Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika ukiendelea jijini Beijing, China. |
Tuesday, September 3, 2024
WAZIRI KOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA MAWAZIRI WA FOCAC.
Monday, September 2, 2024
WAZIRI KOMBO AWASILI NCHINI CHINA KUSHIRIKI FOCAC
Sunday, September 1, 2024
RAIS MWINYI AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA INDONESIA KUWEKEZA NCHINI KATIKA SEKTA YA UCHUMI WA BULUU
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia na sehemu nyingine duniani kuja kuwekeza nchini katika Sekta ya Uchumi wa Buluu hususan kwenye maeneo ya Utalii, Bandari, Uvuvi na Kilimo cha Baharini, Uchukuzi na uchimbaji wa Mafuta na Gesi.
Mhe. Rais Mwinyi ametoa
mwaliko huo wakati akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Zanzibar na
Indonesia lililofanyika jijini Bali, Indonesia leo tarehe 1 Septemba, 2024.
Mhe. Rais Mwinyi ambaye
yupo nchini hapa kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwenye Mkutano wa Jukwaa la Pili la Ushirikiano wa Indonesia na Afrika amesema,
Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kwenye sekta ya uchumi wa
buluu duniani na kwamba Tanzania imejipanga kunufaika kupitia sekta hiyo kwa
kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wawekezaji kutoka Indonesia na kwingine
duniani.
“Tunaamini kwamba uzoefu uliowawezesha
Indonesia kupiga hatua kubwa kwenye Sekta ya Uchumi wa Buluu utatuwezesha na
sisi kujifunza na kufanikiwa. Hivyo tumekuja kuwaonesha na kujifunza kutoka kwa wenzetu waliopiga hatua kwenye
maeneo niliyozungumzia ikiwemo Uvuvi, kilimo cha mwani, uchukuzi, utalii na
uchimbaji wa mafuta na gesi” amesema Mhe. Rais Mwinyi.
Awali akizungumza kwenye
Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury
amesema Sera ya Mambo ya Nje ya Indonesia na ile ya Tanzania zinafanana kwa
kiasi kikubwa ambapo zote zinasisitiza katika kuchochea maendeleo kupitia
diplomasia ya uchumi. Hivyo, Kongamano hilo ni njia mojawapo ya kutekeleza sera
hizo katika kuhamasisha uwekezaji na biashara ili kuinua uchumi wa nchi hizi
mbili.
Pia alimshukuru Mhe. Rais
Mwinyi na ujumbe wake kwa kushiriki Kongamano hilo ambalo linalenga kuangazia
maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Indonesia katika sekta ya
uchumi wa buluu kwa manufaa ya pande mbili.
Wakati wa Kongamano hilo
ambalo limeandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), mada mbalimbali
kuhusu uwekezaji ziliwasilishwa na Taasisi za Tanzania ikiwemo ZIPA na Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Ujumbe wa Mhe. Rais Mwinyi
ulioshiriki Jukwaa hilo unamjumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi,
Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif, Waziri wa Madini, Mhe.
Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango,
Mhe. Amina Khamis Shaaban, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha
Tembele pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Indonesia.
Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika utafanyika jijini Bali, kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia |
Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji akishiriki Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia |
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. John Kambona akiwa na Afisa Dawati kutoka Idara hiyo, Bw. Suleiman Magoma wakishiriki Kongamano la Biashara |
Sehemu ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Indonesia wakishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Zanzibar na Indonesia |
Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia, Bw. Suleiman Saleh akishiriki Kongamano hilo |
Picha ya pamoja |
Saturday, August 31, 2024
RAIS DKT. MWINYI AWASILI INDONESIA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasili jijini Bali,Indonesia leo tarehe 31 Agosti 2024 kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Pili la Indonesia na Afrika unaofanyika jijini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.
Mara baada ya kuwasili Mhe. Rais Mwinyi ambaye ameambatana na mwenza wake Mhe. Mama Mariam Mwinyi pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali alipokelewa na Naibu Waziri wa Biashara wa Indonesia Mhe, Jerry Sambuaga.
Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika ambao utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Bandung Spirit for Africa's Agenda 2063,” unalenga kuangazia kanuni za pamoja ambazo zimeweka msingi imara wa kuwa na uhusiano jumuishi, usawa na endelevu kati ya Indonesia na Afrika.
Maeneo muhimu ya ushirikiano yanayotarajiwa kujadiliwa katika Jukwaa hilo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo na usalama wa chakula, nishati, uchumi wa buluu, madini, afya na ushirikiano wa maendeleo.
Mbali na kushiriki Mkutano huo, Mhe. Rais Mwinyi atafanya ziara ya kikazi nchini Indonesia kuanzia tarehe 04 hadi 06 Septemba 2024.
Thursday, August 29, 2024
Sunday, August 25, 2024
Ujumbe wa Tanzania washiriki Mazoezi ya ‘Walk the Talk’
WAZIRI CHUMI ASHIRIKI MKUTANO MAALUM WA AFYA WA TICAD 9
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi tarehe 24 Agosti 2024, ameshiriki mkutano Maalum wa afya pembezoni ya Mkutano wa Tisa wa TICAD ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo.
Mkutano huo uliongozwa na mada ya Ushirikiano Mpya kwa Usawa wa Afya Barani Afrika: Kuharakisha Ufikaji wa Huduma za Afya kwa Wote kwa Ubunifu kuelekea 2030.”
Mkutano huo uliandaliwa na Muungano wa Chanjo (GAVI) na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ulilenga kuangazia umuhimu wa ushirikiano na ubunifu katika kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote barani Afrika.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bunge la Japani Mhe. Fukazawa Yoichi.
Kwa kushiriki katika mkutano huo Tanzania ilipata fursa ya kujionea namna bora ya kutoa huduma za afya kwa watu wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hizo bila ya kikwazo cha kukosa hela.
WAZIRI CHUMI ASHIRIKI UZINDUZI WA LOGO YA SUMMIT YA TICAD9 2025 JAPAN
Tarehe 24 Agosti,2024, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi ameshiriki katika hafla ya uzinduzi wa logo ya Mkutano wa Tisa wa TICAD wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika 2025 nchini Japan.
Uzinduzi wa Logo hiyo ya Summit ya #TICAD9 umefanyika jijini Tokyo wakati wa Mkutano wa TICAD ngazi ya Mawaziri, ambao unafanya maandalizi ya Summit hiyo inayotarajiwa kufanyika tarehe 20 - 22 Agosti 2025, jijini Yokohama, Japan.
Uzinduzi huo ullihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za nchini
Japan ambao pia, walionesha huduma mbalimbali wanazozitoa katika nchi za Afrika.
Katika tukio hilo, Mhe. Naibu Waziri Chumi akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda walipata nafasi ya kusalimiana na wadau wa taasisi na kampuni za Japan zenye ubia na Tanzania.
Saturday, August 24, 2024
TANZANIA YAZISIHI NCHI ZA AFRIKA KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOZIKABILI NCHI ZAO
Waziri Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Yoko Kamikawa akifungua Mkutano wa
Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.
|
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo |
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo |
Washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa Mkutano huo |
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo. Pia imemewahimiza wadau wote wa maendeleo kutoka nchini Japan kuendelea kufanya biashara na kuwekeza zaidi barani Afrika ili kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya binadamu katika bara hilo ikiwa ni katika juhudi za kuendeleza amani na utulivu kikanda na kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi alipochangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika nchini Japan tarehe 24-25 Agosti 2024.
Ameipongeza Japan kwa kuwa mstari wa mbele kushiriki katika jitihada za kimataifa na kuwaomba washirika wengine wa kimataifa kuiga mfano huo na kuongeza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa ushiriki sawa na ujumuishaji wa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana katika kuhakikisha amani na usalama vinatamalaki.
Amesema kutokana na umuhimu huo Tanzania iko katika hatua za mwisho za kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji (NAP) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2000.
Amesema siku zote Tanzania imekuwa na mchango muhimu katika harakati za upatanishi, mazungumzo ya amani na njia nyingine za kidiplomasia katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa ndani na nje ya mipaka yake na ndio maana imefanikiwa kuondoa mizizi ya vita vya kikabila na migogoro kwa kuunganisha makabila takriban 126 na kutumia lugha moja ya Kiswahili kama lugha ya Taifa.
Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo Tanzania imeendelea na utamaduni wa kuwapatia hifadhi mamia ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka nchi jirani na zaidi na kwa sasa Tanzania inahifadhi wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi wapatao 237,997 huku wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.
Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe.Yoko Kamikawa umehudhuriwa na Mawaziri, washirika wa TICAD, wawakilishi na waandaaji wenza -Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Benki ya Dunia, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na mashirika ya Kimataifa na kikanda, sekta binafsi na Kiraia kutoka Japan na Afrika.
Friday, August 23, 2024
NAIBU WAZIRI CHUMI AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAPAN
Mazungumzo yakiendelea |
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato
Chumi (Mb) amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto
Tsuji ofisini kwake jijini Tokyo.
Viongozi hao wamekubaliana
kuendelea kushirikiana ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo
kati ya Tanzania na Japan kwa manufaa ya pande mbili.
Akizungumza katika kikao
hicho Mhe. Chumi aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuchangia
maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu,
uwekezaji, elimu, na afya.
Amesema Tanzania imejipanga
kuhakikisha inaongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati yake na
Japan na hivyo kuchochea ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya pande zote
mbili.
Naye, Mhe. Tsuji ameelezea utayari wa Japan kuendelea
kushirikiana na Tanzania na kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya
nchi hizo.
Amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuongeza biashara na bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana.
Mhe.
Chumia yuko nchini Japan kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa
Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) ngazi ya Mawaziri
utakaofanyika jijini Tokyo tarehe 24-25 Agosti 2024.