Sunday, August 18, 2024

TANZANIA YAKABIDHIWA UENYEKITI WA SADC ORGAN TROIKA

 

Mkutano wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) leo tarehe 17 Agosti, 2024 umekabidhi jukumu la Unyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ on Politics, Defence and Security) kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Asasi hiyo ina jukumu la kusimamia masuala ya ulinzi na usalama katika kanda ya SADC na ina mamlaka ya kuongoza na kutoa ushauri kwa nchi wanachama katika masuala yanayohatarisha amani, usalama na utulivu katika kanda hiyo. Majukumu hayo huratibiwa katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi hiyo.

Nafasi za uongozi kwa upande wa SADC Organ hufuata mzunguko kama ilivyo katika nafasi ya uongozi wa SADC lakini sio nchi zote zinaweza kuwa Mwenyekiti isipokuwa kwa kigezo cha uwepo wa hali ya ulinzi na usalama katika nchi mwanachama. Tanzania imeshawahi kuwa Mwenyekiti mara tatu katika vipindi tofauti: 2006/2007, 2012/2013 na 2016/2017 na sasa itaongoza kwa kipindi cha 2024/2025 ambapo itakuwa mwenyeji wa vikao vya Asasi hiyo kwa kipindi husika.

Kufuatia utaratibu huo, Troika ya SADC kwa mwaka 2024/2025 inaundwa na Zambia (Mwenyekiti aliyemaliza muda) Tanzania (Mwenyekiti wa sasa) na Malawi (Makamu Mwenyekiti).

Jukumu kubwa linalomkabili Mhe. Rais Samia katika asasi hiyo ni pamoja na kusimamia amani Mashariki mwa DRC hivyo, ataendeleza jitihada zake pale ambapo uongozi uliopita uliishia.

Mkutano huo pia, umemthibitisha Mwenyekiti wa SADC ambapo, Mhe. Emerson Bambudzo Mnangagwa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe amepokea jukumu hilo na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa SADC imeenda kwa Mhe. Andry Rajoelina Rais wa Jamhuri ya Madagascar ambapo nchi hizo zitaongoza katika kipindi cha 2024/2025.

Akihutubia mkutano huo Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Mnangangwa amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea jukumu la uenyekiti wa SADC na amemuhakikishia ushirikiano katika kufanikisha majukumu hayo waliyokabidhiwa kwa ustawi wa kanda na wananchi wake.

Pia, ameeleza kuwa jumuiya hiyo inaendelea kufungua fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kikanda kupitia agenda yake ya kipaumbele ya maendeleo ya viwanda. Jitihada hizo zitakuza ubunifu na kuongeza thamani ya bidhaa katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Kuhusu shughuli nyingine zilizofanyika sambamba na mkutano huo Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa kulikuwa na Kongamano la Uwekezaji lililoandaliwa na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA) na Wiki ya Viwanda ambazo zilitumika kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali kutoka nchi wanachama pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabishara kubadilishana uzoefu na kukuza mtandao wa biashara.

Shughuli nyingine iliyofanyika ni pamoja na mhadhara wa umma ambao unasaidia katika kujenga uelewa wa masuala ya msingi ambayo husaidia katika ubunifu na kuendelea kuimarisha hatua za mtangamano. Hivyo ni muhimu kwa vyuo vikuu na vyuo vingine vinavyofanana navyo kutafakari namna bora ya kuwekeza katika ubunifu ili kuwezesha mikakati ya kikanda kupata matokeo ya kimaendeleo kwa mafanikio.

Pamoja na hayo amesisitiza umuhimu wa kukuza sekta ya nishati, kilimo, biashara, uwekezaji na usafirishaji na kuhimiza umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto zake na kuiwezesha jumuiya hiyo kuinuka kiuchumi.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali pia umemalizika kwa nchi wanachana kusainiwa Itifaki na matamko mbalimbali ya kikanda, kwa upande wa Tanzania imesaini Itifaki ya Ajira na Kazi, Tamko la Kuwalinda Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi na Tamko la Kutokomeza Ugonjwa wa Ukimwi kama Janga la Kiafya kwa Jamii ya Ukanda wa SADC ifikapo 2030.


Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)  wakiwa katika picha ya pamoja  wakati wa Mkutano wao Kawaida wa 44 uliofanyika tarehe 17 Agosti, 2024Harare, Zimbabwe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto) akishiriki Mkutano wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 17 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.

Saturday, August 17, 2024

ZAMBIA YAIHAKIKISHIA TANZANIA USHIRIKIANO KATIKA UONGOZI WA SADC ORGAN TROIKA

 

Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema ameihakikishia ushirikiano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huu inapotarajia kukabidhiwa jukumu la uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) na kuahidi kutimiza majukumu yake kama Mwenyekiti anayemaliza muda wake kwa kipindi cha 2023/2024.

 

Kadhalika, ameshukuru kwa ushirikiano alioupata wakati wa uongozi wake na pia ameonesha kuwa na imani na Tanzania katika kupokea jukumu la unyekiti wa Asasi ya SADC Organ Troika.

 

“Nipende kumhakikishia ushirikiano dada yangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake, pia nina imani utaiongoza Organ na kuifikisha katika hatua ya juu ya mafanikio kama ambavyo umekuwa ukifanya katika majukumu mengine uliyoaminiwa” Mhe. Hichilema.

 

Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi hiyo ya SADC Organ Troika uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe na kuhudhuria na Mhe. Hichilema Rais wa Jamhuri ya Zambia na Mwenyekiti wa sasa ambaye ameshiriki kwa njia ya mtandao.

 

Mbali na Mhe. Hichilema Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mhe. Nangolo Mbumba Rais wa Namibia na Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wake na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti ajaye wa Asasi hivyo, kukamilisha safu ya nchi zinazounda Utatu huo.

 

Aidha, katika hotuba wakati wa kufungua na kufunga mkutano Mhe. Hichilema amewashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kutumia muda wao na rasilimali zao kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika mijadala mbalimbali yenye maslahi ya kanda.

 

“Ni matumaini yangu kuwa agenda zilizowasilishwa mbele yetu zitajadiliwa kwa tija na kwa maslahi ya pande zote kwa ajili ya ustawi wa Jumuiya na watu wetu” alisema Mhe. Hichilema.

 

Hivyo, ni muhimu kuwa tayari kuonesha umoja na nia ya kufanikiwa kwa pamoja katika kuijenga jumuiya yenye amani na usalama hali ambayo itachangia kukuza uchumi kupitia shughuli za biashara na uwekezaji kwenye kanda.

 

Pia, alitoa shukrani za kipekee kwa Jamhuri ya Namibia kwa kipindi ambacho imeongoza kupitia Hayati Rais Hage Geingob na Rais wa sasa Mhe. Dkt. Nangolo Mbumba, sambamba na Sekretarieti ya SADC kwa usikivu, uvumilivu na uongozi wa mfano wa Bw. Elias Magosi ambaye pamoja na timu yake wamekuwa wakifanya kazi bila kuchoka kuratibu kufanyika kwa mikutano hiyo.

 

Vilevile akaeleza kuwa utatu wa asasi hiyo ni utaratibu mzuri wa kuendesha taasisi yoyote yenye lengo la kufikia mafanikio kwakuwa, inaruhusu muendelezo wa utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kikanda na kuhifadhi kumbukumbu ya masuala mbalimbali ili hurahisisha ufuatiliaji na maamuzi.

 

Tanzania inatarajia kukabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) katika Mkutano wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.

 

Pamoja na masuala mengine mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC Organ Troika umepitia na kujadili hali ya ulinzi na usalama katika kanda, hali ya ulinzi na usalama katika Falme za Eswatini na Lesotho, hali ya ulinzi na usalama katika jimbo la Cabo Del Gado na hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Habari katika picha, wakati Rais Samia aliposhiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa  SADC Organ Troika









Friday, August 16, 2024

WAZIRI KOMBO ASISITIZA AMANI NA USALAMA KATIKA KANDA YA SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha amani na usalama katika kanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).


Balozi Kombo ametoa Msisitizo huo wakati wa Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO) wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)  uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.


Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 15 Agosti, 2024 ambapo, mikutano hii miwili ni mikutano ya awali ya maandalizi ya agenda na nyaraka kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika leo tarehe 16 Agosti, 2024.


Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi hiyo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha wajumbe wa mkutano huo kujadili ajenda zilizojikita katika kutafuta amani na usalama wa Jumuiya hiyo na umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kufanikisha jitihada za suala hilo.


Agenda zilizojadiliwa na mkutano huu ni pamoja na Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda, Uimarishwaji wa Demokrasia katika Kanda, Mfumo wa Kuwaenzi Viongozi Waasisi wa SADC na Wagombea wa Nafasi mbalimbali wa Kanda katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.


Akichangia katika mkutano huo Waziri Kombo amesema kuwa Tanzania inalipa kipaumbele suala la kuimarisha ulinzi na usalama katika kanda na katika kufanikisha hili Tanzania inashiriki kikamilifu katika juhudi za kutafuta amani ndani ya kanda, barani Afrika na duniani ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama zake.


“Tuna nia ya dhati ya kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika masuala ya amani na usalama. Tunaamini uzoefu wetu utatuwezesha kuchangia kwa ufanisi katika jukumu la Baraza la Usalama” alisema waziri Kombo.


Aidha, Waziri Kombo amewasilisha ombi la kuendelea kuungwa mkono na nchi za SADC katika nafasi mbalimbali zinazowaniwa na Watanzania ikiwemo nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) – Afrika inayowaniwa na Dkt. Faustine Ndugulile.


Pia, ameomba kuungwa mkono katika nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2026 – 2028 na Ujumbe usio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2029 na 2030.


Mkutano huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

======================================= 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akishiriki Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.

Kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) wakifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024.

Kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) wakifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024.



Kulia ni Mhe. Dkt. Ndugulia anayewania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika. 
Kulia ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Jacob Mkunda akifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.

Ujumbe wa Tanzania ukiwa umesisiamam wakati wimbo wa SADC uliokuwa ukiimbwa kabla ya kuanza kwa mkutano.

Ujumbe wa Zambia

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Tanzania


KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA KIKAO CHA KAMATI YA MAKATIBU WAKUU WA SADC ORGAN TROIKA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu cha Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 15 Agosti, 2024.

Mkutano huo pamoja na masuala mengine umejadili Hali ya Siasa, na Usalama katika kanda.
Nchi zilizoshiriki kikao hicho cha utatu ni pamoja na Tanzania, Zambia na Namibia.


Thursday, August 15, 2024

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA IOM KUWEZESHA VIJANA

Tanzania imesisitiza kuendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa lilanoshughulikia Wahamiaji (IOM) kuwawezesha vijana kiuchumi ili kutengeneza ajira zitakazojenga ustawi wao na kuleta maendeleo kwa taifa.

Msisitizo huo umetolewa leo tarehe 15 Agosti, 2024 wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alipokutana na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER jijini Harare, Zimbabwe.

Aidha, katika mazungungumzo hayo Waziri Kombo ameeleza changamoto ya uhamiaji huwaathiri zaidi vijana wanaotoka katika mataifa yanayoendelea hususan mataifa ya Afrika ambapo wamekuwa wakihama kwenda kutafuta maisha bora kwa ajili yao na familia zao.

"Binafsi ningependa tatizo la uhamiaji lipate suluhisho kwa kufanyia kazi chanzo cha tatizo badala ya kufanyia kazi matokeo au matatizo yanayotokea baada ya watu kuhama na kupata changamoto wakiwa katika harakati za kuvuka mipaka" alisema Waziri Kombo.

Pia ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua changamoto hiyo imetafuta suluhisho la ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwawezesha kiuchumi kupitia mradi wa kilimo ujulikanao kama “Building Better Tomorrow (BBT)’’ ambao, utawawezesha vijana kujiajiri na kuwaajiri wengine, pamoja na kufanya kilimo biashara kwa lengo la kukuza kipato.

Kwa upande wa Bw. ABDIKER ameipongeza Tanzania kwa kuwahudumia wahamiaji ambao sehemu kubwa ni wakimbizi na wale wanaopita kutoka Pembe ya Afrika kuelekea kusini mwa Afrika kutafuta maisha bora na kwamba IOM inaendelea kutoa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

Pia amepongeza kwa uwepo wa chuo cha uhamiaji nchini ambacho kimekuwa kikitoa elimu ya uhamiaji kwa watanzania na kwa mataifa mengine na pia amesema kuwa IOM ina mpango wa kuanzisha chuo kikubwa cha uhamiaji kitakachochukua wanafunzi ulimwenguni kote, hivyo uwepo wa chuo hicho utaongeza ushirikiano na kujenga uwezo wa kitaaluma katika masuala ya uhamiaji.

Vilevile, viongozi hao wamejadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wahamiaji ikiwemo, mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababisha ajali kwenye safari za majini na kupelekea watu kupoteza maisha wakati wa kuhama sambamba na ajira zisizo na staha wanazozipata baada ya kufika uhamishoni pasipo kupata taratibu rasmi za kuhama.

Hivyo, IOM ina matumaini ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania hasa wakati huu ambapo inaenda kukabidhiwa nafasi ya Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security).

================================

Habari katika picha za mazungumzo ya Mhe. Waziri Kombo na Bw. Mohammed ABDIKER

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER (hayupo pichani) jijini Harare, Zimbabwe tarehe 15 Agosti, 2024.

Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (hayupo pichani) jijini Harare, Zimbabwe tarehe 15 Agosti, 2024.

Mazungumzo yakiendelea.


NAIBU WAZIRI CHUMI AFUNGUA KONGAMANO LA KISWAHILI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amefungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo. 

Kongamano hilo linaloongozwa na mada kuu isemayo "Lugha ya Kiswahili kwa Maendeleo Barani Afrika" linajumuisha Wataalam, Watafiti na wadau wa Kiswahili kutoka Nchi za Afrika Mashariki na sehemu mbalimbali duniani. 

Akifungua Kongamano hilo Waziri Chumi ameeleza kuwa kiswahili kimekuwa miongoni mwa lugha inayotuunganisha Waafrika hususan waliopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, na hasa kutokana na mchango wake wakati wa harakati za kupigania uhuru. 

Akizungumzia nafasi ya Wizara katika kueneza lugha ya Kiswahili ulimwenguni Mhe. Chumi ameeleza Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje Nchi ilitoa mchango mkubwa katika kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza Afrika kutambuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). 

Vilevile ameongeza kusema kuwa licha ya mchango huo, Wizara ya Mambo ya Nje inaendelea kukipa kipaumbele cha kipekee Kiswahili kupitia Sera Mpya ya Mambo ya Nje inayofanyiwa mapitio, hatua ambayo itachangia kubidhaisha lugha hiyo adhimu duniani hivyo kuongeza matumizi ya Kiswahili nje ya mipaka yetu. 

"Kwa sasa Wizara yetu ipo kwenye hatua za mwisho za mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Taifa letu. Kutokana na tathmini tuliyoifanya kwenye mapitio hayo, tumekubaliana kuongeza mawanda ya Diplomasia ya Uchumi kwa kujumuisha maeneo ambayo siyo ya jadi (traditional) ikiwemo masuala ya kubidhaisha Kiswahili" Alieleza Mhe. Chumi.

Aliongeza kusema kuwa Wizara kwa siku za usoni inatarajia kuongeza wigo wa upatikanaji wa fursa kwa waalimu wa Kiswahili na wakalimani sehemu mbalimbali duniani pamoja na uuzaji wa vitabu vya kiswahili.

Kwa upande wake, mratibu wa kongamano hilo Dkt. Zainabu Idd ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuenzi na kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya nchi. 

Aidha, Dkt. Zainabu pamoja na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kutoa msukumo wa matumizi ya Kiswahili katika majukwaa na matukio mbalimbali ya kimataifa ikiwemo katika matamasha makubwa ya michezo kama vile AFCON, ili kukiongezea thamani na kuwavutia watu wengi zaidi duniani kutumia lugha hiyo adhimu.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikisha kuongeza wigo wa matumizi ya Lugha ya Kiswahili hususan katika Jumuiya za Kikanda ambapo tayari Jumuiya za SADC, EAC na AU zinatumia lugha hiyo katika kuendesha vikao mbalimbali. 

Vilevile Wizara inaendelea na mikakati ya kukuza na kubidhaisha Kiswahili ikiwemo kufungua madarasa ya kufundishia Kiswahili katika Balozi za Tanzania zilizopo sehemu mbalimbali duniani. 

CHAKAMA ni chama kinachoundwa na wahadhiri wanaofundisha Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki kikilenga kuunganisha wadau wa Kiswahili Kikanda na Kimataifa kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo utafiti na kufanya mijadala fikirishi kuhusu lugha ya Kiswahili
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akitia saini kwenye kitabu cha wageni muda mfupi kabla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akisalimiana na Prof. Albino John Tenge Mkuu wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii, alipowasili katika Chuo Kikuu cha Dodoma kufungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akikabidhiwa cheti cha kutambua mchango wa Wizara katika kufanikisha kufanyika kwa Kongamano hilo na kukuza lugha Kiswahili.
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akifuatilia  hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodom
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea
Mkuu wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii Prof. Albino John Tenge akizungumza kwenye ufunguzi Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa CHAKAMA linalofanyika jijini Dodoma
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea

PROF MKENDA AFUNGA MKUTNO WA ELIMU WA EAC JIJINI ARUSHA

 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti, 2024.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti, 2024.

Mwenyekiti wa Baraza la Kisekta na Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Sudan Kusini Mhe. Awut Deng Achuil akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.



 

washiriki wakifuatilia ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.


washiriki wakifuatilia ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.


washiriki wakifuatilia ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.


Picha ya pamoja na Meza Kuu wakati wa ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.

Picha ya pamoja na Meza Kuu wakati wa ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.

 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amefunga rasmi Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha. 

Akizungumza katika hafla hiyo Prof. Mkenda amezitaka nchi wanachama kuandaa mpango kazi utakaoonesha namna bora ya kutekeleza maazimio yaliyotokana na mkutano huo ili kuhakikisha yanafanyiwa kazi kwa ukamilifu.

Pia ametaka kuhakikisha mafanikio yote yaliyopatikana katika maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU yanasherehekewa na kutafakari jinsi ya kuwa na mifumo bora zaidi ya utoaji elimu kwa vijana na hivyo baada ya miaka miwili mkutano ujao uone matunda ya mkutano huo. 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kisekta na Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Sudan Kusini Mhe. Awut Deng Achuil alıtoa wito wa kuchukua hatua na kujitoa zaidi ili kuhakikisha malengo na maazimio ya mkutano yanatekelezwa kwa vitendo na ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji pamoja na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama kwa kuandaa mkutano huo kwa mafanikio makubwa. 

Mkutano huo wa kwanza na wa aina yake kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki ulijumuisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka Serikalini na sekta binafsi umejadili na kuweka mikakati mipya ya kukabiliana na fursa na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Kufanyika kwa mkutano huo ni utekekezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo; na Umoja wa Afrika. 

Mkutano huo wa elimu na Maadhimisho uliwakutanisha Mawaziri wa Elimu kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wageni mashuhuri wakiwemo Wawakilishi wa Nchi mbalimbali kama Jamhuri ya Watu wa China; Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Kikanda na Kimataifa zinazojihusisha na agenda ya kuendeleza sekta ya elimu kama vile Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika (ADEA), Taasisi ya Haki Elimu, na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ). 

Mkutano huo pia uliwakutanisha Wadau wa elimu zaidi ya 600 kutoka Nchi Wanachama, Taasisi za elimu, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Sekta binafsi, Mashirika ya kimataifa, Asasi za kiraia waliokutana kutathmini, kubadilishana uzoefu wa mbinu bora za uendelezaji wa sekta ya elimu. Mkutano huo uliandaliwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Nchi wanachama, taasisi zisizo za kiserikali , wadau wa maendeleo na bhana vya elimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ulianza tarehe 12 hadi 15 Agosti 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan awasili Zimbabwe

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili Zimbabwe kwa ajilli ya kushiriki Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024.


WAZIRI KOMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA AFRIKA KUSINI NA MADAGASCAR


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Mhe. Dkt. Rasata Rafaravavitafika pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) leo tarehe 14 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.

 

Akizungumza na Mhe. Lamola, Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo baina ya Tanzania na Afrika kusini ili kukuza sekta za kiuchumi ikiwemo biashara, utalii, uwekezaji, elimu, afya na maeneo mengine ya kimkakati kwa maslahi ya pande zote mbili.

 

Naye Mhe. Lamola ameeleza kuwa Afrika Kusini inaendelea kuthamini mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Taifa hilo hivyo, ina nia ya dhati ya kuuenzi mchango huo kwa kukuza ushirikiano katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa ustawi wa wananchi wa mataifa hayo mawili.

 

 

Aidha, katika mazungumzo ya Mhe. Kombo na Mhe. Dkt. Rafaravavitafika wamejadili juu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na taifa hilo hususan katika sekta ya uchumi wa blue ambao Tanzania imeuwekea mkazo ili kukuza uchumi kupitia rasilimali za bahari zinazopatikana na kukuza biashara yake kimataifa.

HABARI KATIKA PICHA: Waziri Kombo alipokutana kwa mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola.







HABARI KATIKA PICHA: Waziri Kombo alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Mhe. Dkt. Rasata Rafaravavitafika