
Tanzania wa kufungua Ubalozi wake Austria na hivyo kuungana na nchi nyingine 16
za Afrika ambazo zina Balozi zao hapa nchini, niwa ahidi na kuwahakikishia kuwa
Serikali ya Austria iko tayari kuusaidia Ubalozi huo kwa kila hali ili ufikie malengo ya kuanzishwa kwake”, alisisitiza Waziri
huyo.
Amesema Austria inaangalia
uhusiano wake na Tanzania ambao una miaka mingi ukiwa imara na
dhabiti na kuongeza kuwa ni imani yao kuwa kufunguliwa kwa Ubalozi huo ni hatua
muhimu ya kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo.
Alisema Tanzania ina picha
nzuri nchini Austria na nchi yao ni mshirika mkubwa anayeamini katika demokrasia
imara na kuongeza kuwa Tanzania kujihusisha na harakati za kutafuta amani
katika ukanda wa Afrika Mashariki na katika maeneo mengine kunavutia zaidi.
“Tanzania ina picha nzuri hapa
Vienna, niseme wazi kuwa Nchi yetu ni mshirika mkubwa anayeamini katika demokrasia
imara na kujihusisha kwa Tanzania katika harakati za kutafuta amani katika
ukanda wa Afrika Mashariki na kwingineko kunaongeza uzuri wa picha yake,” alisema.
Hafla ya uzinduzi wa Ubalozi
huo ulioanzishwa mwaka 2021 ilihudhuriwa na wanadiplomasia mbalimbali walioko
jijini Vienna.