Wednesday, March 3, 2021

BALOZI BRIG. GEN. IBUGE AFUNGUA MKUTANO WA SITA WA TUME YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA BURUNDI

Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) kati ya Tanzania na Burundi umeanza rasmi mjini Kigoma, ukiwa na lengo la kujadili mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kutumia fursa zilizopo baina ya nchi hizo katika kukuza uchumi.


Akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili masuala matano o ambayo ni pamoja na siasa na mahusiano ya kidiplomasia, ulinzi na usalama, maendeleo ya miundombinu, ushirikiano katika sekta ya uchumi na kijamii.

Alisema mafanikio ya mkutano huo yanategemea zaidi jitihada za pamoja kama watendaji katika kutekeleza masuala watakayokubaliana na kwamba kujadili kwa uhalisia na kufikia makubaliano yatakayotekelezeka ni moja ya lengo la mkutano huo.

“Katika mkutano huu tuwe tayari kusimamia na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa makubaliano na kuweka utaratibu wa kufanya mapitio ya utekelezaji wa masuala tutakayokubaliana angalau mara moja kwa mwaka,”alisema Balozi Ibuge.

Alisema kwa upande wa Tanzania utawekwa utaratibu wa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya makubaliano yote yaliyofikiwa kwani kwa kufanya hivyo mkutano huo utatimiza matarajio ya viongozi wakuu na wananchi wa mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaendeleo wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba alisema wanaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono ombi lao la kujiunga na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kuendelea kuwasemea kwenye majukwaa ya kimataifa ili waweze kuondolewa vikwazo vya kiuchumi walivyowekewa na Jumuiya ya Ulaya.

“Tumejidhatiti kuhakikisha tunawaonesha wale wote wanaoiwekea vikwazo nchi ya Burundi kuwa wakati umeabadilika, kwani sasa tunayo amani na utulivu na kwamba tupo kwenye juhudi kubwa za kuimarisha ushirikiano na nchi zote na washirika wa maendeleo wenye mapenzi mema na nchi yetu,”alisema Ntirampeba.

Mkutano huo ambao umefunguliwa leo kwa ngazi ya wataalam utafuatiwa na Mkutano wa Mawaziri wa Wizara za Mambo ya Nje za Burundi na Tanzania ambao wanatarajiwa kusaini makubaliano yaliyofikiwa na pande zote mbili kwa ajili ya utekelezaji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert Ibuge akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi unaofanyika mjini Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. Mkutano huu umeanza kwa ngazi ya wataalam na utamalizika kwa ngazi ya Mawaziri tarehe 5 Machi 2021. Kulia walioketi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba.

Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kutoka Tanzania wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi unaofanyika mjini Kigoma

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko (kulia)  akiwa na viongozi wengine kutoka Tanzania wanaoishiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi ulioanza kufanyika  kwa ngazi ya wataalam.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Frank Mwega akizungumza kuhusu ratiba ya mkutano wa ngazi ya wataalam.

Bw. Mwega akizungumza

Sehemu ya ujumbe kutoka Burundi unaoshiriki mkutano wa wataalam wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Burundi 

Ujumbe wa Burundi

Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wanaoshiriki mkutano sita wa tume ya pamoja ya kudumu kwa ngazi ya wataalam

Ujumbe wa Tanzania

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Ujumbe wa Tanzania ukiwa kwenye mkutano

Sehemu ya ujumbe kutoka Tanzania wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkutano 

Picha ya pamoja

 

Tuesday, March 2, 2021

MKUTANO WA SITA WA TUME YA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA BURUNDI KUFANYIKA MKOANI KIGOMA

Tanzania na Burundi zimejipanga kuutumia Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kama njia mojawapo ya kuhamasisha wananchi wa pande zote mbili kuchangamkia fursa mbalimbali za uchumi zinazopatikana katika nchi hizi ili kunufaika nazo.


Kauli hiyo imetolewa kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge na mwenzake kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba walipokutana na Waandishi wa Habari leo mjini Kigoma kwa ajili ya kuwajulisha kuhusu mkutano huo utakaofanyika mjini humo kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.


Balozi Ibuge alieleza kuwa, Tanzania na Burundi zimeendelea kuwa na ushirikiano wa kihistoria na kindugu kwa muda mrefu huku kila nchi ikinufaika kwa kiasi kikubwa na ushirikiano huo. Hata hivyo alieleza kuwa, bado upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwahamasisha wananchi wa Tanzania na Burundi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye nchi hizo ili ziwanufaishe kiuchumi. Fursa hizo ni pamoja na biashara na uwekezaji.


“Mikutano ya Tume za Pamoja za Kudumu pamoja na mambo mengine inaangalia namna ya kuhakikisha kila mwananchi kutoka nchi husika ananufaika na fursa zilizopo na jukumu letu ni kuendelea kuwahamasisha kuzichangamkia fursa hizo” alisema Balozi Ibuge.


Akizungumzia ukuaji wa sekta ya uchumi kati ya Tanzania na Burundi, Balozi Ibuge alisema pamoja na changamoto mbalimbali,  biashara kati ya Tanzania na Burundi imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kutoa mfano wa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 ambapo Tanzania na Burundi zilifanya biashara zenye thamani ya shilingi Bilioni 619.9 ukiwa ni  wastani wa Shilingi Bilioni 123.9 kwa mwaka.  Katika kiasi hicho, Tanzania iliuza nchini Burundi bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 604.9 na Burundi iliuza Tanzania bidhaa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.4.


Aidha, akizungumzia huduma ya wakimbizi, Balozi Ibuge alieleza kuwa, Tanzania imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi huku Serikali ya Burundi ikiendelea kuwahimiza wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari kutokana na kuimarika kwa hali ya amani na utulivu nchini humo.


“Tanzania imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi, hata hivyo kutokana na kuimarika kwa hali ya amani na usalama nchini kwao Serikali yao imeendelea kuwahimiza kurejea ili kwenda kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa lao. Itakumbukwa kuwa, zoezi la kuwawezesha wakimbizi hao kurejea kwa hiari Burundi limeendelea kuratibiwa na Kamati ya Utatu inayojumuisha Tanzania, Burundi na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo kati ya mwezi Septemba 2017 na Februari 2021, jumla ya wakimbizi 113,488 wamerejea nchini Burundi kwa hiari” alifafanua Balozi Ibuge.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba alisema tume ya pamoja ya ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi na nchi kwani hutoa nafasi kwa nchi mbili kutathmini mafanikio yaliyofikiwa kupitia ushirikiano uliopo, kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali na kuainisha hatua imara zaidi za kufikia malengo kusudiwa. Alieleza kuwa, mikutano hii ni fursa nzuri kwa pande zote mbili kujipanga na kuboresha utendaji kulingana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani na katika nchi yakiwemo yale ya kisera na kimazingira.


Kadhalika, alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Tanzania na kuitaja kama nchi ya kupigiwa mfano katika kuhudumia wakimbizi wakiwemo wale wa kutoka Burundi ambao wamekuwa wakipokelewa tangu mwaka 1972. Aliongeza kuwa, Burundi inajivunia mchango wa Tanzania kwenye ustawi wa nchi hiyo na kwamba nchi hiyo inavutiwa na uongozi imara wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao unalenga kuwaletea wananchi wote maendeleo.


Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi ambao unafanyika miaka 15 baada ya Mkutano wa Tano uliofanyika jijini Dar es Salaam mwaka 2006 unalenga kuendeleza, kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Burundi. Mkutano huu ambao utaanza kwa ngazi ya wataalam kutoka Tanzania na Burundi tarehe 3 Machi 2021utahitimishwa na Mkutano wa Mawaziri kutoka nchi hizo tarehe 5 Machi 2021.

=================================================================



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Ntirampeba akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Tanzania, Prof. Riziki Shemdoe (katikati) pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji wa Tanzania, Mhandisi Nadhifa Kemikimba wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi  wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba naye akizungumza  wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata naye akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jily Maleko akifuatilia  Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Frank Mwega akifuatia Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Sehemu ya wadau kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Burundi walioshiriki mkutano kati ya Baloiz Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Sehemuu nyingine ya wadau

Sehemu ya wadau wakifuatilia mkutano

Wadau wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Mkutano ukiendelea



 

Monday, March 1, 2021

PROF. KABUDI APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO ZA MABALOZI WATEULE

 

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kupokea nakala za hati za utambulisho za mabalozi wateule hapa nchini pamoja na hati ya utambulisho ya Konseli Mkuu wa China Zanzibar.

Mabalozi waliowasilisha nakala za hati za utambulisho kwa Prof. Kaabudi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ni Balozi mteule wa Namibia, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias na Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil, pamoja na Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.

Awali akiongea mara baada ya kupokea nakala ya hati ya utambulisho wa Balozi mteule wa Namibia, Prof. Kabudi amesema kuwa Tanzania na Namibia zimekubaliana kuendeleza kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji, mifugo na uvuvi katika bahari kuu pamoja madini kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

“Tanzania na Namibia tuna historia inayofanana iliyoanza tangu vita vya ukombozi wa uhuru wa Namibia….wote tulikuwa makoloni ya Wajerumani, hivyo tumekubaliana kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, na katika maeneo ya mazao ya mifugo, uvuvi, kilimo, na madini, ambapo katika maeneo hayo Tanzania tunayo mengi ya kujifunza kutoka Namibia hasa katika sekta ya mifugo na uvuvi katika bahari kuu,hivyo tukiimarisha maeneo hayo uchumi wan chi zetu mbili utazidi kukua na kuimarika” Amesema Prof. Kabudi

Kwa upande wake Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Namibia.

“Mimi kama mwakilishi wa Serikali ya Namibia nitajitahidi wakati wa utumishi wangu hapa Tanzania kuhakikisha kuwa uhusiano wetu sisi Namibia na Tanzania unazidi kuimarika kwa maslahi mapana ya wananchi wetu wote,” Amesema Mhe. Tobias     

Kadhalika, Prof. Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho wa Balozi mteule wa Ireland hapa nchini, Mhe. Mary O’Neil ambapo mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho Balozi Mteule ameahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Ireland.

“Ni furaha kwangu kuwepo hapa leo na kukabidhi nakala ya hati ya utambulisho wangu hapa nchini Tanzania, napenda kuahidi kwa kipindi nitakachokuwa hapa nitahakikisha kuwa uhusiano wetu wa kidiplomasia unakuwa na kuimarika kwa maslahi ya mataifa yetu,” Amesema Balozi O’Neil

Kwa upande wake Prof. Kabudi amesema kuwa mahusiano ya kibalozi kati ya Tanzania na Ireland yalianza tangu mwaka 1979 ambapo Ireland ilianzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu vya Ireland kwa watanzania katika taaluma mbalimbali.

“Mbali na kutoe ufadhili wa elimu kwa Watanzania, tumeongelea masuala ya kuimarisha ufadhili wa masomo, biashara na uwekezaji hasa kwa kutumia teknolojia ya habari pamoja na kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini tutaangalia maeneo mapya ya ushirikiano ili tuweze kuendele kuimarisha ushirikiano baina yetu na Ireland,” Amesema Prof. Kabudi.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kupokea hati ya utambulisho wa Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.

Prof. Kabudi amesema kuwa China imekuwa ikiisaidia sana Zanzibar tangu mapinduzi ya mwaka 1964, katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ukarabati wa uwanja wa ndege, hospitali ya Mnazi mmoja pamoja na Abdallah Mzee………na “tumekubaliana kuwa tutaendelea kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania – Zanzibar ikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” Amesema Prof. Kabudi   

Nae Konseli Mkuu wa China Zanzibar amesema kuwa China kama taifa lililoendelea wataendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha mahusiano ya China na Tanzania yanaimarika kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“China inaunga mkono umoja, amani na mshikamano wa Tanzania, sisi tumekuwa marafiki wa muda mrefu na tutaendelea kusaidiana ili kuhakikisha kuwa mahusiano kati ya China na Tanzania yanazidi kuimarika hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Magufuli na Rais Mwinyi,” Amesema Mhe. Zhisheng 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule  wa Namibia, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil akimkabidhi nakala ya hati za utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea hati za utambulisho kutoka Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng 

Friday, February 26, 2021

WAKUU WA NCHI WA AFRIKA MASHARIKI KUFANYAUTEUZI WA VIONGOZI WA JUMUIYA

Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatarajiwa kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa Jamuiya katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi hao unaotarajiwa kufanyika Jumamosi tarehe 27 Februari, 2021. Viongozi waonatarajiwa kuteuliwa ni wale wa ngazi za maaumuzi katika Jumuiya ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya na Katibu Mkuu wa Jumuiya.

Haya yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) muda mfupi baada ya hitimisha Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki. Mkutano huu uliofanyika kwa njia ya ana kwa ana na video umefanyika katika ngazi tatu, ambazo ni; ngazi ya Wataalam (tarehe 22-23 Februari), ngazi ya Makatibu Wakuu (tarehe 24 Februari) na hatimaye ngazi ya Mawaziri tarehe 25 Februari 2021. 

Waziri Kabudi aliendelea kueleza kuwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri limepitia nyaraka mbalimbali zinazohusu maendeleo na utendaji wa Taasisi mbalimbali za Jumuiya ambapo wamebaini kuwa, licha ya kuwepo kwa changamoto za Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) Jumuiya pamoja na Taasisi zake zimeendelea kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Kila mwaka, Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki hukutana mara mbili, mkutano mmoja hufanyika mara moja kabla ya mkutano wa Wakuu wa Wakuu wa Nchi. Mikutano ya baraza husaidia kudumisha uhusiano kati ya maamuzi ya kisiasa yaliyochukuliwa kwenye Mkutano na utendaji wa kila siku wa Jumuiya. Kanuni, maagizo na maamuzi yaliyochukuliwa au kutolewa na Baraza yanatekelezwa na Nchi Wanachama na Taasisi zingine zote za Jumuiya isipokuwa Wakuu wa Nchi, Mahakama na Bunge.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.
Washiriki kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea
Kutoka kushoto; Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiwa unapigwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisaini ripoti ya Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki
Mkutano ukiendelea

Wednesday, February 24, 2021

MKUTANO WA 21 WA WAKUU NCHI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUFANYIKA FEBRUARI 27

 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam   

Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepangwa kufanyika Jumamosi, 27 Februari, 2021 kwa njia ya mtandao (video conference).

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa mkutano huo ni muhimu kwa sababu ya maamuzi ya msingi ya kuiwezesha jumuiya hiyo iweze kuendelea kufanya kazi zake.

 

“………Jambo la kwanza ni uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika mashariki, kwa hiyo Wakuu wa nchi watamchagua Katibu Mkuu mpya siku hiyo,” Amesema Prof. Kabudi na kuongeza kuwa mkutano huo pia utafanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (The East African Court of Justice) kutokana na baadhi ya majaji kufikia umri wa kustaafu wa miaka 70, ambapo Tanzania imempendekeza jaji Yohane Masara kuwa jaji wa jopo la kwanza la mahakama ya Afrika Mashariki.

 

“Pamoja na kuteuliwa kwa majaji hao, pia Wakuu wa nchi watamteua Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (Judge President) pamoja na kumchagua Makamu wa Rais (Vice President) kwa ngazi ya Rufaa ya Mahakama hiyo, lakini katika ngazi ya awali Mkutano huo utamchagua Principla Judge wa Mahakama hiyo, kwa hiyo mtaona hizo ni baadhi ya shughuli zilizopelekea Wakuu wa nchi wakutane ili kuweza kufanya teuzi hizo muhimu ili shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki ziweze kuendelea”  Ameongeza Prof. Kabudi

 

Prof. Kabudi ameongeza kuwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia utajadili Muswaada ulipitishwa na Bunge la Afrika Mashariki kwa ajili ya kupata bajeti.

 

Mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki utakaofanyika Alhamisi tarehe 25 Februari 2021 kwa ajili ya kuandaa mkutano wa wakuu wa nchi. Aidha, mkutano wa Baraza la Mawaziri umetanguliwa na mkutano Wataalam ulifanyika tarehe 22-23 Februari na mkutano wa Makatibu Wakuu ulifanyika tarehe 24 Februari.

 

Tarehe 1 Januari 2019, Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame alikabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo jijini Arusha Tanzania.

 

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi ameelezea kuhusu ziara ya kikazi aliyoifanya nchini Ufaransa kuanzia tarehe 16 mpaka 21 Februari 2021, kufuatia mwaliko wa Mhe. Jean-Yves Le Drian, Waziri anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa na kuelezea mafanikio makubwa ya ziara hiyo.

 

“Pamoja na mambo mengine niliweza kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Ufaransa, Umoja wa Wafanyabiashara wa Ufaransa (MEDEF), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Uongozi wa Kampuni ya Total, Kundi la Maseneta wa Bunge la Ufaransa ambao ni Marafiki wa Tanzania, Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Wadau wa Utalii pamoja na kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchini Ufaransa,” Amesema Prof. Kabudi.


Aidha, kupitia ziara hiyo, Ufaransa imeeleza kuwa itaendelea kuhamasisha Makampuni yake kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kuhamasisha watalii kuja kuwekeza Tanzania, kuiunga mkono Tanzania katika masuala mbalimbali kwenye ngazi ya Umoja wa Mataifa.

Mengine ni kuwa Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la AFD itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleao hapa nchini hususan kwenye sekta ya maji, elimu, nishati, miundombinu, utalii, ulinzi na usalama;na Ufaransa kuwa tayari kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi na Usalama.

Mafanikio mengine ni pamoja na kukubaliana kuanza mara moja mchakato wa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika kwenye Umoja wa Mataifa. Nilimweleza mafanikio yaliyopatikana kwenye lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na kuwa miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi barani Afrika pamoja na kutumika kama lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika (AU) na SADC;

“Tulikubaliana kuanza mchakato ili kuwa na siku rasmi ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani kila mwaka. Nilipendekeza tarehe 7 Julai kila mwaka kwa kuzingatia kuwa tarehe hiyo ndio kilizaliwa Chama cha TANU. TANU ilikifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kupigania uhuru wa Tanganyika wakati huo. Tumeona ni jambo jema kuienzi tarehe hiyo muhimu kwenye historia ya nchi yetu,” Amesema Prof. Kabudi

Kupitia ziara hiyo, Prof. Kabudi aliweza kuyakaribisha Makampuni ya Ufaransa kuja kuwekeza nchini hususan kwenye sekta ya viwanda, kilimo, nishati, maji, elimu, miundombinu, uvuvi na utalii. Makampuni hayo yalionesha kuridhika na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania.

“Baadhi ya Makampuni makubwa yaliyoshiriki majadiliano hayo ni pamoja na Bureau Veritas; Mitsubishi II; Biolore Transport and Logistics; Eutelsat Company; Artelia Company; Catering International Services-CIS; Systra Company;  Transder Group; Credit Agricole Corporate and Investment Bank; Air Bus; na Bouyegues Construction. Mengi ya makampuni haya tayari yamefanya uwekezaji mkubwa nchini katika maeneo mbalimbali,” Amesema Prof. Kabudi.

Aidha, makampuni hayo yameonesha utayari wa kutekeleza miradi hapa nchini kwa kutumia fedha kutoka Serikali ya Ufaransa zitakazotolewa kama mkopo wenye masharti nafuu. Tumeyakaribisha Makampuni hayo kuja nchini ili kukutana na wataalam wetu kwa ajili ya majadiliano.

Prof. Kabudi ameelea kuwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha majadiliano ya miradi ya kimkakati kwa Tanzania katika sekta ya maji safi na usafi wa mazingira, nishati na miundombinu ambapo tayari jumla ya fedha Euro milioni 791.70 tayari zimeshatengwa kwa ajili ya miradi hiyo. Fedha hizo zitaelekezwa katika baadhi ya miradi ambayo ni mradi wa ujenzi wa awamu ya tano ya mwendokasi BRT Phase 5 (Euro milioni 150), mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira mkoani Shinyanga (Euro milioni 70), ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Kakono (Euro milioni 100), mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia jua chini ya TANESCO (Euro milioni 130) na mradi wa kuunganisha umeme Tanzania na Uganda (Euro milioni 100).

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amewasihi watanzania kuheshimu katiba na kuacha mara moja tabia ya kusambaza taarifa za uongo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasomea waandishi wa habari (hawapo pichani) moja ya kifungu cha katiba kuhusu mipaka ya haki na Uhuru na hifadhi kwa haki na wajibu jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) aina za cocoa zinazozalishwa Tanzania na kuuzwa nchini Ufaransa jijini Dar es Salaam