Thursday, September 26, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA OMAN JIJINI DODOMA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshulikia masuala ya Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi, yaliyofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi Ofisini kwake jijini Dodoma. 

Katika mazungumzo yao Mhe. Chumi amemhakikishia Mhe. Al Muslahi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Oman katika kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo kwa manufaa na maslahi ya pamoja kati ya nchi hizo na watu wake.

Mhe. Chumi pia ameishukuru Serikali ya Oman kwa uamuzi wa kuiunga mkono Serikali ya Tanzania kwa kuamua kujenga Ubalozi na Kituo cha Utamaduni jijini Dodoma ambapo waliongozana na Naibu Waziri Chumi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule kutembelea viwanja hivyo, ambavyo Tanzania iliipatia serikali ya Oman kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya ubalozi na makazi vilivyopo katika mji wa Serikali Mtumba, na mradi wa kihistoria wa ujenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Oman jijini Dodoma.

Mhe. Chumi amemhakikishia Mhe. Al Muslahi kuwa Tanzania itashiriki Kongamano la Uwekezaji na Biashara la Oman litakalofanyika tarehe 26 hadi 28 Septemba 2024 Muscat, Oman ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji na Oman. Ameongeza kuwa Ujumbe wa Tanzania utaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Sharriff Ali Shariff.

Tanzania na Oman zinashirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na utalii ambapo Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Oman mwaka huu unatimiza miaka 54 tangu kuanzishwa kwake na kuufanya uhusiano huo wa muda mrefu wa karibu na kirafiki kuendelea kuimarika zaidi.

Kwa mujibu wa TIC kuanzia mwaka 1997 hadi 2023, miradi 66 yenye thamani ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 352.6 imesajiliwa Tanzania Bara, huku Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) inaonesha kuwa kuanzia mwaka 1999 hadi 2023, Oman imewekeza miradi 23 Zanzibar yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1.2.

Aidha, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha kuwa mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda nchini Oman yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 14.6 mwaka 2022 hadi kufikia Dola milioni 16.4 mwaka 2023 na uagizaji wa bidhaa kutoka Oman umepungua kutoka Dola za Kimarekani milioni 207.9 mwaka 2022 hadi Dola milioni 100.1 mwaka 2023.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia masuala ya Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi, jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule na Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud Al Sidhani wakifurahia jambo walipotembelea eneo litakalojengwa Ubalozi wa Oman katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akelezea jambo kwenye ramani ya Mji wa Serikali Mtumba walipotembelea kiwanja cha Ubalozi wa Oman, jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi na ujumbe wao wakiwa katika mazungumzo jijini Dodoma.

NJE – SPORTS YAPONGEZWA NA UONGOZI NA MENEJIMENTI YA WIZARA


Timu ya michezo ya Wizara ya Mambo ya. Je na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports Club) imepongezwa kwa kuendelea kufanya vizuri katika michuano ya 38 Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea Mkoani Morogoro.

Pongezi hizo zimewasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu (ADA) Bw. Kawina Kawina alipotembelea na kuzungumza na wachezaji wa timu hiyo walioweka kambi kwenye milima ya Uluguru.

 Katika mazungumzo na wachezaji hao Bw. Kawina kwa niaba ya Uongozi na Menejimenti ya Wizara amewapongeza wachezaji kwa kuendelea kufanya vizuri katika michezo ya SHIMIWI na kuwahakikishia kuwa wizara ipo pamoja nao kwenye kila hatua wanayopiga katika michezo hiyo.

 “Uongozi na Menejimenti ya Wizara umekuwa ukipata taarifa kupitia Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (GCU), kuwa Nje – Sports inafanya vizuri kwenye michezo ya SHIMIWI inayoendelea hapa Mkoani Morogoro,” alisema Bw. Kawina.

 Aliongeza kuwa, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo anamatumaini makubwa na na timu hiyo na matarajio ya Wizara ni kuwa wataibuka na ushindi na kurejea na Vikombe.

 Bw. Kawina pia amewapongeza wanamichezo wote kwa kuendelea kuwa waadilifu na kuonyesha nidhamu huku wakizingatia Kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma wakati huu wa Michezo ya SHIMIWI na kuwa chachu ya kuzifikisha Timu zote tatu za Nje Sports katika hatua ya 16 Bora.

Akizungumza katika kikao hicho na Mkurugenzi Kawina  Kapteni wa Mpira wa Miguu Bw. Mikidadi Magola ameishukuru Wizara kwa namna inavyokabiliana na changamoto zinazoikabili  timu ya Nje  na kuiwezesha Timu kupata vifaa vyote vya mühimu kwa timu hiyo  ambavyo vimekuwa chachu ya kufanya vizuri kwenye michezo ya SHIMIWI mwaka huu.


Wednesday, September 25, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI NA BALOZI WA JAPAN WAKUTANA JIJINI DODOMA


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisalimiana na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa walipo akutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi amekutana na Balozi wa Japan nchini Mhe. Yasushi Misawa aliyemtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma. 

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Japan kwa manufaa ya pande zote.

Mhe. Chumi aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia sekta mbalimbali na hivyo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mhe. Chumi pia amemhakikishia Mhe. Balozi Misawa kuwa Tanzania inajali na kuthamini uhusiano wake na Japan na kumuahidi kuwa Mamlaka ya Biashara Nje (Tantrade) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan wanaendelea na maandalizi ya kushiriki katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara yatakayofanyika Osaka nchini Japan mwaka 2025.

Naye Balozi wa Japan Mhe. Misawa ameelezea utayari wa nchi yake kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa manufaa ya pande zote mbili.

Pia ameshukuru Ushirikiano anaoupata kutoka Serikali ya Tanzania na hivyo kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Tanzania na Japan zinashirikiana kupitia sekta za biashara na uwekezaji, miundombinu, afya na masuala ya kodi.
Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi yaliyofanyika jijini Dodoma. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea

Tuesday, September 24, 2024

NJE – SPORTS WANAUME YAFUZU HATUA YA MAKUNDI 16 BORA MICHEZO YA SHIMIWI


Timu ya Mpira wa Miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje– Sports) Wanaume imefuzu kuingia hatua ya makundi 16 Bora kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) baada ya kuifunga Timu ya Wizara ya Kilimo na kutoka Sare (0 - 0) na Timu ya Ujenzi.

Timu hiyo ikiwa imevalia jezi nadhifu zilizopendezeshwa kwa rangi ya njano na buluu, yenye kuvutia machoni mwa mashabiki waliojitokeza kuutazama mtanange wa kukata na shoka kati ya timu hiyo na Timu ya Ujenzi uliochezwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (Mji kasoro Bahari) majira ya saa tatu asubuhi ya tarehe  24 Septemba 2024, ilijituma kikamilifu hadi kutoka sare ya 0-0 na timu hiyo hatua iliyofanikisha timu ya Nje kusonga mbele hatua ya makundi.

Akizungumza kwa njia ya simu ili kuwapa hamasa wachezaji hao, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Chiku Keguhe amewapongeza wachezaji wote wa Nje – Sports kwa kuingia 16 Bora, na kuwakumbusha kuwa Wizara ipo pamoja nao hatua kwa hatua. 

“Nawapongeza kwa kufuzu kuingia 16 bora, mmeiheshimisha Wizara na hii ndio maana sahihi ya Diplomasia ya Michezo. Pongezi kwenu wachezaji kwa kuendelea kupambana na kuhakikisha mnachukua ushindi. Tusisahau matarajio ya Viongozi na Menejimenti ya Wizara ni kupata Vikombe” amesema Bi. Chiku Keguhe.

Akizungumza mara baada ya kufuzu hatua hiyo,  Kocha wa Nje – Sports,  Bw. Shabani Maganga amewapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kuonesha mchezo mzuri unaoakisi Diplomasia ya Michezo na kuwasihi kuendelea kupambana na kuhakikisha wanafika fainali.

Nje Sports wanaume imeendelea kupata matokeo mazuri na kuifanya kuwa nafasi ya pili kwenye kundi H, huku wachezaji wake wakiendelea kujifua kikamilifu kwq lengo la kuchukua ushindi wa SHIMIWI kwa mwaka 2024–2025.

Ikumbukwe kuwa, mbali na mpira wa miguu, Timu ya Nje–Sports pia inashiriki Mchezo wa Kamba kwa Wanawake na  Netiboli ambayo yote imeingia kwenye hatua ya makundi 16 bora.

Timu zote za Nje–Sports zitaendelea na mazoezi mepesi huku zikisubiri ratiba ya mchezo wa makundi unaotarajiwa kutolewa na viongozi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).


Waziri Kombo ashiriki kwenye Mkutano wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Foreign Affairs Ministers Meeting - CFAMM)



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Thabit Kombo (Mb.) ameshiriki kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Foreign Affairs Ministers Meeting - CFAMM) uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) tarehe 23 Septemba, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York. 

 

Kikao hicho kilicho hudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi 56 za Jumuiya ya Madola kilijadili ajenda mbalimbali, zikiwemo taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika mwaka 2022, Kigali, Rwanda na taarifa ya maandalizi ya Mkutano ujao wa CHOGM, utakaofanyika mwezi Oktoba 2024, Apia, Samoa.
 

Monday, September 23, 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki Mkutano wa ngazi ya juu wa Wakuu wa Nchi na Serikali ‘Summit of the Future’



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 22, 2024 ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya juu wa Wakuu wa Nchi na Serikali ‘Summit of the Future’ uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa New York nchini Marekani.

Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa nchi na Serikali duniani ili kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo na namna wanaweza kuboresha hali ya sasa na kuzilinda siku zijazo.

Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliambatana na viongozi waandamizi wa Serikali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Hussein Kattanga.

Mheshimiwa Majaliwa yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79).


Sunday, September 22, 2024

TANZANIA NCHI YA MFANO KATIKA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA USHIRIKIANO KATI YA SEKTA BINAFSI JAPAN NA WAKULIMA WADOGO WA KAHAWA UNAOTEKELEZWA NA SHIRIKA LA KIMATAIFA LA MAENDELEO YA KILIMO (IFAD)


Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akihutubia kwenye uzinduzi wa utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano kati ya sekta binafsi na wakulima wadogo wa zao la kahawa uliohusisha Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa ushirikiano wa Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ya Japan (MAFF) na sekta binafsi chini ya makampuni makubwa ya Japan, Septemba 20, 2024.



Tarehe 20 Septemba 2024, Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa ushirikiano wa Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ya Japan (MAFF) na sekta binafsi chini ya makampuni makubwa ya Japan yanayojishughulisha na kahawa ya UCC Holdings na Marubeni; zilizindua utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano kati ya sekta binafsi na wakulima wadogo wa zao la kahawa ambapo, Tanzania imechaguliwa kuwa nchi ya kwanza na ya mfano katika utekelezaji wa Mpango huo. 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na hata uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyinginezo. Amelitaja kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini ambalo, linatumika kibiashara kwa kulipatia Taifa pato kubwa kwa mauzo mengi ya kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan kwa wastani wa asilimia 34 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini Japan. Takwimu hizo zinaiweka Japan kuwa mnunuzi mkubwa na namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini. 

Aidha, Balozi Luvanda alielezea juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, na pia wakulima kujipatia kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini. 

Kwa upande wake, Mheshimiwa Mitsuo Takahashi, Naibu Waziri wa Kilimo, Misitu na Uvuvi wa Japan, anayehusika na Masuala ya Bunge la Japan, katika hotuba yake alieleza kuwa Japan na Tanzania ni washirika wakubwa wa maendeleo hususan, katika sekta ya kilimo. Alibainisha kuwa Japan inaitambua Tanzania kwa uzalishaji wa kahawa yenye ubora ambayo, imejizolea umaarufu na kuwa miongoni mwa kahawa tatu bora nchini humo. Kwa umuhimu huo, alieleza kuwa Serikali ya Japan kwa kushirikiana na sekta binfasi kupitia makampuni ya Marubeni na UCC Hodlings imedhamiria kutekeleza Mpango wa ELSP unaoratibiwa na Shirika la IFAD kuliongezea thamani na uzalishaji zao hilo kwa kuboresha mazingira ya kilimo kwa wakulima wadogo wa kahawa kusini mwa Tanzania, katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma. 

Aidha, Waziri Takahashi, alielezea chimbuko la Mradi huo kuwa mnamo mwezi Aprili 2023, Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi (MAFF) ya Japan ilitangaza kuanza utekelezaji wa ‘Mapango wa Ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Wazalishaji Wadogo (ELPS)” ukiwa ni moja ya maazimio yaliyopitishwa na Marais wa Nchi zenye Nguvu Kiuchumi Duniani wa Kundi la G7 kwenye Mkutano wao uliofanyika jijini Hiroshima, Japan. 

Vilevile, kwa upande wake Bi. Gerardine Mukeshimana, Makamu wa Rais wa IFAD, aliuelezea Mpango wa ELPS unaotekelezwa na Shirika hilo, kuwa unalenga kubadilisha kilimo cha wazalishaji wadogo kwa njia endelevu kwa kuboresha uzalishaji wao na upatikanaji wa soko kwa kuchochea ushiriki wa sekta binafsi na uwekezaji katika kilimo na mifumo ya chakula. Alieleza kuwa Mpango huo una lengo mahsusi katika kuunganisha wazalishaji wadogo na makampuni ya sekta binafsi, kutumia mitandao ambayo IFAD imeianzisha katika maeneo ya vijijini kwa nchi zinazoendelea. Hivyo kufuatia lengo hilo, alifafanua kuwa IFAD, kwa ushirikiano wa karibu na MAFF na kampuni za UCC na Marubeni, imeanzisha Mradi wa Kwanza wa Majaribio wa Mpango huo na kuwa nchi iliyochaguliwa ni Tanzania kupitia zao la kahawa; Mradi huo utasaidia vyama tisa vya ushirika vya wakulima Tanzania (AMCOS) katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma, utakaogharimu takriban Dola za Marekani 460,000. 

Mwishoni mwa mwezi Juni hadi mapema Julai 2024, IFAD pamoja na UCC na Marubeni, zilifanya ziara nchini Tanzania ili kutekeleza Mpango wa ELPS kwa uwekezaji wa pamoja. Tukio la Uzinduzi wa Mpango huo lililofanyika Tokyo, Japan, tarehe 20 Septemba 2024, limelenga kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya wadau hao wakubwa ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa. Pia, kwa upande wa Japan, uzinduzi huo umelenga kuweka Mpango wa ELPS kuwa ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi; na kwa upande wa IFAD, uzinduzi huo umelenga kukuza maslahi na mahitaji miongoni mwa washirika watarajiwa wa sekta binafsi pamoja na Serikali za Kundi la G7 hususan, katika kuujengea uwezo Mpango wa ELPS. 
 Naibu Waziri wa Kilimo, Misitu na Uvuvi wa Japan, anayehusika na Masuala ya Bunge la nchi hiyo Mhe. Mitsuo Takahashi, akisisitiza jambo kwenye uzinduzi wa utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano kati ya sekta binafsi na wakulima wadogo wa zao la kahawa uliohusisha Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa ushirikiano wa Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ya Japan (MAFF) na sekta binafsi chini ya makampuni makubwa ya Japan, Septemba 20, 2024.


Friday, September 20, 2024

NJE - SPORTS Netiboli YAANZA VIZURI SHIMIWI, YAIBAMIZA RAS LINDI

 


Timu ya netiboli ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje - Sports) imeanza kwa kishindo Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) baada ya kuitandika bila huruma Timu ya Ras Lindi kwa magoli 39 -16.

 

Kama wahenga wasemavyo Nyota njema huonekana asubui, katika mchezo huo nyota ya Nje - Sports Netiboli ilianza kuangaza tangu kipenga cha mwamuzi wa mchezo kilivyopulizwa, ikionyesha ustadi wao wa hali ya juu.

 

Akizungumza mara baada ya ushindi huo, Kapteni wa Netiboli Nje – Sport Bi. Faraja Kessy, amesema ushindi huo umetokana na maandalizi mazuri ya muda mrefu, hata hivyo mchezo ulikuwa na ushindani Mkubwa sana lakini tumeibuka na Ushindi Mnono. 

 

"Hakika tunafuraha sana kwa kuanza vizuri katika mchezo wetu wa kwanza wa netiboli. Na matarajio yetu ni kuendelea kufanya vyemza zaidi na kuweza kuibuka washindi katika Michezo hii ya SHIMIWI”. 

 

Vilevile, Bi. Faraja Kessy ameushukuru Uongozi na menejimenti ya Wizara kwa ujumla kwa namna ambavyo wamekuwa mstari wa mbele kutoa hamasa kwa wanamichezo na kuahidi kuendelea kufanya vyema katika michezo iliyobakia katika kundi letu.

 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Michezo Nje – Sports, Bw. Ismail Abdallah ameendelea kuwapongeza na kuwapa hamasa zaidi wana michezo woote. “Kwakweli leo Mambo yako mazuri nifuraha sana kuona tokea asubui tunapata ushindi tuu”.

 

Kesho Tarehe 21 Septemba, 2024 Nje – Sports wanawake wanatarajia kurusha karata yao ya pili ambapo watamenyana na Mahakama, kwa upande wa Mpira wa Miguu Nje – Sports wanashuka dimbani kucheza mchezo wao wa kwanza ambao watachuana na Utumishi.









Nifuraha kweli kweli.







Nje - Sports Wanawake Kamba yaibuka na ushindi dhidi ya Ras Mara


 

Thursday, September 19, 2024

NJE - SPORTS YAJIGAMBA KUFANYA VYEMA KWENYE MASHINDANO YA SHIMIWI - MOROGORO


Ratiba ya makundi katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoanza kufanyika mkoani Morogoro imetolewa hadharani, huku Timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Wanaume (Nje-Sports) inatarajia kurusha karata yake ya kwanza tarehe 21 Septemba, 2024 kwa Kuvaana na Timu ya Ras Mara.

Mwenyekiti wa Nje - Sports Bw. Ismail Abdallah amesema kuwa katika mpira wa miguu, timu ya Nje Sports imepangwa kundi G pamoja na timu za Utumishi, Wizara ya Ujenzi, Ras Mara na Ras Lindi.

Ameeleza pia kuwa timu ya Nje – Sports Kamba (Ke) imepangwa katika kundi B na itapepetana na timu za Hazina, Kilimo na Ras Shinyanga, huku mpira wa Pete ikipangwa kundi H na itaumana na Mahakama, Maadili, na Ras Lindi.

Kwa upande wa Kocha wa Nje – Sports, Bw. Shabani Maganga amesema vijana wote wapo salama na wapo tayari kupambana katika mashindano hayo ili kuibuka na ushindi kwenye kila mchezo kutokana na ubora wa timu waliyonayo.

Leo jioni tarehe 19 Septemba, 2024, Nje Sports imeendelea kufanya mazoezi mepesi ya kujiandaa na mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuanza kesho tarehe 19 Septemba, 2024.

Nje - Sports inayoshiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Mpira wa Miguu Wanaume, Kamba wanawake, Mpira wa Pete, Bao, Karata, iliwasili mkoani Morogoro jumatatu tarehe 16 Septemba, 2024 na kuzua gumzo kwenye viunga na mitaa mbalimbali ya mjini Morogoro (Mji kasoro Bahari).



Wednesday, September 18, 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 11 WA TAASISI YA MERCK FOUNDATION AFRIKA ASIA LUMINARY

 





Balozi Shelukindo aongoza Kikao na Sekretarieti ya SADC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameiongoza timu ya Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-ORGAN)  katika siku ya pili ya kikao na Sekretarieti ya SADC.

Kikao hicho kilichoratibiwa na Bw. Terry Rose, Afisa Mkuu Kamati ya Siasa na Diplomasia ya SADC kimejikita katika kujadili masuala mbalimbali yahusuyo muundo wa kamati hiyo na majukumu yake ndani ya kanda ikiwemo uangalizi wa uchaguzi kwa nchi zinazotarajia kufanya uchaguzi. Nchi hizo ni pamoja na Jamhuri ya Msumbiji, Botswana, Namibia na Mauritius chini ya  Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC (SEOMs) na Baraza la masuala ya Uchaguzi la SADC (SEAC).

Aidha, Kikao hicho kimejadili masuala mengine ikiwemo utekelezaji wa maamuzi  yanayohusu siasa na diplomasia katika Kanda, sera na mikakati ya siasa na diplomasia pamoja na mifumo ya usuluhishi na kuzuia migogoro ili kuimarisha demokrasia na ushirikiano kati ya Nchi Wanachama  kupitia Baraza la Usuluhishi (MRG) na Jopo la Wazee (PoE).


 

Monday, September 9, 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amwakalisha Rais Samia kwenye ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezitaka Mamlaka za Udhibiti na Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.


Dkt. Biteko ametoa agizo hilo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) lililofanyika  Septemba 9, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) cha jijini Arusha.


Mhe.Dkt. Biteko amesema Serikali inatambua kuwa fedha nyingi zinazotengwa kwenye bajeti yake kila mwaka zimekuwa zikitumika kwenye ununuzi wa umma na kuongeza kuwa Serikali imekuwa makini kuhakikisha fedha hizo zinapata usimamizi makini.


“Naomba Wizara ya Fedha mlisimamie hili na haya ni maelekezo ya Mhe. Rais. Majukwaa yaliyofanyika yote yametilia mkazo maadili, weledi, uwazi na uwajibikaji kwani bila ya maadili wananchi hawawezi kupata huduma, pia fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya wananchi kupata huduma zinaamriwa na kundi hili na kama hatuna taasisi imara za ugavi na ununuzi hatutapata matokeo tarajiwa na hivyo  umasikini utaongezeka,” amesema Dkt. Biteko.


Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Dkt. Leonada Mwagike ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma na hivyo kuleta tija na kuongeza uwajibikaji ili kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika.


Hafla ya ufunguzi wa Jukwaa  hilo la 16 la Ununuzi wa Umma kwa Nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), umehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia maswala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Shaibu Mussa.


 Jukwaa hilo la  Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) linafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa AICC, jijini Arusha.

Saturday, September 7, 2024

RAIS SAMIA AWAHIMIZA DIASPORA KUWEKEZA NCHINI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watanzania wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing, tarehe 06 Septemba, 2024.

· Atumia saa 7 kuongea na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya Nchi (Diaspora) kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta mbalimbali nchini. 

Rais Samia ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na Diaspora waishio nchini China katika mkutano uliojumuisha watanzania wanaofanya kazi nchini humo, wafanyabiashara na wanafunzi uliofanyika jijini Beijing tarehe 6 Septemba 2024.

Akizungumza na Diaspora hao waliojitokeza kwa wingi, wakionesha furaha na shauku kubwa ya kuzungumza na Rais Samia, aliwaeleza kuwa licha ya fursa lukuki za kiuchumi zilizopo nchini Serikali imefanya maboresho ya sera na sheria mbalimbali ili kutoa fursa na kutanua wigo kwa Diaspora kuwekeza nchini.

Rais Samia amezitaja fursa hizo zinazopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, viwanda, kilimo na madini. Aliongeza kufafanua kuwa, katika sekta ya ujenzi hivi sasa Serikali imeandaa utaratibu mahususi kwa Diaspora, unaowapa fursa ya kujengewa na kumiliki nyumba nchini. 

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaeleza Diaspora kuhusu hatua liyopigwa na Serikali katika kuboresha utoaji huduma za kijamii kwa Wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, na usafirishaji akitolea mfano wa treni iendayo kwa haraka (SGR) ambayo katika kipindi kifupi imeleta mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo na ujenzi wake ukiwa unaendelea. Sekta zingine ni nishati, kilimo, maji, mawasiliano na ukuaji wa demokrasia.

“Nyumbani tuko vizuri, mfano sasa hivi safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma inachukua saa 3 hadi 4 pekee kwa kutumia treni yetu mpya tuliyoizindua hivi karibuni. Tumefanya maboresho makubwa ya sera na sheria ili kuwapa fursa ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa urahisi. Njoeni muwekeze nymbani”. Alisema Rais Samia.

Mbali na hayo amepongeza juhudi na uzalendo unaoendelea kuonyeshwa na Diaspora katika kuchangia shughuli za maendeleo nchini ikiwemo kuleta watalii, wawekezaji na kusaidia kuratibu shughuli za matibabu. Aliongeza kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la fedha zinazotumwa nyumbani (remittance) kutoka ughaibuni,

Vilevile, Rais Samia ametoa wito kwa Diaspora wa nchini humo na kwa nchi zingine, hususan kwa jamii ya wanafunzi kujiandisha katika vyama vyao vya Jumuiya kwenye maeneo waliyopo. Akasisitiza kuwa hatua hiyo hiyo, licha kusadia kutambuana na kukuza umoja wao inarahisisha namna ya kuwafikia wanapohitaji huma mbalimbali hasa wakati zinapotokea changamoto ikiwemo majanga kama vile mlipuko wa magonjwa. 

Katika hatua nyingine Rais Samia akiwa jijini Beijing amekutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni Sita (6) makubwa ya nchini humo ikiwemo China Academy of Space Corporation (CASC), China Electronics Corporation, Transsion Group, Weihua Group, China Railway Construction Corporation (CRCC), Acme Consultant Engineers PTE Limited na CND jijini Beijing, tarehe 06 Septemba, 2024.

Katika zoezi hilo alilolifanya kwa takribani saa 7 mfulilulizo bila mapunziko, aliambatana na Watendandaji na Mawaziri wanaosimamia sekta mbalimbali wakiwemo; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo (Mb.), Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb.), Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb.), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega (Mb.).

Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (Mb.) Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohamed Khamis Abdullah na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Bw. Gilead Teri.

Rais Samia alikuwa nchini China kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika tarehe 4-6 Septemba 2024. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza Diaspora kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo,akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na watazania wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.
 Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Felista Rugambwa (katika) akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na watazania wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.

Matukio mbalimbali katika mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Watanzania waishio nchini China (Diaspora) uliofanyika Jijini Beijing tarehe 06 Septemba, 2024.






Matukio mbalimbali wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungu na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China Academy of Space Corporation (CASC), China Electronics Corporation, Transsion Group, Weihua Group, China Railway Construction Corporation (CRCC) pamoja na Acme Consultant Engineers PTE Limited na CND ya nchini China jijini Beijing, China tarehe 06 Septemba.